MAKUWADI WA SOKO HURIA (CHACHAGE S. CHACHAGE) KATIKA MUKTADHA WA RIWAYA YA KIHISTORIA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi andishi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=7) +---- Forum: Riwaya (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=52) +---- Thread: MAKUWADI WA SOKO HURIA (CHACHAGE S. CHACHAGE) KATIKA MUKTADHA WA RIWAYA YA KIHISTORIA (/showthread.php?tid=1030) |
MAKUWADI WA SOKO HURIA (CHACHAGE S. CHACHAGE) KATIKA MUKTADHA WA RIWAYA YA KIHISTORIA - MwlMaeda - 08-27-2021 MAKUWADI WA SOKO HURIA (CHACHAGE S. CHACHAGE) KATIKA MUKTADHA WA RIWAYA YA KIHISTORIA KATIKA FASIHI YA KISWAHILI Makuwadi wa Soko Huria (Chachage S. Chachage) katika Muktadha wa Riwaya ya Kihistoria katika Fasihi ya Kiswahili Mugyabuso M. Mulokozi
Ikisiri
Miongoni mwa kazi bora za fasihi duniani ni zile zilizojikita katika matukio na/au mashujaa halisi wa kihistoria. Mifano mizuri ni tendi za Homer za Kiyunani, baadhi ya tamthilia za W. Shakespeare (k.m. Julius Kaisari), na riwaya mashuhuri za Kirusi za Pushkin na Leo Tolstoi. Katika fasihi ya Kiswahili, riwaya ya kihistoria haijaendelezwa sana. Miongoni mwa kazi zilizoinua kiwango cha riwaya ya kihistoria katika Kiswahili ni Makuwadi wa Soko Huria. Makala haya yataichambua riwaya hiyo katika muktadha wa riwaya ya kihistoria katika Kiswahili ili kuona mchango wa riwaya hiyo, na wa Chachage mwenyewe, katika kuuendeleza na kuukomaza mkondo huo wa uandishi wa kubuni.
_______________________________________
“Mtu huandika kitabu kimoja tu katika maisha yake.” Chachage S.Chachage
_______________________________________
“…katika kuandika historia isiyokuza ushujaa wa mtu au watu binafsi, Chachage amemkaribia mwandishi mashuhuri wa kimapinduzi, Maxim Gorky. Kwangu mimi, hili tu linatosha kumweka Chachage katika orodha ya wasanii stadi wa Tanzania, na wa Bara la Afrika” (Issa Shivji ,2002).
_________________________________________
1.0 Utangulizi Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria iliandikwa mwaka 1999-2000, na kuchapishwa mwaka 2002 na kampuni ya E & D. Katika mahojiano aliyoyafanya na Diegner (2004: 228), mwandishi anasema alitumia miaka mitatu (1996-1999) kufanya utafiti wa masuala yaliyomo katika riwaya hiyo. Muda huo mrefu wa utafiti ni ushahidi kuwa C.S. Chachage alikusudia kuandika kazi changamani na yenye mawanda mapana na kina cha kutosha. Makuwadi wa Soko Huria inazo sifa hizo na zaidi. Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria (baadaye Makuwadi) ilihakikiwa kwanza na Shivji (2000/2002) na baadaye Mbonde (2004). Tutazipitia kidogo tahakiki zao kabla hatujajikita katika uchambuzi wetu wa riwaya hiyo katika muktadha wa bunilizi za kihistoria katika Kiswahili.
Makala ya Shivji ni mapitio na utambulisho wa riwaya hiyo na inafanya mambo kadha muhimu: Inatupa mtazamo na mwelekeo wa kitabaka wa kisiasa-kiitikadi wa kuitazama riwaya hiyo, na hivyo kuonesha dhima na mchango wake katika kufafanua na kuendeleza harakati za wanyonge wa Tanzania na Afrika za kupambana na mifumo inayowakandamiza. Pili, tahakiki hiyo inabainisha vizuri mtanziko wa kimawazo na kivitendo wa tabaka la vibwanyenye wa Tanzania linalowakilishwa na wahusika Mjuba na Sifuni. Hili ni tabaka linaloyumba kati ya kukubali kuukumbatia ubepari na raha zake, au kujiunga upande wa mapambano na mawanio ya umma na karaha zake. Mtanziko huu, aliouelezea vizuri Amilcar Cabral mwaka 1966, bado haujasuluhika. Mchango muhimu wa makala ya Shivji ni kutupatia kiunzi cha kinadharia na kiitikadi cha kuitazama riwaya hiyo ya Chachage, maana haingii sana katika uchambuzi wa riwaya yenyewe.
Mbonde anafanya uchambuzi wa
kijadi wa riwaya ya Makuwadi kwa kuzingatia vipengele vya dhamira, muundo na mtindo. Anabainisha dhamira muhimu zinazojitokeza katika riwaya hiyo. Kwa upande wa muundo na mtindo, Mbonde anaonesha kuwa Chachage anatumia kwa ufanisi mbinu-rejeshi; anachanganya usimulizi na uandishi ili kuileta hadhira karibu na msimuliaji. Aidha, anatumia lugha fasaha iliyosheheni tamathali, na anaonesha migogoro (labda hiki ni kipengele cha maudhui kuliko mtindo). Mbonde anadhihirisha kuwa riwaya hiyo inatumia historia kuakisi mapambano ya leo, na kwamba inashabihiana na ile ya Alex Haley ya Roots (siyo The Roots) katika kupekua nasaba na mahusiano ya kiukoo ya makabila mbalimbali ya kusini mwa Tanzania (suala la Roots kuwa riwaya nalo lina mjadala; wengine huweza kudhani kuwa ni historia). Kwa hakika wahakiki hawa wawili
wametupatia mahali pazuri pa kuanzia katika kuiangalia riwaya ya Makuwadi. Makala haya hayakusudiwi kurudia yale waliyokwishasema vizuri zaidi, bali tutajikita katika suala la Makuwadi wa Soko Huria kama bunilizi ya kihistoria, jambo ambalo Shivji na Mbonde hawakulizungumzia sana kwa kuwa halikuwa lengo lao. Chachage mwenyewe, katika mahojiano na Diegner (tumekwishayataja hapo juu), analipa suala la historia uzito mkubwa kuhusiana na riwaya yake. Lengo letu si kujadili sifa za riwaya ya kihistoria kidhahania, bali kuonesha nafasi na umuhimu wa riwaya ya kihistoria katika kuibua riwaya bora ya Kiswahili ya kimaendeleo, tukitumia Makuwadi kama kielezo chetu. 2.0
