MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - NENO NI NINI?

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: NENO NI NINI?
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
Neno ni dhana tata, utata wake unatokana na kupewa fasili tofauti tofauti kutokana na uwanja linamotumika. Hapa tutachunguza dhana ya neno kwa mapana yake.
MGAWANYO WA KAZI
  • Maana ya neno kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali,
  • Kiini cha utata wa neno,
  • Hitimisho.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (toleo la tatu, 2013:420) wametoa fasili tatu za neno. Fasili ya kwanza “neno” limefasiliwa kama mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa pamoja na kuleta maana. Kisha wakafasili neno kama jambo kubwa  mfano nina “neno” nataka kukupa; ameniletea neno, na katika fasili ya tatu wamefasili neno kama mahubiri, mfano “neno” la Mungu.
Kwa mujibu wa Longman Dictionary (2008:1899) wamefasili neno  kama kipashio cha lugha ambacho mtu anaweza akaelewa iwapo kitakuwa kimesemwa au kuandikwa kama kilivyo. (tafsiri yetu)
Habwe na Karanja (2004:71) wanasema neno ni kipashio cha kiisimu kinachoundwa na mofimu moja au zaidi.
Katamba (1994:38) anasema neno ni kipashio kidogo cha maana katika lugha ambacho kina dhima ya kisarufi. Anaendelea kusema, neno linaweza kusimama peke na kuleta maana bila kupachikwa vipande vingine. Hivyo katika neno “childish” (utoto) linaweza kutenganishwa na kubaki “child” (mtoto) na neno hili likatumika kiupwekeupweke kwa sababu ni neno linalojitegemea. Lakini hatuwezi kutenganisha kipande “ish” kikasimama pekeyake na kuleta maana.
Sisi kama kundi (kwa malengo ya kozi hii) tunaona neno ni kipashio cha lugha kinachoundwa na mofu moja au Zaidi ambayo inaweza kusimama pekeyake na kuleta maana katika lugha mahususi.
Ni kweli dhana ya neno ina utata. Utata huo unasabishwa na vigezo tofautitofauti ambavyo hutumika katika kufasili dhana ya neno na mipaka yake.
Mdee (2010:5) anafafanua njia tatu zinaweza kutumika katika kufasili neno, njia hizo ni kama:- neno kama kipashio huru kisichogawanyika; maana ya neno kiothografia, na neno kama kipashio cha maana. Sisi tumeenda mbali kwa kuongeza fasili nyingine za neno kwa vigezo kama vile kigezo cha kisarufi katika kufasili dhana ya neno na kigezo cha kifonolojia.
Neno kama kipashio huru kisichogawanyika. Fasili hii ya neno ni ya Leonard Bloomfield (1933) inayosema “neno ni umbo dogo kabisa lililo huru”. Fasili hii ina mambo makuu mawili, kwanza neno liwe umbo dogo, pili neno liwe umbo huru. Hapa umbo dogo humaanisha umbo ambalo haliwezi kugawanyika bila kupoteza maana yake. Mfano neno “pasi” huwezi kuligawanya katika “pa” na “si” bila kupoteza maana yake. Hivyo umbo dogo ni lile ambalo linashikilia maana. Kwa upande wa neno kuwa huru ina maanisha umbo hilo lazima liweze kutamkwa pekee bila kutegemea au kuliambisha kwenye neno lingine, haya ni maneno kama vile njoo, lete, jua, n.k.
Tatizo(utata) la kigezo hiki: Ugumu wa kigezo hiki neno linalopewa uzito hapa ni lile katika lugha za mazungumzo pekee. Katika lugha za maandishi tunaweza kuwa na vipande vidogo vya maneno lakini ambavyo vikiwa huru hatuwezi kusema vina maana kwa kuwa huwa havirejelei kitu au hali yoyote ile. Mfano katika lugha ya Kiswahili vipande “na”, “kwa”, “tu”, n.k havina maana vikiwa pekee pekee. Katika lugha ya Kiingeza vipande kama “a”, “the”, “and”, “to”, n.k vivyo hivyo havina maana vikiwa pekee pekee.
