MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - KISWAHILI BIDHAA KUBWA DUNIANI

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: KISWAHILI BIDHAA KUBWA DUNIANI
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
[attachment=872]

KISWAHILI BIDHAA KUBWA DUNIANI

Watanzania wana rasilimali adhimu

Gazeti la Alhuda Alhamisi  Februari 3, 2022 linaandika kwamba:

Kiswahili ni bidhaa yenye thamani kubwa inayohitaji kuthaminiwa ili iipatie nchi tija na kueneza mila na tabia zake za kiungwana kwa wengine nje ya nchi.

Aidha bidhaa hiyo haina budi kuuzwa na wamiliki wenyewe ili sanjari na kupata faida wafunze matumizi, miiko na mila zake ili lugha hiyo iathiri tabia zake kwa watumiaji hasa wageni.

Hayo yamesemwa na Nguli wa Kiswahili Profesa Tigiti Mnyagatwa Sengo akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Manzese jijini Dar es Salaam.

“Mimi siafiki kuwa Tanzania tuna makabila 120, ni zaidi ya hapo, lakini Kiswahili kimeweza kuchomoza na kuathiri maisha ya watanzania wote, lazima tukubali tuna tofauti kihulka na kimienendo kulingana na makabila yetu, wako wakali walio tayari hata kutoa uhai wa wengine na wako wengineo, lakini wote hao wamejikuta wakidhibitiwa na mila na tabia zinazotokana na lugha ya Kiswahili katika kuamiliana kijamii ambako kumeleta Amani na utulivu usiopatikana Taifa lingine  Afrika na sehemu kubwa ya dunia”, amesema Profesa Sengo.

Amewataka watanzania waichukulie lugha ya kiswahili kama neema inayopaswa kushukuriwa kwa kumtukuza mwenye lugha yake, Mwenyezi Munga Muumbaji ambaye hakuwajalia wengine ila waishio kipande hiki cha dunia kinachoitwa Tanzania.

“Tunasikia yanayoendelea kwa majirani zetu na nchi nyingine, tujaribu kulinganisha na hali iliyopo nchini, kama isingelikuwa mila na dasturi zinazoedana na lugha yetu adhimu ya kiswahili, hapa penye makabila zaidi ya 120 hali ingekuwa mbaya zaidi”, amekumbusha Profesa Sengo ambaye ni mmoja wanafunzi Waalimu walioasisi idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwanzoni mwa miaka 1970.

Profesa Sengo ambaye kabla ya kustaafu amefundisha Vyuo vikuu kadhaa ndani na nje ya nchi  amewaasa Watanzania na hasa vijana kuzungumza lugha yao kama inavyotakiwa kuzungumzwa badala ya kuchanganya lugha yao na ama lugha nyingine kwa namna isiyoakisi ufahamu au kutumia maneno yasiyozalikana nayo.

“Ninakerwa ninaposikia neno ‘Mtalaa’ linatamkwa ‘mtaala’, neno ‘hakunaga’, ni budi na uwekaji wa ‘R’ kwahala kwa ‘L’ na kinyume chake, neno Mrabaha kutamkwa mrahaba, hatujui hata neno umilisi(fluency) badala yake tunatohoa neno la kigeni bila sababu za msingi”, ametahadharisha Profesa Sengo.

Amesema zama za RTD, uhariri na matumizi ya lugha uliwezesha Kiswahili kuenea na kuathiri watumiaji wa lugha nyingine, badala yake kukosekana kwa umakini huo hivi sasa kumehatarisha hadhi  na nafasi ya lugha hiyo miongoni mwa watumiaji hasa wageni.

“Tujitahidi kuzungumza Kiswahili na kukifunza kitaalamu kwa kuzingatia asili na jadi ya lugha hiyo ili kizungumzwe na kuambukiza tabia na miiko yake kwamba mtu akiweza kuzungumza Kiswahili aondokane na tabia za ukakasi zinatokana na lugha yake mama”, ameasa.

Amesema kwenye Kiswahili kuna maneno ‘naomba’, tafadhali, upole, uungwana na ukarimu hata kwenye kuuza na kununua, hata kwenye magomvi na mivutano kuna aina ya maneno yanayotumika yanayosuluhisha magomvi kimya kimya, lakini pia kuna masuala ya utani baina ya makabila yaliyosigana na kupigana huko nyuma.
Kwa ajili hiyo amewaasa watanzania na hasa wizara husika ya Sanaa na Utamaduni kuhakikisha fursa ya kukifunza Kiswahili na tabia zake nje ya nchi itumiwe vema ili iweze kunufaisha Tanzania kiuchumi na kijamii kwa mataifa ya kigeni badala ya fursa hiyo kubebwa na wengine wasio na asili nacho kwa tamaa ya chumo peke yake.

Hata hivyo Profesa Sengo ameshauri kuwa Wizara ya Utamaduni ingewekwa peke yake kwa kuwa ndiyo Wizara mama iliyozaa Elimu ikikusanya mila, jadi, dasturi, Miiko na Imani za Watanzania zinazohitaji miongozo maalum na umakini mkubwa badala ya kuchanganywa na Sanaa na michezo na hasa mpira wa miguu ambao umebeba utendaji mkubwa wa wizara hiyo.
Profesa Sengo amesifu upenzi wa Simba na Yanga nao umesaidia sana kukuza lugha ya Kiswahili ambapo amefichua matangazo ya RTD ya mpira wa Yanga na Simba zama hizo yalisikilizwa nchi nzima na kwamba lugha iliyotumika ni Kiswahili.