MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MBINU ZA USAWIRI WA WAHUSIKA WA FASIHI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MBINU ZA USAWIRI WA WAHUSIKA WA FASIHI
#1
Mbinu za Ujenzi wa Wahusika na Usawiri wa Sifa Zao: Uhakiki wa Riwaya ya Dunia Uwanja Wa Fujo ya E. Kezilahabi
 Leonard Flavian Ilomo


Ikisiri

Kipengele cha wahusika ni muhimu katika kuunda kazi yoyote ya kifasihi. Kipengele hiki hushirikiana

na vipengele vingine vya kifani katika kutoa maudhui ya kazi yoyote ya kifasihi. Kwa kawaida

wahusika hujengwa kisanaa na mwandishi ili waweze kuwakilisha dhana mbalimbali za maisha katika

jamii (Msokile 1992). Mwandishi huwajenga wahusika wake kwa kutumia mbinu mbalimbali ili

kuwatofautisha na hivyo kuiwezesha hadhira yake kutambua sifa au tabia za mhusika fulani

zinazomtofautisha na mhusika mwingine katika kazi husika. Hata hivyo, ni vema ifahamike kuwa kila

msanii wa kazi ya kifasihi ana mbinu zake za kuwajenga wahusika wake. Hii ina maana kuwa, msanii

wa kazi ya kifasihi anaweza kutumia mbinu moja au zaidi katika kazi fulani kutegemeana na aina ya

utanzu anaoushughulikia. Kwa kutambua hoja hiyo, makala haya yanafafanua mbinu mbalimbali

zilizotumiwa na E. Kezilahabi katika kuwajenga wahusika katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo na

mchango wa kila mbinu katika kubaini sifa za wahusika pamoja na dhamira katika kazi hiyo.Makala

hii imegawanyika katika sehemu nne. Sehemu ya kwanza ni utangulizi unaotoa muhtasari kuhusu

riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo; sehemu ya pili inazungumzia dhana ya wahusika katika fasihi;

sehemu ya tatu inajadili mbinu mbalimbali zinazotumika kuwajenga wahusika na jinsi sifa za wahusika

zinavyosawiriwa kupitia mbinu hizo; na sehemu ya nne ni hitimisho la mjadala katika makala hii.