Maana ya neno kiothografia. Kigezo hiki huchukulia neno kuwa ni maandishi yanayoacha nafasi mwishoni. Rubanza(2010), anaeleza kwamba neno kiothografia ni mfuatano wa maandishi ambao huacha nafasi tupu mwishoni bila uwepo wa nafasi tupu katikati. Neno hudhiirika linapokuwa katika maandishi tu na lisiwe na nafasi katikati. Mfano; ubao, chaki n.k. Maneno kama Askari kanzu, Bata maji, n.k huchukuliwa kama maneno mawili tofauti. Katika Kiingereza neno kama “cannot”, “blackboard”, n.k huchukuliwa kama neno moja. Maneno kama “washing machine” (mashine ya kufulia) na “White House” (ikilu ya marekani) huchukuliwa kama maneno mawili tofauti.
Matatatizo ya kigezo hiki: Hushidwa kuelezea maneno ambatani, kwao uandikaji wa neno ambatani kwa kutenga au kuacha nafasi katikati huchukulia kuwa ni maneno mawili. Hii sio sahihi kwani maneno ambatani huwa na dhana moja hivyo hutakiwa kuchukuliwa kama neno moja. Pia kigezo hiki hushughuliki tu na lugha ya maandishi na kuipuuza lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo hutupatia lugha ya maandishi. Pia zipo kugha nyingine ambazo hazitengi maneno yake katika uandishi, pamoja ya kuwa ndani ya neno moja kunaweza kuwa na dhana nyingi zinazorejelewa. Mfano lugha ya Kigreenland Eskimo neno “uluminippug” maana yake ni “yumo mwanaume ndani ya nyumba yake”.
Dhana ya neno kifonolojia. Kigezo hiki huchukulia neno kuwa ni kipande cha lugha kinachotokana au kujengwa na kipashio kidogo cha kimatamshi. Kufuatana na kigezo hiki kuna vigezo fulani vilivyo wekwa ambavyo hutofautiana kutoka lugha moja na nyingine. Rubanza (ameshatajwa) hueleza kwamba zipo lugha ambazo upo uwezekano wa kulitambua neno kwa kutumia sifa za kimatamshi. Lugha kama hizi ni zile ambazo zina utaratibu wa kuweka mkazo mahali fulani maalumu katika maneno wakati wote. Anaeleza zaidi kwamba sehemu hiyo inaweza kuwa mwanzoni mwa kila silabi ya kwanza ya neno, au silabi ya pili toka mwisho kwa baadhi ya lugha. Kwa mfano chunguza sentensi ifuatayo kutoka katika lugha ya Kingereza; “I didn’t take the test yesterday” Kufutana na utaratibu wa lugha hii sentesi hii ina maneno matatu tu yaliyokolezwa, kwasababu mkazo huwekwa kwenye maneno yenye kubeba maana (content words). Utaratibu huu una vighairi kwa sababu kuna wakati hata yale maneno yasiyobeba maana (grammatical words) hubeba mkazo kwa sababu za kimsisitizo wa neno au maneno husika katika sentensi (prosodic stress) Mfano katika sentensi ilele “I didn’t take the test yesterday” Ikiwa mzungumzaji ataweka mkazo kwenye “I” atakuwa akionyesha msisitizo sio yeye aliyefanya jaribio jana. Ikiwa mzungumzaji ataweka mkazo kwenye “didn’t”atakuwa anasisitiza kuwa yeye hakufanya jaribio jana (labda kafanya jambo jingine). Na ikiwa mzungumzaji ataamua kuweka mkazo kwenye “the” atakuwa akimaanisha kuwa hakufanya jaribio hilo(linalokusudiwa na muulizaji) labda kafanya jaribio lingine tofauti.
Hivyo kwa kutumia kigezo cha mkazo katika maneno tunashindwa kufahamu neno hasa ni lipi. Je vile vipande vya sauti ambayo havibebi maana katika lugha basi navyo ni maneno? Na kama ndio, basi kwa nini lugha hii isivitambue kama ni maneno kamili kiasi cha kubeba mkazo asilia?
Dhana ya neno kwa kigezo cha maana. Kwa mujibu wa Mdee (ameshatajwa) hueleza kwamba neno ni kipashio kidogo cha lugha chenye maana, hueleza zaidi kwamba neno ni lazima liwe na maana. Mfano; baba – mzazi wa kiume, mama – mzazi wa kike. Kwa hiyo kwa kutumia kigezo hiki neno hutambuliwa kuwa ni kipashio cha kiisimu chenye maana.
