HISTORIA YA MJI WA MOMBASA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Maendeleo ya Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=11) +--- Thread: HISTORIA YA MJI WA MOMBASA (/showthread.php?tid=1123) |
HISTORIA YA MJI WA MOMBASA - MwlMaeda - 09-03-2021 Kutokana na mji wa Mombasa kuwa sehemu muhimu kimkakati, makundi ya wafanyabiashara wengi walitaka kulazimisha utawala wao na mji huo uligombewa na mataifa mbalimbali katika historia yake. Ushawishi wa Waarabu ulikua kwa kiasi kikubwa, na maarufu katika nyakati mbalimbali katika historia ya mji wa Mombasa.
Wafanyabiashara wa Kiarabu walijulikana kwa kusafiri kwa meli hadi Pwani ya Kenya tangu karne ya kwanza na kuendelea, na hii iliimarisha biashara katika Pwani ya Kenya. Mwanahistoria ambaye pia ni Meneja Mkuu wa Makumbusho ya Fort Jesus mjini Mombasa Bw. Mbarak Abdulqadir anasema vita vya ukombozi wa Kenya mkoani Pwani vilianza miaka mingi tangu wakati wa utawala wa Kireno. Anasema “Ukombozi wa Kenya hapa Pwani ulianza miaka mingi kutoka wakati wa utawala wa Kireno lakini kwa bahati mbaya vitabu vya historia havizungumzii kabisa. Vita vya ukombozi vilianza hata kabla ya Waingereza kuja, vilianza wakati Wareno walipokuja katika mwambao wa Afrika Mashariki, hasa hapa Mombasa”
Mnamo mwaka 1498, mvumbuzi wa Kireno anayeitwa Vasco Da Gama aliwasili katika fuo za Mombasa. Lengo la safari yake ilikuwa kueneza imani ya dini ya Kikristo na pia kupanua zaidi eneo la biashara la Ureno. Ujio wake mjini haukupokelewa vyema, ulikumbwa na uadui miongoni mwa wakazi wa asili.
Mbarak anasema watu wa asili wa Afrika Mashariki walianza vita vya ukombozi tangu nyakati hizo kwani walikuwa hawako tayari na utawala wa Kireno. “Kwa miaka 200 Wareno walipokuwa wametawala sehemu za Afrika Mashariki kulikuwa hakuna amani, kulikuwa ni vita katika miji tofauti. Kwa mfano mji wa Mombasa ulichomwa karibu mara tano, Lamu ilichomwa mara kadhaa, pia Pate na sehemu nyingine. Sababu ni kuwa hawakuwa tayari kusalimu amri dhidi ya utwala wa Kireno”
Hata hivyo Wareno walifanya urafiki wa karibu na Mfalme wa Malindi. Wareno walitambua kuwa mji wa Mombasa ulikuwa muhimu kwa wao kuweza kuuza bidhaa zao, kwa hivyo mwaka 1592 walitumia nguvu na uwezo wao na kumfanya Mfalme wa Malindi kuwa Sultan wa mji wa Mombasa.
Hatimaye mji wa Mombasa ukawa kituo kikuu cha biashara cha Ureno katika mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki. Hii ilifanya Ngome Kuu maarufu kwa jina la Fort Jesus ambayo iko hadi leo, ijengwe. Ngome hii ilitumiwa kama kituo cha kufanyia biashara, gereza la watumwa, na muhimu zaidi kama sehemu ya kuwalinda Wareno kutokana na uvamizi kutoka kwa wakazi wenyeji na makundi ya kigeni. Utumwa ndio biashara kubwa iliyokuwa ikifanywa wakati huo ambapo watumwa wenyeji walibadilishwa kwa bidhaa mbalimbali. Watumwa waliokamatwa walilazimishwa kufanya kazi katika mashamba ya karafuu na pamba katika hali ngumu na mijeledi kwa juu. Utawala wa Ureno mjini Mombasa uliendelea kwa takriban miaka 200, ambapo baadaye ulipinduliwa na Waarabu wa Omani, kama anavyoeleza mwanahistoria Stambuli Abdillahi Nassir.
“Mwaka 1660 wenyeji waliungana-waswahili na wamijikenda, wakaenda mpaka Oman kuomba msaada ili waje wasaidiwe kumuondoa Mreno. Kitabu cha The Portuguese period in East Africa kilichoandikwa na Justus Strandes kinaeleza miaka 200 hiyo ilikuwa ya unyama kiasi gani na dhidi ya nani. Mreno alimuua mpwani kwa miaka 200 mfululizo.”
Hatimaye Waarabu nao pia walilazimishwa kuuachia mji wa Mombasa kwa wakoloni wa mwisho waliouteka-Waingereza. Waingereza walichukua udhibiti wa mji wa Mombasa mnamo mwaka 1895, baada ya Sultan wa Zanzibar kuukodisha mji huo kwa Waingereza. Mkoloni alianzisha utawala wa ardhi na rasilimali za Kenya. Bado wapwani hawakuridhia bali waliendeleza vita vya kujikomboa kutoka kwa minyororo ya mkoloni vilivyoongozwa na shujaa mwanamke kwa jina la Mekatilili wa Menza. Mbarakak Abdulqadir anasema, “Mkombozi wa kike wa kigiriama kwa jina la Mekatilili wa Menza alianzisha vita vya kutaka kukomboa sehemu za wagiriama dhidi ya minyororo ya kikoloni ya uingereza”.
Mwingereza alipiga hatua na kuanzisha udhibiti wa bandari muhimu ya Mombasa na kumaliza ujenzi wa reli kutoka Mombasa hadi Uganda katika miaka ya 1900. Utawala wa Uingereza Kenya na pia Mombasa uliisha rasmi baada ya Kenya kupata uhuru tarehe 12 Desemba 1963.Rais wa kwanza wa Kenya alikuwa Jomo Kenyatta ambaye alikuwa kiungo muhimu katika vita vya kupigania uhuru kutoka kwa waingereza.
Hata hivyo wanahistoria wa Pwani ya Kenya wanasema kuwa baadhi ya wapwani wanaona kama wametengwa katika sherehe za madaraka kwa muda mrefu na ni vyema iwapo watakumbukwa kwa mchango wao na kuhusishwa kwa njia zote. Japokuwa Kenya ilipata misukosuko ya hapa na pale ya kisiasa baada ya kupata uhuru, hatimaye hivi sasa mambo ni shwari na wakenya wanatarajia maisha mazuri. Kenya inaendelea kuwa kitovu muhimu cha kiuchumi katika kanda miaka 50 baada ya kupata uhuru.
|