SHAIRI: SAFARI YA KILELENI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: SAFARI YA KILELENI (/showthread.php?tid=1246) |
SHAIRI: SAFARI YA KILELENI - MwlMaeda - 09-15-2021 SAFARI YA KILELENI Ukitaka kwenda juu, ufikie kileleni, Kwanza shika vichuguu, mawe yaweke pembeni, Usiheme juu juu, kujichokea mwanzoni, Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Inaweza kuwa ndefu, safari ya kileleni, Hasa ukiwa dhaifu, utaishia njiani, Hupaswi kuwa na hofu, yafaa kujiamini, Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Yataka maandalizi, safari si lelemama, Ule ushibe mchuzi, wali au hata sima, Tena uwe na pumzi, si kidogo wachutama Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Ngazi ikiwa imara, kuteleza ni muhali, Siyo ngazi ya kuchora, bali ngazi kwelikweli, Kama huna ngazi bora, kaa utulie tuli, Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Kamata mawe vizuri, kulia pia kushoto, Yaegemee vizuri, ili upate fukuto, Kwa jua la adhuhuri, yatakutunzia joto, Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Mapango yenye vijito, pia yapo safarini, Maji matamu ya mto, waweza tia kinywani, Si kwa pesa au vito, yalambe ukitamani, Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Utapata burudani, ukifika kileleni, Milima yote nchini, ina uzuri wa shani, Utaona kote chini, kutokea kileleni Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Ili upate pongezi, za mpandaji mzuri, Katu usilete pozi, uonyeshe uhodari Hutopata vizuizi, njia ukiikariri Kufika juu ni kazi, yataka imara ngazi. Shaaban Mwinyikayoka (Mwanaupwa) Iringa |