MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI :MUHADHARA WA KWANZA NA WA PILI

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI :MUHADHARA WA KWANZA NA WA PILI
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI
MUHADHARA WA KWANZA
FASIHI NI NINI?
Dhanna ya fasihi imekuwa ikijadiliwa kwa karne nyingi na wataalamu mbalimbali huko ulaya. Dhanna hii imekuwa ikihusishwa na neno la Kilatini Litera lenye maana ya herufi au maandishi. Neno hilo ndilo limefasiriwa kwa Kiingereza kama Literature.
Mitazamo iliyotawala dhanna hii ni mingi kama ifuatavyo:
(a)    Mtazamo wa kwanza ni ule unaodai kuwa literature ni jumla ya maandishi yote katika lugha fulani. Wellek na Warren wanauelezea mtazamo huu kwa kusema kuwa, “ One way is to define Literature as everything in Print. Wellek na Warren (1986:20)
        Udhaifu wa mtazamo huu:
(i)         Mtazamo huu unapanua sana uwanja wa fasihi na kuingiza vitu vyote ambavyo kwa kawaida watu hawavifikirii kuwa ni fasihi kwa sababu tu vimeandikwa.
Mtazamo huu unabagua sehemu kubwa ya fasihi ya ulimwengu ambayo haikuandikwa au kupigwa chapa (Ambayo ndiyo chanzo cha maandishi ya kifasihi mf. Matambiko, ngoma, majigambo, n.k).Katika taaluma ya fasihi katika Kiswahili neno Literature lilitafutiwa namna ya kuitwa na kupewa maneno kama adabu ya lugha na fasihi.
Hatimaye neno fasihi likashinda na kupewa ufafanuzi kuwa ni sanaa ya lugha bila kujali kama imeandikwa au la.
(b)    Mtazamo wa pili ni ule unaodai kuwa Literature ni maandishi bora ya jamii ya kisasa yenye manufaa ya kudumu. Hollis Summers anafafanua kuwa; The word literature in its strictness sense means more than printed words, is one of the fine arts. Mtazamo huu unaupa uzito usanii na uwezo wa kubaini fasihi kwa kuihusisha na maandishi na maandiko bora tu.
©    Mtazamo wa tatu; unaitazama Literature kama sanaa ya lugha yenye ubainifu bila kujali kama imeandikwa au la. Kwa mtazamo huu nyimbo na masimulizi ya kisanaa ni fasihi.
Mtazamo huu uliambatana na kuzuka kwa tapo la ulimbwende huko ulaya mwishoni mwa karne ya 18. Tapo hili liliathiriwa na falsafa za watu kama Kant na Hegel (Eagleton 1983:120-21). Mtazamo huu ndio unaotawala kwa sasa na unadai kuwa neno fasihi limetokana na neno la kiarabu lenye maana ya Ufasaha au uzuri wa lugha. Kwa hiyo istilahi Literature (fasihi) katika taaluma ya Kiswahili inatofautiana na istilahi Literature katika Kiingereza. Neno fasihi halihusiani na maandishi wala vitabu bali ufasaha wa kauli. Dhanna hii katika Kiswahili inazingatia aina zote za fasihi, iliyoandikwa na ile ya mdomo.
(d)    Mtazamo wa nne; ulizuka hapa Afrika Mashariki na kuenea miaka ya 1970. Mtazamo huu unadai kuwa…..Fasihi ni hisi ambazo zinajifafanua kwa njia ya lugha….. Waumini wa mtazamo huu ni John Ramadhan, Balisidya,A na Sengo na Kiango katika Hisi Zetu. Mtazamo huu unachanganya mambo matatu ambayo ni fasihi yenyewe, mambo yaelezwayo na fasihi na mtindo wa fasihi ya Kiswahili. Fasihi huweza kuelezea hisi, kadhalika mtindo wa kifasihi mara nyingi ni wa kihisiya bali fasihi yenyewe si hisi.
