TASWIRA YA MWANAMKE KATIKA RIWAYA YA SHIDA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi andishi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=7) +---- Forum: Riwaya (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=52) +---- Thread: TASWIRA YA MWANAMKE KATIKA RIWAYA YA SHIDA (/showthread.php?tid=1025) |
TASWIRA YA MWANAMKE KATIKA RIWAYA YA SHIDA - MwlMaeda - 08-27-2021 Taswira ya Mwanamke katika Riwaya ya Balisidya (1981) Shida
Riwaya ya Shida imeandikwa na mwandishi wa kike aitwaye Balisidya N. kilichochapishwa mwaka 1981. Riwaya hii inayasawiri
maisha ya jamii za Watanzania na inaonyesha matatizo jamii hizi zinavyokumbana nayo. Katika riwaya hii, mhusika mkuu Matika anapambana na madhila ya mfumo dume ambayo yanamfanya awaasi wazazi wake. Aidha, riwaya hii inamsawiri mhusika mkuu katika taswira mbalimbali kama vile mwanamke kama pambo la mwanamume, mwanamke kama chombo cha kumfurahisha mwanamume, mwanamke kama malaya na mwanamke kama mtu wa kunyanyaswa. Katika riwaya hii mwandishi ametuonesha tabia ya pekee kwa baadhi ya wanawake kuwa na moyo wa huruma kwa vijana wa jinsia zote mbili. Kama tukiliangalia jina la riwaya Shida tunaona picha ya riwaya nzima. Shida hapa sio jina la mhusika au mtu wa kawaida tu, bila shaka ni taswira inayoimulika dhamira ya Balisidya tofauti na ile ya binadamu wa kawaida. Ni mtu anayepambana na matatizo kuanzia utotoni hadi utu uzima. Shida ni msimbo wa Kihemenitiki wenye kuwaashiria wanawake kuwa kuna ukandamizwaji na uonewaji wa kijinsia miongoni mwao, kwa masilahi wanaume.
Mwanamke kama Pambo na Chombo cha Starehe
Mwandishi wa riwaya hii kwa kiasi fulani anatuonyesha kuwa bado mwanamke amebaki katika nafasi ya chini katika ujenzi wa jamii mpya. Mwanamke bado anaonekana kama pambo na chombo cha kumfurahisha mwanamume. Mwanamke katika riwaya ya hii bado
hajapewa uhuru wa kuchagua mwanamume anayempenda kwa dhati. Mwanamke hususan mabinti bado wangali wamefungwa na mila potofu za kuchaguliwa wenzi wao wa kuwaoa. Matokea ya kulazimishwa huko tunayaona pale Matika analazimika kutoroka nyumbani kwao, kwa sababu baba yake kumlazimisha aolewe na kijana wa familia ambayo mzazi wake ameichagua bila hata kumshirikisha kwa kumuuliza kama anampenda. Picha ya mwanamke kuonekana kama pambo na chombo cha kumstarehesha mwanamume tunaiona pale tunapoelezwa kuhusu maisha ya Shaibu. Mwandishi anasema:
…Shaibu alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha kamba hapa mjini. Alikuwa amepanga katika nyumba moja iliyopo Manzese, Alikuwa na vitu maridhawa pamoja na uhuru wake. Wasichana wengi walimtembelea wakabadilishana nafasi kama alivyopenda yeye. Wasichana hawa waliijaza nyumba ya Shaibu kila leo, kila saa alipokuwa hayupo kazini, wakamstarehesha usiku na mchana (uk. 29).
Lakini uhusiano huu baina ya wanawake na wanaume haukuzuka hivihivi. Wenyewe umeshikamana na mfumo wa kijamii, kiuchumi pia kuzuka kwa miji na utamaduni wake mpya pamoja na maisha ya kibiashara yanayowaunganisha watu kwa kiungo cha pesa, upanikanaji wa pesa umekuwa mgumu sana tena umechangiwa na hali ngumu ya maisha. Pesa imekuwa ndio kitambulicho cha kila kitu, kama huna pesa ni wazi kuwa utopata chakula, mavazi, malazi na mahitaji mengine muhimu, hivyo wasichana katika riwaya hii wako radhi kujiuza miili yao ili kupata chakula kama tuelezwavyo:
…kwa kawaida wasichana hawa hufuata kipato kama huna basi mpige bia moja, mpe
semadarina starehe yote ni yako….. (uk. 30). Mwandishi anatuambia kuwa wasichana wa siku hizi wako radhi kujiuza ili mradi wapate chakula na vinywaji, wako tayari hata kama una kipato kidogo kuwapata si kazi ngumu.
