SHAIRI: SASA NAACHA KUTUNGA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: SASA NAACHA KUTUNGA (/showthread.php?tid=1000) |
SHAIRI: SASA NAACHA KUTUNGA - MwlMaeda - 08-23-2021 SASA NAACHA KUTUNGA Ninapata majaribu, tungo hizi nikitunga, Isijenikuta taabu, mwisho munione bunga, Kuacha Kuna sababu, sitaki tena kutunga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Hunijia kikashani, maneno yao kupanga, Ati wao taabani, kunipenda mie Sanga, Hunitia kitanzini, vijana wenye kilanga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Wengine hunirubuni, kwayo mapenzi machanga, Wataka niweka ndani, kwa malizo kunihonga, Ninaye wangu mwendani, wanaume hilo chunga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Mara umekula nini, ewe mtoto wa Sanga, Wananitega jamani, ninashindwa kuwachenga, Mwisho niitwe muhuni, watu hawa kama wanga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Wengine nimebaini, wanazo nyingi faranga, Japo mie masikini, wameshindwa kunihonga, Sihongeki tambueni, jambo hili nalipinga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Wasomaji buruani, mkono wangu napunga, Na tungo hamzioni, ufundi ninaufunga, Kujitia kitanzini, ni heri ningejitenga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Huniita vipi hani, nami waweza nitunga? Nikutunge kitu gani, wewe umekuwa shanga? Maneno ya kidizaini, watu hawa hunilenga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Sasa nipo kataani, mwisho wa tungo nagonga, Hata wangenipa nini, bilingani au kanga, Nadanganya, jaribuni, katu siwezi kutanga, Tatizo ni wanaume, wananitaka mtunzi. Mtunzi Filieda Sanga MAMA B Mabibo Dsm 0753738704 |