MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - KORASI NA UHUSIANO WAKE NA SANAA ZA MAONYESHO

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: KORASI NA UHUSIANO WAKE NA SANAA ZA MAONYESHO
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
Kioo cha Lugha
Juzuu 1, Na. 2 (1995)
KORASI NA UHUSIANO WAKE NA SANAA ZA MAONYESHO
Uchambuzi wa Kidayakronia
Aldin Kai. Mutembei
Utangulizi
Makala haya yanachambua kipengele muhimu katika sanaa kiitwacho korasi. Uchambuzi huu umegawanyika katika sehemu kuu tatu: kwanza, tutaangalia maana mbalimbali zinazojaribu kuielezea korasi. Katika kufanya hivyo tutaangalia pia udhaifu au uyakinifu wa kila maana hizo. Sehemu ya pili itaangalia chimbuko la korasi. Katika sehemu hii mjadala utazingatia zaidi mabadiliko katika jamii na hasa jinsi ambavyo mabadiliko hayo yaliiathiri korasi. Mabadiliko katika jamii yalileta mabadiliko katika korasi, hivyo korasi ikawa na maudhui na fani tofauti tofauti kutegemeana na jamii ilivyobadilika. Katika sehemu ya tatu mjadala utaangalia japo kwa kifupi uhusiano wa korasi na sanaa za maonyesho. Hapa tutachambua dhima ya korasi katika sanaa za maonyesho na katika jamii kwa ujumla. Tutahitimisha uchambuzi wetu kwa kutoa muhtasari wa mjadala mzima na kuacha maswali yanayoweza kujibiwa katika makala nyingine na utafiti mwingine zaidi ya huu.
Makala haya yanachukua mkabala wa kidayakronia katika uhakiki wa kifasihi. Mkabala huu huichunguza dhana fulani tokea katika maalumu na kuangalia mabadiliko yake katika vipindi mbalimbali vya kihistoria. Mkabala wa kidayakronia utatusaidia kuielewa korasi ambayo imekuwa na mabadiliko ya msingi kifani na kimaudhui. Makala haya yanatoa mchango katika uwanja wa Fasihi ikionyesha kuwa baadhi ya vipengele havina budi kuangaliwa upya na kupewa umuhimu wake.
Maana ya korasi
Baadhi ya wanafasihi wameitumia dhana hii wakiwa na maana ya “kiitikio”. Maana hii ni finyu mno kwa kuwa imezingatia aina moja tu ya korasi. Aidha kwa kuifafanua hivyo maana hii inaonyesha kuwa kipengele hicho hakiwezi kutokea katika tanzu nyingine za Fasihi ambazo si ushairi. Wengine wameiita mkarara. Hawa nao kama wale wa mwanzo wameangalia zaidi fani. Wameiangalia dhana hii kwa ufinyu na kuiondolea matawi yake mapana yanayogusa zaidi masuala ya utamaduni mila na desturi katika jamii. Wakaiita dhana hii ‘mkarara’ kwa maana ya kukariri au kurudia rudia. Ingawa ni kweli kuwa hii ni aina mojawapo ya korasi lakini si maana yake. Ndani ya maana hizi mbili vipengele muhimu vinavyoiunda korasi havionekani. Hatuoni utamaduni, mila wala desturi. Hatuoni dhima ya korasi katika jamii wala hakuna suala la imani katika istilahi hizo mbili. Kwa hiyo maana hizi hazikidhi haja ya dhana tunayoielezea hapa kama korasi. Korasi ni dhana changamano. Ni kiini cha sanaa za maonyesho hasa tamthiliya za kimagharibi. Katika makala haya inapendekezwa kuwa istilahi inayoweza kukidhi dhana pana ya jambo tunalolizungumzia iwe ni korasi.
Neno korasi tunalitohoa kutoka kwenye Kiingereza chorus. Waingereza pia walilichukua kutoka kwa Kilatini chorus. Hali kadhalika Walatini walilitohoa kutoka kwa Kiyunani xopos (choros).
Simpson na Weiner wanaielezea korasi kuwa ni ‘Kikundi cha waimbaji na wachezaji katika sherehe za kidini na sanaa za maonyesho za Uyunani ya kale (Tafsiri yangu). Hapa msisitizo unawekwa katika uimbaji na uchezaji. Kwanini? Waandishi wa Kamusi ya Webster wanalifananisha neno hili korasi na neno la Kilithuania zaras lenye maana ya kisababishi (course). Ufafanuzi zaidi umetolewa na waandishi wa Encyclopaedia Americana ambao wanasema:
Kwa kuwa katika Uyunani ya kale uchezaji ulikuwa, karibu wakati wote, ukiendana na uimbaji, basi [korasi] ilikuja julikana kama kundi la waimbaji na wachezaji wa utungo fulani. (Tafsiri yangu).
