MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - NAMNA KISWAHILI KINAVYOONGEZA AJIRA KWA WASOMI

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: NAMNA KISWAHILI KINAVYOONGEZA AJIRA KWA WASOMI
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
Tangazo la kwanza ni lile la Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ilitangaza nafasi sabini (70) za ajira za maofisa uhamiaji. Katika nafasi hii, waliomba jumla ya vijana wasomi wa Kitanzania wapatao zaidi ya 10,000. Si hivyo tu, lakini pia kulikuwa na tangazo la ajira la TBS ambalo walitangaza nafasi 47 lakini walioomba nafasi hiyo ni vijana wapatao 6,700.
Tukumbuke kwamba, kila mwaka vyuo vikuu vya umma na vile vya binafsi vinaendelea kutoa wahitimu ambao wanahitaji ajira. Lakini kwa kutumia Kiswahili, baadhi ya wasomi hawa wataweza kujiajiri au kutengeneza ajira ili wawaajiri Watanzania wenzao na hivyo tatizo la ajira litapungua makali kuliko ilivyo hivi sasa.
Kiswahili ni lugha ya Kibantu ambayo inazungumzwa katika nchi mbalimbali duniani. Kiswahili ni lugha ya taifa katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda kinazungumzwa japo si kama mataifa hayo mengine. Vile vile Kiswahili ni lugha ya mawasiliano mapana (lingua franca) ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Kiswahili kinazungumzwa katika nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudani Kusini, Somalia na visiwa vya Comoro. Pia kuna baadhi ya nchi zimeanzisha programu za kufundisha Kiswahili nchini mwao kama vile Afrika Kusini katika Chuo Kikuu cha KwaZulu Natal, Botswana katika Chuo Kikuu cha Botswana, Zimbabwe katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe kwa kutaja kwa uchache.
Nje ya Bara la Afrika, Kiswahili kinafundishwa kwenye vyuo vikuu katika sehemu mbalimbali kama vile Marekani, Ujerumani, Korea Kusini na Japan. Kuna uhitaji mkubwa sana wa watu kujua namna ya kuwasiliana kwa Kiswahili katika nchi mbalimbali za Bara letu la Afrika. Jambo hili nilielezwa na mdau mmoja wa Kiswahili anayeitwa Leonard Maganja.
Leonard Maganja ni Mtanzania ambaye amekulia na kusomea elimu ya msingi na sekondari huko nchini Uganda. Katika kutembelea mataifa mbalimbali ya kusini mwa Afrika, amekutana na watu kadha wa kadha wenye kiu ya kutaka kukijua Kiswahili. Watu hawa wanatambua thamani ambayo Kiswahili inacho na hivyo wanataka kupata umilisi (ujuzi) wa lugha hii.
Ni kwa vipi Kiswahili kinaweza kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hapa nchini? Ili kulijibu swali hili, inabidi Kiswahili kitazamwe kama bidhaa. Ni bidhaa ambayo inapelekwa sokoni ili kuuzwa na kununuliwa. Kiswahili ni sawasawa na nyanya au vitunguu au madini. Jambo hili analielezea Mahenge katika kitabu chake cha ‘Kiswahili Bidhaa Adimu: Jiajiri’ (Mahenge, 2012).
Mwandishi anadadavua namna mbalimbali zinazoweza kutumika ili kukiuza Kiswahili. Kwanza, kwa Mtanzania ambaye anakijua vizuri Kiswahili katika stadi zote nne, yaani kuzungumza, kusikia, kuandika na kusoma, anaweza kuwa mwalimu wa ‘Kiswahili kwa wageni’.
Mtu akishakuwa na umilisi wa lugha, yaani ni mzawa wa lugha hiyo (kwa maneno mengine, ni mtu ambaye ameijua lugha hii ya Kiswahili bila ya kukaa darasani na kufundishwa), basi huyo ni mwalimu, ila anachokihitaji ni mbinu za kufundishia.
