MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - FASIHI, UANDISHI NA UCHAPISHAJI (9)

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: FASIHI, UANDISHI NA UCHAPISHAJI (9)
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
SEHEMU YA PILI: UANDISHI
8. Matatizo ya Waandishi Chipukizi
Elieshi Lema
Mada ihusuyo “Matatizo ya Waandishi Chipukizi” ina matatizo yake. Katika mada hii tayari kuna wazo la kificho kwamba kuna matatizo ambayo ni ya kipekee ya waandishi chipukizi, na kwamba matatizo hayo hutoweka mara baada ya mwandishi kufaulu kuchapisha, ama kuwa na mizizi, au kukomaa. Lakini hulka ya uumbaji inafutilia mbali wazo hili kwani kila zoezi la uumbaji ni kitendo kipya, hivyo matatizo ya aina fulanifulani yatajitokeza daima na kuwaathiri waandishi wote. Ni wazi, basi, tofauti kati ya mwandishi chipukizi na yule aliyekomaa imo katika namna mwandishi anavyoyashughulikia matatizo yahusuyo uandishi wa fasihi, katika ujuzi wake wa kutumia vyombo vya kazi yake anapoumba. Baadhi hushindwa katika zoezi hili na kubakia chipukizi daima, na wengine hufaulu na kukomaa.
Makala haya yatajihusisha na waandishi wa riwaya pekee na yatajadili matatizo ya waandishi chipukizi katika mafungu matatu: (1) Matatizo yasiyoisha ya kitendo cha uumbaji, yaani, matatizo yahusianayo na maumbile ya sanaa na dhima yake katika mawasiliano; (2) Matatizo yahusianayo na jamii, kama vile athari ya mazingira kwa mwandishi na katika kazi yake; na (3) Matatizo ya ujumi na usasa; masuala yahusuyo riwaya kama fani na kufaa kwake, na athari za usasa katika kipindi cha kijamii aishicho mwandishi. Makala yatamalizia kwa kutoa maoni kuhusu njia za ufumbuzi wa matatizo yaliyozungumziwa.
1. Matatizo Yasiyoisha Katika Kitendo cha Uumbaji
Sanaa ni mawasiliano. Kuandika ni kuwasiliana, ni itikadi, imani, hisia nzito za mikanganyiko, huzuni au furaha, kupinga yale yasiyo ya haki, au kuyajaribu katika vitendo mawazo mapya yajitokezayo kichwani. Ari ya kuwasiliana na kupeana habari ni tabia iliyokita katika maumbile ya wanadamu, na ni chimbuko la furaha, utambuzi na ukuaji wa nafsi.
Ari ya kuwasiliana ni tofauti na uwezo wa kuwasiliana. Mawasiliano ya dhati yanahitaji utaratibu wa aina yake; yanahitaji utumizi wa lugha na mbinu zake, kama vile ishara, picha, tamathali, n.k., ambazo zinafahamika kwa mwandishi pamoja na wale akusudiao kuwasiliana nao. Msamiati wa lugha hii unatokana na maisha ya kila siku ya mwandishi, tangu utotoni wakati mazingira yanajitokeza kwake kihisia, na kutokana na mwongozo wa watu wazima na wazee wa jamii. Katika ngazi hii ya awali habari na maarifa hutunzwa katika ubongo wa mtu atakayekuwa mwandishi, ubongo ambao daima unajishughulisha. Mwandishi hupata maarifa kutokana na mazingira yake yanayomkuza na huyatumia katika kupanga mawazo yake.
Suala la utaratibu je? Vipi mwandishi anaufikia utaratibu katika kazi ya fasihi ili kuwasiliana? Kwanza yabidi tueleze maana ya utaratibu huu. Kwanza yafaa tuelewe kuwa hadithi ya kubuni si kiini, wahusika na mazingira tu, bali ni ujumla wa mambo yote haya katika mwelekeo wa hadithi nzima yasababishwayo na mahitilafiano, yakuzwayo hadi upeo na hatimaye kufikia mwisho na kutanzuliwa. Huu utaratibu ndio uipayo kazi ya kubuni uzito wake na nguvu yake, na wakati huohuo kuitofautisha kazi ya sanaa na maisha halisi, japokuwa kuna kurandana kwa aina fulani. Pindi mwandishi aufikiapo utaratibu huu katika kazi ya riwaya, umaana wa matendo na kubadilika kwa wahusika hueleweka na kwa hiyo maana ya kazi hiyo kujitokeza. Mtu asomaye hadithi hiyo ataweza kuwatazama wahusika katika mienendo yao kama vile ni watu halisi, msomaji atafuatilia matendo yao na kujitambulisha nao, au kutokubaliana nao au hata kuwahukumu. Hiki kitendo cha msomaji cha kujihusisha, kutokubaliana au kuhukumu mhusika katika riwaya ndicho kimwezeshacho kujifunza na kushiriki kimawazo katika mwenendo wa mabadiliko. Fasihi, kwa hiyo, ina uwezo wa kutupa kile ambacho maisha halisi yasingetupa kirahisi, au yangetupa kwa gharama kubwa. Waandishi wote hutamani kufaulu katika jambo hili na kutoa kazi bora. Hapo ndipo ulipo ugumu kwa waandishi chipukizi walio wengi.