Hawa, wanaona kuwa kutokana na neno la Kiyunani Xopos linalomaanisha mahali pa kuchezea, wahusika katika kundi hili ndio waliosababisha tukio zima. Walikuwa washiriki na wahusika. Hivyo wakatoa maana ya korasi kuwa ni ‘Kundi ambalo lilihusika katika mchezo au kutoa maelezo kuhusiana na tendo. Waandishi wengine wa kamusi ya Webster toleo la pili, hawashikilii uimbaji tu bali wanaongezea kipengele kingine muhimu, kipengele cha maongezi. Wanasema:
(korasi), ni kikundi cha waimbaji au waongeaji (chanters). Dhima yake ilibadilika badilika, ilikuwa ni ile ya wahusika katika kitendo na wafasiri wa kitendo (Tafsiri yangu)
Katika kuipanua dhana hii, korasi ilikuwa na kutokeza tanzia. Hapo korasi ilikuwa imepata dhana pana zaidi. Sasa ilikuwa ni:
Watazamaji wenye usikitivu kuhusiana na yale yawapatayo wahusika katika mchezo, huku wakionyesha kwa maneno au vitendo kuguswa kwao baina ya vitendo vya wahusika, kuhusiana na mambo ya kimaadili na kidini ambayo hutolewa au kuonyeshwa na vitendo katika mchezo (Tafsiri yangu).
Jambo tunaloliona hapa ni kuwa dhana ya korasi inaingiza pia suala la hisi za watu. Tunaona kuwa, kutoka kuwa jamii nzima, kisha wahusika kadhaa katika mchezo, korasi pia iliweza kuwa ni hadhira nzima. Browne anatupeleka hatua zaidi mbele anapoiangalia korasi ki-historia kuwa:
Kihistoria, korasi ilikuwepo kabla ya michezo ya kuigiza ambayo ilitokana nayo, na kwa hakika korasi inatakiwa ibakie kama ilivyokuwa mwanzoni yaani kundi lililoteuliwa kuisemea jamii nzima (Tafsiri yangu)
Huyu ameligusia suala la chimbuko la sanaa za maonyesho ambazo ni maigizo. Jambo ambalo uhusiano wake na korasi utaangaliwa katika sehemu ya tatu ya mjadala huu. Lakini jambo muhimu ni uwakilishwaji wa jamii uliofanywa na watu wachache wateuliwa.
Kutokana na tafsiri hizi zote, na kwa mujibu wa hatua mbalimbali za korasi, makala haya yanaifafanua korasi kuwa ni:
Matendo au maneno ya kisanaa ayatoayo mtu mmoja au zaidi katika kitendo cha kisanaa au kuhusiana na kitendo hicho cha kisanaa ambapo hadhira hushirikishwa au hufanywa ifikirie undani wa kitendo au maneno hayo jinsi ambavyo isingelifanya kama ingelikuwa vinginevyo. Maneno hayo hutolewa kwa njia ya uimbaji au nathari. Tena, matendo yaweza kuambatana na maneno au yakawa peke yake na hivyo kutokeza utendaji bubu (miming)
Historia ya korasi
Chimbuko la korasi
Hatuwezi kugusia historia ya korasi tukaacha kuzungumzia sanaa za maonyesho. Aidha haiyumkiniki kuongelea juu ya korasi bila kuongelea habari za Wayunani. Lakini inawezekana kabisa kuwa dhana hii ilipatikana pia katika mataifa mengine. Jambo la kuwepo kwa korasi katika mataifa mengine litabakia kuwa swali mwishoni mwa sehemu ya tatu.
Baadhi ya waandishi kama vile G. Thomson O.G. Brockett .W.P. Cambridge, Oates na O’neil, jr na wengineo wanashikilia kuwa korasi ilitoka kwa Wayunani. Hii ilikuwa zamani za karne ya nane hadi ya tano kabla ya Kristo. Korasi ilitokana na jamii na ilikuwa jamii. Kila mtu alikuwa ni sehemu ya korasi hapo mwanzoni. Ikumbukwe kuwa wakati wa ujima, umoja na ushirikiano katika kazi yalikuwa ni mambo ya lazima yaliyofanya jamii izidi kuwapo na istawi. Korasi kama kipengele kimojawapo muhimu cha kazi kiliwahusisha watu wote.
