JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: USHAIRI: NADHARIA NA TAHAKIKI (12)
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
11. Shaaban Robert: Kielelezo cha Fasili
SURA YA KUMI NA MOJA
Katika Kielezo cha Fasili, Shaaban Robert kwanza kabisa katutolea nadharia yake ihusuyo fasili na ufafanuzi wa mashairi. Ufasili, katwambia, waweza kufanywa kwa njia kuu mbili: sabilia na sisisi. Twaelezwa kuwa wakati sabilia huhusu fasili kwa ujumla, sisisi hushughulilda vipengele mbalimbali vya kazi inayofasiliwa.
Katika kitabu hiki basi, mwandishi kafasili mashairi yake mwenyewe, akayapa maana alizozikusudia alipoyaandika. Jambo hili limembana msomaji au mhakiki wa mashairi haya kwa kutoachiwa uhuru wa kutoa maana natafsiri imjiayo mawazoni mwake. Hata hivyo, kwa wale ambao ndio kwanza wanauingia ulimwengu wa ufafanuzi wa mashairi, huenda kazi aliyoifanya Sbaaban Robert ikawa ya manufaa kwa kuanzia.
Kwa kifupi, maelezo ya Shaaban Robert yanamwelekeza msomaji wa mashairi kujiuliza na kujaribu kuyajibu maswali kadhaa muhimu baada ya kusoma shairi. Kati ya hayo, mengi yanahusu kiini cha shairi, yaaai mfuatano wa fikra za mshairi hadi kufikia hitimisho fulani. Kwa hiyo basi, kadri msomaji anavyoendelea kusoma shairi hujiuliza kama mshairi anataka kusema nini, na hicho atakacho kukisema anakisemaje.
Baada ya kujiuliza haya, msomaji sasa yuko tayari kulichambua shairi. Katika ukurasa wa (xix) wa Kielelezo Cha Fasili, Shaaban Robert katoa maonyo kadhaa kuhusu namna ya kufasili, yaani jinsi ya kusema habari iliyokwishasemwa na mtu mwingine kwa namna ambayo si ya kukariri au ukuasuku wa habari asilia. Japokuwa rnaonyo ayatoayo Shaaban Robert ni nauhimu sana kwa msomaji na mhakiki wa mashairi, ni wazi kuwa kwa leo hii nadharia yake ya uchambuzi baitoshelezi japo ilikuwa kianzio kizuri. Hapa tutatilia maanani mawazo yake pamoja na yale tuliyotoa katika Utangulizi wa kitabu hiki kuyachambua mashairi ya Kielezo Cha Fasili.
DHAMIRA KUU
Katika diwani hii, Shaaban Robert ameshughulikia dhamira mbalimbali ambazo aghalabu hujitokeza katika kazi zake zinginc za ushairi, riwaya na hata insha na wasifu. Baadhi ya hizo zinahusu mambo yafuatayo:
Quote:
1. Maana ya maisha
2. Maadili (kuadibu)
3. Siasa
4. Mambo mengineyo kwa jumla
Maana ya Maisha
Kuhusu maana ya maisha, Shaaban Robcrt anao msimamo uyaonayo kuwa ni ya utupu, hayana furaha wala amani. Katika shairi la “Sikia Yanena” (uk. 2) twaelezwa vile ambavyo maisha hayawapi watu chochote kingine isipokuwa hofu na wasiwasi.
