MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - UHAKIKI: MWANAMKE NI IBILISI?

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: UHAKIKI: MWANAMKE NI IBILISI?
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
Mwanamke ni Ibilisi?
R.D.K. Mekacha
Katika kuchanganua jinsi mwanamke alivyosawiriwa Mbughuni (1982) anaainisha picha mbili za mwanamke zinazojitokeza katika riwaya. Kwanza lu picha ya mwanamke kama kiumbe mharibifu, na pili ni picha ya mwanamke kama kiumbe mwongofu. Katika picha ya uharibifu usawiri wa mwanamke unashabihishwa na wasifu wa Hawaa (au Eva) katika masimulizi ya kibiblia ya dhambi ya asili, na katika picha ya uongofu usawiri wake unashabihishwa na wasifu wa Maryam (au Maria) mama wa Nabii Issa (Yesu Kristu). Katika picha ya mwanzo mwanamke anaiponza jamii kwa kuipoteza pepo (paradiso), na katika picha ya pili mwanamke ni kiumbe wa kufugwa katika ndoa. Matteru (1982) anaainisha picha tatu za mwanamke zinazobainika katika fasihi simulizi: mwanamke kama mzazi, mwanamke kama chombo cha anasa ya mwanamume, na mwanamke kama chombo au mali ya kumilikiwa. Kama mzazi dhima ya mwanamke ni kuzaa watoto, kama chombo cha anasa dhima yake ni kumburudisha mwanamume, na kama mali uamilifu wake ni kumilikiwa na kuwa zana ya kuzalishia mali. Wahakiki wote hawa wanaafikiana kuwa katika picha zote hizo mwanamke anajitokeza akiwa mtu duni akilinganishwa na mwanamume.
Azma ya makala haya mafupi ni kushadidia hoja hiyo kwa kuchanganua mwanamke alivyosawiriwa katika nyimbo za kisasa za muziki wa dansi. Nyimbo za aina hii hutawala sana matangazo ya redio – vyombo vya mawasiliano ambavyo kwa makisio yetu vina nguvu sana katika jamii hii. Mahususi tutajibana katika kuchanganua namna wasanii wa nyimbo hizo wanavyouonyesha udhalili wa mwanamke kwa kumsawiri kama kiumbe mwenye uovu unaozidi ule wa Hawaa hata ukamithilishwa na ule wa ibilisi. Tunatazamia kuonyesha kuwa sambamba na usawiri huo mwanamume anajitokeza akiwa mbabe na mwadilifu. Tumeteua na kutumia nyimbo chache kwa sababu tu ya maudhui yake.
Kama ilivyo katika kazi nyingine za sanaa mwanamke amesawiriwa kwa namna mbalimbali katika nyimbo za kisasa za muziki wa dansi. Mwanamke ni mchapakazi,1 ni mwenye busara na mshauri wa mumewe,2 ni mnyonge na mwenye kumtegemea mume kupata mradi wake wa maisha,3 ni chombo cha anasa cha kumburudisha mwanamume,4ni fasiki na mwovu sawa na ibilisi.
Hakuna mipaka ya wazi na bayana kati ya picha hizo za wasifu wa mwanamke, bali huingiliana kwa namna ya mwendeleo unaoanzia kwenye zile nyimbo zenye mwelekeo chanya hadi zile zenye mwelekeo hasi. Kwa makadirio yetu idadi kubwa ya nyimbo hizi inaegemea kwenye mwelekeo hasi, na hata zile zinazomsawiri mwanamke kwa mwelekeo chanya hatimaye huzishawishi hadhira kuhitimisha kuwa mwanamke ni kiumbe dhalili mbele ya mwanamume hasa kimaadili.
Motifu ya usawiri wa mwanamke kama ibilisi ni utendekaji wa kosa au jambo lolote linalosababisha madhara kwa mtu mmoja au jamii kwa jumla. Ili kuikamilisha motifu ya aina hii watunzi wa nyimbo hizo huumba chanzo kinachosababisha tendo ambalo hatimaye hubainika kuwa kosa, huumba pia mbinu zitumiwazo kukamilisha tendo hilo, malengo ambayo ndiyo huwa tendo limedhamiriwa kuyakidhi na matokeo, taathira au madhara ya tendo hilo.