Riwaya ya Kihistoria katika Fasihi ya Kiswahili Riwaya ya kihistoria ni hadithi
ndefu ya kubuni iliyojikita katika matukio ya kweli ya historia, hasa yaliyo muhimu kwa taifa au jamii inayohusika, kuyachanganya na matukio ya kubuni, na kuyapangilia upya kisanii ili kutoa ujumbe fulani kwa jamii inayoandikiwa. Riwaya ya kihistoria huwa ni jaribio la kuoanisha mgogoro wa kihistoria na mgogoro wa kisanaa (k.m. wa kibinafsi), ukweli wa kihistoria na ukweli wa kisanaa, na viumbe wa historia na viumbe wa sanaa, ili kujenga simulizi yenye maana, ujumbe maridhawa na kumbukumbu ya kudumu kwa walengwa (Lukacs, 1962; Mulokozi, 1990). Masimulizi ya kihistoria si jambo
geni katika utamaduni wa Waswahili na Waafrika kwa jumla. Kila jamii huwasimulia watoto wao juu ya matukio ya zamani yanayowahusu, hususani yale yanayohusu chimbuko lao, namna walivyofika mahali walipo sasa, harakati walizozipitia, mahusiano yao na majirani zao, na mapambano yao na maadui zao. Masimulizi hayo huweza kuwa ni historia ya moja kwa moja, hasa kuhusiana na matukio ya siku za karibuni, au historia iliyochanganyika na visakale (kuhusiana na matukio ya zamani zaidi) au visakale vilivyochanganyika na visasili (kuhusiana na matukio ya kale sana). Historia halisi husahaulika na kuingia katika kumbo la visakale na visasili kwa kadiri muda unavyopita. Hiyo ni tabia ya kawaida ya simulizi za mdomo. Katika fasihi ya Kiswahili,
simulizi za kihistoria zimekuwapo tangu kale. Vitabu vya Tarihi vinatupa simulizi zilizoandikwa kutokana na mapokeo ya mdomo, hususani zile zinazowahusu watawala. Ni vitabu vyenye historia finyu kulingana na malengo yake ya kuhifadhi habari za nasaba za watawala. Masimulizi ya kihistoria yenye mapana na taarifa zaidi ni yale ya kishairi – hasa yale yanayopatikana katika tendi. Ya zamani zaidi yanamhusu shujaa Liyongo, na yalitolewa kwa njia ya nyimbo na mashairi, na pia tendi-simulizi ambazo sasa zimepotea (Steere, 1870). Zipo pia tendi mashuhuri za miaka ya karibuni, kwa mfano Utenzi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima (Hemed Abdallah, 1895) na Vita vya Maji Maji (Abdulkarim Jamaliddini, 1910; TUKI, 2006), zinazohusu mapambano ya wananchi kupinga uvamizi na utawala wa Wadachi, na Utenzi wa Vita vya Uhuru (Robert, 1961) unaosimulia matukio na mwenendo wa Vita vya Pili vya Dunia. Sambamba na tenzi, zimechapishwa tamthilia kadha za kihistoria tangu miaka ya 1960. Baadhi yake ni: Kinjeketile (Hussein, 1969) na Mashetani (Hussein, 1971); Mkwawa Mahinya (Nkwera, 1968), Mukwava wa Uhehe (Mulokozi, 1979) na Harakati za Ukombozi (1982). Ubunilizi wa kihistoria katika
umbo la riwaya hauna historia ndefu kama ulivyo katika ushairi. Kitabu cha Habari za Wakilindi (Ajjemy, 1895) kinafikiriwa na baadhi ya watu kuwa ndicho riwaya ya kwanza ya Kiswahili. Hata hivyo, dai hili lina walakini, kwani mtunzi wa masimulizi hayo hakuyakusudia yawe riwaya, bali aliamini kuwa alikuwa akiandika historia ya Wakilindi, hususani utawala wa nasaba ya kina Kimweri huko Usambara. Visasili na visakale vinavyojipenyeza katika masimulizi hayo haviondoi ukweli kuwa yale ni masimulizi ya kihistoria yanayotokana na simulizi za mdomo na matukio ya kushuhudiwa na mwandishi mwenyewe, na kwamba mtindo uliotumika ni wa taaluma ya kijadi ya usimulizi wa historia isiyopambanua visakale na historia halisi. Hivyo tunaweza kusema kuwa riwaya
halisi ya kwanza ya historia ni ile ya James Mbotela ya Uhuru wa Watumwa (1934). Riwaya hiyo inasimulia juu ya masaibu ya mateka waliochukuliwa utumwani na baadaye kukombolewa na meli ya Wazungu katika miongo ya mwisho ya karne ya 19. Mengi yanayosimuliwa ni matukio ya kweli ya kihistoria, japo bila shaka hapa na pale mtunzi katia chumvi kwa malengo ya kisanaa. Baada ya hapo hapakutokea riwaya ya kihistoria tena hadi miaka ya 1970. Baada ya mwaka 1970 riwaya ya
kihistoria katika fasihi ya Kiswahili imejitokeza kwa dhati zaidi. Riwaya ya Msewe ya Kifo cha Ugenini iliyochapishwa mwaka 1977 ilihusu kipindi cha uvamizi wa Wadachi – kipindi ambacho kwa hakika ndicho kilichohamasisha kazi nyingi zaidi za simulizi za kihistoria. Baadaye zilichapishwa riwaya mbili za.Shafi; Kuli (1979) na Kasri ya Mwinyi Fuad (1978). Riwaya hizo zilizohusu migogoro ya kijamii-kitabaka huko Zanzibar kabla ya mapinduzi ziliisogeza mbele riwaya ya kihistoria. Riwaya za Kezilahabi za Dunia Uwanja wa Fujo (EALB, 1975) na Gamba la Nyoka (EAPL, 1979) vilevile zina sifa fulani za uhistoria, hasa zile zihusuzo mchakato wa ujenzi wa Ujamaa katika Tanzania katika miaka ya 1967-1977, japo haziingii moja kwa moja katika mkondo huo. Riwaya za Kezilahabi zilifuatiwa
na riwaya za Said Ahmed Mohamed na M.S. Mohamed za Nyota ya Rehema (Mohamed 1978), na Dunia Mti Mkavu (Ahmed, 1980). Hizo nazo zina sifa kadha za uhistoria, maana zinaonesha migogoro ya kijamii-kitabaka ya kipindi cha kabla ya Mapinduzi nchini Zanzibar. Na ingawa riwaya hizo zilitoa mchango mkubwa katika kuitajirisha na kuikomaza riwaya ya Kiswahili, bado fani ya riwaya ya kihistoria, hadi mwaka 1990, ilikuwa bado haijaenea sana. Kutokana na hali hii, mwishoni mwa