Mwanzoni korasi ilikuwemo katika shughuli pana iliyoitwa “dithirambu” (dithyramb)). Shughuli hii au tendo hili lilifanyika kwa njia ya uimbaji wa sauti moja, leng kuu likiwa ni kutambika na/au kutoa zaka kwa mungu wa Wayunani aliyeitwa Dionysus. Katika matambiko haya yaliyofanywa na watu wote, kundi la wanawake lilijitokeza na kuongoza uimbaji huu, wengine wakafuatia huku kutambika kukiendelea. Arion ndiye anayejulikana kuwa mtu wa kwanza hapo Korintho, kuifanya korasi ushairi utakaodumu. Wakati huu bado ilikuwa katika muundo uleule wa uimbaji. Aeschylus alifanya mabadiliko ya msingi katika shughuli ya utambikaji na kuipa korasi nguvu zaidi, kama tutakavyoona baadaye. Korasi ikawa pana na kuenea Uyunani nzima. Kwa hiyo, korasi ilianza kama kundi la waimbaji likisindikiza na kuhusika katika shughuli ya utambikaji. Shughuli hii ilifanywa na vikundi vya wanawake vilivyoitwa thiasos.
Mabadiliko katika korasi
Jamii ilizidi kukua. Maendeleo katika sayansi na teknolojia yalisababisha uwepo ubora wa vitendea kazi. Kutokea mgawanyiko wa kazi na uhusiano katika uzalishaji mali ukawa chanzo cha vijitabaka. Mabadiliko haya yaliuingilia umoja na ushirika wa kale. Nguvu ya mwanamke aliyokuwa nayo pale mwanzoni kutokana na dhima yake katika Dithirambu ikawa inafifia. Hadi yake ikashuka kwa kuwa sasa vifaa vilitumika kutoa milio kuita watu. Vikundi vya kinamama thiasos vikawa vinapungua na mahali pengine kufifia kabisa.
Dhima ya Dithirambu ikabadilika. Kutoka kuwa uimbaji uendao na shughuli ya matambiko, zikawa ni nyimbo kuhusu visa-asili. Ikachukua umbo la kisanaa zaidi na mwigo (imitation) ukachukua nafasi zaidi na zaidi. Katika kufanya hivi, kukatokea badiliko jingine ambapo Arion aliweka mazungumzo au maneno katikati ya nyimbo hizi. Hivyo korasi ikawa ina sehemu ya nyimbo, mazungumzo na uigizaji bubu. Hapa, bado watu wengi walihusika ingawa Dithirambu sasa ilikuwa imechukua sura mpya. Katika badiliko kuu la msingi kuhusiana na korasi, hatuwezi kukosa kumzungumzia Thespis. Huyu aliishi baada ya Arion. Na kwa kumwingiza mwigizaji mmoja katika korasi alipelekea mwanzo wa korasi ya kale kubadilika na kuwa sanaa ya maigizo pengine ikiitwa michezo ya kuigiza. Nagler anamsifu Thespis hivi:
Mtu mwenye akili nyingi aliyewezesha mabadiliko kutoka kwenye umbo la ki ‘ Dithirambu’ kwenda kwenye ‘drama’ alikuwa Thespis wa Icaria. Mwandishi wa michezo ya kuigiza, mwigizaji, Mkurugenzi jukwani na mtoaji michezo (producer). Yeye pia anasemekana kuihusisha korasi katika msuko wa matukio (Tafsiri yangu)
Mhusika aliyeingizwa na Thespis, aliigiza kama Mungu, akijibu maswali au kuuliza kuhusiana na yale yaliyosemwa na watu wengine kwenye onyesho. Huu kwa hakika ulikuwa mwanzo wa kupandwa mbegu ya sanaa za kitanzia. Kuhusiana na hili Aristotle anasema:
Sanaa ya kitanzia ilichomoza kutoka katika viongozi wa Dithirambu.
