MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.

JIFUNZE KISWAHILI - SHAIRI: RWANDA NI KABILA MOJA

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: SHAIRI: RWANDA NI KABILA MOJA
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
RWANDA NI KABILA MOJA.
--------------------------------------
1.
Wasalam-aleikumu, hadhira hini azizi,
ninawagea nudhumu, yakinifu tena wazi,
n'kipenda mzifahamu, habari za pande hizi,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

2.
Nchi hii 'lijaliwa, na Rabana Maulana,
miaka elfu 'mekuwa, nchi 'metulia sana,
jamii 'likaa sawa, tena imeshikamana,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

3.
Aliishi mwananchi, popote nchini Rwanda,
kila sehemu ya nchi, lugha 'kiwa Kinyarwanda,
utamaduni wa nchi, ukiwa mmoja Rwanda,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

4.
Shughuli kuu za jadi, kufuga walimaizi,
wakiwa tena weledi, wakulima chapakazi,
walikuwa ni sitadi, mafundi wa ufinyanzi,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

5.
Hizi shughuli za jadi, na zilitegemeana,
ikiwa ndiyo miradi, ya babu zetu wa'ngwana,
jamii yetu ya jadi, kwazo ikielewana,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

6.
Waliishi kijamaa, kwa ukaribu wa sana,
kwa upendo na heshima, na wakithaminiana,
tangu za azali zama, 'kiwa wajamiiana,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

7.
Wakafika Wakoloni, walikuta ni wamoja,
'kaona utamaduni, na lugha yao ni moja,
hili liliwakwazweni, wakauvunja umoja,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

8.
''Gawanya na utawale," ilikuwa mbinu yao,
wakaziasisi shule, hasa kwa mafao yao,
waliyafundisha yale ya kugawa janja yao.
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

9.
Ninawaenzi wahenga, wali wa'sisi wa Rwanda,
utamaduni kujenga, kwa ari wakaulinda,
lugha iliyowaunga, Kinyarwanda waliunda,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

10.
Siasa za kikoloni, ziliyaleta madhara,
ukabila na udini, ni nguzo zao imara,
kuujenga ufitini, zilikuwa zake sera,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

11.
Abatwa siyo kabila, wafinyanzi maanaye,
Batutsi siyo kabila, wafugaji maanaye,
Bahutu siyo kabila, wakulima maanaye,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

12.
Maana za jadi yetu, kuelewesha shughuli,
zile za jamii yetu, Wazungu walibadili,
'ti ni makabila yetu, Dunia ikakubali,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

13.
Hebu weye tafakari, watu ulimi mmoja,
mila pia desituri, waishi aridhi moja,
jibu lake ni dhahiri, hawa ni watu wamoja,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

14.
Ilipofika nyakati, za uhuru kuutaka,
zilikuwa harakati, ukoloni kuutoka,
Wazungu 'kawa shariti, kutafuta vibaraka,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

15.
Ilikuwa ni rahisi, kuwapata vibaraka,
sababu 'weshanajisi, umoja wetu hakika,
ukoloni ibilisi, pisha mbali Mtajika,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

16.
Vibaraka walijaza, mifarakano nchini,
sana wakasheheneza, ukabila na udini,
yale walopandikiza, mahasidi Wakoloni,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

17.
Uhuru ulipofika, kote kote Afurika,
Rwanda tunasikitika, kusambaratika kote,
pande zote Afurika, tulikimbilia kote,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

18.
Mamboleo ukoloni, na wake vibarakala,
ulijikita nchini, pamwe na wake wakala,
kwa mtindo ja shetani, Rwanda wakaitawala,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

19.
Imetosha ! imetosha !, yametosha matokeo,
yalikotupelekesha, tunakojutia leo,
sana yametujulisha, ''Ukoloni mamboleo".
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

20.
Shukurani Maanani, kuniwezesha fikia,
ubeti wa ishirini, tungo ninamalizia,
nikiweka hadharani, fikira zangu sawia,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.

**********

Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda)
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare, JAMHURI YA RWANDA.