MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - UHAKIKI WA FONIMU NA MIUNDO YA SILABI ZA KISWAHILI

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: UHAKIKI WA FONIMU NA MIUNDO YA SILABI ZA KISWAHILI
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
UHAKIKI WA FONIMU NA MIUNDO YA SILABI ZA KISWAHILI
Utangulizi
Makala hii imechochewa na swali la Mwangi (2007:93) alipouliza iwapo alofoni zipo au hazipo katika Kiswahili. Katika utangulizi wa makala yake, anaibua masuala mengine ambayo yanaonekana kuwa tata na huenda hayajapata kutatuliwa na wanaisimu wa Kiswahili. Suala mojawapo ni kuhusu idadi kamili ya fonimu konsonanti za Kiswahili na vilevile aina zake. Wanaisimu mbalimbali wanaelekea kutambua idadi ya fonimu konsonanti za Kiswahili kwa namna tofautitofauti, kama vile: 32 (Ashton, 1951), 33 (Whiteley, 1956), 29 (Polome, 1967), 29 (Nchimbi, 1995), 24 (Mgullu, 1999), 25 (Habwe na Karanja, 2004), 25 (Kihore, Massamba na Msanjila, 2009), 25 (Obuchi na Mukhwana, 2010), 26 (TATAKI, 2013) na 25 (Akidah, 2013).
Tofauti katika idadi ya fonimu konsonanti za Kiswahili zinawakanganya wasomaji na ndizo zinazoelekea vilevile kuchangia midhihiriko tofautitofauti ya idadi ya miundo ya silabi za Kiswahili pamoja na mifano kinzani inayotolewa. Ukinzani huo hutokea kwa sababu, msingi wa uundaji silabi aghalabu hutokana na fonimu ambayo inaweza kuwa ya herufi moja ya kujisimamia pekee au mwambatanisho wa herufi zinazoweza kutamkwa kwa pamoja kama sauti moja (Mgullu, 1999: 72). Iwapo idadi ya fonimu inatofautiana kama tunavyoona katika makala mbalimbali za wanaisimu wa Kiswahili basi maelezo kuhusu miundo ya silabi za Kiswahili pia yatazidi kutofautiana kama tunavyoona katika kazi za baadhi ya wanaisimu kama vile: silabi 4 (Nchimbi, 1995), 7 (Mgullu, 1995), 6 (Habwe na Karanja, 2004), 5 (Mwita, 2009) na 8 (Obuchi na Mukhwana, 2010).
Katika kufafanua ipasavyo mada hii kuhusu fonimu na miundo ya silabi za Kiswahili, makala hii imeongozwa na madhumuni mawili makuu: kwanza, kuhakiki maandishi mbalimbali kuhusu idadi na mifano faafu ya fonimu za Kiswahili. Pili, kuhakiki maandishi kuhusu idadi ya miundo ya silabi za Kiswahili na mifano yake. Madhumuni haya yamelengwa katika makala hii kwa sababu maandishi mbalimbali ya kiisimu katika Kiswahili yanaelekea kuonyesha tofauti nyingi katika idadi ya fonimu konsonanti na idadi ya miundo ya silabi za Kiswahili. Aidha, mifano inayotolewa kuhusu fonimu na silabi pia huelekea kuwakanganya wasomaji kila mara. Kwa hivyo, wanaisimu mbalimbali wanaelekea kuwa na mitazamo inayotofautiana kuhusu dhana mbalimbali katika fonetiki na fonolojia ya Kiswahili.
Dhana ya Fonimu
Istilahi fonimu imefafanuliwa na wanafonoloja mbalimbali. Trubetzkoy (1969:19) anaieleza fonimu kama ishara ya kifonolojia yenye uamilifu. Vilevile, fonimu huweza kurejelewa kama kundi la sauti katika lugha lenye sauti muhimu na sauti zinazohusiana nayo na zinazoweza kutumiwa pahali pake katika miktadha mingine maalum (Jones, 1975 akirejelewa na Mgullu, 1999: 51). Fonimu ni kipashio msingi cha kifonolojia kinachotumiwa kubainisha maana za maneno katika lugha (Lyons, 1981: 84; Yule, 1996: 54; Batibo, 2000: 161). Kwa mfano, fonimu /a, e, i, o, u/ zina uwezo wa kubadilisha maana katika maneno. Mathalani, maneno pata na peta yanatofautiana kimaana kwa sababu ya tofauti za fonimu /a/ katika pata na /e/ katika peta. Tunapotumia njia ya mlinganuo finyu ambapo mtindo wa nitoe nikutoe hutumika, basi fonimu /p, t, a/ hutoana huku /a/ moja katika pata na /e/ katika peta husalia kama inavyojidhihirisha katika mifano ifuatayo:
Pata = /pa/ / t a/ = /a/
Peta = /pe / /t a/ = /e/
Kwa kuwa fonimu /a/ na /e/ hazitoani, maana za maneno hayo huelekea kutofautiana vilevile. Pata humaanisha ‘kuwa na jambo, hali au kitu’ (TUKI, 2004: 329) na peta humaanisha ‘rusharusha nafaka katika kitunga au ungo ili kuondoa makapi na takataka’ (TUKI, 2004: 333).
Fonimu huwa akilini mwa mtu na aghalabu huhusiana na vivuli vyake au alofoni zake kama vile fonimu /p/ ina kivuli chake /ph/ (Fromkin, Rodman na Hyams, 2007: 261). Kwa jumla, fonimu humaanisha sauti ya lugha au kipashio kidogo dhahania cha lugha chenye uwezo wa kubadilisha, kuvuruga au kuleta maana kusudiwa ya neno (Batibo, 2000:161; Fromkin na wenz., 2007: 266). Fonimu inapotumia alama ya mishazari miwili (/ /) kuonyesha???? mipaka yake, alama ya mabano mraba [ ] hutumiwa kuonyesha foni ya lugha au sauti zozote za lugha ya binadamu (Mgullu, 1999: viii; Fromkin na wenz., 2007: 261).
Batibo (2000: 161-2) anaeleza dhima anuwai za fonimu kama vile: kwanza, husaidia katika uundaji wa maneno ya lugha. Kwa mfano, fonimu irabu /a/ huweza kutumiwa pamoja na fonimu konsonanti /p, t/ na hatimaye kuunda silabi {pa} na {ta}. Silabi hizi za {pa} na {ta} huunda neno pata. Pili, fonimu huonyesha ujumisia katika maana za maneno hasa katika matumizi ya onomatopeya na vihisishi. Tatu, fonimu husaidia katika kubainisha maana za maneno ya lugha kama tunavyoona katika kamusi za lugha husika.
Hatua za Kufafanua Fonimu Kifonolojia
Fonimu hufafanuliwa kifonolojia kupitia hatua mbalimbali (Batibo, 2000: 182-8) kama vile: kwanza, kuwa na hifadhi maalum ya sauti zilizokusanywa na kuziandika kwa kutumia hati ya unukuzi makinifu ya kimataifa kama vile /ʧ (ch), ɲ (ny), ɳ (ng’), θ (th), ʃ (sh), ð (dh), ɤ (gh)/. Pili ni kutambua familia za fonimu kwa kuziweka pamoja fonimu irabu na konsonanti na aina zake. Tatu ni kuainisha fonimu kwa mujibu wa sifa bainifu za kifonetiki na kuwasilisha aina zake katika majedwali au mpangilio maalum. Vilevile, kuna kufafanua fonimu husika kwa mujibu wa sifa bainifu za kiarudhi kama vile mkazo, silabi na toni.