 Utangulizi
Kuna tahakiki na maelezo mbalimbali kuhusu riwaya ya Kezilahabi, Dunia Uwanja
wa Fujo. Tahakiki hizo zimefanywa na wahakiki mbalimbali wa fasihi huku kila
mmoja akiwa na mwelekeo wake kutegemea lengo la mhakiki husika. Suala hili pia
analigusia Mlacha (1991) kuwa, uchunguzi wa riwaya unaweza kufanywa kwa
kuzingatia vipengele tofautitofauti kwa kutegemea kile ambacho mhakiki anakusudia
kukichunguza. Miongoni mwa wahakiki hao ni Senkoro (1982, 2011), Mulokozi
(1983), Wamitila (1997), Wafula (2002) na Diegner (2002).
Senkoro (1982, 2011) na Mulokozi (1983), wanaihakiki riwaya ya Dunia Uwanja wa
Fujo kwa kujikita zaidi katika maudhui yake. Senkoro (keshatajwa) anafafanua kuwa,
riwaya hii inashughulikia migogoro, matatizo na mikinzano ya kijamii, kiuchumi na
kifalsafa katika jamii ya Tanzania baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha.
Mulokozi (keshatajwa) anaenda mbali kidogo kwa kufafanua viwango ambavyo tatizo
la maisha katika riwaya hii linavyojadiliwa. Anavifafanua viwango hivyo kuwa ni
kiwango cha mtu binafsi na kiwango cha jamii. Wamitila (1997) katika makala yake
“Contemptus Mundi and Carpe Diem Motifs in Kezilahabi’s Works” anaielezea
riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo kuwa ni mfano bora wa motifu ya dunia kama
mahali pabaya pa kuishi na kuwa kuanzia mwanzo mwandishi anachora picha ya
ulimwengu ulio duni na usioaminika: sehemu yenye fujo ambapo utu unafifia katika mateso. Ubaya wa ulimwengu kama inavyooneshwa katika riwaya hii unatokana na
uzinzi, unyonyaji, ukahaba, kushushwa thamani kwa asasi ya ndoa, maamuzi
yasiyozingatia maoni ya wengine, dharau na visasi.
Kwa jumla tunapochunguza tahakiki hizo kuhusu riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo,
tunagundua kuwa zimejikita zaidi katika kuchunguza maudhui. Suala hili linajitokeza
si katika riwaya hii tu, bali linajitokeza pia katika tahakiki nyingi, hususan katika
taaluma ya fasihi ya Kiswahili (Mohochi, 2000). Hivyo, katika makala haya
tunachunguza kipengele cha fani cha riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo, hususan
wahusika kwa kuangalia mbinu zilizotumika kuwasawiri na jinsi mbinu hizo
zinavyosaidia kuyaelewa maudhui.
Dhana ya Wahusika
Wahusika wana umuhimu mkubwa katika kuiunda simulizi ya kifasihi. Hii inatokana
na ukweli kuwa, wahusika huweza kuathiri simulizi inayosimuliwa, yaani wao ndio
hupeleka mbele matukio katika simulizi. Wahusika wanaelezwa kuwa ni sehemu
muhimu ya fani (Msokile, 1992; Njogu & Chimerah, 2008), na kwamba, wahusika ni
viumbe wa kisanaa wanaobuniwa kutokana na mazingira na malengo ya msimulizi.
Bal (1997) anaeleza kuwa, wahusika hushabihiana na watu kwa kuwa fasihi
huandikwa kwa ajili ya watu na kwa hiyo huwahusu watu hao. Kwa kawaida
wahusika si watu halisi, bali ni matokeo ya ubunifu wa msanii ili kuakisi masuala
kadhaa ya kijamii ambayo msanii ameyakusudia. Kuhusu hili Bal (khj: 115) anasema:
“They are fabricated creatures made up from fantasy, imitation, memory: paper
people, without flesh and blood…The character is not a human being, but it
resembles one. It has no real psyche, personality, ideology or competence to act but
it does possess characteristics which make psychological and ideological
description possible”.
 
