MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.

JIFUNZE KISWAHILI - SHAIRI: MWANANGU MUME KAHAWA

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: SHAIRI: MWANANGU MUME KAHAWA
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
Mwana kalia kigoda, kabla ya ndoa kupita,
Keti sipoteze muda, muda mwanangu ukuta,
Nikufunze yalo ada, kesho usije kujuta,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Nianze kukupongeza, kupata ubavu wako,
Shukuru sana Muweza, uswalipo swala zako,
Kila pande kaangaza, ela kavutika kwako.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Mume usije mkwaza, wakanye rafiki zako,
Yao na iwe baraza, wasijue chumba chako,
Maneno mkimaliza, rejea chumbani mwako.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Unapotoka nyumbani, kichwa usiwache wazi,
Iwe waenda sokoni, au kuona wazazi,
Inamisha macho chini, simkere mkumbazi.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Sitoke bila kuaga, mwanangu ninakujuza,
Iwe homa yanipiga, au niko kwa jeneza,
Uanze simu kupiga, mumeo kumueleza,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Hodi hodi vijumbani, kama vile paparazi,
Tuli msubiri hani, lala kama huna kazi,
Kushinda kwa majirani, tamkera laazizi,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Usilete ushindani, kwa mume nakuusia,
Msikize wa ubani, kila anokuambia,
Lilo kinyume na dini, kukataa si hatia.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Akikwita itikia, rabeka mpenzi wangu,
Sauti ya kubania, na jicho lako la kungu,
Haraka asije chukia, siku uione chungu,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Siwate dada wa kazi, mumeo kumpikia,
Sawa azikune nazi, na nyama kukukatia,
Ila kuunga mchuzi, sipende kumuachia,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Ukae pembeni yake, anapokula chakula,
Kumlisha usichoke, ugali na amarula,
Mume asiwe mpweke, akatafuta badala.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa

Ugomvi mwishowe ndani, nje wasije sikia,
Usijaribu asilani, ya ndani kusimulia,
Huo ni uhayawani, sidhani nakutania,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Mume ana hadhi yake, hivyo ataka adabu,
Akiwa na jekejeke, sema naye taratibu
Akitishia mateke, kunywa maji simjibu,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Kwa mume kuna furaha, nisiyoweza kukupa,
Ela yapo ya karaha, kuzidi yaliyo hapa,
Nisemayo si mzaha, wa kibogoyo na fupa.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Kuna jambo ulishike, kama wataka thawabu,
Pepo utapata kwake, kwa huyo wako muhibu,
Ukitaka radhi zake, usende kumpa tabu.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Baada jua kutuwa, mwana usende mahala,
Vyovyote itavyokuwa, uwe wa mwisho kulala,
Rauka kama wajuwa, kazi baada ya swala.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Siri sito ifukia, nilonayo kwa mtima,
Ingawa nafurahia, kwa mbali moyo wachoma,
Leo zijue hisia, hisia za wako mama,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Furaha kuoza mwana, mwanangu nakuambia,
Ila ukiwaza sana, majonzi waniachia,
Kule kutegemeana, hivi ndivyo kwaishia,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Najiona nimechacha, sijiwezi kwa huzuni,
Weye ndio wangu pacha, nikiwepo shughulini,
Jembe langu laniwacha, lenda kwa wake ayuni,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Nenda kalete mchicha, alafu wende dukani,
Kisha katupe machicha, usafishe na mezani,
Usiku waenda kucha, niko mwenyewe nyumbani.
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.

Ishirini nimegota, nafunga wangu uneni,
Neno moja nimewata, mwanangu kuna ukweni,
Utaenda kuwakuta, wapende toka moyoni,
Ile chungu ndio tamu, mwanangu mume kahawa.