–   Vivyo hivyo fasihi huweza kuelezea mapenzi lakini fasihi yenyewe si mapenzi.
(e)    Mtazamo wa tano; ni wa karne hii ulioanzishwa na wafuasi wa nadhariya ya umbuji (formalism). Mtazamo huu ulianzishwa na wanaisimu wa Kirusi mwanzoni mwa karne hii miongoni mwao akiwa Boris, Tomashevski, Roman Jakobson na Victor Shklovski. Hawa wanadai kuwa fasihi ni tokeo la matumizi ya lugha kwa njia isiyo ya kawaida ili kuleta athari maalumu. Kwa mujibu wa watu hawa, fasihi hukiuka taratibu za kawaida za matumizi ya lugha katika sarufi ili kumvutia msomaji au msikilizaji.
Lugha ya kifasihi humfanya msomaji aitafakari lugha yenyewe badala ya kutafakari tu ujumbe unaowasilishwa na lugha hiyo.
  Udhaifu wa mtazamo huu
(i)         Unaelemea mno upande wa fani na kupuuza maudhui
(ii)       Unasadifu zaidi ushairi kuliko fani nyingine za fasihi
Kwa maelezo yote yaliyotolewa tunaweza kuhitimisha kuwa fasihi ni sanaa itumiayo maneno teule ya lugha yenye ubunifu inayojaribu kusawiri vipaji vya maisha, mahusiano na hisiya za watu katika miktadha mbalimbali.
CHIMBUKO LA FASIHI
Kuhusu chimbuko la fasihi wataalamu mbalimbali wametoa hoja zao na kuibua nadhariya kadhaa:
  1. Nadhariya ya kidhanifu; nadhariya hii hujiegemeza kwenye dhanna zisizoweza kuthibitishwa kisayansi. Nadhariya hii inadai kuwa chimbuko la fasihi niMungu.
Nadhariya hii ndiyo kongwe na ilikuwepo tangu kabla ya Kristo na ilitumiwa sana na Wayunani wa huko Ulaya ambao waliamini sana miungu kama wa Ushairi na Muziki ambao waliwaita Muse.
Miungu hawa waliaminika ndio waliowapa watunzi Muhu au Kariha (Msukumo) wa kiroho, nafsi na kijazba wa kutunga kazi zao.
Wanaounga mkono nadhariya hii wanadai kuwa Mungu ndiye msanii mkuu na wa kwanza. Wasomi wa kale waliounga mkono nadhariya hii ni Hesiod, Plato, Aristotle na Socrate.
Udhaifu wa nadhariya hii:
(i)         Nadhariya hii inakataa kuwepo kwa dhanna ya ubunifu kwa watunzi
(ii)       Haichochei kujiamini kwa wasanii na huwafanya wajione kama waigaji tu wa mambo yaliyofanywa na Mungu
(iii)     Huwafanya wasanii waonekane ni watu waliokaribu sana na Mungu kuliko binadamu wengine
(iv)       Huibua dharau miongoni mwa wasanii na kusababisha wajitenge na jamii ya kawaida
     DHIMA YA FASIHI
Fasihi ni sanaa itumiayo maneno teule ya lugha kufikisha ujumbe kwa jamii. Hivyo fasihi ina dhima (wajibu/majukumu) mbalimbali kwa jamii kama ifuatavyo:
v Kuelimisha jamii kupitia vipengele mbalimbali kama nyimbo,hadithi,ngoma,nk
v Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii katika vizazi mbalimbali vya jamii.
v Kuburudisha jamii na kuifanya ijisahaulishe madhila mbalimbali yanayoikuta jamii
v Kukuza na kuendeleza lugha ya jamii.
Hata hivyo unapojadili dhima ya fasihi huna budi kuzingatia dhanna ya utabaka na itikadi.
Tabaka; ni makundi ya watu yanayounganishwa na uhusiano wao na njia za uzalishaji mali na mfumo wa mamlaka katika jamii.