Shairi la “Mtu na Malaika” (uk. 11-12) ni kielelezo kizuri sana cha falsafa ya Shaaban Robert kuhusu maisha. Shairi lote ni ndoto imkutanishayo mtu na malaika; na katika ndoto hii mtu anapata “ufunuo” ambao unamweleza kuhusu maana ya maisha. Shairi zima linalinganisha maisha na safari, tena safari yenyewe ni ya mzunguko usio na mwanzO wala mwisho. Twaelezwa:
Quote:
Neno lenye mzunguko, halipatikani mwisho
Wa huku hafiki huko, wala halina malisho
Hapa, shairi linaongelea dira, na dira hii inaonyesha kuwa maisha ni utaratibu maalumu usiobadilika japokuwa ingekuwa vema sana kama watu wangeweza kwenda katika njia iliyonyooka itakayowapeleka na kuwafikisha watakako. Mshairi anaendelea kusema:
Quote:
Heri ya mtu ni kwenda, njia iliyonyooka,
Na milima akapanda, apendako akafika,
Mabondeni akashuka, mwituni akatumbua,
Na mitoni akavuka, hata alikonuia.
Sehemu hii ya shairi inaeleza umuhimu wa kufanya juhudi ya kuendesha maisha hata kama maisha yenyewe yaelekea kuwa “njia” ya dira” ambayo kwa hakika si njia, kwani twaelezwa, “na mzunguko wa dira, mwisho wake ni dirani.”
Kwa hiyo basi, japokuwa taswira ya dira ni ya kukatisha ‘tamaa kwani yatoa kauli kuwa maisha ni mzunguko usio na mwisho, na mzunguko huu umejazana taabu, mashaka na wasiwasi mwingi; shairi hili pia lina upande wake wa pili uibushao moyo wa matumaini mema kuhusu maisha.
Ncha hiyo ya pili ya shairi la “Mtu Na Malaika” inakanusha mawazo ya baadhi ya wahakiki waliomwona Shaaban Robert kuwa daima aliyanunia maisha. Inashirikiana na mashairi mengineyo, kwa mfano lile la “Cheka Kwa Furaha” (uk. 15) kuonyesha upande wa pili wa safaru ya maisha; upande ambao watuusia kuwa maisha si ya kununiwa; kwamba ijapokuwa yamejaa huzuni huweza kuwa ya furaha iwapo mtu atacheka kwa furaha:
Quote:
Cheka sasa kwa furaha; dhiki ingawa usoni,
Dhiki ni kama mzaha, asiyecheka ni nani?
Haya cheka ha! ha! ha!, ndiyo ada duniani:
Cheka mwanadamu cheka, mtu kaumbwa acheke,
Msiba kwake dhihaka, kicheko mtu mwenzake.
Katika shairi hili hili la “Cheka Kwa Furaha” tunagundua mambo makuu matatu yahusuyo falsafa ya Shaaban Robert kuhusu maisha. Kwanza kunao msisitizo Juu ya umuhimu wa juhudi na ari maishani, msisitizo ambao hata katika shairi la “Mtu Na Malaika” unajitokeza. Mistari kadhaa ya “Cheka Kwa Furaha” inaonyesha msisitizo huo:
Quote:
Cheka upone jeraha, yaepuke na mashaka
Na mwili kupata siha, ukianguka inuka
Inuka juu inuka, chini usigaegae
Inuka na kisha cheka, kucheza uendelee
Jambo la pili tuligundualo katika shairi hili ni moyo wa matumaini mema kuhusu maisha; kwani mshairi anatuambia kuwa cheko ni dawa inayotia nguvu mwilini na inayoleta matumaini katika mioyo ya watu.
Hata hivyo, humuhumu katika sbairi hili upo upande wa pili wa falsafa ya Shaaban Robert kuhusu maisha. Huu uko katika jambo la tatu tulionalo shairini: hofu ya mauti. Japokuwa mshairi kashauri watu wacheke, hapohapo anawatahadharisha wajiweke tayari, ndiyo maana anamalizia shairi zima kwa kipande cha: “Cheka usiwe na shaka, itakuja zamu yako”. Hii tahadhari kuhusu kifo ilijitokeza sana katika baadhi kubwa ya maandishi ya Shaaban Robert; kwa mfano, katika riwaya yake ya Siku ya Watenzi Wotekashughulikia zaidi tahadhari hiyo ambayo kimsingi ilinuia kutatua matatizo ya jamii kwa mahubiri na vitisho vya dini.