Mojawapo ya chanzo cha utendekaji wa kosa hilo ni udanganyifu. Katika masimulizi ya kibiblia ya dhambi ya asili ambayo kwa kiasi hushabihiana na picha hii, mwanamke (Hawaa) alishawishiwa na Ibilisi kuchuma na kula tunda lililokuwa limekatazwa.5 Katika idadi kubwa ya nyimbo za kisasa za muziki wa dansi pia mwanamke hushawishiwa. Lakini hapa vishawishi aghalabu huwa tamaa ya maisha ya starehe. Katika kukidhi haja hiyo mwanamke anashawishika ama kuacha masomo, au kumwacha mchumba wake, au kuwatelekeza wazazi wake huko vijijini na kukimbilia mjini.6
Udanganyifu kama chanzo cha kosa hutuelekeza katika kuhitimisha kuwa mwanamke anastahili sehemu tu ya lawama kwa kosa lililotendeka. Sehemu nyingine ya lawama inabebwa na vile vishawishi ikiwa ni shetani (kama ilivyokuwa kwa Hawaa), mali, starehe, au ulaghai wa mwanamume. Lakini pamoja na kugawana lawama hizo, hatimaye nyimbo hizo hutuongoza katika kumwona mwanamke kama kiumbe dhaifu, asiyeweza kuhimili vishawishi, na ambaye kwake yote yang’aayo ni dhahabu. Kwa hiyo madhara yatokeayo hatimaye huwa ni kwa sababu ya udhaifu wake (mwanamke).
Chanzo kingine cha tukio liletalo madhara ni dhiki. Dhiki aliyonayo mwanamke humsukuma kutafuta njia za kukidhi mahitaji yake, na katika kufanya hivyo husababisha madhara au kosa kutendeka.7 Katika chanzo cha namna hii pia inawezekana kuhoji kuwa mwanamke ni mhasirika tu va mahitaji na hivyo lawama anayostahili kubeba ni ndogo. Aidha hapa ile hali ya udhaifu haijitokezi, bali tunamwona mwanamke kama jasiri na mwenye kuthubutu kuchukua hatua za kujiondoa kwenye madhila ya unyonge na umaskini. Lakini si aghalabu hali hiyo kusisitizwa katika nyimbo hizo. Badala yake linalosisitizwa na watunzi ni mbinu aitumiayo (mwanamke) kukidhi haja hiyo na madhara ayasababishayo kwa mwanamume, na hasa kwake mwenyewe.
Katika idadi kubwa ya nyimbo hizo, hata hivyo, chanzo cha matendo au matukio yaletayo madhara si vishawishi vya Ibilisi au tamaa, wala si msukumo wa kukidhi mahitaji ili kukabili dhiki inayomzinga, bali wivu unaochochea nia ya kuharibu “maisha bora” ya ndoa za wenzake. Hapa ubaya wa mwanamke hukiuka ule wa Hawaa katika masimulizi ya dhambi ya asili na kushabihiana na ule wa Ibilisi. Mtunzi wa wimbo uitwao “Mwanameka” anahitimisha kisa cha mwanamke huyo kwa kusema:
Quote:
Hivi sasa nimeshaamini,
Ibilisi wa mtu ni mtu.
Yaani Ibilisi wa Musa (mwanamume) ni Mwanameka (mwanamke). Siyo kwamba kisa hicho kimemfanya atambue hivyo, bali kimethibitisha jambo ambalo alikwishahisi au kudokezwa. Ndiyo maana asema kuwa “sasa nimeshaamini.”
Mbinu zitumiwazo na mwanamke kukidhi malengo yake, ikiwa ni starehe, mali, au uharibifu wa ndoa, ni mbili. Kwanza ni ahadi ya ndoa; ahadi ambayo aghalabu huwa haitimizwi. Msichana aitwaye Mwanaidi katika wimbo wenye jina hilohilo aliahidi kuolewa na mtunzi. Naye mtunzi akatumia mali yake yote ikiwa ni pamoja na kuuza shamba na nyumba ili kumridhisha “mchumba” wake huyo. Lakini hatimaye mtunzi akafilisika na Mwanaidi akamgeuka na kumkataa.