miaka ya 1980 jopo dogo la wapenda fasihi, likiratibiwa na Bi. Elieshi Lema, ambaye wakati huo alikuwa mhairiri katika Shirika la Uchapishaji Vitabu la Tanzania (TPH), lilianza kukutana nyumbani kwa Bi. Lema mara mbili kwa wiki saa za jioni kujadili na kupanga namna ya kustawisha riwaya ya kihistoria kwa Kiswahili, hususani kwa ajili ya wasomaji vijana. Wanajopo walikubaliana wao wenyewe waandike riwaya kama tano za kihistoria zenye kuzingatia matukio yafuatayo: 1. Biashara ya Watumwa (mwandishi A. Lihamba); 2. Vita vya Wahehe dhidi ya Wadachi (mwandishi M.M. Mulokozi); 3. Vita vya Wachagga dhidi ya Wadachi – Mangi Meli – (mwandishi: R. Mabala), na Vita vya Maji Maji (Mwandishi E. Kezilahabi). Wanajopo waligawiana kazi na kuanza kuandika. Walipata msaada mdogo kutoka shirika la Kanada la Misaada ya Maendeleo kupitia Elimu (CODE) ambalo wakati huo kiongozi wake wa ofisi ya Afrika ya Mashariki alikuwa Scott Walter. Afisa huyo alitoa msukumo mkubwa uliowawezesha wahusika kufanya utafiti mdogo wa uwandani kuhusiana na mada hizo. Kutokana na mchakato huo, kufikia mwaka 1991 miswada viwili ya hadithi za historia kwa picha na maelezo mafupimafupi ilipatikana: Miswada hiyo ni Wimbo wa Sokomoko (A. Lihamba) kuhusu biashara ya watumwa; na Ngoma ya Mianzi (M.M. Mulokozi) kuhusu uvamizi wa Wadachi huko Kilosa, uliofuatiwa na vita vya Lugalo vya 1891. Punde ilionekana kuwa shughuli ya
kuandika vitabu kwa ajili ya watoto na vijana ilikuwa nzito, na huenda isingewezekana kuratibiwa na Bi. Lema na shirika la CODE, kwa ufanisi bila kuwa na chombo mahsusi cha kudumu. Ikapendekezwa na kukubaliwa kuwa uanzishwe Mradi wa kuratibu shughuli hiyo ambao awali ungegharimiwa na CODE. Huo ukawa ndio mwanzo wa kuzaliwa kwa Mradi wa Vitabu vya Watoto Tanzania (Children’s Book Project – CBP) mwaka 1991. Vitabu viwili vya jopo hili vikawa miongoni mwa machapisho ya mwanzo ya Mradi huo. Hivi leo jopo hilo halipo tena, na riwaya kuhusu Mangi Meli na Vita vya Maji Maji hazijaandikwa, lakini Mradi umekua na kuzaa vitabu vingi zaidi (kama 300) na shughuli nyingi zaidi, zikiwamo za kuratbu usomaji shuleni. Juhudi za CBP
ziliwezesha kuchapishwa kwa riwaya tatu za kihistoria kwa Kiswahili kwa ajili ya vijana zilizoandikwa na M.M. Mulokozi. Riwaya hizo ni: Ngome ya Mianzi (1990), Ngoma ya Mianzi (1991) na Moto wa Mianzi (1996). Lengo lake lilikuwa ni kuwapa vijana mwamko wa kupenda kusoma na kutafiti historia ya jamii zao kama njia mojawapo ya kujenga mapenzi kwa nchi (uzalendo) na chuki kwa adui, kujiamini na kujithamini. Bahati mbaya si waandishi wengi katika Mradi waliojitokeza kuendeleza mkondo huu wa uandishi, isipokuwa Dumea aliyeandika novela ya Usiku wa Balaa (E&D, 2009). .
Nje ya Mradi, uandishi wa riwaya
ya kihistoria ulifikia hatua ya juu ilipochapishwa riwaya ya Bernard Mapalala ya Kwa Heri Iselamagazi (TPH 1992). Riwaya hiyo ilitupeleka katika historia ya Mtemi Mirambo na warugaruga wake katika muktadha wa ujenzi wa himaya ya Kinyamwezi kwenye karne ya 19. Ni riwaya nzuri ambayo haijapata kutendewa haki (kwa kuchunguzwa kitaaluma na kutumika kwa mapana) na wahakiki, watafiti na wakuza mitaala. Iselamagazi ilifuatiwa na riwaya mbili za Shafi: Vuta N’kuvute (1999) na Haini (2003). Zote mbili zinahusu matukio yenye maana kubwa kwa majaaliwa ya Zanzibar na Wazanzibari, na zinatuingiza katika undani wa matatizo ya mapinduzi ya Zanzibar ambayo yaliwageuka wale waliojitoa muhanga kuyatengeneza. Suala la utawala wa chuma (ambao dola inajaribu kuuhalalisha kwa kurejelea historia ya mapinduzi) dhidi ya haki za binadamu linachanganuliwa vilivyo katika riwaya ya Haini. Riwaya nyingine ya kipindi hiki iliyojaribu kusawiri historia ya Tanzania kisanaa ni ile ya Miradi Bubu ya Wazalendo. (1995). Riwaya hiyo, kama ile ya Kiingereza ya M. Vassanji The Gunny Sack (1989), ilijaribu kusimulia kisanaa historia ya Tanganyika/Tanzania tangu enzi za ukoloni hadi kudai uhuru na ujenzi wa ujamaa, hadi kushindwa kwa ujamaa na kustaafu kwa Mwalimu J.K. Nyerere. Kama riwaya ya Vassanji, riwaya hii inatumia wahusika wa kutoka makundi mbalimbali ya kijamii-kitabaka ili kuonesha majaaliwa ya makundi hayo katika Tanzania “huru”. Tunaoneshwa kuwa wafanyakazi wa kawaida na wakulima hawakunufaika na sera za Ujamaa; walionufaika zadii ni tabaka jipya la vibwanyenye wa dola (kina Nzoka) na wafanya biashara. Kama anavyoeleza Mbonde (2004) kwa usahihi, ni vizuri kuisoma riwaya hii sambamba na riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria, maana maudhui yake yanakamilishana. Kwa jumla tunaweza kusema kuwa
miaka ya 1990 utanzu wa riwaya ya kihistoria katika fasihi ya Kiswahili umekua na kujipatia nafasi muhimu katika historia ya fasihi hiyo. Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria imetokea katika muktadha huu wa kifasihi. Lakini, tofauti na riwaya zilizotangulia, Makuwadi imepanua mawanda na kutazama hata nje ya Tanzania katika kujaribu kulifafanua tatizo kuu la kitaifa la enzi zetu. Kama wanafasihi waliomtangulia,