Miainisho mbalimbali ya Fonimu za Kiswahili
Mgullu (1999: 69) anadokeza kuwa lipo tatizo la ufumbuzi wa idadi kamili ya fonimu konsonanti za Kiswahili hasa lile tatizo la mwambatanisho wa sauti. Anaongeza pia kuwa kuna wanaodai kwamba sauti kama vile [n] na [d] zikifuatana huunda fonimu moja /nd/. Chimbuko la dai kama hili ni ile hali inayodhihirika miongoni mwa fonimu kama vile /t/ na /h/ zinazotamkwa kama sauti moja na hatimaye kuchukuliwa kama fonimu mwambatano /th/. Aidha, inadhihirika wazi katika fonolojia ya Kiswahili kuwa kuna kutofautiana baina ya wanaisimu kuhusu idadi sahihi na kamili ya vipandesauti vya Kiswahili (Mwangi, 2007:93). Hivyo basi, wanaisimu mbalimbali wa Kiswahili wanaelekea kutoa idadi na pia mifano tofautitofauti kuhusu fonimu konsonanti za Kiswahili kama vile:
Ashton (1951:3-4): /p, b, m, w, mb, f, v, mv, th, dh, j, t, d, s, z, n, r, l, nd, nz, ch, sh, nj, ny, y, k, g, kh, gh, ng’, ng, h/ = 32
Whiteley (1956:9): / , , , , , , , , , t, t , d, n, r, l, s, , nt, nd, ch, ch , j, sh, n , ny, y, k, k , g, ng’, nk, ng, h/ =33
Polome (1967:38-9): /p, ph, , t, th, d, c, ch, Ɉ, k, kh, g, , , θ, ð, s, , š, ɤ, h, , n, ɲ, ɳ, l, r, , / =29
Nchimbi (1995:35): / , t, ʗ (ʧ), k, , d, Ɉ, g, , ɲ, ɳ, n, , θ, s, ʃ, h, , ð, , r, l, , , ɤ, , nd, ng, nj/ =29
Mgullu (1999:67): / , ʧ (ch), d, ð (dh), , g, ɤ (gh), h, k, l, , n, ɲ (ny), ɳ (ng’), , r, s, ʃ (sh), t, θ (th), Ɉ ( ), , , x (kh)/ =24
Habwe & Karanja (2004:49): / , , , , ƒ, , θ, ð, t, d, l, r, n, s, , Ɉ, ɲ, , ʃ, ʧ, k, g, ɳ, ɤ, h/ =25
Kihore na wenz. (2009:16): / , ch, d, ð, ƒ, g, ɤ, h, , k, l, , n, ɲ, ɳ, , r, s, sh, t, θ, v, w, y, z/ = 25
Obuchi na Mukhwana (2010:84): / , , , θ, t, l, n, , ɲ, ʃ, k, ɳ, h, , , , ð, d, r, s, , y, ʧ, g, ɤ/ =25
TATAKI (2013: xvi): / , ʧ, d, ð, f, g, ɤ, h, Ɉ, k, x, l, , n, ɳ, ɲ, , r, s, ʃ, t, θ, , , , / = 26
Akidah (2013: 3-4): /p, b, m, f, v, θ, ð, t, d, n, ɲ, s, z, l, r, j, ʃ, k, g, tʃ, ŋ, ɣ, h, w, y/ = 25
Wanaisimu hawa waliorejelewa wanakubaliana kuwapo kwa fonimu irabu 5 msingi za Kiswahili yaani /a, e, i, o, u/. Hata hivyo, wanatofautiana katika idadi ya fonimu konsonanti. Ashton (1951) na Whiteley (1956:9), wanaainisha jumla ya fonimu konsonanti za Kiswahili 32 na 33 mtawalia. Ingawa Polome (1967:38-9) anaainisha fonimu konsonanti 29 za Kiswahili, idadi inayolandana na ya Nchimbi (1995:35), kazi yake haitambui sauti [mb, ng, nj, nd] kama fonimu za Kiswahili ambazo zinatambuliwa na Nchimbi.
Kwa mujibu wa Polome (1967), sauti [mb, ng, nj, nd] si fonimu licha ya kwamba zinaundwa na fonimu konsonanti /m, n/. Hata hivyo, anaendelea kudokeza kuwa fonimu hizi za /m, n/ aghalabu huambatana na konsonanti /b, g, j, d/ katika uundaji wa silabi. Badala yake Polome anaongeza hoja ya kuwapo kwa fonimu nyingine hasa /ph, c, kh, š/ katika msururu wa idadi ya fonimu za Kiswahili. Kwa kweli [ph, kh, š] si fonimu bali ni alofoni, na sauti [c] haipo katika msururu wa fonimu za Kiswahili sanifu. Ile fonimu inayodhihirika katika Kiswahili ni /ch/ inayoonyeshwa kifonetiki kama /ʧ/. Vilevile, wanazuoni wengine wanazungumzia idadi tofauti ya fonimu konsonanti kama vile fonimu 24 (Mgullu, 1999), fonimu 25 (Habwe na Karanja, 2004; Kihore na wenz., 2009; Obuchi na Mukhwana, 2010; Akidah, 2013), na fonimu 26 (TATAKI, 2013).
Makala hii inaegemea mtazamo wa skuli ya Nchimbi (1995:35) na wafuasi wake kwamba kuna fonimu konsonanti 29 za Kiswahili zikiwemo sauti ng’ong’o [mb, ng, nj, nd]. Mtazamo huu unaungwa mkono na Simala (1995:48). Aidha, sauti hizi ziliwahi kutambuliwa na Ashton (1951) na Whiteley (1956). Ingawa Obuchi na Mukhwana (2010:84) hawaorodheshi [mb, ng, nj, nd] kama fonimu konsonanti za Kiswahili, kwa upande mwingine wanatambua kuwapo kwa dai kwamba sauti hizi hutumika licha ya kwamba hazijawakilishwa kwa ishara maalum za kifonetiki. Hata hivyo, zile alama za kifonetiki wanazodokeza kuwa hazijabuniwa zipo kama vile [ ƅ ( ), Ŋ (nd), N (ng), Ɲ(n )] (Nchimbi,1995:35). Vilevile, fonimu hizi tayari zimetambulika na alama za kuziwakilisha kupendekezwa kama vile: /nd/ = /nd/, /mb/ = /mb/, /ng/ = /ng/ na /nj/ = /nj/ (Mwita, 2007:65).
Utambuzi wa fonimu za Kiswahili ungali unaendelea na fonimu zenyewe hufaa kurekodiwa mara kwa mara zinapotambuliwa (Choge, 2009:64). Iwapo hakuna alama katika orodha ya alama za unukuzi makinifu ya kimataifa basi alama mpya au alama saidizi huweza kubuniwa na wanaisimu wa lugha husika (Lyons, 1981:69). Alama saidizi hutumika hata katika lugha nyinginezo za Afrika, Amerika Kusini, Asia Kusini na Pasifika kuwakilisha fungu fonimu zilizokubalika kama vile fonimu /᷇mb, ᷇nd/ zinazotamkwa kama sauti moja (Anderson, 1976 akirejelewa na Mwita, 2007:65).
Isitoshe, utambuzi wa fonimu za lugha hauna kikomo. Hii ndiyo sababu Choge (2009:64) anasema kuwa utambuzi na uwekaji rekodi za fonimu za Kiswahili ungali unaendelea. Utambuzi huo wa fonimu za Kiswahili huonekana katika sauti kama vile /Ɲ, Ŋ, <b, N/ (Nchimbi, 1992 akirejelewa na Choge, 2009:64). Katika kuonyesha kuwa utambuzi wa fonimu ungali unaendelea, Choge (2009:64) anatambua fonimu irabu nyingine za Kiswahili kama vile irabu ndefu /i:, ɛ:, a:, u: & כ:/ na irabuunganifu /au & כa/ na kuzidhihirisha katika data maalumu.
Kanuni za Utambuzi wa Fonimu
Kuna kanuni maalum zilizoangaziwa na Trubetzkoy (1969:56-58) za kufafanua na kutambua sauti mahususi na sauti mwambatano zinazopaswa kurejelewa kama fonimu moja. Kanuni hizo ni:
  1. ‘Mwambatanisho tu wa sauti ambazo vijenzi vyake katika lugha havijasambaa hadi silabi nyingine ya pili zichukuliwe kama fonimu moja inayotambulika’ (Tafsiri yetu).
Kwa mujibu wa kanuni hii, sauti mwambatano (sauti yenye herufi mbili au zaidi) hufaa kudhukuriwa kama fonimu iwapo sauti zenyewe hazijasambaa katika silabi nyingine ya neno. Kama vile neno ngoma lina fonimu nne /᷇ng, o, m, a/ zinazounda silabi mbili za /$᷇ngo$ma$/. Kinachodhihirika hapa ni kuwa sauti mwambatano /᷇ng/ huunda silabi ya kwanza $᷇ngo$ na hakuna sehemu yake nyingine inayosambaa hadi silabi ya pili $ma$.
  1. ‘Sauti mwambatano huweza kufasiriwa kama fonimu moja iwapo imetamkwa katika sehemu moja ya utamkaji au kutokana na urahisishaji wa utamkaji changamano’ (Tafsiri yetu).
