MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI: MUHADHARA WA NNE

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI: MUHADHARA WA NNE
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
MUHADHARA WA NNE
   SEMI
Semi ni mojawapo kati ya kumbo za fasihi simulizi. Semi hutawaliwa na sifa tambulishi mahususi. Semi hufafanuliwa kama tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo maalumu ya kijamii. Kumbo hili lina tanzu zifuatazo.
–   Methali
–   Vitendawili
–   Mafumbo
–   Misimu
–   Lakabu
–   Kauli tauria (tafsida)
(a)    Methali
Ni semi fupi za kimapokeo zinazodokeza fikra au funzo zito linalotokana na tajiriba (uzoefu wa maisha ya jamii).
Mfano:
–   Haraka haraka,haina Baraka
–   Mwenda pole,hajikwai
Mara nyingi falsafa ya methali huelezwa kwa kutumia tamathali hasa sitiari au mafumbo. Methali hubeba hekima na busara ambazo aghalabu hutumika kuonya, kuasa, kutia moyo, kuadilisha na kuadibu.
(b)    Vitendawili
Kitendawili ni usemi uliofumbwa wenye kuchochea fikra na udadisi wa mambo. Vitendawili ni sanaa inayotegemea uwezo wa mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina mbalimbali katika mazingira yake.
Mfano:
–   Wanangu wawili hushabihiana sana- (maziwa na tui la nazi)
–   Ikiwa ya moto hainyweki ikipoa hainyweki –(supu)
©    Mafumbo
Mafumbo ni kauli zenye kuchemsha bongo. Kauli hizi humtaka anayeulizwa atumie akili na udadisi kufumbua fumbo. Mafumbo ni hatua ya juu ya vitendawili.
AINA ZA MAFUMBO
Kuna mafumbo ya kuchemsha bongo na mafumbo majina.
(i)         Mafumbo ya kuchemsha bongo
Ni maswali yenye kutaka kutumia akili na ujuzi ili kujibu .Baadhi ya mafumbo ni ya kimapokeo na mengine hubuniwa na msemaji kwa lengo maalumu.
Mfano:
–   Nina kilo moja ya pamba na kilo moja ya mawe je, kipi ni kizito zaidi? (Jibu: vyote vina uzito sawa)
–   Mtu mmoja alikuwa na ng’ombe fahali wawili akitokea Kenya kuja Tanzania akiwa mpakani ng’ombe mmoja akazaa je, maziwa watakunywa watu wa wapi? (Jibu: Fahali hazai)
(ii)       Mafumbo majina
Huwa ni majina ambayo yamebeba maana fulani inayofungamana na tukio au hali iliyojitokeza kipindi cha kupatikana kwa mwenye jina hilo. Aghalabu hutumika kama njia ya kuhifadhi kumbukumbu inayohusiana na mhusika.
Mafumbo jina huweza kuwa mepesi au mazito kulingana na maana ya fumbo lenyewe lililobebeshwa kwenye jina la mhusika.
Baadhi ya mafumbo jina huwa ya kikabila.
Mfano:
–   Tabu,shida- alipatikana kwa hali hiyo
–   Mwanjaa –alizaliwa msimu wa njaa
–   Mwamvita – msimu wa vita
–   Majuto,riziki,bahati – hali husika
–   Tenahuvo – hana makuu (kipare)
–   Mwendwa – mpendwa (kibena)
–   Gumbo – njaa (kizigua)
–   Aimbora – Baraka (kimachame)
(d)    Simo/misimu
Ni semi za muda na mahali maalumu ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalumu. Misimu ikipata mashiko husanifishwa na kuingizwa katika msamiati, methali au vitendawili.
Mfano:
–   Tamutamu mahonda ukinila utakonda- (msimu uliozuka baada ya kuanzishwa kiwanda cha pombe kali cha Mahonda huko Zanzibar)
–   CCM – Chukua Chako Mapema
–   UPE – Ualimu Pasipo Elimu
–   SU – Soma Ule
(e)    Lakabu
Ni majina ya kupanga ambayo mtu hupewa au hujipa kutokana na sifa au tabia alizonazo. Majina haya hubeba maana iliyofumbwa.
Mfano:
–   Kifimbo,mchonga – Nyerer,J.K
–   Mzee Ruksa – Ali-Hasan Mwinyi
–   Simba wa vita – Kawawa
–   Mkuki uwakao – Jomo Kenyatta
(f)    Kauli tauria/tafsida
Hizi ni kauli zenye mchanganyiko au mfuatano wa sauti zinazotatanisha kuzitamka ambazo hutumiwa kupunguza utusi na ukali wa baadhi ya maneno.
Mfano:
–   Wauwao wawe wao wauwa wewe wauawa
–   Wale wali wale wali wao
–   Pema ujapo pema ukipema si pema tena
–   Ukiona neno usitie neno ukitia neno utapatwa na neno.