MJADALA KUHUSU IDADI YA LAHAJA ZA KISWAHILI NA NAMNA ZILIVYOINUKIA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Maendeleo ya Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=11) +--- Thread: MJADALA KUHUSU IDADI YA LAHAJA ZA KISWAHILI NA NAMNA ZILIVYOINUKIA (/showthread.php?tid=1180) |
MJADALA KUHUSU IDADI YA LAHAJA ZA KISWAHILI NA NAMNA ZILIVYOINUKIA - MwlMaeda - 09-07-2021 Dhana ya lahaja
Dhana ya lahaja ni changamani, hutokana na jinsi mtu aliyefasili dhana hiyo anatumia kigezo kipi. Mfano, kuna kigezo cha isimujamii, hiki ni kigezo cha kuwashirikisha wanajamii au wazungumzaji wa lahaja hiyo na ukapata msimamo wao kuhusu lahaja hiyo. Pia kuna kigezo cha kiisimu; hiki kigezo cha kutofautisha lugha na lahaja nyingine kwa kutumia vigezo vya msamiati wa msingi, fonolojia, pamoja na mofolojia.
Lahaja pia inaweza kufasiliwa kwa kuzingatia utengano wa kijiografia au kijamii. Hii ana maana kwamba unaweza kusikia kuwa lahaja fulani inazungumzwa mahala fulani au huzungumzwa na kundi la watu fulani. Mfano, lahaja ya kitumbatu huzungumzwa sehemu za kisiwa cha Tumbatu vivyo hivyo lahaja ya kipemba huzungumzwa na watu wa Pemba.
Hebu tuangalie uchangamani wa dhana ya lahaja kwa kuangalia fasili zifuatazo:
Msanjila (2009:124) anasema lahaja ni lugha mojawapo kati ya lugha ambazo kimsingi kuhesabiwa kuwa lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani fulani kama vile lafudhi, fonolojia, msamiati usiokuwa wa msingi au muundo kutokana na eneo lugha hiyo inazungumzwa.
Massamba (2002) anasema kuwa lahaja ni lugha mbalimbali za pwani zilizokuwa na uhusianao wa karibu sana. Lugha hizo ni kama vile ci-mbalazi, ki-amu, ki-mvita, ki-jomvu, ki-mtang’ata, ki-makunduchi, ki-tumbatu, ki-mgao na ki-unguja. Wakati wengine wanaziita lahaja mfano, Polome (1967), Bryan (1959) pamoja na Temu (1980).
Kwa mujibu wa Wikipedia, Kamusi elezo huru lahaja ni vilugha vidogo vidogo vya lugha moja ambavyo hubainika kijamii au kijiografia.
Ukizitazama fasili hizi kwa makini utagundu kuwa kila mtu ana mtazano wake kuhusu lahaja, wengine wanasema ni vilugha, ni lugha inayojitegemea, wengine wanasema ni tofauti ndogondogo hasa za kimatamshi katika lugha moja. Lakini pia wengine wanaona lahaja ni tofauti za lugha kwa kigezo cha kijiografia na wengine wanaona ni tofauti za kijamii na kijiografia. Kwa hiyo mitazamo hii ndio hulete utata na uchangamani katika kufasili dhana ya lahaja.
Kimsingi fasili iliyotolewa na Msanjila (keshatajwa) inaweza kutusaidia kujua dhana ya lahaja kwani fasili hii ni ya kiutendaji.Kwa hiyo lahaja ni lugha mojawapo kati ya lugha ambazo kimsingi kuhesabiwa kuwa lugha moja isipokuwa zinatofautiana katika baadhi ya vipengele fulani fulani kama vile lafudhi, fonolojia, msamiati usiokuwa wa msingi au muundo kutokana na eneo lugha hiyo inamozungumzwa.
Mjadala kuhusu idadi ya lahaja za kiswahili na namna lahaja hizi vilivyoinukia:
Mjadala hu ulianza siku nyingi kidogo na hadi sasa hivi hakuna utafiti wa hivi karibuni unaoweza kutusaidia kuthibitisha idadi kamili za lahaji za Kiswahili. Hebu tuangalie wataalam jinsi wanavyojadili idadi ya lahaja za Kiswahili.
Chiraghdin na Mnyampala (1977) wametaja idadi ya lahaja ishirini, lahaja hizo ni kama vile; Kiunguja, Kimrima, Kimgao, Kimvita, Kihadimu, Kipemba, Kirumba, Kiamu, Kipate, Kisiu, Kitikuu, Kingazija, Kingozi, Kitumbatu, Kimtang’ata, Chichifundi, Chibalanzi, Kingwana, Kinyare, na Kijomvu.
Nurse na Spear (1985) wametaja idadi ya lahaja kumi na sita (16), na wamezigawa katika makundi mawili ambayo ni kundi la kaskazini na kundi la kusini. Mfano kundi la kaskazini lina lahaja saba (7) wakati kundi la kusini lina lahaja tisa (9). Baadhi ya lahaja hizo ni;- Kipate, Chimiini, Kibajuni, Kisiu, Kijomvu, Chifunzi, Kipate, Kiunguja, Kimtang’ata, Kimakunduchi na kuendelea.