Kanuni hii ndiyo inachangia ubunaji wa alama moja ya kuwakilisha fonimu kama vile /ʧ (ch), ɲ (ny), ɳ (ng’), θ (th), ʃ (sh), ð (dh), ɤ (gh). Fonimu hizi mwambatano hudhihirika hata katika lugha nyinginezo za kigeni kama vile Kiingereza (Lyons, 1981; 79). Tukumbuke kuwa licha ya kwamba fonimu hizi zinalandana katika takriban lugha zote ulimwenguni ikiwemo Kiswahili na lugha nyinginezo, hakuna kosa iwapo lugha nyingine mahususi zitadhihirisha vilevile fonimu za ziada zenye herufi mwambatano tofauti hata hivyo zinazotamkwa kama sauti moja.
Labda kile kinachopaswa kuelezwa kwanza ni kwa namna gani sauti /ch, ny, ng’, th, dh, gh/ zichukuliwe kama fonimu moja licha ya kuwa na herufi mbili na sauti [nd, nj, ng, mb] ambazo pia huundwa na herufi mbili zisidhukuriwe kama fonimu moja. Mathalani, katika Kiswahili, fonimu [h] huweza kuungana na fonimu nyingine ili kuunda fungu fonimu kama vile /θ (th), ʃ (sh), ð (dh)/ (Ontieri, 2015: 2525). Muungano huu hutakona na hali ya utamkaji na pia mahali pa kutamkia sauti hizi iwapo zinapatikana katika mazingira yaleyale. Mathalani, sauti ng’ong’o hutamkika kwa kung’ong’oeshwa katika sehemu ya utamkaji inayojulikana kama chemba ya pua (Coxhead, 2006:3).
Utamkaji wa sauti kama hizi umeangaziwa na Lyons (1981:74) anapodokeza kuwa sauti [b, p, m], [d, t, n], na [g, k, ɳ (ng’)] zinahusiana kifonetiki au kimatamshi kwa namna inayolingana. Sauti [b, p, m] hutamkika mdomoni huku [b, m] zikiwa ghuna na [p] sighuna. Hivyo basi, ni rahisi kwa sauti ghuna [m, b] kutamkika kama sauti moja na hatimaye kuunda fonimu moja /mb/. Kwa upande mwingine, sauti [d, t, n] hutamkika kwenye ufizi hata hivyo [n, d] ni sauti ghuna na [t] sighuna. Hivyo basi, sauti [n, d] huweza kufuatana na kutamkika kama sauti moja na hatimaye kuunda fonimu moja /nd/ kama katika neno nda-ma. Aidha, sauti [g, k, ɳ (ng’)] hutamkika kwenye kaakaa laini hata hivyo sauti /g, ɳ (ng’)/ ni ghuna ilhali sauti [k] sighuna. Sauti hizi aghalabu hukubali mfuatano na sauti [n] inayotamkika kwenye ufizi na hatimaye kuunda sauti moja kama vile [ng] kama tunavyoona katika neno ngo-ma. Fafanuzi hizi huweza kuonyeshwa kwa njia ifuatayo:
Sauti za midomo: [b, m] ghuna [p] sighuna
Sauti za ufizi: [d, n] ghuna [t] sighuna
Sauti za kaakaa laini: [g, ɳ (ng’)] ghuna [k] sighuna
Kutokana na fafanuzi hizi, imebainika kuwa sifa ya sighuna ndiyo hufanya sauti [p] ikitanguliwa na sauti [m] kutounda fonimu moja bali hudhihirisha fonimu mbili tofauti kama vile /m/ na /p/ zinazodhihirika katika maneno kama vile: m-pa-ka. Katika mfano huu, /m/ husalia kama fonimu ya kipekee iliyo na sauti yake maalum huku fonimu /p/ ikiambatana na /a/ ili kuunda silabi {pa}. Aidha, sifa ya sighuna ya sauti [t] ikitanguliwa na sauti [n] ndiyo huchangia kuundwa kwa fonimu mbili kama vile /n/ na /t/ kama katika neno n–ta.
Kihore na wenz. (2009: 26-7) wanaeleza kuwa kule kuathiriana kunakotokea baina ya sauti nazali [m, n] zenye maumbo tofauti na sauti nyinginezo zisizo za nazali kama vile [b, d, g] aghalabu huchangia uundaji wa maneno kama vile mbawa, ndugu na ngoma. Tunachoweza kujifunza kutokana na maelezo ya Kihore na wenzie ni kwamba nazali hizi kimsingi zinaathiriwa na konsonanti fuatilizi kama vile [m] huathiriwa na [b], na [n] huathiriwa na [d, g]. Kihore na wenz. (2009: 32) wanaendelea kueleza kuwa kwa vile sauti [b] hutamkika kwa kufunga mdomo, nazali [m] vilevile huathirika kwa kutamkwa kwa kufunga mdomo. Hivyo basi, umbo tofauti linaloundwa kwa maoni yetu bila shaka litakuwa [mb]. Kwa upande mwingine, sauti [d] inayotamkika kwenye ufizi huathiriana na [n] ya ufizi na hatimaye kuunda umbo jipya tunaloita [nd]. Konsonanti [g] ya kaakaa laini hulazimisha sauti [n] ya ufizi kutamkika kwenye kaakaa laini na hatimaye kuunda sauti [ng]. Mifanyiko hii yote hurejelewa kama usilimishwaji wa konsonanti.
Isitoshe, Kihore na wenz. (2009:32) wanatuhadharisha kuwa ingawa sauti hizi za [m, n] zinaathiriana na sauti [b, d, g], isichukuliwe kuwa zinawakilisha sauti moja bali zinawakilisha sauti mbili tofauti. Hata hivyo, wanajipinga wenyewe wanaposema kwingine kuwa sauti hizi mwambatano yaani [mb, nd, ng] hutamkwa kwa pamoja kama sauti moja kama tunavyoona katika dondoo lifuatalo:
‘Ingawa mfuatano huu wa herufi hufanana na mfuatano tuliouelezea hapo juu lakini kila moja ya herufi zinazoandamana hapa ni sauti inayojitegemea kwa dhati yake ingawa hutamkwa kwa pamoja’ (Kihore na wenz., 2009:32).
Kimsingi, sauti hizi ng’ong’o za [mb, nd] huundwa kutokana na mchakato wa usilimishwaji unaoitwa kama unazalishaji. Unazalishaji hurejelewa kama utamkaji ambapo kitamkwa kisichokuwa nazali hupata sifa za unazali (TUKI, 1990:41). Utafiti unadhihirsiha kuwa sauti zinazoundwa kutokana na usilimishwaji hufaa kurejelewa kama sauti moja japo huundwa na sauti mbalimbali. Ithibati zinatolewa na Mwita (2007:64) kuwa: kwanza, sauti hizi mwambatano zinafanana na vikwamizwa katika muundo wa ndani. Pili, sauti hizi ni vitamkwa pamwe vinavyotamkwa katika pahali pamoja. Tatu, sauti hizi hufanya kazi katika uundaji wa silabi moja husika yaani hushiriki katika uundaji wa silabi moja maalum.
Aidha, Higgins (2012: 48) anadhihirisha unazalishaji wa sauti ng’ong’o kuwa iwapo nazali [m] imetanguliza [b] basi unazalishaji wa [b] hutokea na kuunda fungu fonimu /mb/. Kwa upande mwingine, iwapo nazali [n] imetanguliza [d] basi unazalishaji wa [d] hutokea na hatimaye kuunda fungu fonimu /nd/. Hata hivyo, tunatahadharishwa kuwa sauti zenye herufi mbili zinaweza kudhukuriwa kuwa sauti tofauti iwapo matamshi yake yanasambaa katika silabi nyingine na hali hiyo huweza kutambuliwa (Mwita, 2007:65).
iii. ‘Sauti mwambatano huweza kudhukuriwa kama fonimu moja iwapo haichukui muda zaidi kutambulika kuliko fonimu nyingine zinazojitokeza katika lugha hiyo husika’ (Tafsiri yetu).
Sauti mwambatano ni fonimu iwapo muda unaochukuliwa kuitambua unalingana na sauti nyingine katika lugha husika. Kanuni hii inaonyesha kuwa fonimu za lugha zinaelekea kuchukua muda unaolingana hata hivyo ule wa kutamkwa kwa fonimu huweza kuathirika kutokana na mkazo. Kanuni hii hudhihirika hata katika kila silabi ambayo hupimwa kwa kutumia sehemu moja ya mia ya sekunde (1/100) inapotamkwa na huchukua muda mrefu kutamkwa inapowekewa mkazo (Mwansoko, 1995:16). Mathalani, mfuatano wa fonimu katika Kiingereza kama vile /mp, mb/ huchukua muda sawa wa kutamkwa ukilinganisha na kutamkwa kwa fonimu /p, b, m/ (Ladefoged na Maddieson, 1996 katika Mwita, 2007:62). Hata hivyo, silabi yenye shadda hutumia nguvu zaidi kutamkwa ikilinganishwa na zile zisizo na mkazo (Mgullu, 1999:36).