Kidogo falsafa yote itolewayo na mshairi katika shairi la “Cheka Kwa Furaha” inatatanisha na hata kuchekesha. Inakuwa vigumu kuelewa jinsi mtu mwenye dhiki ya njaa atakavyoweza kuamua kujichekea tu na njaa yake. Kicheko atushauricho Shaaban Robert ni cha kilevi ambacho hutolewa kusahaulisha matatizo yaliyopo kwa muda mfupi tu wakati kitolewapo, na mara baada ya hapo matatizo huwa palepale. Kucheka hakuondoi dbiki, matatizo wala huzuni, kama sababu na msingi wa dhiki, matatizo na huzuni hiyo haijashughulikiwa kiukamilifu: kwa hakika kicheko hakitoki katikati ya dbiki na matatizo!
Shaaban Robert alisisitiza pia kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika maisha na umuhimu huu unajitokeza vizuri sana katika shairi la “Ukaidi” (uk. 18-19) anaposcma:
Quote:
Nashikilia ukale ambapo hapana budi,
Na huacha vile vile iwapo haunifidi,
Nitabadili milele siwezi kuwa abidi,
Wa kutenda yale yale kuizuia juhudi
Kale sina huba nayo nawachia wakaidi
Na watu wenye mioyo yenye hasira shadidi,
Kupinga mambo yajayo; eti waledi zaidi
Wao na washike yao, nami naridhi fuadi
Umuhimu huu wa mabadiliko twaweza kuupanua na kuuelekeza katika uwanja wa ushairi kwani Shaaban Robert anasema kuwa hatakubali kufungwa na minyororo ya sheria zinazoshikiliwa tu bila sababu muhimu na nzito. Ndiyo sababu hata katika mashairi mengi ya diwani hii, kwa mfano, Shaaban Robert katumia aina mbalimbali za miundo toka katika urefu wa beti (badala ya kushikilia tu tarbia) hadi katika wingi wa mizani. Mkabala huu twaweza kuudondolea ubeti mmoja muhimu katika shairi hili (ubeti wa 11):
Quote:
Sasa nawajitoge kwa sanaa kusanidi,
Majoho yao wavae na vielbe wale Idi,
Na ufundi uzagae kwa marifa kuzidi;
Mazonge wayazongoe kwa kazi siyo madadi.
Mashairi mengi katika diwani hii na katika diwani zinginezo za Shaaban Robert yameyaona maisha kuwa ni msukosuko na fujo tupu. Kwa mfano, katika shairi la “Kinyume” (uk.26) anasema (ubeti wa 7):
Quote:
Masikini akipata, matako hulia mbwata
Na tajiri hutafuta, kamari, bima, karata
Maisha yana matata, na dakika ikipita
Umri umeshakata, kovu kubwa ya kufuta.
Shaaban Robert si mpweke katika ushairi wenye mkabala huu kuhusu maisha. Hata baadhi ya washairi wa leo wanayaona maisha hivyo, kwa mfano E. Kezilahabi ambaye katika diwani yake ya Kichomi (Heinemann, 1971) ana mashairi yanayochukua mkabala huo (angalia, mathalani, shairi la “Nimechoka”). Kila kazi ya sanaa huathiriwa na kufinyangwa na wakati, nayo huwakilisha mawazo, matazamio na mahitaji ya watu katika wakati maalumu wa kihistoria. Kwa Shaaban Robert inakuwa rahisi kuelewa sababu za mkabala wake kuhusu maisha, hasa kwa vile hata kiwango chake cha elimu na cha mwamko wa kisiasa hakikuwa cha juu tukilinganishapo na cha Kezilahabi. Kezilahabi aelekea kuongozwa na falsafa iliyojengwa na athari za elimu aliyoipata (kutoka kwa akina Satre na wengineo) zaidi ya hali halisi za jamii yake. Shaaban Robert yeye anaongozwa na falsafa iliyojengwa na kufinyangwa na kiwango cha mwamko wa jamii yake na hali halisi za jamii hiyo kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi; japokuwa hii haimaanishi kuwa wakati huo hapakuwa na waliokuwa wameamka na kupevuka zaidi kimsimamo kuliko akina Shaaban Robert.
