MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.

SHAIRI: NASIKITIKA HADUMU RAFIKI YANGU UJANA - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
SHAIRI: NASIKITIKA HADUMU RAFIKI YANGU UJANA - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6)
+---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50)
+---- Thread: SHAIRI: NASIKITIKA HADUMU RAFIKI YANGU UJANA (/showthread.php?tid=1402)

SHAIRI: NASIKITIKA HADUMU RAFIKI YANGU UJANA - MwlMaeda - 10-27-2021

KWAKO KIJANA....
Pokea shairi na nasaha wewe kijana kuhusu ujana kutoka kwa Hayati Shaaban Robert mtaalamu wa Kiswahili, mashairi na mwandishi wa vitabu mashuhuri kikiwemo cha Kusadikika.

1.Ujana kitu kitamu, tena ni azizi sana,
Maungoni mwangu humu, nilikuwa nao jana,
Kwa wingi katika damu, tahamaki leo sina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

2. Kichwa kimejaa mvi,kinywani meno hamna,
Nikenda kama mlevi, miguu nguvu haina,
Kumbe ujana ni hivi, ukenda hauji tena,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

3. Jua langu limekuchwa, na nyota nilizoona,
Ukinitazama kichwa, nywele nyeusi hakina,
Kama zilizofikichwa, zikang'olewa mashina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

4. Natatizika kauli,midomo najitafuna,
Nimekusanya adili, walakini hali sina,
Dunia kitu bahili, hiki una kile huna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

5. Nilikuwa ni waridi, furaha ya wasichana,
Neno hawakunirudi, wakati wa kukutana,
Sasa nanuka baridi, wanionapo waguna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

6. Walio wakinihusu, walikuwa wengi sana,
Wanawake wenye busu,uzuri na usichana,
Leo sina hata nusu, ya wanitajao jina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

7. Wazuri wenye uturi, na mikono yenye hina,
Kila mtu mashuhuri, alipenda kuniona,
Nilifaa kwa shauri, na sasa kauli sina,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

8. Dunia bibi harusi,kwa watu kila namna,
Inapendeza nafsi, wakati wa kuiona,
Na leo sina nafasi, kwa uzee kunibana,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

9. Kilichokuwa gizani, niliweza kukiona,
Nikakijua thamani, sura yake hata jina,
Leo sijui ni nini, hata ikiwa mchana,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

10. Kilichotaka fikra, niliweza kukinena,
Kwa mfano na kwa sura, mpaka kikafanana,
Leo tazama hasara, nguvu hiyo sina tena,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

11. Kilichotaka mapimo, sikifahamu mapana,
Marefu yake na kimo, siifahamu bayana,
Nusu nimo nusu simo, duniani najiona,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

12. Hadumu nasikitika, rafiki yangu ujana,
Machozi yamiminika, na kutenda hapana,
Ni wakati umefika, uzee dawa hauna,
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

13. Hauna dawa uzee, mabega yamepetana,
Anionaye ni 'wee", ondoka hapa laana,
Wanaposema na miye, niliyekuwa na jina!
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

14. Kaditamati shairi,uchungu wanitafuna,
Walakini nafikiri, twafuata Subuhana,
Katika ile amri, ya "kuwa" na "kutengana"
Nasikitika hadumu, rafiki yangu ujana

UMEJIFUNZA NINI HAPO KIJANA?

SHAABAN ROBERT (1909-1962)
Alizaliwa na kuzikwa Tanga.