KIDATO CHA NNE: UKUAJI NA UENEAJI WA KISWAHILI BAADA YA UHURU - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Sekondari (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=4) +---- Forum: Kidato cha nne (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=40) +----- Forum: Nukuu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=41) +----- Thread: KIDATO CHA NNE: UKUAJI NA UENEAJI WA KISWAHILI BAADA YA UHURU (/showthread.php?tid=1182) |
KIDATO CHA NNE: UKUAJI NA UENEAJI WA KISWAHILI BAADA YA UHURU - MwlMaeda - 09-07-2021 Ukuaji na Ueneaji wa Kiswahili baada ya Uhuru
Shughuli mbalimbali zinazowezesha Kukua na Kuenea kwa Kiswahili nchini
Baada ya uhuru kuna harakati mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kukiendeleza na kukikuza kiswahili. Harakati hizo ni pamoja na kupendekezwa kuwa lugha rasmi 1962. Mkwaka 1964 kiswahili kilipendekezwa kuwa lugha ya taifa na kuwa kitatumika katika shughuli zote za kiserikali na kitaifa mfano katika elimu hususani elimu ya msingi.
Kuundwa kwa Chombo cha usanifishaji ambacho kilikuwa na kazi ya kuhimiza maendeleo ya kiswahili, kutayarisha kamusi na vitabu mbalimbali vya sarufi na fasihi ya lugha ya kiswahili na kuandaa wataalamu watakaoshughulikia usanifishaji wa Kiswahili
Pia baada ya uhuru kulianzishwa Taasisi mbalimbali zitakazoshughulikia lugha ya kiswahili. Mfano:- BAKITA, TUKI, TUMI, UKUTA, UWAVITA, Idara ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaamu.
Baada ya uhuru nchini Tanzania kiswahili kilienea kwa kasi kubwa sana. Kuna sababu mbalimbali ambazo zilichangia kukua na kuenea kwa kiswahili hapa nchini. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na kuteuliwa kwa kiswahili kuwa lugha ya Taifa, Kiswahili kitumike katika Elimu, mfano kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi. Kuundwa kwa vyombo mbalimbali vya kukuza na kuneza kiswahili, Kiswahili kuwa Lugha rasmi na lugha ya Taifa, shughuli mbalimbali za kidini, shughuli za kisiasa na kiutawala na shughuli za kiutamaduni na uchapishaji wa vitabu na majarida mbalimbali.
Kiswahili kuwa lugha ya taifa
Baada ya uhuru mwaka 1962 kamati iliundwa ili kuangalia uwezekano wa kutumia kiswahili katika shughuli zote rasmi, mfano bungeni na shughuli zote za kiofisi. Pia kiswahili kiliteuliwa kuwa lugha ya taifa 1964 ambapo katika shughuli zote za kitaifa zitaendeshwa kwa kutumia lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili kilihimizwa kutumika katika mawasiliano yote hasa katika shughuli za umma na Wizara zote, Serikali na Bunge, kiswahili kiliendelea kupanda hadhi zaidi wakati wa Azimio la Arusha la mwaka 1967 kwani azimio hilo lilitungwa na kuandikwa kwa lugha ya kiswahili.
Kuundwa kwa vyombo vya ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili
Tanzania baada ya uhuru ilifanya jitihada za kuunda vyombo mbalimbali vya kukuza na kueneza Kiswahili katika nyanja mbalimbali mfano wa vyombo hivyo ni UWAVITA BAKITA, TUKI, Taasisi ya Elimu,TAKILUKI na Chama cha Kiswahili Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Kutumika katika elimu
Kiswahili licha ya kutumika katika shughuli mbalimbali za kiserikali, kilipendekezwa kutumika katika shule za Msingi na kufundishwa katika elimu ya sekondari kama somo na katika vyuo vikuu wanatoa shahada mbalimbali za lugha ya kiswahili. Pia katika Elimu ya watu wazima ambao hawakujua kusoma na kuandika. Watu hawa walijifunza masomo mbalimbali kwa lugha ya kiswahili na kuwafanya watu wengi kujua kusoma, kuandika na kuzungumza lugha ya kiswahili fasaha. Kampeni hii ilikuwa kwa nchi nzima ambapo walijifunza elimu ya Afya, Siasa, Kiswahili, Kilimo na ufundi kwa lugha ya Kiswahili na kuwafanya watu wengi kuzungumza kiswahili sanifu.