Wahusika ni viumbe wa kubuni wanaotokana na fantasia, mwigo, na kumbukumbu:
ni watu bandia wasio na damu na nyama…Mhusika si binadamu lakini anafanana
na binadamu. Hana akili, haiba, itikadi wala uwezo wa kutenda bali ana sifa
zinazotuwezesha kumtolea maelezo ya kisaikolojia na kiitikadi (Tafsiri Yetu).
Katika maelezo hayo, kinachojidhihirisha ni kukosekana akili, haiba, itikadi, na
uwezo wa kutenda kwa wahusika hali inayowafanya kuwa viumbe wa kubuni; yaani,
wanaotokana na ubunifu wa msanii ambaye huwaumba kufuatana na malengo yake.
Maelezo haya yanaungwa mkono na Mohamed (1995:72) anayesema, “mwandishi
anapoumba wahusika wake anaumba watu wasioishi katika ulimwengu wetu wa
bayana, bali wenye kuishi katika ulimwengu wao wa hadithi au tamthilia ambamo
wakitolewa watakuwa hawana maisha…”
Madumulla (2009) akiwarejelea Kasper na Wuckel (1982) anaeleza kuwa, mhusika ni
picha ambayo huchorwa na fasihi na ni kiini cha vitu vyote vipya, dhamira na mada
katika fasihi. Anaendelea kueleza kuwa, katika mhusika kuna uwili: mosi, kuna
usawiri wa kisanaa wa mtu kwa upande mmoja; pili kuna sura ya mtu kwa upande
mwingine. Ufafanuzi huu unashadidia hoja tuliyoitoa hapo awali kuwa, wahusika si
watu halisi bali watu wa kubuni. Ubunifu wa msanii humuwezesha msanii kuwaumba
au kuwasawiri wahusika kinafsia, kiakili, na kimwili. Usawiri wa wahusika
unaofanywa na msanii hutegemea mbinu mbalimbali ambazo msanii huyo
amezitumia. Kwa kuzingatia kauli hiyo, katika kipengele kinachofuata tumebainisha
mbinu mbalimbali ambazo msimulizi-mwandishi amezitumia katika kuwajenga
wahusika wa simulizi yake ya Dunia Uwanja wa Fujo. Mbinu hizo ni matendo,
mazingira, matamshi, uzungumzinafsiya, mazungumzo baina ya wahusika, na
uwasilishaji dhahiri.
Mbinu za Ujenzi wa Wahusika
Mbinu ya Kimatendo
Hii ni miongoni mwa mbinu ambazo msimulizi-mwandishi amezitumia katika kuwajenga
wahusika wa simulizi yake. Kwa kawaida matendo ya mhusika yanaweza
kuainishwa katika makundi matatu kama asemavyo Rimmon-Kennan (2002) ambaye
ananukuliwa na Shen (2006). Makundi hayo ni: tendo linalotendwa na mhusika “act
of commission,” tendo ambalo mhusika anapaswa kulitenda lakini halitendi “act of
omission,” na tendo ambalo halijafanikiwa ingawa mhusika amekusudia kulifanya
“contemplated act.” Mbinu hii humfanya msimulizi atumie ufafanuzi kidogo huku
msimuliwaji akipewa nafasi kubwa ya kutafsiri maana na sifa au tabia ya mhusika
kutokana na matendo yake.
Msokile (1992:43) anaeleza kuwa, “msanii huwaunda
wahusika kwa kutoa matendo nusunusu, hatoi maelezo juu ya matendo yote kwa mara
moja.” Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo, mbinu ya matendo imetumika katika
kuwajenga wahusika.
Tumaini ni miongoni mwa wahusika ambao wamejengwa kwa kutumia mbinu hii ya
matendo. Katika riwaya hii tunasimuliwa kuwa Tumaini alimtorosha Anastasia, binti
wa Mulele na mkewe Bukehele ili asiweze kuozwa kwa Tembo, mtu aliyekuwa mume
wa marehemu dada yake Anastasia. Tunasimuliwa kuwa, Tumaini alifanikiwa
kumtorosha na kwenda kuishi naye Shinyanga bila idhini ya wazazi wake Anastasia.