Suala hili lina maana gani kwa waandishi chipukizi? Jambo mojawapo la msingi na muhimu kwa mwandishi yeyote ni uwezo wa kuhisi juu ya mambo yajitokezayo katika mazingira (watu, hali, matukio, n.k.); upeo wa hali ya juu wa kuyachunguza maisha, kuyatafakari na kuyatafsiri (hata kama si kwa usahihi wakati mwingine).
Mwandishi anahitaji ujuzi wa kumwezesha kuyatafsiri kikamilifu yale ayafahamuyo kisanaa. Anahitaji kuelewa, kwa mfano, kwamba bila msomaji kuwa na hamu ya kazi yake, kazi hiyo haitasomwa hata kama jambo liongelewalo ni muhimu sana. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuelewa nini kitakikanacho katika kubuni hadithi – vitu kama kiini cha hadithi, wahusika, mazingira; jinsi hitilafu zijitokezavyo, upeo na suluhisho; ufundi wa kuchagua kwa makini yale yaliyo muhimu; sauti hai na ulinganifu wa mwendo unaowafanya wasomaji kupata uzoefu kihisia wakati wanaposoma. Mtindo, herufi, sarufi na alama za vituo huiongezea uzuri kazi -iliyoandikwa. Mtindo humwezesha msomaji kupata maana ya kitu kizima na siyo neno mojamoja. Kwa maneno mengine, kile aktfahamucho mwandishi (mtazamo wake wa maisha) lazima kioanishwe vizuri katika kazi yake ya kubuni na kile riwaya yake inachojaribu kukisema. Busara, kipawa na ufundi ni muhimu kwa waandishi wote, na hususa kwa waandishi wachanga ambao inabidi wajitahidi kupita kiasi. Hadi kufikia hapa tunaweza kuelewa kwa nini waandishi wachanga wengi hukwama katika hatua za mwanzo. Siyo kwa sababu hawajui la kusema, au hawana msamiati wa kutosha, bali ni kwamba kunahitajika ujuzi na maarifa ya msingi ya maumbile ya fasihi pamoja na njia maalumu ya kubuni.
2. Matatizo Yatokanayo na Jamii
2.1 Matatizo ya Kluchumi
Hili tatizo halina haja ya kusisitizwa, li wazi kabisa. Hali mbaya ya uchumi wa nchi nyingi za dunia ya tatu ni ya kuhuzunisha. Kijamii na kitaifa hali hii imesababisha mkazo kutiwa katika matatizo yaliyo wazi ya hali ya ujumla na kutozingatia matatizo yampatayo mwandishi. Macho yote yanawatazama wale wanaokufa kwa njaa, mahitaji muhimu ya binadamu, ufutaji wa maradhi, kufa kwa watoto wachanga, kujinasua kiuchumi, n.k.
Sasa mwandishi, na mwandishi mchanga pia, atafanya nini katika hali kama hii? Licha ya sabuni, sukari, mchele, unga, n.k., pia anahitaji karatasi, wmo au peni na kalamu, na mashine ya kutaipu (wengine watasema hiki ni kitu cha anasa, bali mwandishi anahitaji kutaipu kwa sababu wachapishaji wengi wanasisitiza kwamba miswada lazima iwe imetaipiwa). Mwandishi pia anahitaji muda. Hebu mfikirie mwandishi mfanyakazi anayeanza kazi saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni, ujira wake shilingi elfu nne. Hakuna hata haja ya kutazama matumizi ya kiasi kama hiki. Kwa wengi – na hata wale wenye kubana matumizi hasa – kipato hiki kinakuwa kimekwisha baada ya juma la kwanza la mwanzo wa mwezi. Na hapa hatujaweka katika makadirio hayo kahawa, sigara au hata bia, vitu ambavyo katika hali fulanifulani baadhi ya waandishi huvihitaji sana ili kuwasaidia kuyapanga mawazo yao barabara. Baada ya kazi na kuchoka, mwandishi anatamani kuandika kitu kutokana na vidokezo alivyovipata kwa watu au vitu mbalimbali mchana huo, wakati aiipokuwa hana kijidaftari kuweza kuviandika. Lakini anashindwa kuandika, kwani wakati huohuo anawajibika kufanya “mipango” ili aweze kuishi siku inayofuata. Kufikia siku ya pili, vidokezo hivyo huwa vimechuja, mawazo yale hayapendezi tena kama vile alivyohisi jana yake. Bado anahitaji kuandika, lakini matatizo ya kiuchumi yangalipo. Wengi wa waandishi wachanga, katika hali kama hii, wataamua kuchukua njia ya mkato, ambayo daima si nzuri.
