KISWAHILI NA UTANGAMANO WA AFRIKA MASHARIKI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Maendeleo ya Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=11) +--- Thread: KISWAHILI NA UTANGAMANO WA AFRIKA MASHARIKI (/showthread.php?tid=1179) |
KISWAHILI NA UTANGAMANO WA AFRIKA MASHARIKI - MwlMaeda - 09-07-2021 Dhima ya Kiswahili Afrika Mashariki katika Ujenzi wa Utangamano
Makala hii imejikita katika kuangalia nafasi ya kiswahili katika ujenzi wa utangamano wa nchi za Afrika Mashariki. Marejeleo ya makala haya ni mapitio ya kimaktaba ambayo yametokana na makala, tasnifu, kamusi elezi-huru na vitabu. Lugha ya kiswahili katika utendaji wa dhima ya kimawasiliano katika Afika Mashariki, imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kuwaunganisha wanajamii. Lugha hii ya Kiswahili ni lugha yenye wazungumzaji wengi katika bara la Afika na imekuwa ikitumika katika shughuli mbalimbali za kijamii kama vile dini, harusi, sherehe na hata misiba. Hali kadhalika katika shughuli za kiuchumi kama biashara na masuala ya kidiplomasia. Pia shughuli za kidini kama vile nyimbo za kanisani kwa wakristo na Kaswida kwa Waislamu. Vilevile shughuli za kielimu, siasa na kiutamaduni kama jando, unyago na maombolezo.
Shughuli hizi ziliwaunganisha wanajamii katika mwingiliano wao wa majukumu ya kila siku. Kulikuwepo na taratibu mbalimbali zilizolinda mienendo na tabia za wanajamii hao. Taratibu hizo zimekuwa zikifuatwa na watu wote kwa kuwa waliziridhia. Jamii za Afrika Mashariki zilipoongezeka wazungumzaji wa Kiswahili waliongezeka pia na kuifanya lugha kusambaa. Katika Afrika, licha ya kuwepo kwa lahaja tofauti za Kiswahili lakini haikuwa kikwazo katika masikilizano na maelewano. Na ndio maana watu waliweza kuhusiana katika shughuli mbalimbali na kujenga utangamano baina yao.
Shughuli mbalimbali za kijamii, uchumi, biashara, elimu na nyinginezo zimeifanya jamii ya Afrika Mashariki kuwa na maridhiano na utangamano kwa sababu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Pamoja na Kiswahili kuenea miongoni mwa jamii za Afrika Mashariki; ubinafsi, chuki, upendeleo katika baadhi ya mambo vimekuwa changamoto katika mahusiano ya mataifa ya Afrika Mashariki. Hata hivyo upendeleo, ubabe, ubaguzi na ukabila hautegemewi kuwa mfumo wa kudumu.
Katika katiba ya jumuia ya Afrika Mashariki Ibara ya 119 inayohusu utamaduni na michezo, nchi wanachama zimehimizwa kukuza ushirikiano na kuimarisha utamaduni na michezo ikiwemo lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha ya mawasiliano baina ya watu. (Ripoti ya tume ya Blair kuhusu Afrika (Rasimu ya tafsiri) 2005
Maitaria & Monyanyi 2005 katika makala yao wanasema ‘hata hivyo, ni jambo mustahili kujaribu kujenga amani hiyo chini ya vivuli vya ukabila, ubahili na ufisadi. Mfano, katiba ya nchi ya Kenya, utangamano pia huhusisha kukuza na kulinda haki za binadamu kama zinavyofafanuliwa ili kuhakikisha uwiano mzuri miongoni mwa jamii mbalimbali.’