Je, Mtazamo wa Nchimbi kuhusu Fonimu Konsonanti za Kiswahili
Unafaa?
Iwapo, tutafuata kikamilifu mtazamo wa skuli ya Nchimbi (1995) na wafuasi wake na pia kanuni kuhusu fonimu zilizodokezwa na Trubetzkoy (1969), basi kwa jumla kunafaa kuwa na fonimu irabu tano msingi (5) kama vile /i, e, a, o, u/. Aidha, kunafaa kuwa na fonimu konsonanti 29 /p, t, ʧ, k, , d, Ɉ, g, , ɲ, ɳ, n, , θ, s, ʃ, h, v, ð, z, r, l, j, w, ɤ/ zikiwemo fonimu nyingine za ziada / ᷇ , ᷇nd, ᷇ng, ᷇n / za Kiswahili.
Japo fonimu hizi za /᷇mb, ᷇nd, ᷇ng, ᷇nj/ zinazodhihirika katika Kiswahili hazitambuliwi na baadhi ya wanaisimu wa Kiswahili, fonimu zenyewe zinaelekea kutambulika moja kwa moja katika lugha nyinginezo za Kiafrika zinazotumia mfumo wa matamshi unaolingana na wa Kiswahili. Kama vile, Kiluo kina fonimu (/ , ch, d, dh, , g, h, , k, l, , n, ng’, ny, , r, s, t, th, , y, mb, nd, ndh, ng, nj/) (Okombo, 1982; Tucker, 1994: 31; Owino, 2003; de Lacy, 2009: 5; Cable, 2009:4). Kuna pia lugha za Kibantu ambazo zina sauti ng’ong’o zilizotambuliwa na kurekodiwa kama fungu fonimu zenye uwezo wa kutamkwa kama sauti moja. Mathalani, Kikongo kina /mb, nd, ng, mv, nz/, Kikuria kina / , nd, ɳk, ɳg, nt, ns/ na Kiluganda kina / , nd, ɳ , ɳg, mp, nt/ (Mwita, 2007:58-60). Aidha, lugha ya Ki-Chagga hudhihirisha fonimu /mb/ inayotamkwa kama sauti moja (Mwita, 2007:62).
Lugha nyingine ya Kibantu inayoitwa Ikoma inayozungumzwa katika eneo la Mara kule Tanzania vilevile ina fonimu /mb, nd/ (Higgins, 2012:48), Kimeru na Kiembu zina fungu fonimu /mb, nd, ng, nj/ (Starzmann, 2014: 5) na Kikuyu pia kina /mb, nd, ng/ (Mwaniki, 2013:10). Katika Kikuyu, /mb, nd, nj, ng/ hudhihirika katika maneno kama vile: ‘mbembe’, ‘nduma’, ‘njira’ na ‘ngoro’ (Cable, 2010:4-5). Fonimu hizi zina alama maalum zinazotumiwa kuziwakilisha kifonetiki katika Kikuyu kama vile: /mb/ = /mb/, /nd/ = /nd/, /nj/ = /nɟ/, na /ng/ = /ng/ (Cable, 2010:4-5).
Isitoshe, lahaja ya Kiswahili inayoitwa Kikae vilevile ina fonimu ng’ong’o /mb, nd, nj, ng/ (Furumoto, 2015:20). Hivyo basi, utamkaji na utambuzi wa sauti hizi nne za [mb, nd, ng, nj] hufaa kutafitiwa zaidi na wanaisimu ili tuwe na taarifa inayojitosheleza kuhusu idadi kamili ya fonimu na aina za fonimu katika Kiswahili bila kuwapo na idadi tofautitofauti na mifano mbalimbali inayochanganya wasomi wa Kiswahili.
Dhana ya Silabi
Silabi imefafanuliwa na wanaisimu kwa namna mbalimbali. Mathalani, Fudge (1990) akirejelewa na Mgullu (1999:72) anaifafanua silabi kama kipashio cha kifonolojia ambacho ukubwa wake upo kati ya fonimu na neno, na ndefu zaidi kuliko fonimu lakini ndogo ikilinganishwa na neno kamili. Naye, Batibo (2000:175) anaifasili silabi kama kipashio katika neno chenye uwezo wa kuathiriwa na mkazo au toni. Aghalabu, silabi huwa na konsonanti yenye usonoranti kama vile nazali au likwidi na vokali yenye usonoranti ambayo wakati mwingine hurejelewa kama kiini. Juu ya hayo, kwa mujibu wa TATAKI (2013:512), silabi hurejelewa kama sehemu ya neno inayoundwa na konsonanti na irabu au irabu pekee na hutamkwa pamoja kama fungu moja la sauti linalojisimamia. Vilevile, silabi hufafanuliwa kama sehemu ya neno inayoweza kutamkwa mara moja kama fungu moja la sauti (Kihore na wenzake 2009:18). Huweza kurejelewa pia kama kipashio cha matamshi ambacho sauti za lugha hutamkwa mara moja kama fungu maalum linalojitegemea (Obuchi na Mukhwana, 2010: 91). Sauti hizi za lugha zinazotamkwa mara moja aghalabu huunda mapigo ya sauti kwenye neno husika na kuweza kusikika (Longhorn, 2011: 464). Kwa jumla, silabi ni tamko au kipashio kidogo au mapigo ya sauti yanayotamkwa mara moja katika neno kama fungu moja. Aghalabu, silabi ni kubwa kuliko fonimu hata hivyo ni ndogo ikilinganishwa na neno. Aidha, silabi huweza kuathirika kutokana na mkazo na toni na huwa na konsonanti na irabu zenye usonoranti mkubwa. Wanaisimu wa kifonolojia wanaafiki kuwa aghalabu silabi moja huweza kuwa na sehemu tatu kama vile mwanzo, kiini/kitovu na koda/mwisho/kifungio (Yule, 1996:57; Batibo, 2000:176; Fromkin na wenzake 2007: 287). Sehemu ya mwanzo aghalabu huwa na konsonanti. Hata hivyo, wakati mwingine konsonanti inakuwa haipo ikiwa neno limeanza na irabu inayosimama peke yake kama silabi (Yule, 1996:58). Kiini au kitovu aghalabu huwa irabu na husikika zaidi kuliko konsonanti inayoambatana nayo. Aidha, koda/mwisho/kifungio huwa konsonanti kama tunavyoona katika Kiingereza kilicho na silabi funge. Yaani silabi inayoishia na konsonanti. Kimsingi, sehemu za mwanzo na mwisho husaidia kuweka mipaka kati ya silabi zinazofuatana.
Aina za Silabi
Kuna aina kuu mbili za silabi yaani silabi wazi au huru na silabi funge (Yule, 1996: 57; Batibo, 2000: 176; Fromkin na wenz., 2007: 286-7; Kihore na wenz., 2009:18; Obuchi na Mukhwana, 2010:92). Silabi wazi huishia na irabu kama katika neno kata kuna silabi mbili yaani /$ka$ta$/ zinazoishia na irabu. Aidha, silabi wazi hudhihirika zaidi katika lugha ya Kiswahili na lugha nyinginezo kadha za Kiafrika. Nayo, silabi funge huishia na konsonanti na aina hii aghalabu hudhihirika mno katika lugha kama vile Kiingereza. Mathalani, neno good lina silabi mbili, yaani /gʊ:d/ huku silabi ya mwisho ikiishia na konsonanti pekee. 3.2 Uhakiki wa Miundo ya Silabi za Kiswahili
Kimsingi, silabi zozote za lugha huelekea kuchukua mfumo wa konsonanti (K) na irabu (I) (Yule, 1996:58; Aswani, 1995 akirejelewa katika Oduma na Odhiambo, 2008: 170; Fromkin na wenzake 2007:287). Vilevile, silabi za Kiswahili huchukua mfumo kama huo. Hata hivyo, idadi ya miundo ya silabi za Kiswahili hudhihirisha mkinzano mkubwa baina ya wanaisimu mbalimbali wa Kiswahili kama tunavyoona katika Nchimbi (1995), Mgullu (1999), Habwe na Karanja (2004), Mwita (2009), na Obuchi na Mukhwana (2010) miongoni mwa wengine. Katika kuonyesha mifano ya miundo ya silabi katika neno, hati mlazo iliyo na wino mzito imetumiwa: Nchimbi (1995:36) anafafanua miundo minne ifuatayo ya silabi za Kiswahili: 1. Silabi ya irabu pekee (I): ua = ua 2. Silabi ya konsonanti pekee (K): nta = nta 3. Silabi ya konsonanti na irabu (KI): maji = maɈi, washa = waʃa 4. Silabi ya konsonanti, konsonanti na irabu (KKI): mpya = mpja, mgonjwa = mgo᷇njwa
Mgullu (1999:73) anafafanua miundo saba ya silabi za Kiswahili kama ifuatayo:
  1. Silabi ya irabu pekee (I): adui = a-du-i
  2. Silabi ya konsonanti pekee (K): mtu = m-tu
  3. Silabi ya konsonanti na irabu (KI): kitabu = ki–ta–bu
  4. Silabi ya konsonanti, konsonanti na irabu (KKI): ndama = nda-ma.
  5. Silabi ya konsonanti, nusu irabu na irabu (K½II): afya = a-fya
  6. Silabi ya konsonanti, konsonanti, nusu irabu na irabu (KK½II): mbweha = mbwe-ha
  7. Silabi funge inayoishia na konsonanti na inayohusiana vilevile na maneno yenye mkopo: labda = lab-da
Habwe na Karanja (2004:67-8) wanaainisha miundo sita ifuatayo ya silabi za Kiswahili:
  1. Silabi ya vokali pekee (V): iga = i-ga
  2. Silabi ya konsonanti vokali (KV): panga = pa-nga
  3. Silabi ya konsonanti pekee (K): mtu = m-tu
  4. Silabi ya konsonanti, nusu vokali na vokali (K½VV): pigwa = pi-gwa
  5. Silabi ya konsonanti, konsonanti, nusu vokali, vokali (KK½VV): bingwa = bi-ngwa
  6. Silabi ya konsonanti nazali, konsonanti na vokali (KKV): pinga = pi-nga
Mwita (2009:49) anaainisha miundo mitano ya silabi za Kiswahili kama vile:
  1. Silabi ya konsonanti na irabu (KI): kiti = ki.ti
  2. Silabi ya irabu (I) moja pekee: oa =o.a
  3. Silabi ya konsonanti pekee (K) hasa konsonanti nazali: mtu, nne = m.tu, n.ne
  4. Silabi ya konsonanti, konsonanti na irabu (KKI): mwezi = mwe.zi
  5. Silabi ya konsonanti, konsonanti, konsonanti na irabu (KKKI): chungwa = cu.ɳgwa
Obuchi na Mukhwana (2010:93-5) wanaeleza kuwa kuna miundo minane ya silabi za Kiswahili:
  1. Muundo wa konsonanti na irabu (KI): wivu = wi–vu
  2. Muundo wa konsonanti, konsonanti na Irabu (KKI): njama = nja-ma
  3. Muundo wa konsonanti, nusu irabu na irabu (K½II): bweka = bwe-ka
  4. Muundo wa konsonanti, konsonanti, nusu irabu, irabu (KK½II): mbweha = mbwe-ha
  5. Muundo wa irabu pekee (I): oa = o–a
  6. Muundo wa konsonanti pekee (K): mtu = m-tu
  7. Muundo wa konsonanti, irabu, irabu (KII): kaakaa = kaa–kaa
  8. Muundo wa konsonanti, konsonanti, konsonanti, irabu (KKKI): skrubu = skru-bu
Kutokana na wanaisimu hao, imebainika kuwa wanaisimu wote wanakubaliana kuwapo kwa miundo minne msingi ya silabi kama vile I, K, KI, KKI licha ya kutoa mifano tofauti inayokinzana na kukanganya wanaisimu. Hata hivyo, kuna baadhi yao wanaoongeza miundo mingine zaidi kama vile (K½II, KK½II, na silabi funge) (Mgullu, 1999), (K½VV, KK½VV) (Habwe na Karanja, 2004), (KKKI) (Mwita, 2009) na pia (K½II, KK½II, KII, KKKI) (Obuchi na Mukhwana, 2010). Wanaisimu hawa wanaelekea kutofautiana hasa katika orodha ya idadi ya silabi za Kiswahili na mifano yake. Labda hali hii imetokea kwa sababu ya tofauti katika idadi na miundo ya fonimu na maneno mengine ya Kiswahili sanifu yenye sauti ambazo kiotografia huandikwa kwa kuwakilishwa na herufi zaidi ya moja. Vilevile, imebainika kuwa baadhi ya sauti hizi zinajitokeza katika maneno ya kukopwa kutoka lugha ya Kiarabu na kurasimishwa katika mfumo wa Kiswahili kama ulivyo lugha nyinginezo za Kibantu. Aidha, tunadhani shida inayokanganya wapenzi wa Kiswahili kuhusu miundo ya silabi za Kiswahili inaweza kutatuliwa iwapo fonimu katika kila neno itaandikwa kwa kutumia alama au hati za unukuzi makinifu ya kimataifa hata katika kiwango cha silabi. Hivyo basi, hati hizi za unukuzi makinifu zinaweza kudhihirika katika uchanganuzi wa muundo wa silabi hasa {KI} kama tunavyoona katika mifano ifuatayo iliyoandikwa kwa kutumia chapa iliyokoza na kwa italiki: Chakula = /$ʧa$ku$la$/ sio /$cha$ku$la$/ KI KKI Washa = /$wa$ʃa/ sio /$wa$sha/ KI KKI Thamani = /$θa$ma$ni$/ sio /$tha$ma$ni$/ KI KKI Dhana = /$ða$na$/ sio /$dha$na$/ KI KKI
Ng’oa = /$ɳɔ$a$/ sio /$ng’o$a$/ KI KK I Lugha = /$lu$ɤa$/ sio /$lu$gha$/ KI KKI Kimsingi, fonimu zilizochanganuliwa na kuandikwa kwa herufi zaidi ya moja zinaweza kushughulikiwa kwa kutumia hati ya unukuzi makinifu ama kwa kurejelea alama zilizopendekezwa na Nchimbi (1995:36) yaani / ƅ (mb), Ŋ (nd), N (ng), Ɲ (nj)/ au kutumia visaidizi kama vile /᷇mb, ᷇nd, ᷇ng, ᷇nj/ au /nd, mb, ng, nj/ (Mwita, 2007: 65). Tunajua kuwa sehemu hii huzua utata na kutokubaliana miongoni mwa wanaisimu wengi wa Kiswahili. Utata huu hutokea kwa sababu kuna baadhi ya wanazuoni wanaoshikilia kwamba sauti ng’ong’o hasa [mb, nd, ng, nj] si fonimu. Hata hivyo, ithibati zinaonyesha kuwa fonimu mbili zinaweza kutamkwa kama sauti moja kama tunavyoona miongoni mwa fonimu vikwamizwa hasa /th, dh/.
Kulingana na Mwita (2007:60-61), ithibati zifuatazo zimetolewa kufafanua kuwa sauti ng’ong’o zinazounda fonimu moja hutamkwa kama sauti moja: i. Unazalishaji hutokea iwapo sauti nazali itafuatwa na sauti nyingine isiyo nazali kama tunavyoona baina ya /n/ na /d/: Fonimu Fonimu [+nazali] [-nazali] = n [+nazali] d [-nzali] = [nd] ii. Fonimu ng’ong’o huundwa kutokana na sauti pamwe hasa zinapotokea mwanzoni mwa silabi na aghalabu hutajwa hivyo zinapochukua muda ulio sawa ukilinganishwa na fonimu nyingine katika lugha hiyo moja husika (Ewen, 1982 akirejelewa na Mwita, 2007:61). Hii inamaanisha kwa mfano, katika neno kama vile mboga, fonimu ng’ong’o /mb/ huja mwanzo kabla ya irabu /a/ hivyo basi hutokea mwanzoni mwa silabi. iii. Sauti ng’ong’o huunda silabi moja na hutamkwa kama sauti moja kama tunavyoona katika maneno kama vile: shamba = /sha.mba/ na kenda = /ke.nda/. Iwapo alama za Nchimbi (1995) zinaelekea kutoungwa mkono na wanaisimu wa Kiswahili basi alama zilizobuniwa na Mwita (2007: 65) hasa /nd, mb, ng, nj/ na zinazodhihirika pia miongoni mwa lugha nyinginezo za Kibantu huweza kutumiwa au kutumia alama saidizi kama vile /᷇mb, ᷇nd/, ᷇ng, ᷇nj/. Hali hii inaweza kutupa mifano ya silabi kama ifuatayo: Mboga = /$᷇mbo$ga$/ au / $mbo$ga$/ sio /$mbo$ga$/ KI KI KKI Kanda = /$ka$᷇nda$/ au /$ka$ nda$/ sio /$ka$nda$/ KI KI KKI Ngoma = /$᷇ngo$ma$/ au / $ngo$ma$ / sio /$ngo$ma$/ KI KI KKI Kunja = /$ku$᷇nja$/ au /$ku$ nja$/ sio /$ku$nja$/ KI KI KKI Kutokana na mifano hii minne, imebainika kuwa sauti moja inawakilishwa na alama moja. Kwa hivyo, {᷇mbo, ᷇nda, ᷇ngo, ᷇nja} ni silabi zilizoundwa na fungu konsonanti na irabu. Hali hii inatukumbusha kuwa kimsingi muundo mojawapo wa silabi ya Kiswahili ni konsonanti (K) na Irabu (I) yaani KI (Aswani, 1995 akirejelewa na Oduma na Odhiambo, 2008:170). Hivyo basi, {mbo} ni silabi moja iliyoundwa na fungu fonimu moja ya /᷇mb/ pamoja na irabu /o/.