Itikadi; inafafanuliwa kuwa ni imani juu ya yale yasemwayo na jamii na kuyaamini yale yanayohusiana na mahusiano ya kiutamaduni ya jamii tunamoishi.
Dhanna ya utabaka na itikadi zinajitokeza katika fasihi kwa sababu zifuatazo:
(i)         Kwanza fasihi hufungamana na muktadha (mazingira maalumu ya kijiografia), kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na hivyo kila kazi ya fasihi ni zao la muktadha ulioizaa kazi husika.
(ii)       Pili, fasihi hudhihirisha aina fulani ya urazini (kujitambua kibinadamu/kuwa na utashi) na utambuzi wa hali ya maisha alionao mtunzi pamoja na wale anaowawakilisha.
(iii)     Tatu; zipo jamii za aina mbili nazo ni jamii zenye usawa na mshikamano ambazo hazina matabaka nazo huitwa jamii zenye utabaka usio wa kinyonyaji mfano jamii za wavuvi, wafugaji, wakulima, n.k. katika jamii hizo fasihi zao zitabeba dhima tofauti.
Kwa ufafanuzi huo waweza kubaini kuwa kwa ujumla dhima ya fasihi inajikita katika mambo yafuatayo:
–   Itikadi, utamaduni, falsafa, uchumi, siasa, nk.
(a)    Dhima ya itikadi
Kila jamii hutawaliwa na itikadi fulani ambayo ndiyo huzalisha misimamo ya jamii husika katika uzalishaji mali. Kila mtunzi wa fasihi mtiifu kwa jamii yake lazima ataathiriwa na itikadi ya jamii yake na hatimaye utunzi wake kuwa na mwelekeo wa utetezi wa itikadi iliyommeza.
 Mfano:
–   Kipindi cha ukoloni watunzi wengi walibanwa na itikadi za kikoloni na kujikuta wakitetea tabaka la wakoloni. Mifano ya kazi za fasihi kama Mashimo ya Mfalme Suleman, Uhuru wa Watumwa, Hekaya za Abunuwasi, n.k.
Maandishi hayo yalijaribu kutetea itikadi ya ukoloni kwa kuwaonesha wakoloni wa kizungu kama watu wenye uwezo wa hali ya juu, wema na wachapakazi, wenye akili nyingi waliojua kukomboa na kumuendeleza mwafrika. Pia maandishi hayo yalisisitiza maadili ya utii ambao ulisaidia watawala kuwadhibiti watawaliwa kimawazo.
(b)    Dhima ya kiuchumi
Dhima ya fasihi katika uchumi huonekana zaidi kupitia nyimbo za kazi ambazo hutungwa ili ziimbwe wakati wa kufanya kazi ngumu. Mfano: kazi kama kulima, kutwanga,kuvua samaki,kuwinda na shughuli nyingine.
Katika uchumi wa kibepari dhima ya fasihi ilijikita zaidi kwenye kuburudisha,kutafuta pesa kwa kurekodi na kuuza kazi za fasihi. Ni katika kipindi hiki palizuka fasihi pendwa iliyojikita kwenye kujipatia pesa zaidi na kusahau maadili ya jamii.
©    Dhima ya kiutamaduni
Katika dhima hii fasihi ina majukumu yafuatayo:
–   Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii
–   Kuburudisha
–   Kukuza lugha
–   Kuelimisha,kuasa na kurekebisha jamii.
Amali za jamii ni pamoja na mila, desturi, mtindo wa maisha, imani, jiografia, visasili, maarifa ya kijadi n.k.
Amali hizi huweza kuendelezwa na kuhifadhiwa katika fasihi na kurithishwa vizazi vijavyo. Kwa mfano; Tamthiliya ya Kinjeketile imehifadhi mengi kuhusu hali ya maisha wakati wa ukoloni wa kidachi. Kurwa na Doto hali kadhalika, Bwana Muyombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali, Mirathi ya Hatari na Mashetani ni kazi za fasihi zilizohifadhi amali nyingi sana za jamii za kiafrika hasa Tanzania.
