BEN R. MTOBWA ALISTAHILI ‘ZAWADI YA USHINDI’ - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Watunzi wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=17) +--- Thread: BEN R. MTOBWA ALISTAHILI ‘ZAWADI YA USHINDI’ (/showthread.php?tid=1369) |
BEN R. MTOBWA ALISTAHILI ‘ZAWADI YA USHINDI’ - MwlMaeda - 10-25-2021 Kwa ufupi
Ni kweli ‘Tutarudi na Roho Zetu? au hizi ni ‘Salamu Toka Kuzimu’. Pengine hii ni ‘Roho ya Paka’ lakini inawezekana hawa ni ‘Malaika wa Shetani’ wanaotaka kumuweka ‘Mhariri Msalabani”. Hapana nadhani ‘Najisikia Kuua Tena’.
Na Florence Majani ,Mwananchi
Ni kweli ‘Tutarudi na Roho Zetu? au hizi ni ‘Salamu Toka Kuzimu’. Pengine hii ni ‘Roho ya Paka’ lakini inawezekana hawa ni ‘Malaika wa Shetani’ wanaotaka kumuweka ‘Mhariri Msalabani”. Hapana nadhani ‘Najisikia Kuua Tena’.
Naam, kwa wasomaji wa vitabu hasa riwaya pendwa, aya hii ya kwanza haina mushkeli kwao.
Kwa wewe ambaye pengine hujaielewa, maneno yote yaliyo katika fungua na funga semi ni vitabu vilivyowahi kuandikwa na Ben Mtobwa aliyefariki dunia mwaka 2008.
Nimeishika kalamu yangu kumkumbuka kutokana na umahiri wake wa uandishi wa vitabu ambao naweza kusema umechochea mimi kuwa mwandishi leo.
Nilianza kusoma kazi za Mtobwa nikiwa darasa la tatu, nakumbuka nilikuwa sijali kama hakuna umeme nyumbani. Nilikaa pembeni ya taa ya kandili usiku na kukisoma kitabu chake cha Tutarudi na Roho Zetu hadi usiku wa manane.
Mtobwa atakumbukwa kwa umahiri wake katika uandishi. Uandishi ulioweza kumfanya msomaji asikiweke kitabu chini.
Alikuwa ni mwandishi aliyeweza kutunga hadithi inayofanana na ukweli kiasi cha msomaji kuamini yupo mtu anayeitwa Joram Kiango ambaye siku zote huwa ni mhusika mkuu wa kazi zake.
Aliwaumba wahusika wake na kuwapa sifa ambazo msomaji angedhani ni kweli wanaishi au ni binadamu wa kweli.
Kwa mfano, Mtobwa alimuumba Joram Kiango kama kijana mtanashati, hodari na mwenye mapenzi tele kwa nchi yake.
Tofauti na waandishi wengine, Mtobwa hakuwa msahaulifu, bali alizitumia tabia zile zile za Joram Kiango katika kila kitabu.
Kadhalika alimjenga Nuru kama msichana mwerevu, mzalendo na mwenye uzuri wa kipekee. Fasihi ya aina hii ilimfanya msomaji aamini Nuru na Joram ni watu wanaoishi, lakini kumbe walikuwa ni wahusika wa kubuniwa tu.
Pamoja na umahiri wa kuwaumba wahusika, Mtobwa alikuwa ni mwandishi aliyekuwa akijidhatiti kwa kusoma, kwani kazi zake nyingi zilihusisha taarifa na mada za kitaalamu.
Mwandishi huyu atakumbukwa kwa uwezo wake wa kuunganisha matukio katika mtiririko unaomfanya msomaji aendelee kusoma, na si hivyo tu bali si ajabu msomaji akarudia vitabu mara kadhaa bila kuvikinai.
Mwanafasihi huyu hakuwaegemea riwaya za mapenzi tu, kazi zake nyingi zilihusisha upelelezi, uzalendo na harakati za ukombozi wa Afrika na hata kufichua ufisadi.
Tutampata wapi Ben Mtobwa mwingine ambaye atakuwa na kipaji cha uandishi kiasi hiki? Nchi imepoteza waandishi wa riwaya pendwa, kuanzia Elvis Musiba na Willy Gamba wake hadi Ben Mtobwa na Joram Kiango!
Siwezi kuisahau riwaya ya Zawadi ya Ushindi. Riwaya hii, niliisoma nikiwa shule ya sekondari na mpaka sasa nimerudia kuisoma mara mbili.
Katika riwaya hii, Mtobwa anaonyesha vita vya Kagera, anaonyesha uzalendo aliokuwa nao msichana Russia kwa nchi yake hata akamshawishi, mchumba wake Sikamona akapigane vita vya Kagera.
Mtobwa alionyesha jinsi Watanzania walivyohamasishwa wakati ule kujumuika na kumng’oa Iddi Amin.
Miaka nane sasa imepita tangu Ben Mtobwa afariki dunia, kilichobaki ni kumpa ‘Zawadi ya Ushindi’ kwa kuzisoma kazi zake zilizofichua mafisadi waliofanana na ‘Malaika wa Shetani’ na wahujumu uchumi wenye ‘Roho ya Paka’.
Waandishi wajifunze kutoka kwake kwa kufichua yale yaliyo ‘Nyuma ya Pazia’ kwa kuwa kalamu ya mwandishi lazima itatufanya ‘Turudi na Roho Zetu’ Ben Mtobwa hakika unastahili ‘Zawadi ya Ushindi’
fmajani@mwananchi.co.tz
0715-773366
|