Aidha, muundo mwingine wa silabi ya Kiswahili huweza kuwa Konsonanti, Konsonanti na Irabu yaani KKI ambapo konsonanti husika huweza kuwa nazali au viyeyusho (Aswani, 1995 akirejelewa Oduma na Odhiambo, 2008:170). Kwa hivyo, iwapo silabi huonyesha hali ambapo nazali hutangulia na kufuatwa na konsonanti nyinginezo basi tunaweza kuwa pia na muundo wa silabi KKI. Hiyo konsonanti inayofuata nazali husika huweza kuwa kiyeyusho /w/ na /y/. Kwa mfano: Kandwa /$ka$᷇ndwa$ au /$ka$ ndwa$/ K K I KKI Aidha, muundo wa silabi hasa wa KKI hudhihirika pia katika matumizi ya kiyeyusho /y/ na /w/ hasa zinapofuata konsonanti nyingine isiyokuwa nazali katika silabi moja.
Hivyo basi, tukawa na hali kama vile {pya} yaani /pja/ na vilevile {pwa} yaani /pwa/. Silabi kama hizo hudhihirika katika mifano ifuatayo: Mpya = /$m$pja$/ sio /$m$pya&/ KKI K½II Mpwa = /$m$pwa$/ sio /$m$pwa$/ KKI K½I I 3.3 Je, kuna Uwezekano wa kuwa na Miundo mingine ya Silabi za Kiswahili? Wanaisimu mbalimbali wa Kiswahili wanakubaliana kuwa kuna miundo minne msingi ya silabi za Kiswahili kama vile I, K, KI, KKI. Hata hivyo, kuna wengine wanaoendelea kushikilia kwamba kuna miundo mingine zaidi hasa ile inayotokea katika baadhi ya maneno yaliyokopwa au kutoholewa na yenye silabi za mkopo. Ijapokuwa pendekezo kama hili linaelekea kuungwa mkono na baadhi ya wanaisimu, hatudhani kuwa neno linapokopwa na na kutoholewa na hatimaye kuingizwa katika lugha pokezi basi huelekea kuwa na muundo wa silabi mkopo. Ukopaji hujumuisha hali ya kuchukua moja kwa moja neno kutoka lugha chasili na kuliingiza katika lugha pokezi jinsi lilivyo kimuundo. Mathalani, neno ugali la Kiswahili limekopwa moja kwa moja kutoka Kiswahili hadi Kiingereza jinsi lilivyo (Hornby, 2010:1613). Utohozi humaanisha kuchukua neno la lugha chasili na kulinukuu kwa kuzingatia fonolojia ya lugha pokezi (TUKI, 1990:2) na pia mofolojia ya neno husika ili kuweza kulandana na kanuni za lugha pokezi. Mathalani, maneno yaliyokopwa kwa kutoholewa kutoka Kiingereza ni kama vile springi, skrubu, faksi na elektroni. Maneno kama haya ya kutoholewa yamezua hali kwamba kuna uwezekano wa kuwa na muundo mwingine wa silabi za Kiswahili hasa KKKI. Mathalani, neno skrubu hurejelewa kana kwamba lina muundo wa silabi KKKI (Obuchi na Mukhwana, 2010:95). Neno hili linafafanuliwa kuwa lina silabi mbili kama vile: {skru} inayoundwa na {KKKI} na {bu} inayoundwa na {KI}. Tunadhani kuwa hali hii inazua utata mwingi tunapofafanua silabi za maneno yaliyokopwa kwa kutoholewa. Inaelekea kuwa bado hakuna maafikiano kamili kuhusu jinsi ya kutamka na kuandika baadhi ya maneno mengine yaliyotoholewa kutoka lugha za kigeni hadi Kiswahili. Labda hii ndiyo sababu Kiango (1995:50) alidokeza kuwa kuna utata katika matamshi ya maneno yaliyotoholewa kama vile afisa na ofisa, na disemba na desemba. Anatamatisha hoja hii kwa kusema kuwa kuna haja ya kuwapo na makubaliano kuhusu utamkaji hata hivyo ana hofu kuwa matamshi hayo yatakayotolewa na yatakayokubaliwa yatakuwa ya nani (Kiango, 1995:50). Tunakubaliana na maoni haya ya Kiango kwa sababu, neno skrubu (TATAKI, 2013:517) hurejelewa pia kama skurubu (TATAKI, 2013:517). Iwapo hali hizi mbili ni sahihi basi miundo ya silabi itakayotokea itachukuliwa pia kuwa sahihi kama tunavyoona kati ya (a) na (b): a). Skrubu /$skru $ bu$/ KKKI KI b). Skurubu /$sku $ ru $bu/ KKI K I KI Kutokana na mifano hii, neno (a) lina silabi ya mwanzo inayoundwa na KKKI na neno la pili (b) lina silabi ya mwanzo inayoundwa na KKI. Swali tunaloweza kujiuliza ni kuwa silabi gani basi ni sahihi? Aidha, tukifuata uzi huo huo wa kuwa na vibadala katika matamshi katika maneno yaliyotoholewa basi mwanaisimu mwingine anaweza kujitokeza na neno ‘sikurubu’ na kuainisha silabi zake kama vile: Sikurubu /$si &ku $ru &bu$ KI K I KI KI Kuna uwezekano wa kuwa na ‘sikurubu’ iwapo kwa kweli tunataka kuzingatia kanuni za muundo wa maneno ya Kiswahili. Kama vile tunapopata mlolongo wa konsonanti katika neno hatuna budi kuuvunjilia mbali mlolongo huo kwa kutumia mbinu ya uchopekaji kama tunavyoona katika neno la Kiarabu ‘iblis’ yaani /ibliConfused/ linalotoholewa katika Kiswahili kama ibilisi yaani /i.bi.li.si/ (Mwita, 2009:54). Hali ikiwa hivyo basi tunaweza kuvunjilia mbali pia mlolongo wa konsonanti /skr/ katika skrubu na hatimaye kuwa na neno ‘sikurubu’. Hata hivyo, dai hili lingali linahitaji mdahalo wa wanaisimu.
Kimsingi, maneno ya Kiswahili huundwa kutokana na silabi huru au wazi. Hivyo basi, silabi hizi za maneno aghalabu huishia na irabu (Kihore na wenz., 2009:18) isipokuwa maneno ya mkopo (Habwe na Karanja, 2004: 67). Hata hivyo, si maneno yote ya mkopo huishia kwa konsonanti. Hii ni kwa sababu maneno ya mkopo na hasa yaliyotoholewa hufaa kuchukua sifa za kifonolojia na kimofolojia za lugha pokezi. Kama vile, neno la Kiarabu ‘sultan’ hutoholewa katika Kiswahili kama sultani ambapo irabu /i/ huongezwa mwishoni (Mwita, 2009:54).