Kama utanzu wa Fasihi katika uchanga wake Dithirambu ilikuwa na watu mia tano, waliojigawa katika vikundi vya watu hamsini hamsini. Vikosi hivi ndivyo korasi kama ilivyokwisha elezwa. Katika makundi haya, mhusika mmoja (muigizaji) alijitokeza akiuliza jambo, akitoa ushuhuda fulani, akichokoza hoja au akipinga maamuzi ya tabaka tawala kwa njia ya kisanaa. Kwa kufanya hivi, vile vikosi vya korasi vilijibu hoja za mhusika kwa nyimbo na maelezo huku zumari na filimbi zikipigwa. Baada ya Thespis, Aeschylus (525-456 BC) aliongeza mhusika wa pili katika michezo yake. Baadaye Sophocles (497-406 BC) aliongeza mhusika wa tatu. Wahusika walikuwa wakiongezeka na kupungua kadri ya mahitaji ya sanaa ya jamii. Katika maendeleo haya, korasi ilikuwa imeathirika kuwili: kwanza umuhimu wake, kama shughuli ya kiibada ulikuwa umepungua sana. Sasa ilikuwa ni ‘mchezo wa kuigiza’ ingawa ndani ya igizo hili mambo muhimu yalitolewa kuifundisha jamii. Pili, idadi ya watendaji katika korasi ilipungua mno. Wale waigizaji watatu walitoa ujumbe na kuonyesha sanaa vizuri zaidi kuliko kundi kubwa. Hapa wahusika – waigizaji (actors) wakawa wanaongezeka huku watendaji (nyimbo au mazungumzo) wakipungua mno.
Uhusiano wa korasi na Sanaa za maonyesho – Tamthiliya
Korasi iliingizwa katika tamthiliya kama muundo, kama mtindo na baadaye kabisa kama mhusika. Sophocles katika tamthiliya zake kama vile Mfalme Edipode, Ajax na Antigone aliongeza namba ya wahusika (waigizaji) kufikia kumi na watano. Wahusika hawa walipunguza kabisa umuhimu wa korasi, kiasi kwamba korasi sasa ilikuwa ni vikundi vya watu wachache walioingia mchezoni mara chache chache. Hapa tunaiona korasi kama muundo. Waliingia mwanzoni au katikati au kila mwanzo wa onyesho; wala hapa haikuwa ni lazima. Nafasi ya korasi ilikuwa imebadilika kabisa! Freedley na Reeves wanasema:
Hadi kufikia wakati huo, korasi haikuwa na umuhimu mkubwa katika tendo la kisanaa. Kwa mtazamo wake haikuhusishwa moka kwa moja na maigizo, bali ilibakia kuwa ni mtu mmoja kitu cha kusaidia waigizaji walioko jukwaani.
Sophocles alianzisha majibizano baina ya wahusika wake katika tamthiliya, ambapo hapa na pale aliweka korasi ambayo sasa ilibeba dhima tofauti na umbo tofauti. Jambo muhimu pia ni kuwa idadi ya korasi ilipungua sana. Sasa haikuwa lazima liwe ni kundi kubwa. Aliweza kuwa ni mtu mmoja au zaidi akitoa maelezo kuhusu onyesho, akiiuliza hadhira kuhusiana na onyesho au akiunganisha onyesho moja na jingine wakati wahusika wanabadilisha mavazi nyuma ya jukwaa au penginepo.
Katika kuangalia pia uhusiano wa korasi na tamthiliya hatuna budi kugusia nadharia ya mfarakisho (alienation) iliyoendelezwa sana na Brecht. Hili lilikuwa ni badiliko la msingi katika korasi. Nadharia hii inawatenga kwa muda watazamaji (hadhira) na ile tamthiliya waitazamayo, huku ikiwaandaa kuwa watazamaji washiriki. Inawaondoa katika ule mtiririko wa maonyesho unaowazuga watazamaji, na inafanya hivi kwa lengo maalumu. Lengo hili linafanywa na korasi, pale mtu mmoja au zaidi anapoingia ghafla mahali fulani maalumu katika tamthiliya ili kuionyesha hadhira uhalisia na uyakinifu wa tendo linaloigizwa jukwaani kama mchezo tu. Lakini hadhira ione uhalisi zaidi kuliko maisha ya kawaida, kuliko jinsi ambavyo ingelifikiriwa. Na kama ni jambo nyeti, basi ionekane kama mchezo au mzaha tu korasi ilikuwa imepata mawanda mapana na dhima zake zilikuwa bayana katika tamthiliya. Dhima za korasi zimeorodheshwa na Brockett katika andiko lake kuhusu tamthiliya. Anasema:
  1. Alikuwa ni mhusika katika mchezo akitoa ushauri, akitoa maoni, akiuliza maswali na wakati mwingine akiwa kama mtendaji wa mara kwa mara katika mchezo. (Tafsiri hii na zinazofuata hapa chini ni zangu).
  2. Mara nyingi korasi ilikuwa muhimili wa matukio ya kijamii na kimaadili na iliweka vigezo ambavyo kwavyo mchezo uliweza kupimwa.
  3. Mara kwa mara korasi ilichukuwa nafasi ya mtazamaji kama wa mawazoni tu ambaye huibuka akaongea juu ya matukio au juu ya waigizaji kwa kadri msanii atazamiavyo hadhira itende.