Chachage alifahamu umuhimu wa historia katika harakati za maendeleo na ukombozi wetu. Alijua kuwa kosa kubwa mojawapo linalofanywa na matabaka tawala ya sasa ya Afrika ni kudharau au kupuuza historia. Baadhi yamediriki hata kufuta somo la historia katika mitaala ya shule (mfano: Tanzania wakati wa Awamu ya Tatu), na mengi bado yanafundisha historia iliyoasisiwa na mkoloni – ile ya ustaarabu wa mzungu na jusura zake katika bara la Afrika. Riwaya hii inatuonesha kuwa kudharau historia ni hatari, kwa kuwa ni kukinyima kizazi kipya haki ya kujitambua na kujua tulikotoka, tulipo na tuendako. Bila kujua matatizo yetu ya kihistoria ya nyuma na ya leo, ni vigumu kubuni njia sahihi ya kufuata kwa siku zijazo. Maana adui wetu wa zamani, wa sasa, na wa kesho bado ni yuleyule, na mbinu zake hazijabadilika sana. Tunaposahau historia tunaishia kumkumbatia adui huyo tukidhani ni rafiki, na madhara tunayoyapata katika uhusiano wetu naye yanazidi kuongezeka. Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria inajaribu kuturudisha nyuma katika mizizi ya
kihistoria ya matatizo yetu ya leo ili historia hiyo iwe ni mwega wa kutuwezesha kusonga mbele katika mapambano yetu ya kudumu ya kutafuta ukombozi kamili na maisha bora kwa ajili ya jamii zetu. Katika kufanya hivyo, Chachage anaturudisha katika jadi bora ya wahenga wetu ya kuhifadhi historia na kuipokeza kwa vizazi vyao; jadi ambayo ilipigwa vita na ikakaribia kuuliwa na tawala za kikoloni na asasi zake kwa kuwa zilitambua fika hatari za mwamko wa kihistoria wa wenyeji kwa utamalaki wao. Kwa ufupi, huu ndio muktadha wa
kifasihi uliochipuza riwaya ya Chachage ya Makuwadi wa Soko Huria. Sasa tuiangalie riwaya yenyewe. 3.0 Makuwadi
wa Soko Huria Riwaya ya Makuwadi wa Soko Huria iliandikwa na hayati Chachage S. Chachage
mwaka 1999-2000 na kuchapishwa na E & D Publishers mwaka 2002. Hii ndiyo riwaya ya mwisho inayofahamika aliyoiandika Hayati Chachage kabla hajafariki mwaka 2006, ingawa katika mahojiano yake na Diegner anasema wakati huo (2004) alikuwa amemaliza kuandika sura kama mbili za riwaya nyingine. Riwaya hii iliandikwa wakati wa kipindi cha ukomavu wa utandawazi wa Kimagharibi na Kimashariki katika Tanzania na Afrika, kuvamiwa kwa uchumi wa Tanzania na “wawekezaji”, pamoja na mawakala wao wa kidini na kitamaduni kutoka Magharibi na Mashariki, kuundwa kwa utatu usio mtakatifu wa mabepari wenyeji, mabepari wa kigeni, na viongozi wa serikali ili kushirikiana kupora rasilimali za nchi, na hivyo kujigeuza kwa tabaka la watawala kuwa mafisadi wakubwa na mawakala wa ubepari wa kigeni dhidi ya wananchi. Mchakato huu uliambatana na kufukarishwa kwa wananchi walio wengi kutokana na kufungwa kwa viwanda, kufukuzwa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi katika maeneo yao ya jadi ili kupisha “wawekezaji”, kutelekezwa kwa watoto wa maskini katika mfumo wa elimu (kuwapa baadhi yao mikopo ya elimu badala ya ruzuku), na kuvurugika kwa vyama vya ushirika na bei za mazao ya wakulima wadogowadogo. Mwenendo huu ulimwudhi sana Chachage, ambaye aghalabu alikuwa akiandika makala na kuhutubia kuhusu utandawazi, ambao aliuita “utandawizi.” Riwaya yake ya Makuwadi wa Soko Huria ilikuwa ni mwendelezo wa mapambano yake dhidi ya ubepari na utandawazi katika medani ya kifasihi. 3.1 Muhtasari wa Riwaya
Hadithi inaanza na “kifungua
pazia” ambacho kinaelezea kuhusu kutekwa kwa Mjuba na Sifuni (ambao ni waandishi wa habari) na kundi la Kaboko kutokana na kuandika habari zenye kufichua njama za kukwepa kulipa kodi. Inamalizika na “kifunga-pazia” ambapo kesi ya kutekwa kwa Mjuba na Sifuni imepanuka na kuwa kesi ya mauaji yenye kuhusisha masuala mengi na watu wengi, wakiwamo watu wakubwa katika uchumi na utawala. Baina ya “kifungua-pazia” na “kifunga pazia” kuna sura 12 zenye masimulizi kuhusu maisha, masaibu na mahusiano ya wahusika wakuu wa hadithi: Fidelis, Mjuba, Sifuni na Binti Wenga; na wahusika muhimu wengine – kina Amina, Japhet Lupocho, Joshua Lupocho, Mooney, Alibhai, Chaurembo, Sorrenson, Sadiki Mazengo, Hakimu Mazengo, Mzee Mrisho, Mzee Miraji, na Mzee Abdurahaman. Maisha na masaibu yao yanapambanishwa na yale ya wananchi wa vijijini (Delta ya Rufiji na Ruhimba) kwa upande mmoja, na mizengwe na vitendo vya mabepari wa kimataifa na mawakala wao wa ndani kwa upande mwingine. Waandishi wa habari wanakuwa ndio kiungo na kioo cha kumulikia uhusiano wa kihasama uliopo kati ya pande kuu mbili: upande wa wananchi (wakulima, wavuvi, wafugaji) na upande wa mabepari wa dunia au watandawazaji (wawekezaji, wahisani, “wataalamu”) na “Makuwadi” wao wa ndani. Waandishi wa habari za mazingira
wenye mwelekeo wa kimaendeleo: Fidelis, Mjuba, Sifuni na Saada wanaamua kwenda Rufiji kufuatilia suala la “Mradi wa Kamba” Rufiji, hususani baada ya kuhudhuria Mkutano wa Wanarufiji uliofanyika Dar es Salaam kujadili Mradi huo. Wanaahidiwa msaada wa fedha na wahisani kupitia kwa Sorrenson, afisa wa Kiswidi mwenye kazi ya kuratibu suala hilo. Safari ya Mjuba na wenzake