Kulingana na hoja tulizodokeza hapo juu kuhusu silabi za mkopo, hatudhani kuwa kuna uwezekano wa kuwa na miundo mingine zaidi. Hali inayotokea ya kuwa na KKKI kuashiria silabi mkopo ni jambo linalotokea kwa sababu ya shida ya namna ya kutamka maneno ya mkopo kwa njia iliyo bora kutoka lugha nyingine. Hata hivyo, tukizingatia kanuni ya utohozi ya kufuata fonolojia na mofolojia ya lugha pokezi hatuwezi kuwa na hali kinzani kama tunavyoona baina ya skrubu na skurubu ambayo yanaleta miundo miwili tofauti ya silabi yaani KKKI katika /skru/ na pia KKI katika /sku/. Maneno yote mawili huchukuliwa kuwa sanifu na kufasiliwa katika kamusi za Kiswahili. Hata hivyo, mwanazuoni wa taaluma ya fonolojia atachukua muundo gani kuwa sahihi? Hivyo basi, makala hii inashikilia kuwa kuna miundo minne ya silabi za Kiswahili na miundo mingine zaidi inayodokezwa haina msingi. Mtazamo huo wa kuwa na miundo minne hutokana na msingi wa Kanuni ya Alfabeti ya Kifonetiki ya Kimataifa ya kuwa sauti moja iwakilishwe na alama moja. Sauti hiyo inaweza kuwa yenye herufi moja au mwambatano wa herufi hata hivyo hutamkika kama sauti moja. Aidha, alama hizo za kifonetiki ndizo hufaa kuzingatiwa katika udhihirishaji wa miundo ya silabi za maneno ya Kiswahili ili kupunguza mikanganyo baina ya wanaisimu.  
Je, Viyeyusho hufaa Kurejelewa kama Konsonanti au nusu irabu katika Uainishaji wa Miundo ya Silabi za Kiswahili?
Ikumbukwe kuwa kuelewa miundo ya silabi za Kiswahili kunahitaji ung’amuzi wa dhana ya fonimu na pia idadi kamili ya fonimu za Kiswahili pamoja na sheria za ufonimu. Maelezo yanayotolewa na Kihore na wenz. (2009:15) ya kuwapo kwa konsonanti 23 na viyeyusho 2 huelekea kuwafanya wanaisimu wengine kuvidhukuru fonimu viyeyusho kama aina nyingine za fonimu hivyo basi si aina mojawapo ya konsonanti. Kwa hivyo, maelezo hayo huweza kudokeza maana nyingine kwamba huenda kuna makundi matatu ya fonimu kama vile irabu, konsonanti na viyeyusho. Kwa upande mwingine, wanaisimu wengine hufafanua viyeyusho moja kwa moja kama aina za konsonanti miongoni mwa makundi mengine kama vile vipasuo, vikwamizo, vipasuo kwaruzo na likwidi (Habwe na Karanja, 2004:50). Hata hivyo, swali linaloweza kuchipuka ni kwamba: kwa nini katika orodha ya makundi ya konsonanti fonimu viyeyusho /w, j (y)/ hukubaliwa moja kwa moja kama aina za konsonanti yenye jina jingine la viyeyusho? Hata hivyo, wakati wa kuzitumia katika uainishaji wa miundo ya silabi konsonanti hizi huanza kurejelewa kivingine kama nusu vokali (½V) au nusu irabu (½I). Mathalani, Mgullu (1999:76) anarejelea fonimu /j (y)/ kama nusu irabu katika mfano ufuatao:
Afya = (a) + (f+y+a) I K+½I+I
Habwe na Karanja (2004:68) hurejelea pia /w, j (y)/ kama nusu vokali katika mfano ufuatao: Pigwa = pi-gwa K+½V+V) Obuchi na Mukhwana (2010:93) wanatoa pia mfano wa matumizi ya nusu irabu kama vile: Mwizi = mwi -zi K ½I I + KI)
Mgullu (1999:67) anatambua kuwa kuna fonimu viyeyusho /w/ na pia /j(y)/ katika orodha ya fonimu za lugha ya Kiswahili. Hata hivyo, katika ukurasa mwingine hatambui kuwapo kwa viyeyusho miongoni mwa makundi mengine ya konsonanti kama vile vikwamizwa, vizuiwa, nazali, vizuiwa kwamizwa, kitambazi na kimadende. Aidha, tunadhani kuwa fonimu hizi /w, j(y)/ ni konsonanti kamili moja kwa moja hata hivyo hupewa jina jingine kama viyeyusho kwa sababu huundwa kutokana na mabadiliko ya kifonolojia ya vokali kuwa nusu vokali. Uundaji wa viyeyusho hutokana na mchakato wa mabadiliko ya kifonolojia jinsi tunavyoona fonimu /ch/ ikiundwa kutokana na mabadiliko ya kifonolojia yanayoitwa ukaakaishaji. Licha ya kwamba /ch/ huundwa na mabadiliko yanayoitwa ukaakaishaji, fonimu hii hairejelewi kama fonimu ukaakaishaji jinsi wanazuoni wengine wanavyoita fonimu viyeyusho /w, y/ kama nusu irabu au nusu vokali. Ili kujenga msingi imara wa mtindo wa kuandika miundo ya silabi za Kiswahili, inafaa turejelee Alfabeti ya Kifonetiki ya Kimataifa (AKIKI). Ishara hizi za AKIKI zikitumiwa basi mifano inayokanganya na inayotolewa katika miainisho mbalimbali ya silabi za Kiswahili kama vile (K½VV, KK½VV) itaepukwa. Naye, Lyons (1981:69) anatujuza kuwa kanuni msingi ya kuundwa kwa AKIKI ilikuwa kwamba tuwe na alama moja ya kuwakilisha kila sauti na iwe alama inayoweza kutambuliwa katika lugha husika na iwapo alama haipo basi kuna haja ya kuongeza kisaidizi juu ya sauti hizo ili kuipa hadhi ya ufonimu. Kama vile, fonimu /᷇nda/ yenye maana sawa na /Ŋa/ kwa mujibu wa Nchimbi (1995:36) imeongezewa alama saidizi ili kuweza kuitambua kama fonimu. Maelezo haya yanatusaidia kung’amua kwamba ingawa silabi aghalabu huundwa kwa konsonanti na vokali au hata vokali pekee, kuna sauti zenye usonoranti kama vile nazali, kimadende na kitambazi zinazoweza kuunda silabi zikiwa pekee (Batibo, 2000:176).
Hivyo basi, tunadhani kuwa anazorejelea Batibo ni zile fonimu ng’ong’o kama vile /m, n/ pamoja na /ny, ng’, n , , ng, nd/ zinazoundwa kutokana na usilimishwaji na pia fonimu /l/. Kwa hivyo, sauti ng’ong’o hasa zenye herufi mbili zinafaa kuwakilishwa kwa alama moja ya kifonetiki kama tunavyoona baina ya /th, dh, gh, sh, ch/ zenye alama maalum. Alama hizo tayari zinadokezwa na Mwita (2007: 65) kama vile /nd, mb, ng na nj/ au tunaweza kutumia alama saidizi kama vile /᷇ , ᷇nd/, ᷇ng, ᷇n /. Aidha, istilahi kama vile konsonanti au irabu zitumiwe badala ya kutumia majina yanayodhihirisha aina za konsonanti au irabu. Hivyo basi, fonimu husika hufaa kurejelewa moja kwa moja kama irabu au konsonanti na sio kwa msingi wa utamkaji wake au mchakato wa uundaji wake kama tunavyoona katika viyeyusho. Hii ni kwa sababu uainishaji wa fonimu aghalabu hufanywa kwa kutumia alama kama vile I/V (irabu/vokali) na K (konsonanti) bila kujishughulisha na aina zake.
