MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JIFUNZE KISWAHILI - Mzee Mwinyi ni mwalimu ‘darasa maalumu la Kiswahili’

JIFUNZE KISWAHILI

Full Version: Mzee Mwinyi ni mwalimu ‘darasa maalumu la Kiswahili’
You're currently viewing a stripped down version of our content. View the full version with proper formatting.
Kwa ufupi
Mzee Mwinyi ni mtumiaji mzuri wa lugha fasaha. Matumizi yake ya lugha hayana ubanangaji wa taratibu za lugha. Yeyote anayemsikiliza, huvutiwa na jinsi anavyotamka maneno kwa vituo na lafudhi yenye mvuto kiasi cha kumfanya kila mmoja aweze kuelewa ujumbe anaoutoa.
Na. Erasto Duwe
Lugha ya Kiswahili ni tunu iliyositirika kwetu, haina budi kuenziwa. Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, ni mfano mzuri na wa kuigwa katika kukienzi Kiswahili.
Mzee Mwinyi ni mtumiaji mzuri wa lugha fasaha. Matumizi yake ya lugha hayana ubanangaji wa taratibu za lugha. Yeyote anayemsikiliza, huvutiwa na jinsi anavyotamka maneno kwa vituo na lafudhi yenye mvuto kiasi cha kumfanya kila mmoja aweze kuelewa ujumbe anaoutoa.
Apatapo nafasi ya kuongea na wadau wa Kiswahili, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya Kiswahili fasaha. Katika Uzinduzi wa machapisho ya TATAKI, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 19. Machi 2015 , alibainisha kuwa vijana ndilo kundi litumialo ovyo Kiswahili. Hivyo, akawasihi vijana na wadau wa Kiswahili kukitumia kwa ufasaha.
Amekuwa akitumia Kiswahili na kukipamba kwa semi na tamathali za semi. Pindi anapotoa hotuba au ufafanuzi wa mambo, aghalabu hutumia semi na tamathali zake. Matumizi ya aina hii huufanya ujumbe wake uwe mzito, hivyo kuwafanya wasikilizaji kumakinika zaidi.
Apatapo nafasi kuwa mgeni rasmi au kutoa neno katika mikusanyiko ihusuyo Kiswahili, Mwinyi hutoa ‘darasa’ kwa hadhira yake kuhusu Kiswahili.
Katika uzinduzi alitoa ‘darasa’ lililowavutia wengi. Katika kufundisha kwake, alisisitiza kuacha ‘kukinyofoa’ Kiswahili. Hapo alimaanisha kuwa baadhi ya watumiaji wa Kiswahili, hawatumii maneno halisi ya Kiswahili badala yake huchukua maneno ya kigeni na kuyapachika katika Kiswahili bila sababu za msingi.
Alitoa mfano wa neno ‘wiki’ ambalo wengi hupenda kulitumia badala ya ‘juma’ likimaanisha siku saba za juma.
Akiendelea kukosoa matumizi mabaya ya msamiati, alisema maneno “tahadhari” na “hadhari” hubanangwa na watumiaji wa lugha. Neno ‘tahadhari’ linapaswa kutumika kama kitenzi na ‘hadhari’ kama nomino. Vilevile, katika utamkaji wa tarehe, alirekebisha na kusisitiza kuwa, mtumiaji wa lugha hapaswi kusema tarehe moja au “tarehe mbili bali tarehe mosi na tarehe pili.
Katika mkutano wa mwaka wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu), uliofanyika Maryland, Marekani hapo Aprili 2015; akiongea na wadau alisisitiza ufasaha wa Kiswahili katika matumizi.
Alisema kutumia neno “nawaahidini” (kwa watu ambao wapo karibu nawe na unawaahidi wao) ni makosa makubwa, kwani kiambishi awali ‘wa’ kinasimama kuwakilisha nafsi ya tatu ‘wao’ yaani watu wanaozungumziwa. Kama ahadi hiyo unaitoa mbele ya watu walio karibu yako, basi unapaswa kusema “nakuahidini”.
Maneno mengine ambayo Mwinyi amewahi kuyatolea ‘darasa’ ni pamoja na ‘onya’ na ‘ona’. Kitendo cha kutaka mtu aone kitu fulani ni ‘onesha’ na siyo ‘onyesha’ neno linatokana na ‘onya’ likimaanisha ‘kataza kwa konesha hatari itakayojitokeza.’
Huu umekuwa mtindo wake Rais Mstaafu Mwinyi apatapo nafasi za namna hiyo. Kwa njia hii huwafungua masikio wengi na kutanabahi makosa yao katika Kiswahili.
Mmahiri huyu wa Kiswahili si mpenzi wa lugha mseto kama walivyo baadhi ya watumiaji wa Kiswahili. Pamoja na kuzifahamu lugha za kigeni, hasikiki akichanganya ovyo maneno ya Kiswahili na lugha nyingine, labda kwa sababu maalumu za kiufundishaji.
Wapenzi wa Kiswahili, tuige mfano wa Mzee Mwinyi katika kuwafundisha wengine Kiswahili.