Utata wa kigezo hiki: Je, maneno yote ya lugha yana maana ya kisemantiki? Pia kuna maneno mawili au zaidi yenye maana moja, Kwa mfano; mkono wa birika, maana yake mchoyo. Yapo maneno mengine yenye maana zaidi ya moja, mfano; kaa, paa, na kata, maneno haya yakisimama yenyewe huwezi kupata maana moja mpaka yawe katika mahusiano na maneno mengine kwenye sentensi.
Dhana ya neno kisarufi. Kwa mujibu wa Katamba (1993:19) ili neno litambulike lazima liwe katika muktadha wa matumizi. Katamba, anasema neno moja linaweza kuwa na dhima mbalimbali na dhima hiyo itagundulika tu litakapokuwa ndani ya muktadha wa matumizi kwenye sentensi. Anatoa mtano wa neno la kiiingereza “cut” kwamba likiwa kiupweke upweke mtu hawezi kutambua linarejelea nini, pamoja kwamba neno hilo katika lugha ya Kiingereza ni kitenzi yaani “kata” lakini kuna wakati linaweza kutumika kurejelea nomino. Chunguza mifano hii: “I need my cut” na “I have cut my finger”. Ukiichunguza vizuri mifano hii “cut” katika sentensi ya kwanza hurejelea nomino yaani “nahitaji stahiki yangu”(tafsiri yetu)  na “cut” katika sentensi inayofuata hurejelea kitenzi yaani “nimekata kidole changu”(tafsiri yetu). Kigezo hiki pia huenda mbali kwa kufafanua kuwa pia maneno kama; na, tu,si, n.k katika Kiswahili na maneno; and, an, the, on n.k katika Kiingereza nayo hayawezi kutambulika yanarejelea nini lazima yawe katika muktadha wa matumizi ndio tunaweza kusema ni aina gani za maneno au kutambua maana zake.
Udhaifu wa kigezo hiki ni kwamba kuna maneno mengi sana ambayo maana zake hutambulika hata yasipokuwa katika muktadha wa matumizi kwenye sentensi, aya au kifungu cha habari. Maneno haya ni kama vile nomino za mahali kama vile Dar es Salaam, Ulaya, Bukoba n.k; nomono za pekee zinazorejelea majina ya watu kama vileMutashobya, Mwendamseke, Rubanza, n.k. Sasa tunajiuliza kuwa aina hizi za nomino na nyingine nyingi ambazo ni kama hizi je si maneno? Hivyo na kigezo hiki hakijajitosheleza katika kutupatia maana ya “neno” itakayokidhi mahitaji ya taaluma zote.
Tunahitimisha kwa kusema kwamba Pamoja na vigezo mbalimbali vinavyotumika kufasili neno kuonekana ndicho kiini cha ugumu wa fasili ya neno lakini pia tofauti za lugha nazo huchangia kufanya fasili ya neno kuwa ngumu. Hii ni kwa sababu tabia za lugha hutofautiana, kwa sababu neno linaweza kuwa neno katika lugha fulani lakini lisiwe neno katika lugha nyingine. Pia mitazamo tofautitofauti ya wataalamu nayo ni sababu nyingine ya ugumu huo. Hivyo ni muhimu kama wanafunzi wa kozi ya Mofolojia kuelewa vizuri vigezo hivi na kuhusisha mawazo ya wataalamu mbali mbali katika kuijadili dhana ya neno. Hii itatusaidia kutoyaacha maneno ambayo kwa fasili ya Kimofolojia hayaonekani kama ni maneno. Uchanganuzi wa kimofolojia wa maneno hushughulikia pia aina za maneno kama  vihusishi, viunganishi, vihisishi maneno ambayo kwa fasili ya kimofolojia yanaonekana kama si maneno kwa kuwa tu hayana maana hasa pale yanapokuwa pekee pekee bila kuhusishwa na maneno mengine kwenye muktadha wa matumizi.
MAREJELEO.
Bloomfield, L. (1933). Language. Henry Holt: New York.
Habwe, J. na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Phonex Publisgers: Nairobi
Katamba, F. (1993). Morphology. Mac Millan Press Ltd: London
Katamba, F. (1994). English Words. Routledge: London
Mdee, S. (2010). Nadharia na Historia ya Leksikografia. TUKI: Dar es Salaam
Quirk, L. (2005). Longman Dictionary of Contemporary English. Pearson Longman: New York
Rubanza. (2010). basic Reading. Yaliyoandailwa na Rubanza.
TUKI (2013). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la tatu). Oxford: Dar es Salaam