MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - ETIMOLOJIA YA NENO 'ARUBAINI'

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: ETIMOLOJIA YA NENO 'ARUBAINI'
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'ARUBAINI'

Neno arubaini  katika lugha ya Kiswahili ni Nomino [Ngeli: i-/zi-] yenye maana zifuatazo:

1. Kumi mara nne; makumi manne.

2. Siku ya arubaini baada ya mwanamke kujifungua.

3. Kumbukumbu inayofanywa siku ya arubaini  toka mtu kufariki Dunia kulingana na itikadi za kimadhehebu au kimila. 

4. Kipindi cha uhuishwaji, kupewa nguvu mpya na ukombozi kunakofanywa kwa siku arubaini za kujitakasa katika madhehebu ya Kikristo.

Neno arubaini limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu arbauun ( soma: arbauuna/arbaiina  اربعون/اربعين)  neno lenye maana ya idadi inayoundwa na makumi manne.

Kinachodhihiri ni kuwa neno la Kiarabu  arbauun اربعون lilipoingia  katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno arubaini halikubadili maana yake katika lugha asili - Kiarabu bali lilibeba maana mpya zinazohusiana na mila, desturi na itikadi wakati wa kujifungua  mwanamke, kufa mtu na kipindi cha uhuishwaji katika imani ya Kikristo.

TANBIHI:
Katika Uislamu neno arubaini hususan siku arubaini huhusishwa na mchakato wa makuzi ya mimba toka kutungwa hadi kupuliziwa roho.
Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ameuelezea mchakato huu wa makuzi ya mimba katika Hadith kutoka kwa Swahaba Abuu Abdir-Rahmaan Abdillaah bin Mas-uud (Allaah Amridhie) ambaye amesema: “Ametusimulia Mjumbe wa Allaah (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arobaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arobaini zijazo huwa ni donge la damu, kisha arobaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake). Na huamrishwa mambo manne; kuandika riziki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, na (ni) mtu muovu au mwema. Wallaahi! Naapa kwa Yule Ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa Peponi hadi ikawa baina yake na Pepo ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali za watu wa motoni na akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali za watu wa Peponi akaingia Peponi." (Hadith hii inapatikana katika vitabu cha Hadith za Mtume Muhammad viitwavyo Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim).

Shukran sana.

Khamis S.M. Mataka.