MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - SHAIRI: UPAMBAUKAO HUTWA

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: SHAIRI: UPAMBAUKAO HUTWA
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
UPAMBAUKAO  HUTWA
(KWAHERINI!)
 
Upambaukao hutwa, na kutwapo huwa giza
Mtana hupetwapetwa, ukanyang’anywa mwangaza
Nyoyo zikawa kukotwa, japo mwezi waangaza
Laliza hili laliza!
 
Na sisi ule mtana, uliotupambauza
Ulotupa kujuwana, na mengi kuyafanyiza
Leo waanza kununa, mitima kuiumiza
Laliza hili laliza!
 
Hikumbuka tangamano, vyema tulivyolikuza
Mi nanyi ‘kawa mfano, wa lulu katika shaza
Kisha leo saa hino, hiona twalikatiza
Laniliza! Laniliza!
 
Hikumbuka ukarimu, na wema wenu nduguza
Jinsi mulivyonikimu, myaka saba hatimiza
Nahisi najidhulumu, Tanzania kuipeza
Ndipo hamba laniliza!
 
Ingawa ‘menilazimu, na nyinyi kujiambaza
Yondokayo ni sehemu, sehemu najibakiza
Moyo wangu umo humu, Tanzania ‘tausaza
Japo hivyo – laniliza!
 
Ni yangu matumaini, kwenu nayapendekeza
Kwamba hwenda si jioni, nuru ingajipunguza
Pengine wingu angani, ndilo lilojitandaza
Litakoma kutuliza?
 
Na iwapo si hakika, hili nalowaambiza
Jambo moja liso shaka, tusoweza lipuuza:
Utwao hupambauka, hauwezi ukaiza
Hapo halitatuliza!
 
 
Abdilatif Abdalla
Dar es Salaam:
Septemba 8, 1979
 
____________________
Shairi hili nililitunga kuwaaga Watanzania nilipokuwa naondoka Tanzania, baada ya kufanya
kazi Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa miaka sabaa.
Lilichapishwa katika Lugha Yetu, jarida la Baraza la Kiswahili la Taifa  (BAKITA), Toleo la 35/36 (1979-1980), na katika magazeti ya Uhuru, Ngurumo na Mzalendo.