Taswira ya Unyanyaswaji wa Mwanamke
Hii ni taswira iliyotamalaki sana katika riwaya ya Shida. Shida ni msichana mdogo aliyemaliza darasa la saba. Ana sifa za ziada ukilinganishwa na wasichana wengine wa rika lake. Jina lake ni la kiishara na la picha zinazompata Shida ni ishara ya matatizo ya vijana kama Shida. Pia ni picha ya matatizo yanayotokana na harakati za vijana kutaka kuyabadili maisha yao. Kazi hii inatueleza maisha kuwa maisha mazuri yapo mjini suala ambalo hata Shida mwenyewe alitamka waziwazi pindi aliposema:
……nimezoea maisha ya fedha na starehe ….( uk. 9).
Mwandishi Balisidya anaonyesha unyanyasaji katika ngazi mbalimbali kama ulivyojitokeza katika riwaya ya Shida. Unyanyasaji huo unafanywa na wanaume ambao wanadhani wanayo mamlaka juu ya wanawake. Dhana hii imepewa nguvu zaidi na mila na
desturi zinazomfanya mwanamke asiwe na haki ya kutoa hoja zao hata katika mambo yanayomhusu. Mhusika Shida analazimishwa na baba yake aolewe na kijana ambaye si chaguo lake. Shida alitakiwa kukubali bila kutoa hoja au ushauri wowote, kama baba yake anavyotuthibitishia anapomwambia Shida kuwa:
Wanaleta mahari ukoo wa Mbukwasemwali, nasi tumeamua kupokea mahari hiyo. Sipendi ubishi utaolewa na Njasulu. Tunafanya hivi kukuokoa na janga, maadamu sasa huna kazi wala chochote, usije ukaingia uhuni ….. (uk. 3).
Baba Shida alidhani kuwa Shida atakubaliana naye, lakini Shida hakuwa tayari kuolewa. Kutokana na shurutisho hilo aliamua kuondoka huku akiazimia kufanya safari ya kuusaka uhuru wa kujiamulia mambo yanayohusu maisha yake. Shida hakukubali kunyanyaswa na mfumo dume ingawa baba yake aliona ni njia ya kumwepusha na janga la kupotea. Hapa mwandishi amempa mwanamke uwezo wa kuyakimbia matatizo sio kuitikia tu kila kitu unachoambiwa na mwanamume. Mtafiti anazua maswali kwamba: Je, tatizo hili la wanawake kulazimishwa kuolewa na mwanamume asiyemtaka limetatuliwa vipi? Je, suala la kukimbia matatizo na kuanza maisha mapya ni suluhisho? Je kuyakabili matatizo yanapokukabili sio suluhisho la kweli? Kwa hakika maswali haya na mengine yanahitaji suluhisho la utafiti huu.
Unyanyaswaji mwingine unaosawiriwa na Balisidya katika riwaya yake hiyo ni kuwa wanawake hawashirikishwi katika maamuzi mbalimbali ya kifamilia. Mathalani, mama Shida hakushirikishwa kabisa katika suala la ndoa ya binti yake. Aidha, mama Shida
alipata kipigo toka kwa mumewe baada ya binti yake kutoroka. Sababu ya mwanamke huyu kupigwa kwa upande mmoja ni kwamba, inasemekana kuwa alionekana kushiriki katika kumtorosha binti yake na kwa upande mwingine ni unyanywaswali wa kuwa mwanamke hana uwezo wa kuhimili miguvu ya mwanamume. Mwandishi anathibitisha haya asimuliapo: Huku nyumbani baba yake alipata habari, Alilaani na kugombana na mkewe hata Akampiga Sana (uk. 6).
Unyanyasaji wa wanawake unasawiriwa na mwandishi kwa kuwachora wanawake kama viumbe wanaozalishwa au kuzaa watoto kisha kutelekezwa na waume zao. Katika riwaya ya Shida, mke wa Machupa anatelekezwa kijijini ambapo Machupa anaenda jijini
kutafuta kazi. Hata baada ya kupata kazi, Machupa haijali familia yake, anamnyanyasa mke wake hatimaye anampatia talaka ati amezaa watoto wengi. Machupa anathibitisha azma yake kama inavyojitokeza asemapo: Tatizo langu……ni matoto a-a tatizo lilikuwa matoto mengi mno nikamtupilia mbali yule mama na mizigo yake ya kila siku. Angekuwa pekee yake, loo (uk. 62).