Vyombo vya habari
Tangu uhuru ulipopatikana kuna vyombo mbalimbali vya habari vilivyoanzishwa. Vyombo hivi hutumika kueneza kiswahili kwa kiasi kikubwa na hufikiwa na watu wengi licha ya kuwepo kwa changamoto za kiuchumi. Vyombo hivyo ni magazeti na majarida mbalimbali ambayo huandikwa kwa lugha ya kiswahili lakini kuna redio na runinga ambazo matangazo yake hutangazwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo kukifanya kiswahili kuenea kote ndani na nje ya nchi.
Biashara
Shughuli za kibiashara nchini husaidia kuenea na kukua kwa kiswahili kutokana na kuwepo kwa makabila tofauti tofauti ambapo wafanyabiashara huweza kuunganishwa kwa lugha ya kiswahili. Hivyo kiswahili hudumishwa na kutumika katika biashara hizo.
Shughuli za siasa na utawala
Tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru kiswahili kimetumika kama nyenzo muhimu kuwaunganisha wananchi. Shughuli za kisiasa zimetumia lugha hii katika kujiimarisha; mfano wakati wa chama kimoja, Azimio la Arusha na Mfumo wa vyama vingi Kiswahili kimetumika kama njia kuu ya mawasiliano. Pia katika utawala chama kinachotawala kimekuwa na harakati za kukiendeleza kiswahilli katika nyanja zote. Ambapo kiswahili kimekuwa kikitumika katika shughuli zote za kiutawala. Hivyo shughuli za kisiasa na kiutawala zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza, kukieneza na kukiendeleza kiswahili.
Uandishi na uchapishaji wa vitabu
Kuibuka kwa waandishi wa vitabu mbalimbali vya kiswahili vya sarufi na fasihi ambavyo vilichambua kwa kina mambo mabalimbali yahusuyo lugha ya kiswahili na utamaduni wake, mfano :- F Nkwera, Shabani Robart, Mathias Mnyapala na Shaffi Adam Shaffi. Waandishi wengine chipukizi walijitokeza na wanaendelea kujitokeza katika tasnia hii ya uandishi wa vitabu.
Shughuli za kiutamaduni
Shughuli za kiutamaduni zimechangia kueneza kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili. Shughuli hizo ni pamoja na harusi, misiba, matanga na sherehe mbalimbali za kijamii ambazo zimesaidia kukiendeleza Kiswahili kwa kuwa huwakutanisha watu tofautitofauti katika shughuli hizo, ambapo huwalazimu kutumia lugha ya kiswahili katika mawasiliano na kufanya kiswahili kuendelea. Pia katika Sherehe mbalimbali vikundi vya sanaa na muziki vinavyotumia lugha ya kiswahili kutumbuiza. Vikundi vingine huandaa nyimbo zao kwa ajili ya kukieneza Kiswahili.
Vyombo vya Ukuzaji na Uenezaji wa Lugha ya Kiswahili
Tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa kuna vyombo kadha wa kadha vilivyoanzishwa kwa ajili ya kukuza na kueneza Kiswahili baadhi ya vyombo hivyo ni hivi vifuatavyo:
BAKITA
Hii ni taasisi ya serikali iliyoundwa kwa sheria ya Bunge Na.27 ya mwaka 1967 kwa madhumuni ya kukuza Kiswahili. Kutokana na sheria hii Baraza ndilo mratibu wa kusimamia asasi zote na mawakala wote wanaokuza Kiswahili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
BAKITA imekuwa na mchango mkubwa sana katika ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili kupitia majukumu yake. Majukumu ya Baraza kama yalivyofafanuliwa katika sheria hiyo ni haya yfuatayo:
TAKILUKI
Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ilianzishwa mwaka 1979 kwa lengo la kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Zanzibar, ili kutimiza lengo hilo TAKILUKI inajishughulisha na kazi zifuatazo:
TUKI/TATAKI
Majukumu ya TUKI ni pamoja na kuunda sera muafaka za kustawisha Kiswahili na pia kufanya utafiti katika lugha ya Kiswahili.
Majukumu mengine ya TUKI ni kuhariri, kuchapisha vitabu na kutawanya vitabu na majarida ya kitaaluma katika Kiswahili.
Kwa sasa TATAKI inatoa shahada ya awali na uzamili katika lugha ya Kiswahili, kwa njia hii inawaandaa wataalamu wa lugha ya Kiswahili ambao watatumika sehemu mbalimbali za ulimwengu kufundisha lugha ya Kiswahili.