Zaidi ya kutuelcza kuwa maisha ni vurugu tupu na kwamba kitu hiki ni cha kupita tu, hakidumu (angalia shairi la “Umri,” uk. 29), Shaaban Robert katoa utatuzi mwingine wa mashaka hayo ya maisha. Ikiwa wakati mwingine aliouona utatuzi huo katika siku ya ufufuo (angalia shairi la “Mbioguni,” ul. 32), kwa hiyo akaona kuwa kila tendo jema ni daraja ituongozayo kwenda mbinguni; na kama wakati mwingine dawa ya mashaka hayo ya maisha aliiona katika kicheko; sasa katika shairi la “Kinyume” anatueleza dawa nyingine: mapenzi, ambayo alikwishaiandikia diwani nzima ya Mapenzi Bora (Nelson, 1967). Katika ubeti wa 11 wa shairi la “Kinyume” anatuambia:
Quote:
Watu wanachukiana, hawataki kujivuta,
Pamoja wakapendana, kama mimea na tuta
Hawataki kupatana, kama maji na mafuta
Naghafula wawaona wenyewe wanajiseta
Ni wazi kwamba, ijapokuwa “dawa” ya “mapenzi” inasikika vizuri sana masikioni, hatimaye udhaifu wa “dawa” hii ni sawa na ule tuliouona katika “kicheko”.
Maadili (kuadibu)
Daima katika uandishi wake, Shaaban Robert alikuwa sawa na babu na bibi waliowaketisha wajukuu zao na kuwapigia hadithi kwa madhumuni ya kuwatolea maadili yaliyobeba amali za jamii. Kwa hiyo itaonekana wazi kuwa mashairi mengi ya Shaaban Robert ni ya kimaadili yamfanyayo aonekane kama mwalimu wa walimwengu; na baadhi kubwa ya maadili hayo hutokana na uzoefu wa maisha aliyoyapitia yeye mwenyewe.
Kati ya maadili hayo amesisitiza kuhusu umuhimu wa watu kupatana na kuepuka ugomvi (angalia shairi la “Ubora Wetu” uk. 42, hasa ubeti wa 2), umuhimu wa kuepuka moyo wa kijicho na chuki (“Sumu” uk. 51), na pia umuhimu wa kuoa. Katika shairi la “Jina” (uk. 54) twaelezwa kuwa furaha huletwa na vitu vikuu vitatu: akili ya kufikiri na kutambua jema na baya, fikra ya kutafakari mambo, na matendo yenye maana nzuri maishani mwa watu.
Sifa nyingine iibukayo mara kwa mara katika maadili ayatoayo Shaaban Robert ni ile ya uchaguzi bora wa maneno. Katika shairi la “Maua na Maneno” (uk. 13) mshairi anasema:
Quote:
Maua huchaguliwa, ndipo nyuki akaweza,
Asali kuyachujua, tamu naya kupendeza,
Mpaka katika mew, warembo wanayaweka,
Ni yakung’ariza, siyo yale ya kunuka,
Ua lolote porini, nyuki shida kuchukua,
Unga uliyomo ndani, ama mnato wa ua.
Kitu gani achelea? Maua mengine sumu,
Kwa nyuki kuyatumia, na pia kwa mwanadamu,
Licha nyuki hata ndege, wana maua wahofu
Panzi pamoja na nzige, wakiyala huwa wafu.
Palipo ua dhaifu, rw hapakaribii,
Mlaji kila uchafu, huhofu nanwa hii!!