Mwanamke bado yungali ananyanyaswa, tena kwa makosa ambayo si yake. Mfano wa Machupa hapo juu anamfukuza mtoto wake kisa amezaa watoto wengi ambao hawezi kumudu kuwalea. Machupa anadai wingi wa watoto ni kosa la mkewe, naye akidhani
hakushiriki katika kuwaumba hao watoto. Huu ni uonevu mkubwa unaofanywa na wanaume kumgandamiza mwanamke. Hali hii imeshamiri hadi hii leo kwamba, mwanamke anapozaa watoto wa kike watupu, mumewe haridhiki ilhali ndiye mwenye kumwezesha mkewe kuzaa mtoto/watoto wa kiume. Vilevile mwanamke anapokosa uzazi mwanamume humwacha na kutafuta mwanamke mwingine ili afanikiwe kupata mtoto. Dhuluma hii huwadhalilisha wanawake kila iitwapo leo na bila kikomo. Kwa upande mwingine, huku kutokuwa na uhuru kwa mwanamke, na kuwafanya kuonekana kwao kama mapambo na vyombo vya starehe kunawarudisha wanawake nyuma na vilevile kunarudisha nyuma juhudi za ujenzi wa jamii. Hivyo kama mwanamke na mwanamume wote wangetumika sawa na wangekuwa bega kwa bega katika kujenga uchumi wa nchi. Vitendo kama vya Machupa vinamnyanyasa na kudhalilisha mwanamke kwa kiasi kikubwa. Wanawake wamekuwa wakiachiwa majukumu ya kuwalea na kuwatunza watoto katika familia zetu. Hii dhna inakwenda sambamba na ufeministi wa kiafrika unaotenga
majukumu kati ya mwanamume na mwanamke katika jamii. Wazazi wenzao wa kiume hudiriki kutumia kipato chao cha ziada kwenye masuala yasiyo ya msingi kama vile ulevi, ukahaba, uasherati, na kadhalika na kuziacha familia zao zikiwa na hali duni ya kiuchumi. Suala hili litashadidiwa kwa undani katika sura ifuatayo. Taswira ya Umalaya kwa Mwanamke
Taswira ya umalaya tunaipata katika Riwaya ya Shida. Mwanamke anasawiriwa akiendesha umalaya huko jijini. Matika alipofika jijini Dar es Salaam aliamua kutafuta njia muafaka za kukidhi mahitaji yake, ingawa alikuwa akifanya kazi katika baa, hakuweza kupata pesa inayokidhi mahitaji yake na ndipo alipoamua kufanya umalaya na kujikuta ana mimba bila kumtambua aliyempatia ujauzito huo. Umalaya huu unathibitishwa na maelezo ya wafanyakazi wenzake walipohojiwa na Chonya, wao walimjibu:
….kazi yetu ilivyo, mtu hawezi kujua ni nani amemnasa. Kwa kuwa Mwarabu, Mzungu, Mbantu wote huwa tunakubali ….(uk. 63).
Maelezo haya yanatushawishi tukubaliane na usawiri huu kwani unaakisi hali halisi iliyopo katika jamii yetu. Hali hii imemfanya mwandishi wa riwaya hii amsawiri mhusika wa kike katika hali ya umalaya wa kutisha ilhali ni mwandishi wa kike tulitegemea kuwa angepinga taswira hii ya kumdhalilisha mwanamke mwenzake lakini kumbe nao wapo mstari wa mbele katika kumdunisha mwanamke.
Taswira ya Wanawake ya Upendo na Huruma
Taswira ya kumchora mwanamke mtu mwenye upendo na huruma inaonekana kukubalika katika jamii. Taswira hii inajitokeza katika riwaya ya Shida, ambapo mama Upendo anachorwa kuwa na upendo na huruma kwa Chonya. Mama Upendo anamshauri Chonya juu ya maisha mema; anamshauri ajiwekee fedha benki na ajinunulie vitu vitakavyomsaidia katika maisha yake. Mwandishi anathibitisha upendo huo anapomchora mama Upendo akimweleza Chonya kuwa:
Mshahara wako hautakutosha kwa mahitaji yote ya mji huu. Ndiyo maana tumekupa chumba, chakula maji na umeme bure…. (uk. 29). Katika maelezo haya, mama Upendo anatekeleza wajibu wake wa malezi kwa vijana. Mama Upendo amesawiriwa kuwa mwenye huruma na hekima kwa sababu anamlea Chonya, pia anamwasa juu ya maisha ya jijini wakati Chonya alipoamua kuacha kazi. Mama
Upendo alimuasa Chonya akisema:
….Mji huu una anasa nyingi tena zisizo na faida. Mimi nakuonya Chonya jiwekee akiba kidogo, endelea kama ulivyoanza, usipoteze pesa yako bure ….umri wa kuoa ufikapo chagua binti asiyependa mambo ya mji usiyoyaweza mkaanze maisha pamoja….. (uk. 30).
Hapa inathibitika wazi kuwa wanawake wana jukumu kubwa la kuilea jamii yetu, hivyo Chonya anaasa katika uchaguzi wake asikosee kwani kima chake ni kidogo hivyo awe mwangalivu katika kumpata mwenza atakayempenda kama alivyo na sio kufuata pesa. Jamii ya leo mapenzi ya pesa yameshamiri sana, kuna baadhi ya wanawake wanaopenda hela kuliko utu.
|