MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
TOFAUTI YA TUZO NA TUNZO

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
TOFAUTI YA TUZO NA TUNZO
#1
Baina ya TUZO na TUNZO
Bwana Mohamed Swaleh, maneno yote mawili yatumika. Yategemea tu sehemu kuzungumzwako Kiswahili. Kwa mfano, katika lugha za Kiswahili za Pwani ya Kenya, neno la asili ni "tuzo", na kitenzi chake ni "kutuza"; hakukuwako na neno "tunzo" kwa maana hii tuizungumzayo hapa - ingawa siku hizi kuna pia watumiao "tunzo",  kwa sababu ya kuathiriwa. Ni kama ule mfano wa neno "taazia" (ambalo ndilo la asili) watu wengine kulitamka na kuliandika "tanzia"; au "suitafahamu" (ambalo ndilo la asili) wengine kulitamka na kuliandika "sintofahamu". Matokeo yake ni kwamba leo watu wana uhuru wa kulitumia neno mojawapo kati ya hayo.
Huko Pwani ya Kenya kuna kitenzi "kutunza" pia (ambacho kina maana mbili tafauti) - kutegemea na jinsi utakavyoitamka hiyo "t" iliyoko kwenye neno hilo. (Katika lugha hizo, kuna namna nne za kuitamka harufu "t", ambazo hubadilisha maana ya neno). Neno "tunza" ukilitamka kwa "t" laini - kwa kuiweka ncha ya ulimi na kuishikamanisha baina ya meno ya mbele ya juu na ya chini - neno hilo litakuwa na maana ya kuhifadhi au kuhakikisha kwamba hicho ukitunzacho hakifikwi na madhara au uharibifu, kwa mfano. Lakini ukiitamka "t" kavu (kwa mfano, kama iliyoko kwenye neno "pita"), basi neno "tunza" litakuwa na maana ya kidonda, au sehemu ya mwili, kuwa na usaha; yaani kutunza usaha. Kama ujuavyo, kwa maana hii ya pili, neno litumikalo katika Kiswahili Sanifu, (kutokana na lugha za Kiswahili za Pwani ya Tanzania - Zanzibar na Bara), ni "kutunga usaha."
Kwa hivyo, kwa lugha za Kiswahili za Pwani ya Kenya, mtu afanyapo jambo zuri na ukalifurahikia, basi utamtuza mtu huyo; humtunzi.
Katika hizo lugha za Kiswahili za Pwani ya Kenya, hiki kitenzi  "kutuza" ni ufupisho wa kitenzi "kutuliza" (kwa mfano, kutuza moyo) - ambavyo vyote viwili viko katika hali ya kusababisha. Vitenzi vya asili ni "kutua" au "kutulia" - kwa maana ya  kuwa katika hali ya utulivu baada ya kuwa na wasiwasi, wahaka au jaka la moyo, yaani kumakinika; au baada ya kuhangaikahangaika; au baada ya kulifanya jambo likafanyika kisawasawa na watu wakatosheka nalo.
Kama nilivyoeleza, vitenzi "kutuza" na "kutuliza" viko katika hali ya kusababisha. Na nomino/ jina "tuzo" lawa ni ufupisho wa neno "tulizo" kwa maana ya kitu apawacho mtu ili kumtuliza baada ya kufanya jambo fulani zuri na watu wakalifurahikia. Kwa maoni yangu ya kiwanafunzi, hapa ndipo niionapo sababu ya kwa nini katika baadhi ya lugha
za Kiswahili, kwa muktadha huu, maneno yatumiwayo ni "tuzo" na "kutuza", na wala si "tunzo" na "kutunza". Au wewe wasemaje, Bwana Mohamed Swaleh? Nitafurahi sana kupata maoni zaidi, na yaliyo tafauti na haya, ili nifaidike nayo na kuniongeza maarifa.
- *Abdilatif Abdalla**
Hamburg, Ujerumani
25 Machi, 2021
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)