2.2 Tatizo la Kutotambuliwa
Hadi hivi leo, Tanzania haijashughulikia suala la nafasi na dhima ya mwandishi katika kukuza na kuathiri maendeleo ya utamaduni. Hata taasisi zinazoshughulikia vitabu – wachapishaji, wachapaji, watawanyaji – zinapewa msaada mdogo sana na serikali. Licha ya hayo, ijapokuwa kumekuwa na kilio kwamba kuna ukosefu wa vitabu, suala la hali au maslahi ya waandishi bado halijashughulikiwa. Hili lina maana kwamba kumekuwepo mteguko kati ya mwandishi na kazi yake – hususa mwandishi wa kazi za kubuni kuliko yule wa kazi za taaluma.
Maana ya hili ni kwamba waandishi wachanga hawafikiriwi kuwa muhimu katika jamii, na jamii haiwajali wala kutilia uzito mapambano yao, hivyo hawana kwa kutegemea au kutoa malalamiko yao. UWAVITA je? Kabla ya kufanyika semina hii, UWAVITA ulikuwa dhaifu na haukufahamika kwa waandishi wachanga wengi hapa nchini.
Kutokuwepo kwa masomo yafundishayo uandishi mashuleni (kinyume cha uchoraji, ufmyanzi, uchongaji na ufundi mwingine), tangu shule za msingi hadi chuo kikuu, ili kuwaendeleza wale wenye vipawa vya uandishi na kuwaongoza hadi wakomae, kunadhihirisha ukosefu wa ufahamu wa suala hili muhimu la kitamaduni. Mtu anafikia hali ya kujiuliza: hii jamii yenye kilio cha ukosefu wa vitabu inatarajia hao waandishi wa vitabu vizuri watoke wapi? Sehemu kubwa ya matatizo haya inaachiwa waandishi wachanga, ambao juhudi zao kubwa zinaishia katika miswada yao kukataliwa na wachapishaji, au hata kama wakipata wachapishaji (kama itokeavyo mara nyingine), kazi zao zinapambana na wahakiki wasomi, wasio huruma, ambao wanazitupa nje kama fasihi finyu au duni.
2.3 Uhusiano wa Mwandishi na Mchapishaji
Hapa tunayafikiria mahusiano ya aina mbili ya mwandishi na mchapishaji. Kwanza ni yale ya kutotoa ahadi thabiti (noncommital). Baada ya mchapishaji kupata muswada, mwandishi anaarifiwa kwamba muswada wake umefika na utasomwa kisha atapelekewa ripoti. Hili ni jambo lifanyikalo wakati wote na hakuna ahadi kutoka kwa mchapishaji kwamba ataichukua kazi hiyo.
Kama muswada unaonyesha hali ya matumaini, mchapishaji anagharamia na kuwapa wasomaji wa kitaalamu wawili nje ya shirika ili wauchunguze na kutoa maoni kwa marekebisho zaidi. Kutokana na maoni ya mhariri na hao wasomaji wawili, kamati ya wahariri huamua kama huo muswada utafaa kuchapishwa. Je kitabu kitauzika? Hili ni jambo muhimu ambalo wachapishaji lazima wazingatie kabla ya kukubali kuchapisha muswada. Kama muswada hauwezi kuchapishwa, japo unaonyesha matumaini au pengine masahihisho yaliyopendekezwa ni mengi, muswada hurudishwa kwa mwandishi pamoja na maelezo. Mchapishaji hawezi kuwasaidia waandishi zaidi ya hapa. Kwa hiyo, mwandishi chipukizi anaachwa peke yake tena kuendelea kutambaa katika uwanja huu mgeni wa sanaa. Baadhi ya waandishi ambao hushindwa kuendelea na kuusahihisha muswada hukata tamaa na kuacha kabisa, na wengine wenye moyo hujaribu kutafuta mchapishaji mwingine.
