MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - SHAIRI: NIJILE TAKA IDHINI

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: SHAIRI: NIJILE TAKA IDHINI
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
NIJILE TAKA IDHINI
 
Nijile ndimi nijile, nijilepo pa kujiwa
Nami sijile na kele, zitazozusha beluwa
Nijile tuteze lele, na shingo tukizitowa
Kama idhini ‘tapawa
 
Nijile tuteze lele, na masogora wenzawa
Na ngoma hizi na zile, zipibwapo kutezewa
Nami ‘tateza vivile, midundo hiinyakuwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Nami ‘tateza vivile, uwandani sitakawa
Na watezewa waole, wafurahi watezewa
Na ijapo mizingile, ‘tangiya kuizinguwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Na ijapo mizingile, izingayo wazingiwa
Hata yangawa ni mile, ‘tajit’atuwat’atuwa
Nazo kumbi zilo tele, ‘tazingiya za kungiwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Nazo kumbi zilo tele, ziso matango na t’uwa
‘Tazingiya nizikale, nikeleti kwa sitawa
Kwa hayano na hayale, nizishize zangu ngowa
Kama idhini ‘tapawa
 
Kwa hayano na hayale, na mengine sitotowa
Mhariri nikujile, ufanye vya kufanyiwa
Na ambavyo vilekele, ni hayano kuchapiwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Na ambavyo vilekele, naweta wa kuwajuwa
Zuberi Lesso nijile, nawe nalishawishiwa
Ahadi nitimizile, ‘siwe mbwa kulaumiwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Ahadi nitimizile, Shabani Gonga tambuwa
U miyongoni mwa wale, walio wana welewa
Numa numa ‘siketile, nikaja nikakutiwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Numa numa ‘siketile, John Komba wagotewa
Mwandani wako ningile, nataraji kupokewa
Sambe nikusahawile, ukanipakaza towa
Kama idhini ‘tapawa
 
Sambe nikusahawile, J. Mayoka pumuwa
Hilino halilekele, la nami kusahawiwa
U mwenzangu mwenginele, upokee ujiliwa
Kama idhini ‘tapawa
 
U mwenzangu mwenginele, siwi mbwa kukuk’utuwa
Salim Ali yuyule, “Kibao” wafahamiwa
Ni mlangoni nikele, nangoja kufunguliwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Ni mlangoni nikele, watunzi nawamkuwa
Wa Ngurumo musikile, salamu nyote mwapawa
Na ambako nitoshile, ‘tanena mupate juwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Na ambako nitoshile, ni Mvita mwakwelewa
La zaidi sitashile, kwongeza mengi yakawa
Nikomilepo komele, nangoja kuchapishiwa
Kama idhini ‘tapawa
 
Nikomilepo komele, sendi nyengine hatuwa
Na ambalo lisalile, ni kwombeyana afuwa
Tupate liteza lele, mitima kufurahiwa
Kama idhini ‘tapawa
 
 
Abdilatif Abdalla
Dar es Salaam
Aprili 7, 1973
 
______________
Hili lilikuwa ni shairi langu la pili kulitunga Tanzania, tangu nilipohamia Dar es Salaam kutoka Mombasa, Kenya, mwezi wa Agosti 1972; na ambako nilifanya kazi Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili (baadaye Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mpaka mwaka 1979. Madhumuni yake yalikuwa ni kuwaomba idhini washairi wa Tanzania wanikubali mimi mgeni kuwa matengoni mwao. Maombi yangu yalikubaliwa, na nikakaribishwa kwa mashairi na washairi kadha wa kadha. Lilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Ngurumo la tarehe 12 Aprili, 1973, na gazeti la Uhuru la tarehe 19 Mei, 1973.