Ubeti huu pamoja na wa pili hujenga taswira inayohusu aina mtrili za maua; picha ambayo kwa muda huweza kumchota na kumdanganya msomaji kuwa shairi linahusu maua. Halafu baada ya kuijenga na kuikamilisha taswira hii, ndipo katika ubeti wa 3 wa shairi mwandishi anatoa kauli:
Quote:
Hali ikiwa hivi, na maneno kadhalika,
Watu wasiwe walevi, wakati wa kutamka.
Wakati ambapo neno zuri limefananishwa na ua zuri, neno baya limeitwa risasi, kinywani likishatoka. Kwa hiyo basi, watu watakapo-weza kuchagua maneno mazuri, watafaulu kutengeneza uhusiano mzuri kama asali ya nyuki itokanavyo na maua mazuri.
Huenda kwa baadhi ya wasomaji wa shairi la “Udhia Wa Mali” (uk. 2), Shaaban Robert ataonekana kuwa anapinga kuwa na mali kwa vile tu yeye mwenyewe hanayo mali. Lakini kwa wasomaji wanaochambua kwa undani, wataona kuwa shairi hili ni la kimaadili lituasalo kuwa ili mali isiwe na udhia yafaa wote wawe nayo; na kwamba ni udhia mtupu ikiwa una mali nyingi na wenzako wakuzungukao hawana. Twaweza kupanua maana hii na kuipa welekeo wa kisiasa kuwa shairi hili linatetea usawa baina ya watu.
Mashairi mengine katika diwani hii ambayo tunaweza kuyaita ya kimaadili ni “Cheka kwa Furaha,” “Ukaidi,” “Heshima.” “Woga,” “Fitina,” na “Kweli.”
Siasa
Masuala mbalimbali ya kisiasa yaliishughulisha sana kalamu ya Shaaban Robert. Kwa vile mshairi huyu aliishi nyakati za ukoloni ni wazi kuwa asingeweza kukwepa uhalisi wa maisha ya kikoloni yaliyokuwa yakiwaonea na kuwadhulumu wananchi.
Katika shairi la “Kashata na Ladu” (uk. 37), mshairi anaongea kuhusu serikali mbovu ziongozwazo na watu; serikali ambazo ni duni kuliko zile za wanyama, ndege na wadudu.
Kama luunavyu kutika diwani yake ya Maisha Yangu Baada ya Miaka Hamsini (Nelson, 1968), Shaaban Robert ameonyesha ubaguzi wa rangi uliokuwepo katika jamii yake ambapo Wazungu walipewa (au walijipa) nafasi yajuu wakifuatiwa na Wahindi, halafu Waarabu, na wa chini kabisa wakiwa Waafrika. Katika diwani hiyo Shaaban Robert aliilalamikia vikali hali hii iliyowagawagawa watu katika mafungu kufuatana na rangi zao. Katika Kielezo cha Fasili jambo hili amelisisitiza katika shairi la “Kama Upindi wa Mvua” (uk. 44) ambalo linatueleza kuwa rangi mbalimbali alizoziumba Mungu si za kuletea ubaguzi bali ni kama mapambo tu ya kuongezea uzuri wa dunia.
Shairi la “Vivuli” (uk. 55) linakumbusha yale yasemwayo na mshairi huyuhuyu katika shairi lake lingine la “Gharika” (lililoko katika diwani ya Masomo Yenye Adili, uk. 62). Mashairi haya mawili yanaongea kuhusu uhasama na machafuko ya kisiasa yaliyoko duniani. Sehemu ya mwanzo ya “Vivuli,” kwa mfano, inaeleza kuhusu migongano ya mataifa makubwa ambayo imeleta machafuko na maangamizo makubwa duniani. Mshairi anasema:
Quote:
Wenye kuchana magando, na sumu ya kuulia,
Wamo katika mkondo, na tufani ya tabia,
Na ghasia ya matendo, uhalifu na hatia,
Hapana chembe upendo, kwa ualili na ria,
Pamebakia uvundo kila pembe ya dunia.