Utata kuhusu idadi za lahaja za kiswahili unatokana na sababu zifuatazo;
Kigezo kilichotumika katika kufanya utafiti wa lahaja za kiswahili. Unaweza kufanya utafiti wa lahaja za kiswahili kwa kutumia kigezo cha kijiografia, kijamii, pamoja na kiisimu. Vigezo hivyo vyote vinaweza kukupatia idadi tofauti za lahaja mfano, Massamba katika utafiti wake kwa kutumia kigezo cha kiisimu (1977) alifanya utafiti katika jamii za chi-ruri, chi-jita, na ki-kwaya akathibitisha kuwa hizi ni lahaja za lugha moja na si tofauti, pia kwa kutumia kigezo cha utengano wa kijiografia na kijamii mfano katika lugha ya Kiswahili kwa kiasi kikubwa uanishaji umefanywa kwa utengano wa kijiografia kama vile, kipate kinazungumzwa sehemu za Pate na lahaja ya kipemba huzungumzwa Pemba. Hivyo kutokana na sababu kama hizi husababisha watafiti wengi kutofautiana katika kupata idadi kamili za lahaja.
Kutokana na kukurubiana na kusigana kwa namna fulani kwa lahaja za Kiswahili, kukurubiana huko kwa lugha na mipaka ndiko kunakofanya wazungumzaji wake wajihisi wanazungumza lugha moja. Pia kusigana kwake kwa lahaja hizi husababisha hawa watu wajihisi wanazungumza lugha tofauti. Mfano, lakabu ya lugha ya Kiswahili tunaweza kuifananisha na lugha ya kichaga. Wachaga na lugha zao zote kuhesabiwa kuwa kichaga lakini lugha hizo pia zinatofautiana mfano, ki-machone, kinatofautiana na ki-rombo, ki-marangu, ki-kibosho na kusababisha wasemaji wa lugha hii ya kichagga kushindwa kuelewana kabisa ( Massamba 2002: 258) na hata Wazaramo,Wakwele,Waruguru hujihisi wanazungumza lugha zenye nasaba moja.
Kutokana na kutofautiana kwa majina ya lahaja kuna baadhi ya majina ya lahaja moja hutajwa tofautitofauti na wataalamu mbalimbali, mfano Chiraghdin na Mnyampala (1977) wanataja jina la lahaja ya kihadimu wakati Temu (1980), anasema lahaja ya kihadimu aliita kimakunduchi. Vivyo hivyo Nurse na Spear (1985) wanasema lahaja hiyo ni Kimakunduchi. Hivyo inaleta utata katika kujua kwamba hii ni lahaja moja au ni lahaja mbili tofauti. Pia Bryan (1959) anaitaja lahaja ya Kimbalazi na Polome (1967) ameiita kibrava, Whiteley (1969) ameiita Chimiini, Chiraghin na Mnyampala wanaiita Chibalazi.
Pia kutokana na maendeleo ya Kiswahili sanifu, mfano mpaka sasa kunabaadhi ya lahaja zimebakia kimaandishi lakini kiuhalisia hazipo na hazitumiki katika lugha ya Kiswahili, mfano, lahaja ya Kimgao iliyokuwa inapatikana sehemu za Kilwa imo kwenye maandishi ya wataalamu kama vile Chiraghdin na Mnyampala (1977), Nurse na Spear (1985), Temu (1980). Lakini watumiaji wake hivi sasa wanatumia Kiswahili sanifu, kwa hiyo inaleta utata katika kupata idadi kamili ya lahaja za Kiswahili.
Pia kuna baadhi ya lahaja zipo na zinatumika lakini baadhi ya wanazuoni hawajaziweka katika maandishi. Mfano, kiunguja kinachopatikana Unguja kipo lakini cha kushangaza baadhi ya wanazuoni kama vile Whiteley (1969), Temu (1980) pamoja na Nurse na Spear (1985) hawajaziweka katika maandishi.
Kwa ujumla hakuna idadi kamili ya lahaja. Unaweza kupata idadi ya lahaja kwa kuzingatia mtaalamu na kigezo alichotumia, suala la muda, na mahali unapoenda kufanyia utafiti wa hizo lahaja.
Kuinukia kwa lahaja
Kuna wataalam mbali mbali wanaeleza namna ambavyo lahaja mbalimbali za lugha ya Kiswahili zilivyoinukia. Wataalamu hawa wamegawanywa katika makundi mawili:
Kundi la kwanza; hili ni lile kundi la wanaoamini kuwa lahaja za lugha ya Kiswahili kwa ujumla zilianza sehemu fulani maalum.
Kundi la pili; Wanaoamini kuwa lahaja zilianzia sehemu mbalimbali kwa wakati mmoja japo kwa kiwango tofauti.