Mbinu ya pili ni mapenzi na uzinzi. Mwanameka katika wimbo tulioutaja ni msichana aliyetumia uzuri wake, vipodozi, na mbwembwe ambazo zilimzuzua Musa hata zikamghilibu akili licha ya kujitahidi kuvumilia. Alipopotea njia na kumtaka mapenzi Mwanameka, basi naye akayatumia hayo mapenzi kumfanya Musa asahau kwake, jambo ambalo lilisababisha ndoa yake kuvunjika. Mtunzi analieleza hilo ifuatavyo:
Quote:
Ukajikuta mrembo
Ukazidisha na mapambo
Kipini wanja kwa poda
Na mwendo wako maringo
Musa macho yake yameona
Na moyo ukaanza sononeka
Ukabadili na njia
Lazima upite kwa Musa
Ukenda sokoni kwa Musa
Musa amevumilia
Mwisho kapotea njia
Kakusimamisha bila kutambua
Akazungumza neno la mapenzi
Ukakubali bila kusita
Uliyotaka yamekuwa
Kazi ikawa ni moja
Ni mapenzi moto moto
Lakini mara tu baada ya ndoa ya Musa kuvunjika Mwanameka pia akavunja mapenzi yake na Musa.
Mbinu hizi mbili, kwa kweli, ni sura mbili za sarafu moja. Zote zinaelekea katika kuhitimisha kuwa mbinu aitumiayo mwanamke kuleta madhara ni ile jinsi yake ya kike. Hii ni jinsi ambayo pia inahusika na dhima muhimu ya kuiendeleza jamii. Kwani mwanamke ni mzazi na mlezi wa kizazi cha kesho, dhima ambayo wasanii hawa huonyesha kuiheshimu sana.8 Lakini hapa inashushwa hadhi na kuonekana kama silaha kuu au ya pekee ya mwanamke kufanyia hila zake za kiovu. Pengine mtazamo huu unaakisi ukweli: (i) kuwa bado jamii yetu inaiona dhima ya msingi ya mwanamke kuwa ni kuzaa watoto (Matteru 1982);9 (ii) kuwa bado jamii yetu inauona wajibu wa kuzaa na kulea kama ni wajibu binafsi hasa kwa mwanamke na wala sio wajibu wa jamii nzima;10 na (iii) kuwa mwanamke katika jamii yetu harithi wala kumiliki chochote isipokuwa uwezo wake wa kuzaa – na kama akizaa – watoto wake.
Mbinu hizi hutumika kukidhi malengo tuliyoyadokeza hapo juu. – Mojawapo ni kupata “maisha bora” hasa katika ndoa. Kwa kweli nyimbo nyingi humwona mwanamke kama “mateka wa saikolojia ya unyonge wake” (Mohammed 1980). Wasanii hudhani kuwa mwanamke mwenyewe huitazama ndoa kama mwokozi. Kwamba anapokuwa ameolewa ndiyo anakuwa amekombolewa kutoka kwenye majanga na madhila ya kilimwengu, na anapokuwa ameachika hujuta kwa kuwa anakuwa ameadhibiwa kwa kutumbukizwa tena katika majanga ya “dunia hadaa ulimwengu shujaa.” Hapa itakumbukwa kuwa wahusika wanawake takriban wote wa nyimbo hizi ni wale walioathiri au kuathiriwa na kuvunjika kwa ndoa, au wale ambao hawajaolewa. Si aghalabu kukutana na mhusika ambaye ndoa yake ni imara au ni wa kijijini.
Hii ni kusema kuwa kuolewa, hasa na mume mwenye mali, ndiyo tamaa ya mwanamke, kwani huko ataishi raha mustarehe. Hata hivyo, kadiri nyimbo nyingi zinavyoonyesha mwanamke anapofanikiwa kuolewa na mume mwenye mali hatimaye hugundua kuwa maisha ya ndoa hiyo siyo raha mustarehe. Ama mume humsahau akamgeuza kuwa pambo au mlinzi wa nyumba akamwacha aghalabu akiteseka na huku yeye (mume) akiendelea kutumbua raha,11 au ndoa huvunjika, au mali kutoweka na mume akafilisika.
