MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - ETIMOLOJIA YA NENO 'AKILI''

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: ETIMOLOJIA YA NENO 'AKILI''
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO 'AKILI''

Neno akili  katika lugha ya Kiswahili ni Nomino [Ngeli: i-/zi-] yenye maana zifuatazo:

1. Uwezo wa ubongo wa kiumbe kuhisi, kufikiri, kuamua, kutambua, kutamka na kufanya mambo inavyotakiwa; uwezo wa mtu wa kujua kitu au jambo, -enye akili hodari, -enye akili timamu -sio na wazimu.

2. Wepesi, ubora na uhodari katika kufikiri na kutenda mambo.

3. Mbinu au mpango wa kufanikisha au kutatua jambo linalotatiza.

Methali:
Akili ni nywele kila mtu ana zake : watu hawafanani katika maarifa.

Nahau:
Rukwa na akili: potea akili, pata kichaa.

Misemo:
1. Fanya akili: Tumia maarifa katika kutatua jambo linalotatiza.

2. Hana akili: hana maarifa ya kutatua jambo linalotatiza.

Neno akili limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu 'aqlu ( soma: 'aqlun/'aqlan/'aqlin عقل)  ambalo ni nomino yenye maana ya uwezo wa kufikiri, kujenga hoja na kupanga ya kufikirika na kusadikika; uwezo wa kutofautisha kizuri na kibaya, heri na shari, haki na batili.

Maana zingine za neno aqlun عقل katika lugha ya Kiarabu ni hizi zifuatazo:

1. Moyo.

2. Fidia aliipayo muuaji kwa familia ya aliyeuawa; diya.

3. Ulinzi, hifadhi, ngome.

4. Mahali pa kukimbilia kupata hifadhi na usalama.

5. Kivuli cha wakati wa mchana.

Kinachodhihiri ni kuwa ne la Kiarabu  'aqlun عقل lilipoingia  katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno akili lilichukua maana ya uwezo wa mtu wa kujua kitu au jambo, kuacha maana zingine katika lugha ya Kiarabu na kulipa maana mpya ya wepesi, ubora na uhodari katika kufikiri na kutenda mambo na maana ya mbinu au mpango wa kufanikisha au kutatua jambo linalotatiza.

TANBIHI:
Waarabu wamemuita mwanadamu jina la hayawaanun 'aaqilun حيوان عاقل mnyama mwenye akili kwa kuamini kuwa ni mwanadamu pekee ambaye kibailojia yuko sawa na wanyama wengine lakini anatofautiana nao kwa kuwa ni yeye tu ndiye mwenye akili.

Shukran sana.

Khamis S.M. Mataka.