Picha tuipatayo katika shairi hili ni ile ya wasiwasi na ‘ghasia tupu pamoja na vitisho viletavyo maangamizi makubwa hadi woga umewaingia hata simba na nondo. Picha hii ya wanyama wakubwa-simba na ndovu-walioingiwa na woga na hali kwa kawaida si waoga, na ile ya nondo – mdudu ambaye ana ujasiri mwingi wa kuchezeachezea ndinu za moto ila sasa yu aogopa-ni taswira ikamilishayo mabadiliko mabaya yatokanayo na mivutano kati ya wenye kucha “na sumu ya kuulia.”
Shairi lingine la kisiasa ambalo limewahi kuzusha ubishi kati ya wanazuoni kuhusu maana aliyokuwa nayo mshairi alipolitunga ni la “Kufua moyo.” Kimsingi linaongea kuhusu ushujaa wa askari apiganaye vitani na ambaye hata kama atauawa hafi kwani huendelea kuishi katika kumbukumbu za watu wote, wazee kwa watoto. Hata “uvundo wa mashujaa’ mwandishi kaufananisha na manukato kuonyesha jinsi ambavyo, kama asemavyo mwandishi mwenyewe katika fasili yake, “uvundo wa maiti ya mashujaa ni sawasawa na mafuta ya uturi na marashi usio na harufu ya karaha wala fukuto.”
Kijuujuu shairi hili huweza kusifiwa sana kuwa linasisitiza kuhusu ushujaa na uzalendo. Lakini, kimsingi hili ni shairi ambalo halitupeleki mbali sana kwani linaongelea kijumla tu kuhusu vita na ushujaa wa kufa katika vita hivyo bila kutueleza hasa ni vita gani, vya kumtetea nani na kumsuta nani, na kama ushujaa huo ni kwa jicho la nani. Huu basi ni uzalendo na ushujaa usio na welekeo kamili.
Shairi la “Kuondoana Njiani,” sawa na la kupinga ubaguzi wa rangi, linatetea usawa baina ya watu, nalo linakemea wanyonyaji wanaofanyiza watu kazi bila ujira:
Quote:
Kazi za sasa hasara, kwa jamii wafanyao
Nyingi kukuru kakara, hazitimizi chajio;
Wenye nguvu wadodora, wako wapi wachumao?
Fanya kazi kwa imara, tajiri apate cheo,
Kichwa kiote kipara, macho uvae vioo;
Huzidishwi mshahara, wala huna fanikio,
Tutatenda ndivyo sivyo tuondoane njiani.
Mvutano baina ya waajiri, wanyonyaji na waajiriwa wanyonywaji, umeonyeshwa jinsi unavyowadidimiza watu wa chini huku wanyonge hao wakiandamwa na ghera, hasira na matusi ya waajiri.
Hata hivyo, kama kawaida, baada ya kueleza maovu ya waajiri kwa waajiriwa, Shaaban Robert anatoa suluhisho lilelile la kidini la kuwaambia watu kuwa maamuzi yote yatatolewa huko ahera. Haya anayaeleza katika ubeti wa 10:
Quote:
Kutumiwa kama nyara, mimi furaha sinayo,
Takwenda nayo ahera, machungu niliyo nayo;
Kuna maamuv bora, ya dhuluma kama hiyo.
Ni wazi kuwa hapa Shaaban Robert kaitumia dini kuwa kimbilio la mnyonge ambaye kakata tamaa; kimbilio ambalo halimsaidii mnyonge huyo kumuondolea unyonge uliomzingira. Ndiyo sababu hata yasemwayo katika sbairi la “Sala na Saumu” inakuwa vigumu kuyakubali moja kwa moja kwani aghalabu sala na saumu pekee bila vitendo muhimu vilivyohusishwa na mizizi ya matatizo ya jamii ni bure tu!
