MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.

JIFUNZE KISWAHILI - SHAIRI: MCHUMBA HANA TALAKA

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: SHAIRI: MCHUMBA HANA TALAKA
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
*MCHUMBA HANA TALAKA*

1.Ya Karimu Ya Jalia, nakuomba Ya Rabuka,
Hekima kunijalia, kalamu ninaposhika,
Niweze kusimulia, gazeti kuyaweka,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

2.Ukishindwa unakacha, Mchumba hana Talaka,
Uchumba kama Pakacha, rahisi chini kuweka,
Ni rahisi kumuacha, bila kwa Kadhi kufika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

3.Uchumba si kama ndoa, kuachwa si kuachika
Unapoingia doa, ndiyo mwisho umefika,
Atabaki kukodoa, maji yameshamwagika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

4.Ndoa niseme jamani, ni ahadi imeshika,
Waraka utasaini, ni Mkataba hakika,
Ukileta kisirani, sheria zinakushika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

5.Uwe ‘mepeleka posa, nyumbani kwao kufika,
Ya nguo pamwe na pesa, na vyote walivyotaka,
Kamwe halijawa kosa, uchumba ukifutika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

6.Mchumba wamtazama, usije kukurupuka,
Je atamjali Mama, nyumbani akishafika?,
Au taleta zahama, watu kuparaganyika?,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

7.Walii hutamuona, mkono wako kushika,
Kukuozesha kimwana, kwa maneno kutamka,
Mshenga ndo utaona, barua ameishika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

8.Mchumba ni kama koti, kirahisi linavuka,
Hata palipo kikoti, waweza kulipachika,
Ubanakia na shati, hakuna wa kukucheka,
,Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

9.Uchumba kiti cha basi, popote waweze shuka,
Wamwambia mie basi, kwa meseji kuandika,
Nikutoe wasiwasi, korti hamtafika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

10.Uchumba kama Bokingi, nyingine tunazoweka,
Ukiviona vigingi, visoweza kukwepeka,
Hakuna maneno mengi, uchumba unafutika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

11.Kalamu naweka chini, nimesema nilotaka,
Nashukuru Manani, *WIGO* hapa nimefika,
Angalia kwa makini, usije kukasirika,
*Mchumba hana Talaka, ukishindwa unakacha.*

Kailima Ramadhani [WIGO – I.C.B.M]
Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mtumba – Mji wa Serikali
*DODOMA*