CHAUKIDU
CHAUKIDU ni kifupi cha Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani, makao makuu ya chama hiki kwa sasa yapo chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani
Madhumuni makuu ya CHAUKIDU ni: Kuwajumuisha pamoja wakuzaji wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kuchochea kasi ya malengo mahususi yafuatayo:
CHAWAKAMA
CHAWAKAMA husimama badala ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili vyuo vikuu Afrika Mashariki. Chama hiki kilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo lote la Afrika Mashariki kupitia wanafunzi wanaosoma Kiswahili vyuoni. Wanachama wa chama hiki ni wale wanosoma Kiswahili na hata wale wenye mapenzi ya lugha ya Kiswahili pia wanaweza kujiunga na chama hiki.
Chama hiki kina utaratibu wa kuandaa makongamano ambapo wanachama wake kutoka nchi zote za Afrika Mashariki hupata fursa ya kukutana mara moja kila mwaka. Pamoja na utaratibu wa chama kuandaa makongamano pia uanzishwaji wake umeambatana na malengo kadhaa ambayo ndiyo dira inayoiongoza chama kwa mujibu wa katiba, malengo hayo ni haya yafuatayo:
Pamoja na malengo hayo, lengo kuu la chama hiki ni kueneza Kiswahili lakini sasa wanakienezaje? Wanachama wa chama hiki ambao ni nchi wanachama wa jumuia ya Afrika mashariki wanakawaida ya kuandaa makongamano kwa ngazi ya kitaifa na ngazi ya kimataifa.
Kwa ngazi ya kitaifa kila nchi huandaa kongamano kila mwaka ambalo linawakutanisha wanachama wote kutoka vyuo mbalimbali katika nchi husika. Katika kongamano hilo mada mbalimbali zinazohusu lugha ya Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa lakini pia maazimio mbalimbali huchukuliwa juu ya maendeleo ya chama. Sasa katika mijadala kama hii inatoa nafasi ya Kiswahili kukua kwani makala mbalimbali huandikwa ambazo pia husomwa na watu mbalimbali. Makala hizi pia zimekuwa zikichapishwa katika majarida ya chuo husika na pia zimekua zikichapishwa mtandaoni ambapo hutoa fursa kubwa kwa watu wengi zaidi kuzifikia na kusoma, hivyo kwa njia hiyo Kiswahili kinakua kimeenea.
ZOEZI
Kiswahili kilienea kwa kasi sana katika kipindi gani?
A Kipindi cha Waarabu
B Kipindi cha Waingereza
C Wakati wa kupigania uhuru
D Baada ya uhuru
Mwaka ___ ni mwaka ambao Kiswahili kiliteuliwa kuwa Lugha ya Taifa.
A 1964
B 1960
C 1956
D 1962
Ni wakati gani ambapo Kiswahili kilitumika katika elimu?
A Wakati wa waarabu
B Wakati wa waingereza
C Kabla ya uhuru
D Baada ya uhuru
Vyombo vya ukuzaji wa Kiswahili vilivyoundwa baada ya uhuru ni pamoja na hivi vifuatavyo isipokuwa___.
A UKUTA
B TUKI
C CHAUKIDU
D BAKITA
Kuenea kwa kasi kwa lugha ya Kiswahili baada ya uhuru kulichangiwa na lugha hii kuteuliwa kuwa___
A Lugha sanifu
B Lugha ya Afrika
C Lugha ya taifa
D Lugha ya kimataifa
Dhima ya kila Asasi inayokuza Kiswahili
Mafanikio na Changamoto Zinazovikabili Vyombo vya Ukuzaji wa Kiswahili
Mafanikio
Changamoto
ZOEZI
___ ni taasisi inayohusika na kukuza Kiswahili nje na ndani ya Zanzibar.
A TAKILUKI
B TUKI
C CHAUKIDU
D TAKIKUZA
Utafiti na sera ni moja ya majukumu chini ya uanzishwaji wa___.
A TUKI
B BAKITA
C TEHAMA
D TAUSE
Baada ya uhuru kuna asasi ziliundwa kwa ajili ya kukuza na kueneza Kiswahili ambazo ni___.
A CHAUMA, TATAKI
B CHAKIMA, TUKI
C BAKITA, TUKI, TAKILUKI, CHAWAKAMA
D CHAKAM, BAKITA, TUKI
Mojawapo ya Kazi za Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Afrika Mashariki ni___.
A Kueneza Kiswahili
B Kufanya utafiti
C Kueneza Kiswahili Afrika Mashariki
D Kusanifisha Kiswahili
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahli ilibadilisha jina na sasa inaitwa___.
A TATAKI
B CHAUKIDU
C TAUKI
D BAKITA
|