Kuna matatizo mengine ambayo hutokea hapa, hususa yale ya ucheleweshaji. Japokuwa tatizo hili linamwathiri mwandishi, lakini linahusiana zaidi na matatizo ya uchapishaji.
Mchapishaji hutoa ahadi thabiti kwa mwandishi baada ya kuukubali mswada na baada ya hapo mkataba husainiwa. Uhusiano wa mwandishi na mchapishaji hukomazwa na kuwa wa karibu zaidi mwandishi anapofanya kazi pamoja na mhariri. Na hapa tena tatizo la ucheleweshaji hutokea. Ucheleweshaji huo hutokea kwa sababu ya mambo yafuatayo:
Quote:
(a) Waandishi wachanga wengi huwa na kiherehere na hawajui njia ambazo muswada yabidi upitie. Wanataka kazi yao itoke baada ya mwezi mmoja.
Quote:
(b) Mwandishi anaweza kuwa mgumu kushughulika naye katika masahihisho madogomadogo kwa sababu anaithamini kazi yake kihisia.
Lakini hivi ni vikwazo viwezavyo kuvukwa.
Mrabaha Kablaya Muswada Kuchapishwa au Kuuzwa Msaada wa kifedha kwa mwandishi hutofautiana katika mashirika mbalimbali. Kwa mfano, Tanzania Publishing House hutoa malipo ya awali ya mrabaha kufuatana na vipengele vifuatavyo:
Quote:
(a) Wakati mchapishaji ameridhika na thamani na taadhima ya kazi na mwandishi.
Quote:
(b) Kama mwandishi ana kazi nyingine ambayo iko katika shirika hilo yenye mauzo mazuri, basi mchapishaji hutoa malipo ya awali na kujaribu kulipiza kutokana na kazi ambayo tayari inauzika.
Quote:
© Kama, kutokana na sababu za ugonjwa au umri, mchapishaji anahisi kwamba mwandishi anaweza asiishi muda mreru. Kwa mfano mrabaha wa awali ulitolewa kwa mwandishi wa Myombekere na Bugonoka kutokana na thamani ya kazi na taadhima ya mwandishi pamoja na umri wake.
Waandishi wachanga wengi, kwa bahati mbaya, hawajafikia taadhima kama hiyo katika kazi zao.
2.4 Kutokujua Matokeo
Msimulizi wa hadithi asimuliapo hadithi kwa watoto au watu wazima, kwa kawaida huwepo aina fulani ya itiko – mafarakano, mshangao, machozi katika nyuso za wasikilizaji; huwepo kupiga makofi na kushiriki katika masimulizi;
au huwepo mfadhaiko – wasikilizaji wakizungumza wao kwa wao au wakisinzia. Matokeo ya usimuliaji hujidhihirisha palepale, kiasi kwamba msimulizi hufahamu kama anawagusa wasikilizaji au hapana.
Kuna upungufu mkubwa wa uhakiki wa kazi za fasihi Tanzania. Kundi dogo lililopo la waandishi waliokomaa na wahakiki ambalo ni la kisomi limekazania sehemu ndogo ya fasihi na maarifa yao yamebakia kwao wenyewe na kuishia katika madarasa ya chuo kikuu. Mwandishi mchanga anabakia kurudia makosa na kuendeleza utoaji wa fasihi hafifu. Matokeo ya hali hi’ ni ukosefu wa kichocheo ambacho hutokana na uhakiki wa kazi za fasihi. Na hili linatabiri hali mbaya zaidi, maana fasihi ya Tanzania itakosa mwongozo muhimu, wa kuyasukuma maendeleo ya fasihi katika mweleko fulani. Swali ambalo yabidi tujiulize ni: kama waandishi wenyewe na wahakiki hawajali jambo hili muhimu, nani basi achukue jukumu hili?
Waandishi, na hususa waandishi wachanga, wanahitaji baraza – jarida la fasihi ambalo linatoa kazi zao haraka kuliko katika fani ya kitabu, na ambapo uhakiki wa maana unaweza kufanyika. Jarida la fasihi lingekuwa uwanja wa kufanyia majaribio kwa waandishi wachanga, na matatizo ya kukomaa hayangekuwa na mateso mengi.