Lengo jingine ambalo mbinu hizo hutumika kulikidhi ni tamaa ya mali au utajiri. Mwanamke humlaghai mwanamume, hasa mwenye utajiri, kwa mapenzi “motomoto” au ahadi za kuolewa naye ili aweze kuchuma mali toka kwake. Aghalabu mwanamke huwa hampendi mwanamume huyo, lakini mwanamume anakuwa anampenda mwanamke. Naye mwanamke hutumia hali hiyo kujineemesha, na mara nyingi huwa hata siyo kujitajirisha bali kujisheheneza mavazi na vipodozi tu.12 Anapokuwa amekidhi haja yake, au anapobaini kuwa hawezi tena kuambua chochote kwa mwanamume huyo humpa kisogo akamsahau.
Lengo jingine huwa ni kutibua ndoa au uchumba wa watu wengine. Wasanii hawa wala hawajali kutueleza mwanamke ananufaika vipi kwa kufanya hivyo. Kinyume chake hujaribu kutuaminisha kuwa analolifanya mwanamke amelidhamiria. Tazama maneno haya kutoka wimbo wa “Mwanameka”
Quote:
Uliposikia ee ee
Kwamba Musa ameoa
Kaoa mke wa ndoa
Musa sasa katulia
Uhuni kaacha kando
Ukatumia kila uwezo,
Kuyabadili mawazo ya Musa
Quote:
                                            (Msisitizo umeongezwa)
Tumeelezwa katika beti tulizozidondoa mwanzoni jinsi Musa alivyovumilia. Lakini hatimaye tunaambiwa akapotea njia akamsimamisha Mwanameka “bila kutambua” na kuzungumza neno la mapenzi. Naye Mwanameka kusikia hivyo “akakubali bila kusita” kwani alilolitaka ndiyo hilo nalo likawa.
Matokeo ya matendo hayo ya mwanamke ni madhara. Madhara hayo huathiri mwanamume na mwanamke. Baadhi ya nyimbo huonyesha kuwa mwanamume kahasirika na mwanamke kanufaika. Katika wimbo “Mwanaidi” kwa mfano, mwanamke alinufaika akapata kujineemesha yeye na ukoo wake na mwanamume akahasirika kwani alifilisika na hatimaye hakuwa na la kufanya. Tukichunguza zaidi tunabaini kuwa kilio cha msanii ni kuwa mwanamume ni mwaminifu na mkweli wakati mwanamke ni mwongo na mwenye kujinufaisha kwa hila. Hadhira inashawishiwa imhurumie mwanamume na imbeze mwanamke.
Katika idadi kubwa zaidi ya nyimbo za aina hii wasanii hufanya juhudi ya makusudi kabisa kuonyesha kuwa ingawa mwanamume amehasirika pia, lakini mwanamke ndiye amehasirika zaidi. Mwanamke aitwaye Edita katika wimbo uitwao “Kipenzi Edita”, kwa mfano, anapewa talaka kwa kufanya “mapenzi ya pembeni.”13 Mwanamume anamkosa mke, lakini kinachosisitizwa ni kuwa mwanamke ameadhibiwa kwa kupewa talaka (rejea maelezo hapo juu).
Katika baadhi ya nyimbo wasanii hujitahidi sana kuonyesha kuwa ingawa mwanamume amehasirika, lakini pia amenufaika walau kwa kiasi kidogo. Hivyo ndivyo inavyotubainikia katika wimbo wa “Mwanameka.” Mwanamke alimsababishia mwanamume hasara maradufu: “kakosa mwana” (msingi wa ndoa) na “maji ya moto” (mapenzi). Uteuzi wa maneno katika sehemu ya mwisho ya wimbo huo, hata hivyo, umefanywa makusudi kuonyesha kuwa mwanamume amenufaika au ana liwazo. Nalo ni funzo. Tazama ubeti huu:
Quote:
Bwana Musa hatakusahau mpaka kufa
Tena amekwisha apa
Mambo ya upuuzi hataki tena
Kishaumwa na nyoka
Akiona unyasi anastuka.
Lakini mwanamke hana funzo wala haliwazwi. Badala yake anashutumiwa na kulaaniwa kwa kufanya mkasa, madhambi, na mambo ya kusikitisha. Msanii asema:
Quote:
Kweli Mwanameka
Umefanya madhambi makubwa
Mambo uliyomfanyia Bwana Musa
Yanasikitisha
Mwanameka mkasa uliofanya ni wa mwaka.