inawekewa vikwazo na Wizara ya Misitu na wawekezaji ambao hawataki habari za mipango yao na mapambano yao na wananchi huko Rufiji zifahamike. Hata hivyo, waandishi wa habari wanafanikiwa kufika Rufiji katika kijiji cha Nyamisati na kupokewa kwa uhasama na viongozi wa kijiji hadi wanapodhihirisha kuwa wao wako upande wa wananchi na wala hawakutumwa na wawekezaji au serikali. Wanaelezwa masuala yote yanayohusu Mradi wa Kamba na uchumi wa delta wa mikoko na uvuvi, na wanatembezwa katika visiwa mbalimbali kujionea wenyewe hali ilivyo. Wanaelezwa pia historia kuhusu maisha na mapambano ya wananchi wa delta na Tanzania nzima kupinga uvamizi na unyonyaji wa wageni. Safari hii inatokea pia kuwa ni ya
ugunduzi kwa Fidelis, ambaye anakutana na ndugu zake waishio Rufiji ambao alikuwa hawafahamu. Ni safari ya utakaso pia kwa wale walioikosea jamii – ama kwa usaliti ama kwa kuvunja miiko. Wanarejea Dar es Salaam huku Fidelis akiwa ameufahamu ukoo wake na akiwa ameandamana na baadhi ya ndugu zake wa Rufiji. Safari hii ya Rufiji ya kusaka
habari na ufahamu kutoka kwa wananchi kuhusu matatizo yao ndiyo mkondo mkuu wa hadithi. Mikondo mingine inahusu hadithi binafsi za wahusika wakuu, hasa Fidelis, Mjuba, Sifuni, Amina, Binti Wenga, Japhet Lupocho, Joshua Lupocho, Paul Mooney, Alibhai, Chaurembo, Sorrenson, Sadiki Mzengo, na wengine. Masimulizi kuwahusu watu hawa na wasifu wao na matazamio yao yanatuingiza katika undani wa mahusiano na hisia zao za mapenzi na za chuki, za upevukaji wao kwa kadiri hadithi inavyoendelea, hadi kufikia hatua ya baadhi yao kujitambua wao ni nani (Japhet, Fidelis, Joshua, Amina), baadhi kubadilika kimtazamo (Sorrenson, Japhet, Salama – mkewe Mjuba, na Oscar Mayowe – mzinzi anayegeuka mlokole), na baadhi kuathirika kisaikolojia kutokana na aibu ya usaliti na uvunjaji miiko hadi kufikia hatua ya kujaribu kujiua (Japhet). Hatimaye tunaona mabadiliko
mwishoni mwa hadithi: baadhi ya waovu wanaadhibiwa, wema wanatunukiwa, na mshikamano wa wananchi na “wasomi” wapenda maendeleo unakuwa umejengeka na kuimarika. Tunabaki na hisia kuwa msingi wa mapambano yajayo tayari umejengeka, na kwamba “Makuwadi” na mabwana zao watakuwa na kazi ngumu sana katika kuendeleza ajenda yao yenye madhara kwa wanyonge. 3.2 Mawazo Makuu
Muhtasari huu unaonesha kwamba
mgogoro wa riwaya hii una pande tatu: Upande wa wananchi wa Rufiji na Ruhimba ambao ndio waathirika wa mfumo wa ubinafsishaji na uhuria unaosimikwa; upande wa wawekezaji na mabepari wa kigeni na mawakala wao wenyeji (wa kisiasa na wa kibiashara), ambao ndio wanaopambana na wananchi kwa sera na vitendo vyao; na upande wa waandishi wa habari, ambao wako katikati na wamegawanyika kati ya wale wanaowatetea wananchi (Mjuba, Sifuni, Fidelis) na wale wanaowatumikia maadui wa wananchi (Mwenerumango, Jonathan Massawe, na Alhaji Seif Said). Kundi hili la waandishi linawakilisha kundi au tabaka dogo la wasomi na vibwanyenye uchwara kwa ujumla, na mgawanyiko wao unaakisi mgawanyiko halisi ndani ya tabaka hilo miongoni mwa Watanzania. Hata hivyo, tabaka hili ndilo lenye jukumu la kuuchunguza na kuuelezea mwenendo wa kijamii na mivuvumko iliyomo, kutuonesha mahusiano ya kihasama ya makundi ya kijamii, kiini chake na mustakabali wake. Hivyo tunaiona jamii ya Watanzania na migogoro yake kupitia katika macho, mawazo, uwezo na udhaifu wa kundi hili. Mipaka ya muono wa kundi hili la waandishi wa habari ndio unaojenga mipaka ya muono wa riwaya hii. Je, kwa nini Chachage kalichagua tabaka hili, ambalo aghalabu hulegalega kimsimamo na bila shaka lina ufinyu wa kimawazo, liwe jicho letu la kuiangalia jamii yetu? Hatujui; labda kwa kuwa yeye mwenyewe, akiwa ni msomi na mtafiti, alikuwa katika kundi hili, au uhusiano wake na wale aliowatafiti (wakulima na wavuvi) haukuwa tofauti na wa wahusika hawa na wananchi wanaoandika habari zao. Mwandishi anatuonesha kuwa
ubinafsishaji na uhuria si sera zilizobuniwa na watawala wetu hivi karibuni, bali zina mizizi yake katika historia ya kutawaliwa kwetu, ya ubeberu, ambao kwa sasa ndio unaoitwa utandawazi. Hivyo, kupitia kwa mhusika Fidelis Msakapanofu anatushauri turejee huko kwenye mizizi iwapo tunataka kuielewa vyema tanzia ya Mwafrika wa leo: “Kwa nini usianzie mwanzo wa hayo mambo, kule
yalikoanzia? Lakini, akili inaniuliza, mwanzo huo ndio upi?” (uk. 50) Binti Wenga, na wazee wengine,
kina Mzee Mrisho, Mzee Abdurahaman na Mzee Miraji, na Bi. Khadija, wanaletwa katika masimulizi haya wakiwa na jukumu la kuturejesha huko tulikotoka, kutupa historia ya mababu na mabibi zetu, ya namna tulivyovamiwa na kuporwa tangu enzi za biashara ya watumwa na ukoloni wa Wadachi na Waingereza, na mwitiko wa hao wahenga wetu kwa ubeberu wa wakati wao. Riwaya, kupitia masimulizi ya
wazee hao, inatuonesha kuwa uporaji wa ardhi na maliasili za nchi hii ulianza mapema kabisa, na ulifanywa na Wazungu na wengineo kwa zaidi ya miaka mia, na kwamba wananchi, ambao kabla ya hapo walikuwa na maingiliano na uhusiano mzuri wa kibiashara na kijamii, walivurugwa na ukoloni na kutenganishwa na kugeuzwa tribes. (Neno la Kiingereza “tribe”, kwa namna walivyolitumia, halimo katika lugha ya Kiswahili, na si tafsiri ya neno “kabila.” Tribe linabeba dhana ya dharau na matusi ambayo haimo katika neno “kabila”). Hata hivyo, wananchi wenyewe waligundua njama hizo za kuwagawa mapema na wakaamua kuungana ili kupambana na adui yao. Matokeo ya mchakato huo yalikuwa ni Vita vya Maji Maji. Mto wa Rufiji na matawi yake,