Hitimisho
Kama zilivyo lugha nyinginezo, kuna fonimu za aina mbili za Kiswahili nazo ni fonimu irabu na konsonanti. Aidha, makala inaunga mkono msimamo kuwa Kiswahili kina fonimu irabu 5 msingi kama vile /a, e, i, o, u/ na fonimu konsonanti 29 kwa mtazamo wa skuli ya Nchimbi (1995). Fonimu hizo ni kama vile: / , t, ʧ, k, , d, Ɉ, g, , ɲ, ɳ, n, , θ, s, ʃ, h, , ð, , r, l, , , ɤ, , nd, ng, nj/. Iwapo alama za fonimu hasa / ƅ (mb), Ŋ (nd), N (ng), Ɲ (nj)/ zilizopendekezwa na Nchimbi (1995:35) au za Mwita (2007: 65) hasa /nd, mb, ng na nj/ hazijakubaliwa na wanaisimu wengi basi aghalabu tunahimizwa kufuata kanuni za wanafonetiki wa kimataifa za kutumia alama kisaidizi kama alivyoeleza Trubetzkoy (1969) na hatimaye kuwa na maumbo ya fonimu kama vile /᷇mb, ᷇nd, ᷇ng, ᷇nj/. Maumbo ya fonimu kama vile /᷇ , ᷇nd, ᷇ng, ᷇n / au /nd, mb, ng na nj/ huweza kutumiwa na wanaisimu wa Kiswahili kwa kufuata msingi wa kanuni za Alfabeti ya Kifonetiki ya Kimataifa. Kanuni mojawapo ni kuwa na alama moja ya kuwakilisha sauti moja. Hiyo sauti moja inaweza kuwa irabu pekee, konsonanti pekee au mwambatano wa konsonanti kama tunavyoona katika /ʧ (ch), ɲ (ny), ɳ (ng’), θ (th), ʃ (sh), ð (dh), ɤ (gh)/. Iwapo, msingi wa uundaji silabi ni konsonanti na irabu, basi hatuna budi kushikilia uzi huo huo mmoja na hatimaye kutambua miundo ya silabi za Kiswahili kama alivyoeleza Nchimbi (1995:36) kama vile (I, K, KI, KKI) au (V, K, KV, KKV). Aina nyingine ya muundo wa silabi kama vile KKKI inayodaiwa kuwa hutokana na maneno ya kutoholewa ingali ina utata kwa sababu baadhi ya maneno hayo huweza kudhihirisha mifumo miwili ya maandishi kama vile skrubu na skurubu. Aidha, fonimu zinazounda silabi aghalabu hufaa kurejelewa kwa kutumia alama au hati za unukuzi makinifu ya kimataifa kwa kufuata kanuni kuwa kila sauti au kitamkwa kimoja kiwakilishwe na alama moja au kutumia alama kisaidizi.
Marejeleo
Akidah, M. A. (2013). ‘Phonological and Semantic Change in Language Borrowing. The Case of Arabic Words Borrowed into Kiswahili’, katika International Journal of Education and Research, 1(4), 1-20. Kutoka www.ijern.com/images/April-2013/42.pdf.
Ashton, E. O. (1951). Swahili Grammar. Kenya: Longman.
Batibo, H. (2000). ‘Systems in the Sounds of Africa’, katika African Voices. An Introduction to the Languages and Linguistics of Africa. Southern Africa: Oxford University Press, 160-196.
Cable, S. (2009). Some Basic Facts about the Dholuo Language. Kutoka people.umass.edu/scable/LING748-FA09/Materials/Handouts/Dholuo-Basics.pdf.
Cable, F. (2010). Some Basic Facts about the Gikuyu Language. Kutoka http://people.umass.edu/scable/LING404-F...Basics.pdf.
Choge, S. (2009). ‘Understanding Kiswahili Vowels’, katika The Journal of Pan- African Studies, 2 (8), 62-77. Kutokahttp://www.jpanafrican.org/docs/vol2no8/2.8_UnderstandingKiswahiliVowels.pd
Coxhead, P. (2006). Natural Language Processing and Application: Phones and Phonemes. Kutoka https://www.cs.bham.ac.uk/~pxc/nlp/NLPA-phon1.pdf.
De Lacy, P. (2009). Morpho – Phonological Polarity. Kutoka www.paudelacynet/polarity/delacy-2009-Morphophologicalpolarity.pdf.
Fromkin, V., Rodman, R. na Hyams, N. (2007). An Introduction to Language. Boston: Thomson Wadsworth.
Furumoto, M. (2015). ‘On the Copula in the Kikae Dialect of Swahili’, katika Swahili Forum, 22, 20-41. Kutoka http://afrikanistik.gko.uni_Leipzig.de/Swafo/images/documents/SF_22_Furumoto.pdf.
Habwe, J. na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi. Nairobi: Phoenix Press.
Higgins, H. A. (2012). Ikoma Vowel Harmony: Phonetics and Phonology. Kutoka
Hornby, A. S. (Mh.) (2010). Ox ord Ad anced Learner’s Dictionary (8th ed.). Oxford: Oxford University Press.
Kiango, J. G. (1995). ‘Uundaji wa Msamiati Mpya katika Kiswahili: Zoezi Lenye Njia Mbalimbali’, katika Kioo cha Lugha, 1 (1), 46-54. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kihore, Y. M., Massamba, D. P. B. na Msanjila, Y.P. (2009). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA). Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: TUKI.
Longhorn (2011). Kamusi ya Karne ya 21. Nairobi: Longhorn. Lyons, J. (1981). Language and Linguistics: An Introduction. Cambridge: Cambridge University Press. Mgullu, R. S. (1999). Mtalaa wa Isimu. Nairobi: Longman.
Mwangi, I. (2007). ‘Swala la Alofoni (Zipo au Hazipo?) katika Ufundishaji wa Fonolojia ya Kiswahili’, katika Kiswahili na Elimu Nchini Kenya, 93-102. Nairobi: Twaweza Communications and CHAKITA-Kenya.
Mwangi, P. I. (2011). ‘Nasal Consonant Processes in Standard Kiswahili’, katika Baraton Interdisciplinary Research Journal, 1 (1), 77-84. Kutoka http://ueab.ac.ke/BIRJ/download/birj_vol...0consonant %20Processes%20inStd%20Kiswahili.pdf.
Mwaniki, I. N. (2013). ‘The Underlying Reality of Phonological Simplification of Loan Words by Speakers of Gikuyu’, katika International Journal of Education and Research, 1 (8), 1-8. Kutoka http://www.ijern.com/journal/August-2003/52.pdf.
Mwansoko, H. J. M. (1995). ‘Shadda Katika Kiswahili,’ katika Jarida la Kiswahili, 1 (1), 15-20, Dar es Salaam: E.S.C. Ltd.
Mwita, L. C. (2007). ‘Prenasalization and the IPA’, katika UCLA Working Papers in Phonetics. 106, 58-67. Kutoka http://www.ku.ac.ke/schools/humanities/i...arship.pdf.
Mwita, L. C. (2009). ‘The Adaptation of Swahili Loanwords from Arabic: A Constraint-Based Analysis’, katika The Journal of Pan African Studies, 2 (8), 46-61. Kutoka http://www.jpanafrican.com/docs/vol2no8/...nwords.pdf.
Nchimbi, A. S. (1995). ‘Je, Mang’ong’o ni Fonimu au si Fonimu katika Kiswahili Sanifu?’ katika Baragumu, 25-39. Maseno: Chuo Kikuu cha Maseno.
Obuchi, S. M. na Mukhwana, A. (2010). Muundo wa Kiswahili. Ngazi na Vipengele. Nairobi: A~Frame Publishers.
Oduma, R. na Odhiambo, K. (2008). ‘The Adequacy of CV Phonololgy in Syllabifying African Languages: The Case Study of Kiswahili Loanwords in Ateso’, katika Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika, 167-174. Chuo Kikuu cha Moi: Moi University Press.
Okombo, D. O. (1982). ‘Dholuo Morphophonemic. A Generative Framework’, katika The Language and Dialect Atlas of Kenya Supplement 2. Berlin: Dietrich Reimer. Ontieri, J. O. (2015). ‘Phonological Influences of First Language on Kiswahili: A Case Study of Kenyan Bantu Languages’, katika International Journal of Science and Research, 4 (1), 2522-2526. Kutoka https://www.ijsr.net/archive/v4i1/SUB15856.pdf. Owino, D. (2003). Phonological Nativization of Dholuo Loanwords. Doctor of Philosophy Thesis, University of Pretoria, South Africa. Kutoka www.upetd.up.ac.2a/thesis/available/etd-02092004-112729/unrestricted/00thesis.pdf. Polome, E. C. (1967). Swahili Language Handbook. Washington: Center for Applied Linguistics.
Simala, I. K. (1995). ‘Uziada wa Sauti (Alofoni) za Kiswahili Sanifu’, katika Baragumu, 41-49. Maseno: Chuo Kikuu cha Maseno.
Starzmann, P. (2014). A Dialectology of Central Kenyan Bantu: Quantitaive and Qualitative Analysis. Kutoka https://www.iaaw.hu_berlin.de/de/afrika/...1_2014.pdf.
TATAKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la 3. Nairobi: University of Dar es Salaam and Oxford University Press.
TUKI (1990). Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la 2. Nairobi: Oxford University Press.
Trubetzkoy, N. S. (1969). Principles of Phonology. Berkeley and Los Angeles: University of California Press.
Tucker, A. N. (1994). A Grammar of Kenya Luo (Dholuo). Koln: Rudiger Koppe Verlag.
Whiteley, W. H. (1956). Studies in S ahili Dialect 1: Ki tang’ata. East African Swahili Committee.
Yule, G. (1996). The Study of Language. 2nd Ed. Cambridge: Cambridge University Press.