Kutokana na kitendo hiki tunaweza kumuelezea Tumaini kama mtu aliyekuwa hajali
taratibu za jamii yake na pia kitendo hiki kinadokeza mgogoro kati ya vijana na
wazee, mgogoro ambao ni matokeo ya vijana kujitafutia uhuru wao katika masuala
mbalimbali. Kitendo hiki cha Tumaini kumtorosha Anastasia kinaingia katika tendo
linalotendwa na mhusika kama inavyoelezwa na Shen (keshatajwa) ambaye anamnkuu Rimmon-Kenan. Kitendo hiki cha Tumaini kinajidhihirisha katika ukurasa
wa 48 wa riwaya hiyo kama ifuatavyo:
Anastasia alikuta Tumaini anafika kutoka mjini kupeleka vitu vyake. Tumaini
alimbeba Anastasia kwa baiskeli kuelekea Lutare. Njiani Tumaini alimweleza
Anastasia mpango aliokuwa nao. Anastasia alisikiliza kwa makini.
“Anastasia, unafahamu nimekuleta huku ngomani kwa sababu wazazi wako
hawataweza kuvumbua ni nani amekutorosha…”
Zaidi ya kitendo chake cha kumtorosha Anastasia, Tumaini alifanya kitendo cha
mauaji baada ya kumpiga kwa risasi mkuu wa wilaya aliyekuwa akihutubia mkutano
kuhusu ujamaa ambao Tumaini aliupinga. Tumaini alimpiga kwa risasi mkuu wa
wilaya baada ya mashamba yake kutaifishwa na kugeuzwa kuwa mali ya kijiji cha
ujamaa. Hiki ni kitendo ambacho kinamsawiri Tumaini kama muuaji na hivyo kuibua
dhamira ya mauaji. Hili linajitokeza ukurasa wa 128 ambapo tunasimuliwa:
Kelele za watu zilikuwa hazijatulia mlio wa bunduki uliposikika. Hapo hapo Mkuu
wa Wilaya alitotoma chini akaanguka. Mlio wa pili ulisikika pale pale. Tumaini
ambaye alikuwa akijaribu kutoroka alianguka chini. Watu wakasambaa ovyo huko na
huko kwa mbio. Kila mtu akajua roho yake. Uwanja wa mpira ukawa mdogo; mlango
ukawa hauonekani, na ukuta ukawa mfupi.
Katika dondoo hilo tunaona Tumaini akijaribu kutoroka baada ya kumpiga Mkuu wa
Wilaya kwa risasi, kitendo ambacho kinamfanya akamatwe na baadaye kuhukumiwa
kunyongwa. Pia, kitendo cha Tumaini kutozingatia ushauri wa mama yake, ushauri
uliomtaka kutafuta mchumba kwa kuzingatia tabia njema na kisha kuoa kinamsawiri
Tumaini kama mtu mkaidi, na pia kinaibua dhamira ya kiburi na umalaya. Katika
riwaya hii tunasimuliwa kuwa, badala ya kutafuta mchumba na kuoa, Tumaini
alijishughulisha zaidi na kutembea na wasichana tofauti tofauti pale kijijini kama
inavyosimuliwa katika ukurasa wa 17 kuwa:
Wasichana wengi kijijini walimpenda. Siyo kwa sababu alikuwa na pesa lakini kwa
sababu walimwona ni mwenzao: Tumaini hakuwa na kazi ya ofisini. Kwa hiyo
aliweza kuwaoa. Kule tu kutaja jina lake kulimfanya kila msichana kijijini awe na
tumaini la kuolewa naye.
Mama Resi ni mhusika mwingine ambaye amesawiriwa na msimulizi-mwandishi kwa
kutumia mbinu hii ya matendo. Kitendo kimojawapo ambacho alikifanya mhusika
huyu ni kile cha kukataa kushuka kwenye basi, ‘Tanganyika Bus,’ ili abiria wengine
wasukume basi hilo lililokuwa limekwama matopeni. Kitendo hiki cha kukataa
kushuka kwenye basi kinamsawiri mhusika huyu kama mtu mwenye kiburi na dharau.
Katika ukurasa wa 57 msimulizi-mwandishi anatusimulia:
Zilikuwa zimebaki maili arubaini kufika Shinyanga basi lilipokwama matopeni.