3. Matatizo ya Ujumi, Fani na Usasa
Katika sehemu hii tunatoa madokezo tu ili kuibusha maswali ambayo yatazaa mjadala.
Fasihi kama chombo cha utamaduni haibuniwi wala kukua katika ombwe bila uhusiano na vitu vingine. Kuna mambo ya kifalsafa na kiujumi, ambayo yanatoa mwongozo kuhusiana na maana, ukuaji na upanuzi wa fasihi, na kadhalika kutoa kanuni za utambuzi wa manufaa yake.
Ujumi unayakinishwa na utamaduni uliopo, yaani mahusiano ya watu katika jamii kufuatana na wakati na mahali. Utamaduni unaathiri sana matendo ya binadamu dhidi ya mazingira. Kwa mfano, tunafurahia kile kilicho kizuri kifani, kiaina, krosemi, n.k., na kwa maana hii ujumi unakipa kitu thamani na maana.
Maarifa haya yanaweza yasimsaidie mwandishi katika kuandika, lakini yanamsaidia mwandishi kuelewa fasihi katika hali yetu ya kitamaduni. Haya maarifa yanaweza kuathiri kazi za sanaa kama ilivyotokea kwingineko. Bado tunamsoma Aristotle ili kuelewa tanzia. Lakini shujaa aishiaye katika tanzia katika jamii yetu ya Tanzama yukoje? Hatukatai kwamba maarifa ni kwa ajili ya dunia nzima, lakini hata hivyo yanatokana na upekee wa mataifa fulanifulani.
Je, mwandishi mchanga wa Kitanzania ambaye hajapambana na fasihi ya nchi za Magharibi anaitazama fani ya riwaya kama ya kigeni? Hili linaathirije uandishi wake? Labda hapa tunahitaji kutoa heshima kwa Aniceti Kitereza. Mafunzo tuwezayo kupata kutoka kwake ni mengi.
Usasa umebomoa mipaka ya makundi ya jamii za Kiafrika ambazo zilikuwa na misingi ya kuwezesha fasihisimulizi kushamiri. Msimulizi na wasikilizaji walikuwa na lengo moja – wote walitaka utaratibu na upatano katika jamii, na kwa hiyo basi msisitizo ukawa katika mafunzo ya kiitikeli katika hadithi. Wote walikuwa na lugha moja na hata methali. Utunzi ulikuwa ni wa kijumuia.
Makundi ya kijamii ya sasa yako mengi na yenye matakwa tofautitofauti. Hali hii imesababisha kwamba daraja linalounganisha utunzi na usomaji lilegelege: mwandishi yuko peke yake wakati atafutapo lugha ya kumwezesha kuwasiliana na msomaji; na msomaji kwa upande wake hana habari na matatizo haya. Vipi mwandishi, hususa mwandishi mchanga ambaye hana uzoefu, aishughulikie hali kama hii?
Kutofautiana kwa wasomaji, kwa hakika, ni jambo zuri kwa mwandishi, kwani kunasaidia kukuza wasomaji wa aina mbalimbali. Lakini kutofautiana huko kunabadili hali ya mwandishi, kitendo cha kutunga na matokeo yake. Mwandishi anapomaliza kazi yake anapambana na matatizo ya kupata wanunuzi wa kitabu chake au watetezi kwa sababu ya matatizo na mipaka ya mahusiano ya kijamii, ambayo, yeye kama mzalishaji, anayategemea. Hii ndio siasauchumi ya uandishi, kwa maneno rahisi.
4. Ufumbuzi wa Matatizo
Sisi wote tumeona katika uzoefu wetu kwamba njia za ufumbuzi wa matatizo kwa kawaida si halisi. Zipo, lakini pia hazipo. Hata hivyo hapa tumejaribu kutoa maoni.
Quote:
(a) Waandishi, wahakiki, waalimu (hususa wale wa lugha na fasihi) wachukue hatua za kushirikisha na kukuza vipawa na moyo wa kupenda kazi za sanaa mashuleni kwa kufundisha, kuandika, na kufanya mashindano. Taasisi mbalimbali za utamaduni nazo zifanye hivyohivyo au zitoe msaada.
(b) UWAVITA ufanye mpango wa kuendesha karakana za uandishi kila mwaka au baada ya miaka miwili kwa baadhi ya watu watakaochaguliwa ambao wanaonyesha matumaini na ari ya kuandika. Kadhalika umoja huo uanzishe makundi ya waandishi.
© UWAVITA ukiombe Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kianzishe mafunzo ya uandishi, ama kama idara tofauti au katika idara ya fasihi.