MAANA YA VICHEKO KATIKA FASIHI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Chuo (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=3) +---- Forum: Shahada (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=20) +----- Forum: Maswali na majibu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=24) +----- Thread: MAANA YA VICHEKO KATIKA FASIHI (/showthread.php?tid=1216) |
MAANA YA VICHEKO KATIKA FASIHI - MwlMaeda - 09-10-2021 Vicheko katika kazi za waandishi mbalimbali huwa na maana tofautitofauti ilimradi hufanikisha maudhui ya kazi hizo na huweza kuleta maana kama vile ushindi, kejeli, furaha, uchungu, unafiki, kutisha, ujinga au kumlipiza mtu kisasi.
Kazi za kifasihi za waandishi mbalimbali zimesheheni vicheko vya wahusika wake.
Baadhi ya kazi za kifasihi zenye kutumia sana vicheko ni Amezidi (Said Ahmed Mohamed).
Vingi ya vicheko vinavyotumiwa hapa ni vya kejeli.
Kwa mfano, kuna sauti inayomcheka Ame kwa kumwambia Mari aketi kwenye kochi lisilokuwepo. Vilevile tunaona mhusika akijidharau nafsi yake, ‘Nafsi yako inajicheka’.
Zaidi ya hapo ni kuwa kipo kicheko cha furaha pale ambapo Ame na Zidi wanapocheka kwa furaha wakizungumzia magari yao ya kifahari yaliyokuwa nje ya pango lao.
Wanacheka kwa furaha na pia kejeli. Kuonesha ujinga darasani, mwalimu anawaambia wanafunzi wake, ‘Tucheke basi.’ Kisha wanacheka pamoja.
Mwishoni mwa tamthiliya, Ame anacheka kicheko cha uchungu. Anacheka kwa muda mrefu kutokana na maumivu ya tumbo na njaa.
Vicheko pia vinatumiwa sana na mwandishi wa tamthiliya ya Mashetani (Ebrahim N. Hussein).
Mojawapo ya vicheko hivi ni kile cha shetani chenye kumtisha binadamu.
Shetani pia anacheka kicheko cha ushindi kwa kuwa binadamu hawezi kumuona kwani amejigeuza upepo. Hiki ni kicheko cha dharau dhidi ya binadamu kwamba hana uwezo wa kubaini maumbo mbalimbali ya shetani.
Kuna hali ya mazungumzo ya kuchekesha baina ya baba, Mama Kitaru na daktari kuhusu ugonjwa wa Kitaru unaoambatana na vicheko vyao.
Kiko pia kicheko cha huzuni ambapo Kitaru anamwambia rafiki yake Juma, ‘Usitafsiri kicheko changu kuwa ni furaha. Nacheka kwa sababu sitaki kulia.’
Kicheko pia kinajitokeza katika tamthiliya ya Kilio Chetu, kwa mfano Anna anatoa kicheko cha dharau dhidi ya Mwarami baada ya kugundua kuwa Mwarami hana elimu ya kutosha juu ya madhara ya mahusiano katika umri mdogo.
Vilevile kicheko cha Mama Joti dhidi ya mama Suzi anayeonekana kutoelewa maana ya maneno yanayotumiwa na vijana wa kisasa kama kukanyaga nyaya kicheko hiki kinaashiria hali ya dharau kwa Mama Suzi na kumuona kuwa ni mshamba na asiyekwenda na wakati.
Kicheko cha Musa kwa Peter katika riwaya ya Watoto wa Maman’tilie kinaonesha hali ya kudharau ambapo Musa analenga kumfanya Peter ajione mjinga kwa baadhi ya mambo anayoyafanya kama kumpokea Kurwa na kwenda dampo hali ambayo Musa anaiona kama ni kujidhalilisha tu.
Kicheko cha Bi.Kirembwe kwa wazee kinaashiria kejeli dhidi ya wazee kwa jinsi alivyobaini njama zao dhidi yake, kicheko kwa Mtolewa kama ishara ya kumtisha, pia kuna kicheko cha kikatili dhidi ya Mkulima kabla ya kumpa adhabu.
Tunapochambua vicheko katika fasihi, ni lazima tutambue maana yake ya ndani ili kupata ujumbe wa kifasihi unaowasilishwa na mhusika katika kazi husika ya Fasihi.
|