Watu wote waliombwa kutoka nje abaki dereva ndani peke yake. Watu wote
walitoka nje lakini yule mama na mtoto wake alikataa kutoka nje.
Kitendo hiki cha Mama Resi kinasawiri sifa ya kiburi aliyokuwa nayo mhusika huyo
na pia kinaibua dhamira ya ukaidi. Aidha, katika ukurasa wa 70 tunaona msimulizimwandishi
anaendelea kutumia mbinu ya kimatendo kumsawiri Mama Resi. Katika
ukurasa huo tunaelezwa matendo ya Mama Resi ya kuwa anaosha vyombo nusu saa
kabla ya kula. Tunasimuliwa kuwa:
Ukifika nyumbani kwa Dennis hukosi kukuta vyombo vimewekwa nje bila
kuoshwa. Kwa Dennis vyombo huoshwa nusu saa kabla ya kula hata vyombo
vilivyotumika usiku.
Kitendo hicho cha kuacha kuosha vyombo kwa muda mrefu, zaidi ya kumsawiri
Mama Resi kama mtu mvivu na mzembe, pia kinasaidia kuibua dhamira ya uvivu na
uzembe miongoni mwa wanajamii. Aidha, kupitia mpango ambao Mama Resi
alishiriki kuuandaa, mpango wa kumuua Tumaini kwa sababu tu ya kutopenda
maendeleo yake, unamsawiri Mama Resi kuwa mtu mwenye wivu, roho mbaya na
mwuaji. Pia, kitendo hicho cha Mama Resi kinaibua dhamira ya wivu na mauaji. Hata
hivyo, tunasimuliwa kuwa mpango wa kumuua Tumaini ulishindikana baada ya
washiriki wa mpango huo kutoelewana. Kitendo hiki kinaingia katika ile aina ya
tendo ambalo mhusika anakusudia kulitekeleza lakini linashindikana kutekelezwa.
“Tukishatenda jambo lazima tulitimize. Hatuwezi kuacha mambo nusu nusu.
Angalieni sasa tumo matatizoni. Huenda tukanyongwa au kufungwa maisha!”
Mama Resi alisema maneno hayo kwa kelele. Alitoa shilingi mia tano na kuzitupa
chini. “Bwana Makoroboi! Chukua hizo pesa. Mimi nataka uniletee kichwa chake!”
(ukurasa wa 88).
Katika maelezo ya dondoo hilo tunaona Mama Resi akinung’unika baada ya mpango
wao wa kumuua Tumaini kushindikana.
Mbinu ya Matamshi
Katika mbinu hii msimulizi huwajenga wahusika kwa kuwafanya wazungumze ili
lafudhi zao ziweze kuwabainisha. Kwa mfano, katika simulizi fulani msimulizimwandishi
anaweza kumjenga mhusika wake kwa kumfanya azungumze kwa lafudhi
ambayo ni tofauti na wahusika wengine ili kumtofautisha na wahusika wengine.
Lafudhi itakayosikika kutoka kwa mhusika huyo huweza kusawiri usuli wake na
kuibua dhamira fulani.
Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo mbinu hii imetumika katika kumjenga
Kasala ambaye anaonekana kuongea Kiswahili ambacho kimeathiriwa na lugha yake
ya asili. Katika ukurasa wa 5 msimulizi-mwandishi anatusimulia:
Polisi walipokuja walimkuta ameinama kichwa, damu ikimtoka puani.
“Mzee! Umekuwaje!” walimwuliza.
“Batoto bamenisondogorasondogora na chichwa! Bengine bamenikorotorakorotora
na kucha!” alijibu kwa Kiswahili alichokuwa anazungumza siku zile.
“Walikupiga kwa hedi labda?”
“Hapana na chichwa!”
“Na ngumi na makofi!”
“Ndiyo balikuwa kumi na kofia!’’
Katika mazungumzo hayo inabainika wazi kuwa matamshi ya Kasala, yaani jinsi
alivyokuwa akitamka maneno yake, na wale polisi yalikuwa tofauti. Kwa mfano,
dondoo hilo linaonesha neno ‘kichwa’ lilitamkwa kama ‘chichwa’, ‘walikuwa’
lilitamka kama ‘balikuwa’ na kadhalika. Zaidi ya matamshi inaonekana Kasala
