UTETEZI WA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA ENZI ZA UTANDAWAZI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Maendeleo ya Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=11) +--- Thread: UTETEZI WA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA ENZI ZA UTANDAWAZI (/showthread.php?tid=1154) |
UTETEZI WA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA ENZI ZA UTANDAWAZI - MwlMaeda - 09-06-2021 UTETEZI WA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA ENZI ZA UTANDAWAZI NCHINI KENYA
YAMKINI changamoto kubwa kuliko zote kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili ni kuiendeleza lugha hiyo wakati wakiingiza maneno na miundo ya lugha za kigeni zilizo mbali kabisa na utamaduni wa Mswahili.
Je, Kiswahili kinakumbwa na mabadiliko gani kwa sasa? Na je, kukuwa na kubadilika kwa Kiswahili kunamaanisha kuiondoa lugha hiyo kwenye asili yake? Mabadiliko ya Kiswahili yako kwa namna mbili. Ya kwanza ni kutokana na matumizi ya lugha katika mazingira yake yenyewe.
Ya pili ni yale yanayoletwa kutoka nje. Mabadiliko ya kindani yanatokana na maneno kubadilika maana kwa kutegemea jinsi ya kutumiwa kwayo. Mabadiliko ya nje hutokana na teknolojia mpya, mitindo mpya, michezo, athari za utangamano wa tamaduni na itikadi za jamii mbalimbali.
Watu wanahoji kwamba kukua na kubadilika kwa Kiswahili kuna maana mbaya ambayo ni kukiua Kiswahili kutoka katika uasili wake. Kwamba kila Kiswahili kinapoongeza msamiati au miundo mipya ya sentensi, ndivyo kinavyozidi kuhama kutoka kwa uasili wake na kwenda sehemu nyingine.
Pamoja na baadhi ya watu kuibeza lugha ya Kiswahili, harakati za wadau kuikuza lugha hiyo kitaifa na kimataifa zimepamba moto.
Asasi mbali nchini, ikiwemo Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) zimeongeza idadi ya watetezi wa Kiswahili wanaoamini lugha hiyo inakidhi mahitaji ya kitaaluma na kimawasiliano ndani na nje ya Kenya. Chama hicho kinalenga kutoa fursa ya kumulika na kutafakari mabadiliko na maendeleo ya Kiswahili katika ulimwengu wa utandawazi ili kuleta uhuru na maendeleo ya kweli. Wasomi wa lugha wanaeleza kuwa lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa rasilmali wanazoweza kutumia Wakenya ili kufikia maendeleo ya kweli.
Hata hivyo, mfumo mpya wa kimaisha ujulikanao kwa jina la utandawazi umekuja na upepo mkali ambao kama juhudi za makusudi hazitochukuliwa, upo uwezekano wa Kiswahili kuzolewa na kutupwa baharini na chamchela hiyo. Ili kukumbatia lugha na utamaduni wetu, yatupasa kujenga ukuta imara ambao hautatikisika kwa kimbunga cha utandawazi.
Kupigiwa chapuo
Kudharauliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo kwa lugha nyinginezo za kigeni kwamba ndizo pekee zinazofaa kutumiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa zina hadhi ni changamoto kubwa.
Kuna kasumba mbaya na mtazamo hasi kuhusu Kiswahili ambao unawafanya Wakenya kukitukuza na kushabikia zaidi Kiingereza kwa kutojua kuwa Kiingereza ni sawa na lugha nyinginezo tu kihadhi.
Huku tukichunguza nafasi ya Kiswahili katika mfumo wa elimu nchini Kenya, ni vyema tukumbuke kuwa, mfumo wa elimu wa nchi yoyote inayotegemea lugha ya kigeni hasa lugha ya waliokuwa watawala wao wa kikoloni huendeleza maadili ya kigeni na utegemezi mkubwa (Mbaabu 1996).
Ingawa kwa sababu ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, lugha huathiriana duniani kote, lugha za kigeni katika mfumo wa elimu hunuia kuendeleza mila na desturi za kigeni ambazo nyingi yazo haziambatani wala kulingana na matarajio na mahitaji ya kimaendeleo ya nchi kama ya Kenya.
Kwa hivyo, ni muhimu kwa wataalamu, watafiti na wasomi wa Kiswahili kujaribu kuipa nafasi inayostahiki lugha hii katika mfumo wetu wa elimu ili kuustawisha mustakabali wake.
Ni ukweli kuwa lugha hiyo kwa sasa ina sifa ya kutumika kitaaluma shuleni na hata vyuoni. Kuna kasumba imejengeka kuwa hatuwezi kwenda mbele bila Kiingereza au huwezi kuwa umesoma bila kujua Kiingereza.
Kiwanda cha ajira
Kuna nchi kama vile Japan ambayo imeendelea kwa kutumia lugha ya kiasili. Wapo wanaosema Kiswahili hakijitoshelezi kimsamiati. Inastahili tuwatumie wanafunzi katika madaraja mbalimbali kama sekondari na vyuo vikuu kuthibitisha namna wanavyoweza kuitumia lugha hii kama kiwanda kikuu cha maarifa na ajira.
Yafaa tujue thamani ya Kiswahili, tujivunie nayo badala ya kushabikia lugha za kigeni hususan Kiingereza ambayo kwa hali ilivyo imeshawafanya Wakenya wengi kuwa watumwa wa utamaduni wake.
Ukweli wa mambo kwa sasa ni kuwa Kiswahili kinachobezwa na baadhi ya watu wenye mitazamo na kasumba za kikoloni tayari kimeshavuka mipaka ya kitaifa.
Ni lugha inayoshuhudia mageuzi na kupiga hatua kubwa katika nchi kadhaa duniani. Watu wengi wanajifunza Kiswahili na vyuo vingi vikiifundisha lugha hiyo; kujivunia lugha yetu na utamaduni wake, tuipe nafasi na dhima maalum katika nyanja zote za elimu, siasa, uchumi na utamaduni.
Ipo haja ya kushirikisha vyombo mwafaka na wadau mbalimbali wa lugha, ikiwemo wasomi, katika kutangaza, kueneza, kuendeleza na kuinua lugha ya Kiswahili na utamaduni wake ndani ya zama hizi za mfumo wa utandawazi uliotamalaki duniani. Katika wiki ya sauti ya Kiswahili kutafanyika makongamano, mashindano ya uandishi wa kazi za kubuni kwa shule za sekondari, vyuo vikuu na watunzi wasio wanafunzi.
|