Shairi la “Muadhama Richard Turnbull” limetajwa kuwa moja ya mashairi aliyoyaandika Shaaban Robert yanayotatiza na yanayotufanya tuushangae msimamo wake kwa wakoloni. Hatuoni sababu hasa – zaidi ya kujipendekeza kwa watawala – ya kumwombea afya njema kiongozi huyu wa kikoloni!
Mambo Mengiaeyo
Zaidi ya falsafa kuhusu maisha, maadili na siasa kwa jumla, diwani hii ya Kielezo cha Fasili imeshughulikia pia masuala mengine ingawa si kwa kirefu kama hayo tuliyoyachambua. Kati ya hayo, kubwa ni suala la “ukweli” wa maisha linalohusu hatua mbalimbali za maisha ya mtu tangu kuzaliwa, kuzeeka na kufa. Hapa yapo mashairi ya “Umri,” “Fumbo,” “Sichelei Kufa,” “Uzee,” na kadhalika.
Katika hatua hizo mbalimbali za maisha ya mtu, hatua ya ndoa imepewa uzito na nafasi kubwa zaidi ya zingine katika diwani hii. Katika ubeti wa mwisho wa “Sichelei Kufa” mshairi anasema:
Quote:
Ndoa kitu ashrafa utumwa wajia nini?
Ndoa jambo mzofafa huwaje umajununi?
Ndoa ni lulu nadhifa nimehuni kifu gani?
Ushairi wa Shaaban Robert ulithamini mno taasisi ya ndoa, na ndiyo sababu hata katika malumbano mengi tuyakutayo katika diwani nyingine ya nashairi huyuhuyu ya Ashiki Kitabu ffiki (Nelson, 1967), anatetea sana ndoa. Shairi la “Ndoa Ni Kanuni” Kielezo cha Fasili (uk. 70-71), laielezea ndoa kuwa ni kanuni na ni amri ya Mungu. Ubeti wa 7 wasema:
Quote:
Ndoa rutuba ya A llah, kuoa ubaya gani?
Ndoa hukuza mahala, mmoja huwa theneni,
Kuoasi mghafala, kuoa kwetu kanuni
Hivyo basi, ndoa kwa Shaaban Robert ni wajibu kwa watu wote. Mkabala huu unajitokeza si katika ushairi tu wa Shaaban Robert, bali hata katika baadhi ya riwaya zake, kwa mfano katika Utubora Mkulima na Siku Ya Watenzi Wote,
Wakati ambapo kidini huenda mkabala huo ukakubalika, kimaisha halisi inaonyesha kuwa taasisi ya ndoa haina budi kuangaliwa sambamba na hali halisi za jamii amazo ndizo zilizoizaa na ndizo zinazoilea ama kuiua taasisi hiyo. Si kila ndoa ni nzuri; na mara kwa mara katika jamii ambayo haijawa na usawa kati ya watu kiuchumi na kimaisha kwa jumla, taasisi hii hujazana mafarakano na ugomvi mwingi ambao kuibuka kwake kunahusiana na maisha mabaya yatokanayo na mfumo mbaya wa jamii. Hii ndiyo sababu talaka zimejazana sana katika jamii za kibepari kwani taasisi hii, sawa na zinginezo za jamii hiyo, hukuzwa katika mismgi ya kibepari.
MATUMIZI YA VIPENGELE VYA FANI
Tumekuwa tukitaja hapa na pale kuhusu matumizi ya vigezo mbalimbali vya fani katika diwani hii, hasa kigezo cha taswira. Taswira zimejitokeza mahali pengi sana katika mashairi haya, nazo zimetumiwa vizuri kuyajenga maudhui ya ashairi. Katika shairi la “Maua na Maneno” kwa mfano, Shaaban Robert katujengea kwanza taswira kamili ya maua mbalimbali, taswira ambayo iunganishwapo na kauli aitoayo mshairi kuhusu umuhimu wa kufanya uchaguzi mzuri wa maneno msomaji huupata ujumbe kwa uwazi zaidi.