  4. Korasi ilisaidia kuumba mazingira ya mchezo kwa ujumla na yale ya kila onyesho na hata kukuza athari za tamthiliya ionyeshwayo.
  5. Korasi huongeza miondoko, nyimbo, ngoma na ukubwa wa wahusika katika tendo na hivyo kuchangia sana katika ukamilifu wa tamthiliya.
  6. Hufanya kazi ya ridhimu ikitokeza mapumziko na utendaji wa pole pole wa matukio na katika kufanya hivi huipa nafasi hadhira ijitathmini ikiangalia yale yaliyotokea na kufikiria yajayo.
Katika dhima hizi sita, Brockett anatuonesha kuwa kwa hakika korasi ni pan asana. Inaweza kuangaliwa kama mhusika mmoja au wengi katika sanaa za maonyesho. Inaweza pia kuangaliwa kama tukio au matukio yanayojirudia rudia katika onyesho moja au zaidi. Tena korasi inaweza kuangaliwa kama wimbo au sauti tu inayotokea mara kwa mara ikimrudisha nyuma mtazamaji au ikimpeleka mbele ya tukio au hata ikimtolea ujumbe ambao haukuonyeshwa wala hautaonyeshwa na wafanyao maonyesho hayo. Dhima ya saba ya korasi imezungumziwa sana na Brecht ingawa kwa hakika sio yeye aliyeibuni. Dhima hii tumekwisha kuieleza hapa juu kuwa ni ile ifanyayo kazi ya ufarakisho au mtengo. Yaani matukio au mawazo fulani katika onyesho huwekwa na yakaonekana sio ya kawaida au hayakutazamiwa na hivyo kuutenga mchezo au onyesho kutoka katika mtiririko wake. Kujitenga huku hufanya mtazamaji makini afikirie zaidi maana ya onyesho kwa ujumla.
Kwa hakika korasi ni kiungo muhimu sana kati ya tamthiliya na hadhira. Ni kipengele kilichojitokeza kutokea katika ibada za Kiyunani na matambiko kwa miungu wao na hata kuwa suala la kisanaa. Inajitokeza kama mhusika, kama muundo lakini zaidi kama mtindo katika tamthiliya ambao hauwezi kuepukika. Dhana hii ya korasi imetumiwa pia na wasanii wa tamthiliya za Kiafrika hasa Ibrahim Hussein na Penina Muhando. Lakini je dhana hii ni ya Kiafrika?
Marejeleo
Brecht, B. Plays Vol. 1, (1960) Methuen and Co. Ltd London
Brockett, O.G. History of the theatre, sixth edition, (1991) Allyn and Bacon. Boston
Browne, E.M. The Making of  T.S. Eliot’s plays, (1969), Cambridge University Press. Cambridge.
Cambridge, A.W.P. The theatre of Dionysus in Athens, (1956) Oxford University Press, London.
Fredly, G. na Reeves, J. A. A history of the theatre (1968), Crown Publishers, Inc.N.Y.
Hartnoll, P. (mh) The Oxford Companion to the theatre, third edition,(1967), Oxford University Press, London.
Lihamba, A. Politics and theatre in Tanzania After Arusha Declaration 1967-1984, Unpublished Ph.D Thesis (1985) University of Leeds.
Muhando, P. Tanzanian traditional theatre as a pedagogical Institution: The Kaguru case study. Unpublished Ph.D thesis (1983) University of Dar es Salaam.
Muhando, P na Balisidya, N. Fasihi na Sanaa za Maonyesho, (1976), Tanzania Publishing House, Dar es Salaam.
Nagler, A.M. A source book in theatrical history, (1952) Dover Publishers, Inc. N.Y.
Oates W.J. na O’neill, E.jr. (Wah). The Complete greek drama Vol.1 (1938), Random House; N.Y.
Smith, C.H. T.S. Eliot’s dramatic theory and practice (1963), Princetown University Press, New Jersey.
Thomson, G. Aeschylus and Athens, (1973), Lawrence and Wishart, London.
Willet, J. (Mh). Brecht on theatre, (1977), Hill and Wang New York.
Weisstein, U. Comperative Literature and Literary theory (1973), Indiana University Press Bloomington.
Kamusi na insaiklopedia
Encyclopedia Americana, Intaernational edition, Vol 6 (1980) Grolier Incoporated, Connecticut.
Simpson J. A na Weiner E.S.C. The Oxford English Dictionary. Second edition Vol. 3 (1979) London.
Webster’s New International Dictionary, Second edition (1961), Merrian Webster Inc. Springfield.
Webster’s Third New International Dictionary, (1986), Merrian Webster Inc. Springfield.