Kwa sababu ya mkasa aliofanya, tunaambiwa kuwa watu wanamdharau, wanamkashifu na kumlaani:
Quote:
Mwanameka umetuachia hadithi mtaani
Kila mmoja anashangazwa na vitendo vyako
Kila mtu anasimulia mambo yako
Ati watu wanasema… mgombanishi
Kweli watu wanasema… mhuni
Ati watu wanasema… mdanganyifu
Kwa jumla mwanamke amekuwa mhasirika mkuu wa maovu yake mwenyewe. Kwa hiyo wakati hadhira inashawishiwa imsikitikie mwanamume, inatakiwa pia imlaani na kumshutumu sana mwanamke.
Mambo mawili yanajitokeza katika uchanganuzi huu. Kwanza ni kwamba mwanamke ni mwenye tamaa, mwenye wivu, dhaifu na mwanzilishi wa matatizo katika jamii. Mwanamke hutumia jinsi yake ya kike, tena kwa hila, ili kutenda mambo ambayo huleta madhara. Katika kufanya hivyo mwanamke humshawishi mwanamume na hata hutokea akamshurutisha kwa kumghilibu akili, akamshirikisha katika kutenda maovu. Mwanamke hupania ama kujinufaisha au kutibua maisha bora ya ndoa za wenzie. Madhara yatokanayo na matendo ya mwanamke humdhuru pia mwanamume, lakini mhasirika mkuu wa maovu hayo ni mwanamke mwenyewe.
Pili ni kwamba mwanamume hahusiani na msingi wa matendo hayo maovu. Yeye hushawishiwa tu au wakati mwingine kwa hila akashurutishwa kushiriki katika maovu hayo. Yeye hana hatia. Lakini hudhurika kwa madhara yaletelezwayo na maovu ya mwanamke. Yeye, hata hivyo, aweza kuliwazwa kwa kunufaika walau kidogo, hata kama liwazo lenyewe ni kuhurumiwa tu.
Kwa hiyo hatimaye inabainika kuwa mwanamke ni mwovu, mwanamume ni mwongofu; mwanamke ni fasiki, mwanamume ni mwadilifu; mwanamke ni ibilisi, mwanamume ni malaika!
Ni vigumu kuamini kuwa wasanii wa nyimbo hizi wanaamini kwa dhati kuwa hii ni picha mojawapo ya mwanamke, Nyimbo hizi, kama kazi nyingine za sanaa, hueleza tu jinsi uyakini wa maisha unavyoakisiwa akilini mwa msanii. Lakini pia msanii huwa na uhuru wa kusawiri uakisi huo kisanaa, aweza ama kulitia jambo chuku, au kulidhalilisha ili kukidhi malengo yake ya kisanaa. Licha ya matakwa yake binafsi, msanii pia hudhaminiwa na nguvu mbalimbali za kijamii ambazo zinamzinga. Mojawapo, au zaidi ya moja, ya mambo hayo yaweza kusababisha usawiri wa aina fulani kwa kundi fulani la watu katika jamii.
Usawiri huu wa mwanamke, kwa maoni yetu, unatokana na nia ya wasanii ya kumtaka mwanamke, hasa aishiye mjini na ambaye hajaolewa,14 aendelee kukiri nguvu za mfumo wa mahusiano ya kijamii unaotawala hivi sasa. Asiwe na tamaa ya maisha bora na ya starehe, aepuke au ahimili vishawishi mbalimbali, na aheshimu pingu za maisha katika ndoa yake na zile za wenzake. Au la atasababisha madhara sawa na asababishayo Ibilisi, tena kwake yeye mwenyewe. Wasanii wanajaribu kumwadibu mwanamke kwa kubeza tabia zinazokiuka mahusiano yaliyopo. Hivyo chimbuko la mtazamo huu wa mwanamke ni hofu ya wasanii kuhusu madhara yatakayotokea endapo mwanamke atakiuka mwenendo ambao wasanii hao wanadhani ndiyo murua katika jamii. Ikiwa hofu yao yaweza kutetewa au la ni hoja inayodai mjadala ulio nje ya mipaka finyu ya makala haya.