Anahitaji kufundishwa mbinu za ufundishaji wa ‘lugha ya pili’ yaani ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni. Baada ya walimu hawa kupata mafunzo hayo, wanachohitaji ni kuchangamka ili kuyatafuta ‘mavuno’ huko yaliko. Mavuno ninayoyarejelea hapa ni wanafunzi wanaotaka kujifunza lugha hii ya Kiswahili.
Ninamaanisha kuwa, baada ya kujua namna ya kumfundisha mgeni lugha ya Kiswahili kama lugha ya pili, anachotakiwa kukifanya mtaalamu huyu ni kutoa matangazo kupitia njia mbalimbali. Kuna njia nyingi ambazo ‘mvunaji’ anaweza kuzitumia ili kuwajulisha wateja wanaotaka kujifunza Kiswahili.
Njia kama ujumbe mfupi wa simu, kupitia vyombo vya habari kama vile: magazeti, redio, kwenye televisheni, wavuti na mabango. Mbali na kutumia njia hizo, njia ya mdomo pia inaweza kutumika. Njia ya mdomo inaweza kufanywa kwa kutembelea sehemu ambazo zinajulikana kuwa zina watalii au wageni mbalimbali (yaani unakwenda huko waliko kama ni hotelini na unajitangaza kuwa unafundisha Kiswahili kwa wageni).
Unaweza kutengeneza vipeperushi vinavyotoa maelezo ya wapi darasa lako lipo, ada ya mafunzo, viwango vya mafunzo na mambo mengine. Kwa kufanya hivyo, utakuwa umefikisha ujumbe kwa mteja na yeye ni uamuzi wake kuchukua hatua stahiki ili apate elimu hiyo ya lugha ya Kiswahili.
Kama mwalimu huyu anataka kufundisha nje ya nchi, anahitaji kufuata taratibu zinazohitajika katika nchi husika za kupata vibali vya kazi n.k. Labda huyu ni mwalimu ambaye atakwenda kuomba kazi sehemu rasmi kama vile kwenye shule za msingi, sekondari, au vyuoni na kwenye taasisi rasmi.
Huyu anaweza akawa hana mambo mengi yanayomlazimu kuyatekeleza ili aifanye kazi yake. Kwa mfano, kama umeajiriwa katika shule, tayari kuna nyenzo unazozihitaji ili kuendesha darasa. Kuna majengo na samani. Kwa hiyo, anachohitaji mwalimu huyu ni zana za kufundishia.
Lakini kwa mfundishaji ambaye hatafanikiwa kuingia katika mfumo rasmi, anahitaji kuwa na kampuni itakayomwezesha kufanya kazi kadha wa kadha katika nchi ya kigeni. Mathalani, hapa Tanzania na sehemu zingine duniani tunashuhudia makampuni kama Samsung, LG, Hyundai ambayo ni ya Korea Kusini kwa kutaja kwa uchache, yakiuza bidhaa zao katika nchi yetu.
Ni kwa nini na sisi tusifungue kampuni zetu huko kwao ambazo pamoja na kazi zingine zitakuwa zinaweza kufanya kazi za ufundishaji lugha? Hili linawezekana kwa kuunganisha nguvu. Ninashauri vijana waunganishe nguvu ili kupata mtaji wa kuanzia. Kisha wafungue kampuni zao zitakazowawezesha kuuza Kiswahili ndani na nje ya nchi, kisha wachangamkie fursa hiyo ya ajira.
Kwa hiyo, kwa kufanya mambo haya ya awali, yaani kujifunza namna ya kufundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni; pili, kwa kujitangaza na kujiuza kuwa, wewe ni gwiji wa ufundishaji Kiswahili kwa wageni; na tatu, kwa kuzitafuta ajira katika maeneo rasmi nje ya Tanzania au kwa kufungua kampuni zinazohusu kuuza bidhaa ya Kiswahili, vyote hivyo kwa pamoja vitamwezesha kijana Mtanzania kupata ajira.
Katika makala inayofuatia, tutadadavua hatua mbalimbali za ufundishaji wa lugha ya ‘Kiswahili kwa wageni’. Mwandishi wa makala haya ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampasi ya Mwalimu J.K. Nyerere.
Wasiliana naye kwa lizmahenge@udsm. ac.tz.