ambao sasa unaporwa na wageni, kina Mooney na Vangalatus, ukawa ndio kiungo kikuu cha wananchi na barabara kuu iliyopeleka ujumbe wa ukombozi hadi pembe zote za kusini mwa Tanzania: Tulikuwa tunasafiri katika mto ambao maji yake
yalikuwa yamesafiri zaidi ya maili mia nne, mto mkubwa kuliko yote nchini ambao sehemu kubwa ya maji yake yalitokea mto Ruaha ulioanzia Mbeya, mto Kilombero ambao ulianzia sehemu za Njombe kama mto Ruhuji na mto Luwengu ulioanzia sehemu za Ruvuma. Mto huu uliwaunganisha watu wa sehemu mbalimbali, nao wakajihisi kwamba ni wamoja, na labda ilikuwa ni kwa sababu hii, watu wote wa sehemu hizi waliungana pamoja wakati wa vita vya Maji Maji (uk. 219). Hadithi hii ni kielezo cha picha
hii ya muungano wa watu kufuata Mto Rufiji: inahuisha, kupitia kwa wahusika wakuu wa familia za kina Lupocho Msakapanofu, Wenga, na Nguvumali, muungano huo wa Maji Maji wa jamii za kutoka Uzaramo hadi Rufiji hadi Ubena (Njombe), Songea mpaka Mbamba Bay. Huu ni mtandao unaounganisha jamii za Wazaramo na nyinginezo za upwa wa Mzizima kama vile Wandengereko, Wamatumbi, Wangindo, Waluguru, Wamakonde, Wamakua, Wangoni, Wabena, Wapangwa, Wandendeule, Wamatengo, Wakinga, n.k. Ni muungano unaojumuisha watu wa imani mbalimbali – za jadi na Uislamu. Familia ya kina Lupocho ni kielezo cha muungano huu: mababu na mabibi zao kutoka Mbamba Bay (Msakapanofu na Wenga Mhalule) walikutana katika harakati za mapambano na wazee wa Rufiji (Nguvumali na Samadi) na baadaye watoto wao wakaoana na kuzaa wana na wajukuu ambao walisambaa kwenda kuishi Rufiji, Songea, Njombe, Tabora na Dar es Salaam, na wakawa hawafahamiani. Hatimaye ndugu hao wanakutanishwa tena na harakati za kupinga ufugaji wa kamba Rufiji na uuzaji wa ardhi Ruhemba. Baadhi yao (Japhet na Amina) wanataka kuoana bila kujua kuwa ni ndugu, na wanapogundua udugu wao inabidi lifanyike tambiko la utakaso). Hivyo historia ya familia hii imebeba historia ya nchi na misukosuko yake. Hivyo basi tunaweza kusema kuwa
riwaya hii ni istiara ya vuguvugu la ukombozi la Maji Maji katika mazingira ya leo: kutoka Rufiji hadi Ungoni hadi Mbamba Bay. Ni kama mwandishi anataka kutuambia kuwa kama ambavyo babu zetu waliungana bila kujali mipaka, lugha au kabila ili kupambana na ukoloni, sisi wajukuu zao pia tunawajibika kufuata mfano wao na kuungana ili kupambana na utandawazi unaokuja katika umbo la uhuria, uwekezaji wa kigeni, ubinafsishaji na ukuwadi. Mto wa Rufiji uwe ni kiungo chetu kama ulivyokuwa enzi za Maji Maji. Ukombozi huu, kwa mujibu wa riwaya
hii, sharti ujengwe katika utaifa mpana ambao unavuka mipaka ya kabila, na hata taifa, na kuwa Upanafrika (Umajumui wa Afika). Maana Afrika ni moja na Waafrika ni watu walewale popote pale walipo. Mawazo ya Mjuba huenda yanawakilisha mawazo ya mwandishi: Wakombozi wa kweli wa nchi yetu hawakuipigania Tanganyika tu, bali mama Afrika: Hao walikuwa watu kama akina Dennis Phombeah, akina
Austin Shaba, akina Oscar Kambona, na wengine – watu waliomjua mama mmoja tu bila kujali kama walizaliwa wapi. Naye alikuwa mama Afrika (uk. 213). Sentensi ya mwisho inakuwa na
maana zaidi tunapokumbuka (kwa wale wenye kufahamu) kuwa baadhi ya mashujaa walioipigania Tanganyika anaowataja Chachage, kwa mfano Eric Fiah na Osare Otango, hawakuwa Watanganyika. Osare Otango, ambaye aliendesha mapambano huko Tanga dhidi ya walowezi, alikuwa Mmaragoli wa Kenya. Hivyo riwaya hii inatusogeza mbele
na kutupeleka kwenye dhana ya umoja wa Afrika iliyohubiriwa na kina William du Bois, George Padmore, Kwame Nkrumah na Julius Nyerere. Uhuria ni zao la utandawazi, na
unakuja na sura mbalimbali. Kuna sura ya uchumi – ubinafsishaji na uwekezaji wa kigeni. Wananchi wananyang’anywa ardhi na maeneo yao, wanapewa wawekezaji kutoka nje. Kuna utalii – mbuga za wanyama zinabinafsishwa, wanyama wanauliwa kwa ajili ya starehe za wawindaji matajiri kutoka Magharibi (Rais Roosevelt), na kuna udini – makanisa ya kilokole (bila shaka kutokea Marekani) yanaenezwa nchi nzima na kuwateka na kuwapumbaza watu. Ndoa ya Mjuba na Salama inavunjika kutokana na kuokoka kwa Salama. Na haya yote yanawezekana kwa kuwa wapo watu – wenyeji, wafanyabiashara na wanasiasa, ambao wako tayari kununuliwa na wageni na kuiuza nchi kwa manufaa yao binafsi. Kina Japhet Lupocho, Chaurembo, Jonathan Massawe, Moddy Mwenerumango, Alibhai, Njovu Luhala – Mbunge, wako katika mkumbo huo. Hao ndio wanaoitwa Makuwadi, yaani “washenga-nuksi” wanaosaidia kufanikisha mipango ya waporaji wa kigeni hapa nchini. Mh. Luhala anawakilisha wanasiasa,
na tunaona namna anavyoshiriki katika kuuza/kubinafsisha ardhi ya wananchi huko Ruhimba, na anavyokataa kukutana nao wanapokuja kumwona Dodoma. Hatimaye, wabunge wanapokubali kukutana na wananchi, wanadai posho, na wanapoona hakuna posho, wanataka mkutano uishe haraka ili wawahi nyama choma mnadani! Uhuria unaambatana na ufisadi.