Tanbihi
1. Kwa mfano katika wimbo uitwao “Kwini Lusi” wa Kimulimuli Jazzband.
2. Katika wimbo uitwao “Mabruki” wa Marquis Orchestra.
3. Kwa mfano katika nyimbo “Ndoa ya Mateso” wa Dar Intemational Orchestra; “Mume Wangu” wa Makassy Orchestra, na nyingine.
4. Hii ndiyo picha inayobainika katika nyimbo nyingi sana ambapo mwanamke kaltwa tausi, tunda, nyota, mwezi, ua, na mengine mengi. Mohammed (1980) ameiita picha ya “sili – sikogi – silali”.
5. Masimulizi haya yamejitokeza vizuri sana Katika Utenzi wa Adamu na Hawa uliotungwa na AbdilatifAbdalla. Rejea pia makala ya Mbughuni
6. Msichana katika wimbo “Mume Wangu”, kwa mfano, anashawishika kupuuza ushauri wa wazazi na kukatisha masomo yake kwa kutamani raha za “nyumba kubwa kama Kilimanjaro, pesa na gari” alizoahidiwa na mwanamume.
7. Mwanamke aitwae Mwanaidi katika wimbo wenye jina hilohilo wa Or- chestra Toma Toma anasukumwa na mahitaji ya kupata mali “ili kuneemesha ukoo wake”, na msukumo huo ndio unaomwingiza katika kutenda kosa.
8. Wahusika takriban wote wa nyimbo hizo huwa ama wasichana wa mjini ambao hawajaolewa au wale ambao ndoa zao zinayumba. Ni nadra sana kusawiriwa mwanamke mzazi isipokuwa pale anapolalamika kuwa kalemewa na mzigo wa kulea watoto. Aidha ni nadra sana kusawiriwa mwanamke anayeheshimu pingu za ndoa yake na za mwenzake.
9. Kwa hiyo mwanamke asiyezaa huonekana kuwa duni zaidi au asiye na thamani. Katika wimbo mmoja wa Juwata Jazz Band, mwanamke anamlalamikia mumewe aliyemfukuza akisema yeye “mwanamke gani asiyezaa”.
10. Katika wimbo uitwao “Ndoa ya Mateso”, kwa mfano, mwanamke analalamika hivi:
Quote:
Niulizieni enyi walimwengu
Huyu mwanamume sijui mume gani
Ananipa mateso huku ugenini
Na mimi nina watoto sijui ni tabu gani
Na mimi nina watoto sijui ni tabu gani.
11. Katika wimbo uitwao “Mume Wangu”, kwa mfano, mwanamke analalamika kuwa hamwoni mume nyumbani, anapika “ubwabwa, chai, chapati” lakini vinachacha. Wenzake wote wametulia na waume zao, naye alitaka mumewe atulie ili wazae, lakini bahati imemtoka. Katika wimbo “Ndoa ya Mateso” inasemekana kuwa mume anakula “makuku ya kukaanga” lakini yeye mwanamke ashindia “mkate mkavu”.
12. Kwa mfano, mtunzi wa wimbo uitwao “Esta” wa Orchestra Marquis du Zaire anadai kuwa msichana Esta “anaponzwa na ujana kwa tamaa ya mavazi” kwani kila wanapokutana hudai fedha za matumizi.
13. Katika wimbo huo ulioimbwa na Mlimani Park Orchestra kitu kinachomfanya mtunzi amtilie mashaka Edita awali ya yote ni kutokumkuta nyumbani arudipo kazini. Kwani mahali pa mwanamke aliyeolewa ni nyumbani. Kuhusu hili rejea Mbunguni (1982).
14. Kwani kama tulivyoeleza juu (tazama maelezo Na. 8) wahusika takriban wote ni wale ambao hawajaolewa na waishio mijini.
Marejeo
Abdalla, A. (1971) Utenzi wa Maisha ya Nabii Adamu na Hawaa. Oxford University Press, Nairobi.
Matteru, M.L.B. (1982) “The Image of the Woman in Tanzania Oral Literature: A Survey” katika Kiswahili, TUKI, Dar es Salaam, Juzuu 49/2.
Mbughuni, P. (1982) “The Image ofWoman in Kiswahili Prose Fiction” katika Kiswahili, TUKI, Dar es Salaam Juzuu 49/1.
Mohamed, S.A. (1980) “Mwanamke katika Ushairi wa Kiswahili” makala yasiyochapishwa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.