Shairi la “Mtu na Malaika” pia limetumia taswira nadto ya dira kusisitiza falsafa ya Shaaban Robert kuhusu maisha yalivyo mzunguko usio na mwisho.
Vile vile shairi la “Kama Upindi wa Mvua” ni mfano mzuri wa uundaji wa taswira ambao unalitoa wazo kuu la shairi kwa njia inayonata vizuri sana akilini mwa msomaji.
Zaidi ya mbinu hii ya fani, mashairi mengi humu hutumia pia miundo mbalimbali ambayo hutofautiana katika wingi wa mizani, aina za vina, urefu wa beti, na kadhalika. Jambo hili limeyafanya mashairi haya yasichoshe na yasomeke vizuri zaidi.
Ni dhahiri kuwa kwa Shaaban Robert hatuna haja ya kutaja sifa ya matumizi bora ya lugha kwani anayo tangu mwanzo mpaka mwisho. Ni sifa ambayo humweka msomaji katika hali ya kutaka kusoma zaidi kwani uchaguzi wake wa maneno ni mzuri mno hata ni vigumu kuona neno lolote lile lililochomekwa tu au lililolazimishwa kutokana na kanuni za vina na mizani, kama ilivyo kawaida ya washairi wengi wa leo wajitokezao hasa katika magazeti.
Kwa upande wa lugha pia yapo matumizi ya tamathali mzo mzo za usemi ambazo zaidi ya kuyapamba mashairi haya zimeongeza uzito wa maudhui yaibushwayo. Baadhi ya tamathali bizo zimejikita katika taswira au ishara kama zile tuzionazo katika mashairi ya “Mtu Na Malaika,” “Maua na Maneno,” na kadhalika. Katika shairi la “Ushairi” (uk. 23) twaona vile ambavyo Shaaban Robert anauthamini sana ushairi kwa jinsi anavyoupamba kwa tamathali nyingi. Anauita “hirizi ya sudi,” “malaika,” “madini za shani,” “huba,” “johari na mvua yenye samadi,” na kadhalika. Kijicho na chuki vimeitwa kuwa ni “sumu” katika shairi la “Sumu” kuonyesha jinsi ambavyo hudhuru uhusiano mzuri baina ya watu. Vivyo hivyo shairi la mwisho, “Kweli” (uk. 93-94), limedhihirisha ufundi wa Shaaban Robert wa kutumia tamathali zinazosadifu sana jambo aliongelealo. Kweli imeitwa “kito mahabubu,” “siri ya ajabu,” “chimbo la johari,” “maadeni nzuri,” “vunjo la kiburi,” “jambo ashrafu,” “nuru takatifu,” “nguvu ya imani,” “kitu cha thamani,” na kadhalika.
Ufundi wa Shaaban Robert wa kutumia tamathali za usemi, hasa za sitiari na tashbiha, na matumizi mazuri sana ya lugha pamoja na ya ishara na taswira, ni baadhi ya vigezo muhimu vya fani vinavyofaulisha maudhui ya mashairi yake, na ndivyo vimpavyo sifa ya ushaha wa malenga na kumweka sambamba na washairi wengine maarufu kama vileMuyaka bin Haji wa Mvita.
Maswali
1. Chunguza nadharia ya fasili aitoayo Shaaban Robert katika “Utangulizi” na ujadili uhusiano wake na uchambuzi wa mashairi.
2. Cbagua dhamira kuu mbili alizozishughulikia Shaaban Robert katika Kielezo cha Fasili ujadili zilivyoibushwa kwa kuzitolea mifano mahsusi.
3. Yajadili matumizi ya lugha taswira na isbara katika mashairi ya Kielezo cha Fasili.
4. Je, “vivuli” ni nini katika shairi la “Vivuli”?
5. Chagua shairi moja kati ya “Mfua Bati,” “Kufua Moyo,” na “Kweli” ujadili ujumbe wake na jinsi taswira zilivyotumiwa kuuibusha.