Rushwa, ukwepaji kodi, magendo, uuzaji wa madawa ya kulevya, usaliti na upotoshaji wa habari vimetawala. Mtandao wa ufisadi unawahusisha kina Alfred Chaurembo (kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali-NGOs), Roshan Alibhai, A. Kongoro, K. Kongoro, Maua Mutabingwa na Sadiki Mazengo. Pia, Wazungu wa mashirika ya “hisani” wanaishi kwa anasa kwa kutumia misaada ya wakimbizi (uk. 185). Kuna uharibifu mkubwa wa
mazingira; wawindaji wanateketeza wanyama wa pori (Roosevelt, Pretorius na Louis); mikoko katika delta inakatwa bila mipangilio; samaki wanavuliwa na kuuliwa ovyo. Kuna unyanyasaji wa wanawake, na
mwenendo wa kuwanyima haki yao ya ardhi. Wanawake wa Ruhimba wananyang’anywa ardhi yao na uongozi wa wilaya bila malipo wakati wanaume wanalipwa (uk. 45). Kwa wananchi, uhuria huu
unaonekana kuwa wa bandia kwa kuwa unawanyang’anya wananchi haki yao na kuwakabidhi wageni badala ya kuruhusu ushindani halali ambao unapaswa kutoa nafasi kwa ushirikiano pia miongoni mwa umma (uk. 199). Mzawa wa Rufiji anayeleta mitambo yake kuwekeza pale Rufiji anakataliwa na serikali wakati mgeni (Mgiriki) anakubaliwa. Kwa jumla, tunaweza kusema kwamba
riwaya hii inasawiri dhana ya uhuria na madhara yake kwa wananchi wa kawaida (wakulima/wavuvi/wafugaji/ wachimba madini). Mfumo mzima wa uhuria unasailiwa kwa mtazamo wa umma – wa walio wengi, kuonesha nani ananufaika, na nani anadhurika. Riwaya inadhihirisha kuwa uhuria ni mkono wa utandawazi ambao nao ni mwendelezo wa ubeberu wa tangu karne ya kumi na tisa na hata kabla. Jina lenyewe la riwaya linabeba
ujumbe mzito: “Makuwadi (makuwadi) wa soko huria” ni usemi unaowasawiri waasisi na waendelezaji wa mfumo wa soko huria kama watu waovu wanaohudumia mfumo uliokosa uadilifu. “Makuwadi” ni watu wafanyao kazi ya kuwatafutia watu wengine wenzi wa kufanya nao umalaya au uzinzi kwa ujira maalumu. Ni mawakala wa ukahaba. Katika riwaya hii Chachage anawalinganisha mawakala wa soko huria na mawakala hao wa uzinifu kwa lengo la kuonesha kwamba hawatofautiani katika kazi zao na madhara yao kwa jamii. Na tunaoneshwa wazi kwamba mawakala wa soko huria, kama walivyo makuwadi halisi, wanafanya biashara ya kuuza watu kwa mabepari wa kigeni. Hivyo jina la riwaya hii ni kauli thabiti na hasi ya mwandishi kuhusu mfumo mzima wa ubepari huria anaouchambua. Ili kujinusuru kutokana na hali hii, mwandishi anatuasa turejee nyuma katika historia yetu, tujue kwa nini haya yametokea, na tujifunze kutoka kwa wahenga wetu namna ya kupambana na mfumo huu wakati huo huo tukibuni mbinu mpya zinazolingana na hali na enzi zetu. Udhaifu wa usawiri wa mgogoro mkuu
wa riwaya hii unatokana na ufinyu wa mtazamo na uwezo wa tabaka linalotumika kuendeleza na kufafanua mapambano haya kwa msomaji – tabaka la vibwanyenye wasomi (waandishi wa habari). Hili ni tabaka tegemezi ambalo takriban shughuli zake za kimaendeleo zinategemea misaada ya wahisani. Fidelis, Mjuba na wenzao wanakwenda Rufiji na kwingineko na kuchunguza madhara ya uhuria kwa msaada wa shirika la Kiswidi la Sorrenson. Bila shirika hilo hawawezi kufanya kitu. Huu ndio udhaifu na unyonge wa tabaka hili na asasi zake. Hivyo ni kejeli na ni njozi kwamba chombo cha utandawazi–mashirika ya hisani–ndicho kinachotumika kuuchambua na kuupiga vita utandawazi huo. Je, kitafanikiwa? Mbali na kiwango hiki cha
kijamii-kisiasa cha masimulizi ya riwaya hii, kuna kiwango cha binafsi cha mahaba kati ya jozi mbili za wahusika, ambao wote bado ni vijana: Mjuba+Sifuni; Makoba+Amina. Safari yao ya kutafuta maarifa na taarifa inakuwa pia ni safari ya kujigundua kuwa wanapendana na kukomaza mapenzi yao hadi kufikia hatua ya kuoana. Ni hitimisho murua la uhusiano wao unaojengwa katika mapambano. Chachage S. Chachage anatumia
mbinu nyingi za kisanaa na kimasimulizi ili kutimiza malengo yake. Mbinu kuu anayoitumia ni uchanganyaji wa ubunifu na uhistoria, yaani uchanganyaji wa historia halisi na mambo ya kubuni, wakiwemo watu halisi na wa kubuni. Mbinu hii inafanikiwa kuileta hadithi karibu zaidi na msomaji, hasa wa Tanzania, kiwakati na kihisia. Tunahisi kuwa tunachokisoma ni habari za kweli kama zile za magazetini au katika vitabu vya historia. Watu halisi waliopata kuishi, kama Kinjikitile, Pretorius, Nguvumali na Nyerere, na hata ambao bado wanaishi (wakati kitabu kinaandikwa), kama Issa Shivji na Edward Barongo, wanapambanishwa na kuingiliana na wahusika wa kubuni kama Binti Wenga, Japhet Lupocho, Mazengo na wengineo. Mchanganyiko huu unakolezwa na mbinu ya udokezi (allusion) ambayo inaifinya historia katika maelezo au madokezo mafupi mafupi. Hii ina maana kwamba msomaji wa riwaya hii sharti awe na welewa mpana kiasi wa historia na habari nyinginezo za nchi hii, vinginevyo anaweza asiupate vilivyo undani wa baadhi ya maelezo na masimulizi. Kwa mfano, madokezo kuhusu Mganga Nguvumali, Osare Otango, madawa na mizimu ya Maji Maji, na wapigania uhuru kama Phombeah na Abduwahid Sykes yana maana zaidi kwa mtu mwenye fununu ya kutosha kuhusu watu hao. Mafanikio haya ya kimaudhui
yanaungana pia na mafanikio katika kujenga taharuki na mvuto. Riwaya hii inasomeka vizuri na haraka, angalau kwa msomaji aliyepevuka kiasi. Aidha, mara kwa mara mwandishi anaingiza ucheshi, lakini wenye maana, ili msomaji asichoke. Mfano ni ile michapo ya “Padri wa Musoma” (Sura ya 6: 136-7) na “Mzungu Kala Fenesi” (Sura ya 7: 145-7). Matumizi ya kejeli hapa na pale
pia yanaongeza ucheshi. Kwa mfano, uk. 287 tunaambiwa: “nani asiyejua mchango wa wawekezaji hawa katika kuinua uchumi wa nchi?” Lakini kusudi la riwaya ni kinyume chake: ni kutuonesha mchango wa wawekezaji katika kuudidimiza uchumi wa nchi! Riwaya hii inazo dosari kadha za