Fasihi hasa nyimbo na visasili hutumika kukoleza shughuli za kijamii kama ibada,matambiko,sherehe, n.k. Nyimbo licha ya kuburudisha pia hubeba ujumbe kuhusiana na tukio husika.
Kinafsiya fasihi pendwa kwa mfano ile ya masaibu na vituko vya ujambazi na uhalifu humpa msomaji imani kuwa anashuhudia na kushiriki katika matukio ya ushujaa yanayosimuliwa na hivyo kusisimua mwili na kuridhisha ari yake ya kujihusisha na matendo ya kishujaa.
Malighafi ya fasihi ni lugha, kwa kadiri lugha inavyotumiwa na kufinyangwa na watunzi ndivyo inavyokua na kupanuka. Maneno mengi yanayotumika katika utunzi wa mashairi, riwaya, nyimbo na tamthiliya hufanya lugha ikue. Kwa mfano: katika sanaa ya ushairi maneno kama vina na mizani, mshororo, muwala, tathilitha, takhmisa, tarbia, n.k huchochea ukuaji wa lugha katika jadi ya ushairi ambao huchukuliwa kama ghala la maneno.
Fasihi hubeba elimu za kila aina, baadhi ya watunzi ni mabingwa wa kuonesha ufundi katika maandishi. Mfano: maandishi ya Ngugi wa Thiong’o kama vile Petals of Blood na Nitaolewa Nikipenda vilevile Alamin Mazrui katika: Kilio cha Haki, na F. Katalambula katika Simu ya Kifo husawiri vizuri mandhari ya kijiografia na maneno yaliyokuza watunzi na ujuzi wao katika kumudu lugha.
Hadithi za kisayansi kwa mfano: Jina langu ni Sifuri na Kipeo na Kipeuo na Mahakamani zimekusudia kuwafundisha watoto dhanna hizo za kisayansi kwa njia ya kisanaa.
Elimu ya ukweli sharti iambatane na tabia ya uchunguzi, uchambuzi na udadisi. Tabia hiyo ni usomaji wa uhakiki wa fasihi ya msomaji ambayo humsaidia msomaji kupanua upeo wa kudadisi na kukosoa.
Fasihi hutoa maonyo, huasa na kuiadilisha jamii ili iendane na mila na desturi za jamii husika mfano: hadithi kama vigano vyenye kuhusu tabia za fisi husaidia watoto kujirekebisha kitabia.
(d)    Dhima ya kisiasa
Fasihi imetumika sehemu nyingi sana kuendeleza au kudumaza harakati za kisiasa nchini Tanzania kwa mfano; fasihi imetoa mchango mkubwa sana kupitia ngonjera za Azimio La Arusha. Nyimbo za kizalendo kama Tanzania, Tanzania na Tazama ramani, ni miongoni mwa kazi za fasihi ambazo zimetoa mchango katika siasa. Hadi sasa nyimbo za kizazi kipya zinaendelea kushughulika na siasa mifano ipo mingi ila kwa uchache tu: Ndio Mzee na Sio Mzee (Joseph Haule/Prof.Jay), Tanga Kunani Pale? (Wagosi wa Kaya), Muungano CCM na CUF (Juma Kassim/Juma Nature) n.k
(e)     Dhima ya kifalsafa
Baadhi ya kazi za fasihi hujaribu kuelezea falsafa fulani kuhusu maisha. Falsafa hiyo watunzi wengine huita ukweli wa maisha ingawa si kila wakati ukweli huo hukubalika kwa wote.
Kazi za fasihi za kifalsafa huchambua masuala mazito kuhusu maisha ya mwanadamu duniani na hatima yake. Fasihi hii huchochea wasomaji na wasikilizaji kutafakari masuala hayo kwa umakini na undani zaidi.
Mifano ya fasihi za kifalsafa ni Utenzi wa Al-Inkishafi, Nagona, Mzingile, Karibu Ndani, Kusadikika, Kufikirika, Rosa Mistika, n.k