Wafuasi wanaoamini kuwa lahaja kwa ujumla zilianza sehemu fulani maalumu au sehemu moja wanajikita katika hoja ya msingi kuwa lugha huanzia sehemu moja maalum na kusambaa sehemu nyingine na hii hutokana na kadri matumizi yanavyoongezeka na idadi ya watu inavyoongezeka ndivyo watu hawa hutawanyika kwenda sehemu tofautitofauti na kusababisha kutokea kwa lahaja tofautitofauti za kiswahili.
Kwa mujibu wa Nurse na Spear (1985) lugha huanzia mahali fulani pamoja katika kipindi fulani kadri wasemaji wanavyoongezeka na lugha huanza kubadilika na kuwa ya ana kwa ana. Hivyo kutokana na sababu ya kutawanyika kunapelekea kutokea kwa lahaja tofautitofauti. Mfano; hawa wanazuoni wanadai kuwa lahaja za kiswahili zilianzia kaskazini mwa Mombasa katika eneo la Lamu na kuendelea sehemu nyingine ya pwani ya Afrika Mashariki na hii ni kutokana na kwamba utafiti wa akiolojia unaonesha kuwa mbantu wa kwanza kabisa aliishi katika mji wa Lamu. Udhaifu wa mtazamo huu ni kwamba kama watu hao wametokea katika jamii moja yenye lugha moja, hivyo ni vipi wanaweza kutambulishwa kutumia lahaja zao yaani lahaja za kaskazini na lahaja za kusini.
Pia suala la muingiliano wa lugha kutokana na mabadiliko na maendeleo katika jamii halina nafasi katika maendeleo ya lugha. Kutokana na udhaifu huu kukapelea kutokea kwa kundi jingine.
Kundi la wale wanaoamini kuwa lahaja zilianzia sehemu mbalimbali kwa wakati mmoja ila kwa kiwango tofauti. Ugunduzi wa kiakiolojia wa hivi karibuni unaonesha maeneo mengine kama vile Unguja, Pemba na Kilwa. Mfano, Mji wa Kilwa kuwa maarufu kuliko mji wa Lamu. Ugunduzi huu unaonesha kuwa mbantu wa mwanzo aliishi Kilwa na sio Lamu kama inavyoelezwa na Nurse na Spear (1985). Kwa hiyo maelezo hayo yanatuonesha kuwa mji wa Kilwa ulikuwa maarufu zaidi kuliko Lamu.
Ni kutokana na ukinzani wa mji wa Kilwa na Lamu kiumaarufu ndipo wataalum wengine wakasema kuwa lahaja za Kiswahili ziliinukia sehemu mbalimbali kwa kipindi kimoja japo kwa kiwango tofauti.
Grenville (1959) katika makala yake ya “Medieval Evidence for Swahili” anasema wazo la kuinukia mapema kwa Kiswahili katika Kilwa na hakubaliani na fikra za kuwa lugha ilianzia Lamu kwani hata kumbukumbu za kihistoria kipindi cha kati zinadai kuwa mji wa Kilwa ulikua maarufu kuliko Lamu, hii ni kutokana na shughuli za kiuchumi zilizokuwa zinaendelea.
Pia Massamba (2007) anasema, hizi zinazoitwa lahaja za Kiswahili za sasa ziliinukia sawia sawia katika maeneo mbalimbali na kwa sababu ya kuingiliana kibiashara, kiuchumi na kijamii na huu ndio ukawa ndiyo mwanzo ya lahaja ya Kiswahili sanifu. Kwa mtazamo wake, Massamba anadai kuwa, lahaja za Kiswahili tunazozifahamu hivi sasa kama vile; kimakunduchi, kipate, kiamu, kimvita pamoja na kiunguja hapo zamani ziliitwa lugha zinazojitegemea. Lugha hizi ziliathiriana kutokana na ukaribu wake na zaidi kwa sababu zilitokana na mame bantu moja. Hivyo ukizichunguza kwa umakini utagundua kuwa zilizokaribu zinafanana sana kuliko zilizo mbali. Pia lugha zilizo malikuu moja hufanana lakini lugha zilizokaribu hufanana zaidi.
Hitimisho
Kwa ujumla lahaja za lugha ya kiswahili zilianzia sehemu tofauti tofauti na zikaendelea kukua sambamba na hii ni kutokana na muingiliano wa masuala ya kiuchumi, kijamii pamoja na kibiashara ndiko kulikopelekea kufanana kwa hizi lahaja za kiswahili. Ni dhahiri muingiliano wa watu katika jamii ni suala lisiloepukika kutokana na mabadiliko na maendeleo ya maisha.
MAREJEO
Chiraghdin, na M. Mnyampala (1977) Historia ya Kiswahili.Nairobi:Oxford University Press.
Massamba,D. P.B (2002). Historia ya Kiswahili: 50 BK hadi 1500 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta
Foundation.
Msanjira, Y.P na wenzake (2009). Isimu Jamii: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili.
Nurse, D na T. Spear (1985). The Swahili. Reconstructing the History and Language of an
African Society. Philadelphia: University of Pennsylvania.
www.s.w.wikipedia.org/wiki/lahaja[url=http://www.s.w.wikipedia.org/wiki/lahaja][/url]
|