lugha na mtindo. Mathalan, neno “ibura” linatumika sehemu nyingi kama kivumishi ilihali halipaswi kutumika hivyo. (Mfano: hali ngeni ibura ilimwingia moyoni” – uk. 203). Kadhalika, kuna makosa mengi kiasi ya tahjia na matumizi ya lugha ambayo yangeweza kusahihishwa na mhariri makini. Mifano ni mingi, hapa tutatoa michache tu: ·
“Makuwadi” badala ya “makuwadi” (mahali pengi) ·
“maaluni” badala ya “maluuni” (uk. 13) ·
“ngombe” badala ya “ng’ombe” (uk. 14) ·
“karatasi zingine” badala ya “karatasi nyingine” (uk. 19) ·
“mmojawao” badala ya “mmoja wao” (uk. 23) ·
“Al-Bussaidy na na ukoo” badala ya “Al-Bussaidy na ukoo” (uk. 53) ·
“asili ya Kidachi” badala ya “asili ya Kiholanzi” (uk. 53) ·
“askari wa kijerumani” badala ya “askari wa Kijerumani” (uk. 54) ·
“mume wa baba yangu mkubwa” badala ya…?, n.k. Hata hivyo, haya ni matatizo
madogo. Tatizo kubwa zaidi ni la usimuliaji. Mwandishi kaamua kutumia nafsi ya kwanza ya usimulizi kupitia mhusika mmoja: Fidelis Mvumi. Usimulizi wa nafsi ya kwanza unaitwa usimulizi-tinde, kwa kuwa una mipaka yake ambayo inamnyima uhuru mwandishi. Mathalan, haiwezekani kuelezea mambo ambayo msimulizi hakuyashuhudia au kuyashiriki, na wala haiwezekani kueleza, kama afanyavyo Fidelis, mambo yaliyomo moyoni au katika fikra za wahusika wengine. Hayo yanaweza kufanywa tu katika usimulizi maizi (omniscient) ambao unawezekana tu katika nafsi ya tatu. Lakini katika riwaya hii tunamwona Fidelis akisimulia habari za mawazoni mwa wahusika wengine bila wasiwasi – yaani akiwa msimulizi maizi ambaye kihalisi ni tinde! (Mifano; Sura ya 4.III – fikira za Japhet. Pia kur. 212-216 – mawazo ya Mjuba na Sifuni). Hii ni dosari. Dosari nyingine ni ile ya kutumia
wahusika kama Binti Wenga kuelezea historia na kufanya uchambuzi wa matatizo ya maeneo yanayohusika kwa namna ambayo haielekei kusadifu uzoevu wao wa kitaaluma. Masimulizi ya watu wa kijijini kwa kawaida huwa na umbile tofauti na yale ya wasomi au waandishi wa vitabu (ambao hutumia marejeleo, huelezea miaka ya matukio n.k.). Wasimuliaji wa mdomo hutumia mbinu simulizi, ambazo mara nyingi huepuka kutaja miaka na tarehe, na si rahisi kwao kuzungumzia mambo ya mbali kama Ulaya. Katika riwaya hii, sifa hizi zimechanganywa katika mtu mmoja, na kumfanya msomaji aamini kwamba anayeongea si Binti Wenga bali ni Chachage mwenyewe kupitia kwa mhusika huyo (kur. 67-8). 4.0 Hitimisho
Mbali na dosari chache hizi,
riwaya hii ni mchango wa pekee kabisa katika fasihi ya Kiswahili. Kwa hakika, riwaya hii ni majumuisho ya kazi, fikra, mawazo, mtazamo, mawanio na harakati za maisha za Chachage S Chachage. Ni kana kwamba alikuwa akituaga kwa kutuandikia “wosia” au ushuhuda wa yote aliyokuwa nayo moyoni kuhusu matatizo na mustakabali wa Tanzania na Afrika. Marejeo
Abdallah,
H (1960), (uliandikwa kama 1895) Utenzi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima. (Mh. J.W.T. Allen). Dar es Salaam: East African Literature Bureau (EALB) Ajjemy,
A.H (1972); (1895), Habari za Wakilindi (Mh. J.W.T. Allen). Nairobi: EALB, Allen, J.W.T 1971 Tendi. London: Heinemann Cabral,
A (1966), “The Weapon of Theory” (Silaha ya Nadharia). Address delivered to the first Tricontinetal Conference of the Peoples of Asia, Africa and Latin America held in Havana in Janury 1966. Hotuba inapatikana katika Revolution in Guinea: Selected Texts (Mfasiri R.Handyside). New York: Monthly review Press Diegner,
L (2002), “Mahojiano na Chachage Seithy L. Chachage Juu ya Riwaya Yake Makuwadi wa Soko Huria (2002)” katika Swahili Forum 11 (2004): 227-234 Heepe,
M (1928), “Suaheli-Chronik von Pate.” M.S.O.S. XXXI: 145-92 Hichens, W (1938) “Khabar al Lamu — A Chronicle of
Lamu.” Bantu Studies 12(1):1-33 Hussein,
E (1969), Kinjeketile. Nairobi: Oxford University Press (OUP) Hussein,
E (1971), Mashetani. Nairobi: OUP Kezilahabi,
E (1975), Dunia Uwanja wa Fujo. Nairobi: EALB Kezilahabi,
E (1979), Gamba la Nyoka. Arusha: EAPL Knappert,
J (1979), Four Centuries of Swahili Verse. London: Heinemann Lihamba,
A (1990), Wimbo wa Sokomoko. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House (TPH) Lukacs,
G (1962), The Historical Novel. , Harmondsworth: Penguin Books Mapalala,
B (1992), Kwa Heri Iselamagazi. Dar es Salaam:TPH Mbonde,
J.P (2004), “Chachage Seithy L.Chachage: Makuwadi wa Soko Huria (2002)Uchambuzi na Uhakiki” Katika Swahili Forum11 ( 2004): 214-226 Mohamed,
M.S (1978) Nyota ya Rehema. Nairobi: OUP Muhando, P Balisidya, N na Lihamba, A (1982) Harakati
za Ukombozi. Dar es Salaam: TPH Mulokozi, M.M (1990)
“Utunzi wa Riwaya ya Historia.” Mulika Na.22: 1-12 ________
(1990) Ngome ya Mianzi. Dar es Salaam: MPB Press, ________ (1991) Ngoma
ya Mianzi. Dar es Salaam: TPH ________ (1996) Moto wa
Mianzi. Morogoro: ECOL, Morogoro ________
(1997) Utenzi wa Nyakiiru Kibi. Morogoro: ECOL Mohamed,
S.A (1980) Dunia Mti Mkavu. Nairobi: Longman Robert, S (1967) Utenzi
wa Vita vya Uhuru. Nairobi: OUP Ruhumbika, G (1995)
Miradi Bubu ya Wazalendo. Dar es Salaam: TPH Shafi, A (1978) Kasri
ya Mwinyi Fuad. Dar es Salaam: TPH Shafi, A (1979) Kuli.
Dar es Salaam: TPH Shafi, A (1999) Vuta
N’kuvute. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Shafi, A (2003) Haini.
Nairobi: Longhorn Publishers Shivji, I (2000) (2002) “Makuwadi wa Soko Huria.” Mulika
Na. 26 (2000): 93-97 Tolmacheva,
M (1993) The Pate Chronicle. East Lansing: Michigan State University Steere, E (1870) Swahili Tales, as Told by the Natives of Zanzibar . London: Bell and Daldy
Vassanji, M (1989) The Gunny Sack. Oxford: Heinemann International
|