MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - SHAIRI: KISWAHILI KINAFAA, KUJENGA JAMII PANA

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: SHAIRI: KISWAHILI KINAFAA, KUJENGA JAMII PANA
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
KISWAHILI KINAFAA, KUJENGA JAMII PANA
*****************************************************
1.
N'napofanza utunzi, Mola unigee mwanga.
shukurani Mwenyienzi, nudhumu hini kutunga.
Lugha hino naienzi, ni ulimi unaunga,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
2.
Kiswahili lugha hii, ni gundi yaunga nyufa,
za kitaifa jamii, hata za kimataifa.
Inaunga dini hii, makabila na taifa,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
3.
Dini zawasiliana, kupitia Kiswahili,
makabila hukutana, yakiwamba Kiswahili.
Wanasiasa hunena, kutumia Kiswahili,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
4.
Na inavuka mipaka, lugha hini laazizi.
hadi ndani Afurika, 'mekita yake mizizi.
Duniani kadhalika, ina wengi watambuzi,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
5.
Mathalani Ujapani, Uchina na Marekani,
Uingereza Irani, aidha Ujerumani,
wana vipindi makini, vya Swahili redioni,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
6.
Ni ulimi watumika, jamii kusitawisha,
biashara 'kifanyika, watu kuwaendelesha.
Rahisi kueleweka, ujumbe kuwasilisha,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
7.
Ni ulimi muafaka, kuitafuta amani,
aidha unatumika, kuileta burudani,
nyimbo ze zinapendeka, hadi mbali Marekani,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
8.
Kula mpenda umoja, m'endeleo na amani,
Kiswahili ana haja, kwa sana kukithamini.
Tangia huko Ngadzija, Unguja na Mwambaoni,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
9.
Hata bara twaafiki, waamba ulimi huu,
Afurika Mashariki, kote Maziwa Makuu.
Lugha hii nahakiki, ndiyo ulimi mkuu,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
10.
Nitumie hu' wakati, kuwaenzi washairi,
Shabani bin Robeti, aliyekuwa mahiri.
Nawakumbuka kwa dhati, washairi walopita,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
11.
Napaswa nimuhongere, aliyetazama mbali,
Hayati baba Nyerere, alikuza Kiswahili.
Mchango wake si bure, wasifu asitahili,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.
12.
Nawatakia baraka, na wa Mola ufadhili,
Washairi watukuka, kwendeleza Kiswahili.
Kalamu chini naweka, hatima ya tungo hili,
Kiswahili kinafaa, kujenga jamii pana.

*******************
Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda)
JImbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,RWANDA.
Shairi makini sana