Aidha wasanii mbalimbali katika Afrika Mashariki wamekuwa wakitumia fasihi kueleza njia za ujenzi wa utangamano katika kazi zao za kisanii. Baadhi wamekuwa wakiandika mada mbalimbali ambazo zimeshughulikiwa na zilizokuwa zikihusiana na ujenzi wa jamii ya mshikamano. Mfano wa kazi zilizoandikwa ni pamoja na uzindushi wa jamii, umoja katika jamii, masuala ya kisiasa, nafasi ya mwanamke katika jamii, umuhimu wa subira na matumizi ya kauli zinazofaa. Jamii haiwezi kuwa na utangamano unaofaa iwapo kuna mazonge na figisufigisu zinazopingana na amani na upendo miongoni mwa wanajamii.
Lugha ya Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na waafrika walio wengi katika nchi za Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda Zambia, Sudani kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo. Kutokana na idadi kubwa ya wazungumzaji wa Kiswahili mataifa ya ulaya huona sababu ya kuwafundisha watu wao Kiswahili ili waweze kuwekeza na kufanya tafiti katika nchi zinazozungumza lugha hii. Katika utafiti wake Ababaker, (2003) anaeleza kuwa mmoja wa wasailiwa wake walikiri kuwa lugha ya kiswahili inapendwa na wageni na ni rahisi kueleweka pindi wanapoamua kujifunza. (Ababaker E.A. 2003). Suala hili linaonesha dhima ya lugha katika hitaji la kukidhi mawasiliano.
Hata hivyo, ni jambo mustahili kujaribu kujenga amani hiyo chini ya vivuli vya ukabila, ubahili na ufisadi. Utangamano pia huhusisha kukuza na kulinda haki za binadamu kama zinavyofafanuliwa katika katiba za baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ili kuhakikisha kunakuwepo na uwiano na maelewano mazuri miongoni mwa jamii mbalimbali.
Maitaria na Momanyi (2012) wanaeleza kuwa katika, kuhakikisha usalama wa mtu binafsi popote pale anapoishi na usalama wa umma kwa ujumla ni nguzo muhimu katika kujenga utangamano miongoni mwa watu wa asili mbalimbali. Utangamano mzuri pia ni ule unaotokana na uimarishaji wa uhuru wa kijamii na kisiasa utakaochangia kuwepo kwa jamii tulivu inayojiamini.
Attafuah (2012:89) kama alivyonukuliwa na Maitaria na Momanyi (2012) utangamano wa kitaifa unahusu uhusiano mzuri wa kijamii uliojengwa juu ya mhimili mkuu wa amani. Nakubaliana na hoja hii kwa vile ithibati ya kuwepo kwa utangamano mzuri miongoni mwa jamii za Afrika Mashariki ni amani. Uwepo wa amani utaleta ushirikiano na mahusiano yenye tija.
Athari zinazoweza kuharibu utangamano mzuri
Wakati mwingine mapingamizi ya utangamano mzuri na wenye manufaa huathiriwa na Utashi wa kisiasa. Kwa mujibu wa Post na wenzake (2008) utashi wa kisiasa ni uungwaji mkono na viongozi wa kisiasa ambao husababisha mabadiliko ya kisera.
Charney (2009) naye anaelezea kuwa vikundi vinavyoongoza vyama vya siasa au serikali huweza kuwa na nguvu isiyoonekana nguvu hii ndiyo tunayosema ni utashi wa kisiasa amabayo husukuma na kusababisha maamuzi ya kisiasa. Maamuzi yanaweza kuwa na nguvu na kusababisha kutokuwepo kwa utangamano mzuri baina ya jamii za Afrika Mashariki.
MAREJELEO
Ripoti ya tume ya Blair kuhusu afrika (Rasimu ya tafsiri) 2005
https://repositories.lib.utexas.edu/bitstream/handle/2152/5029/2389. pdf Dar es Salaam 2002 © Friedrich Ebert Stiftung East African Community 2002 ISBN 9987 22 036 3
Emad Ahmed Ababaker(2003) Chimbuko na Maendeleo ya Kiswahili na athari zake kwa jamii ya kiarabu: mtazamo wa vilughawiya jamii
Maitaria& Monyanyi 2005
Charney (2009)
|