alishindwa kuelewa maana ya neno ‘ngumi’ kwa kudhani ni ‘kumi’, na ‘makofi’ kwa
kudhani ni ‘kofia’. Kwa hiyo, kutokana na matamshi yake Kasala anasawiriwa kama
mtu aliyekuwa hajui lugha ya Kiswahili vizuri. Zaidi ya kumsawiri kama mtu
aliyekuwa hajui Kiswahili vizuri, mbinu hii ya matamshi inasaidia kubainisha tofauti
za watu kijiografia na kuibua dhamira ya tofauti baina ya miji na vijiji. Matamshi ya
Kasala yanaibua dhamira hii kutokana na ukweli kuwa katika jamii za Kitanzania,
watu waishio vijijini matamshi yao ya lugha ya Kiswahili huwa yameathiriwa sana na
lugha za makabila tofauti na watu waishio katika miji ambako lugha za makabila
hazipewi nafasi kubwa katika mawasiliano ya kila siku.
Mbinu ya Kimazingira
Mbinu hii inajitokeza zaidi tunapozichunguza tabia mbalimbali za Tumaini ambazo ni
matokeo ya mazingira aliyoishi hapo awali. Katika ukurasa wa 11 tunasimuliwa:
Tumaini alikuwa kwa kutengwa. Alinunuliwa vijigari vidogo vingi; kila alicholilia
alipewa. Siku moja Tumaini alimchoma mlezi wake jichoni. Yule mvulana alimpiga
Tumaini kidogo. Tumaini alikimbia kwenda kushitaki kwa mama yake.
Kutokana na maelezo hayo tunapata picha nzima ya mazingira ambayo Tumaini
alilelewa. Tunaelezwa kuwa Tumaini alikulia katika mazingira ya kuengwa sana,
yaliyomfanya awe na tabia zisizokubalika. Ni kutokana na malezi hayo, Tumaini
alijenga dharau kwa watu wengine. Pia, tunasimuliwa kuwa, zaidi ya mazingira ya
kuengwa Tumaini alikulia katika mazingira ya uyatima baada ya wazazi wake
kufariki na ndugu zake kutokuwa tayari kuishi naye. Katika ukurasa wa 16
tunasimuliwa:
Baada ya kifo cha mama yake, Tumaini alikata shauri kuacha shule…Tumaini
alipoacha kusoma aliishi ndani ya nyumba ya baba yake. Marehemu baba yakealikuwa hakai ndani ya nyumba za serikali…Tumaini alirithi shilingi elfu hamsini.
Kwa sababu hii jamaa zake walikataa kuja kuishi naye.
Maelezo hayo yanaendelea kufafanua mazingira aliyokulia Tumaini, mazingira ya
uyatima ambayo yalimsababisha akose mwongozo katika maisha yake. Hali hii
ilimfanya Tumaini aishi kwa kujiongoza mwenyewe. Pamoja na mazingira magumu
aliyoishi, tunaelezwa kuwa Tumaini alipambana na mazingira hayo na hatimaye
alifanikiwa ingawa Azimio la Arusha lilimpotezea matumaini yake. Kwa hiyo,
kutokana na mazingira hayo matendo ya baadaye ya Tumaini yaliathiriwa sana. Kwa
mfano, mazingira ya kuengwa yalisababisha Tumaini aamini kuwa kila alichokifanya
kilikuwa ni sahihi na kwamba ilikuwa ni haki yake. Hali hii ilimfanya Tumaini kuwa
kiumbe aliyetenda kinyume na matarajio ya jamii iliyomzunguka kwa sababu ya
kiburi na dharau. Mbinu hii ya kimazingira, zaidi ya kumsawiri Tumaini kama yatima
pia inaibua dhamira ya malezi na umuhimu wa wazazi.
Mbinu ya Uzungumzinafsiya
Wamitila (2008:379) anaifafanua mbinu hii kuwa ni “mtindo wa kuyawasilisha
mawazo ya mhusika kwa mtindo au njia ya kujizungumzia.” Anaendelea kueleza
kuwa, “katika uchunguzi wa dhana hii tunaweza kubainisha kati ya aina kuu mbili: (a)
uzungumzinafsiya wa moja kwa moja, na (b) uzungumzinafsiya usio wa moja kwa
moja…” Kutokana na maelezo hayo tunaweza kueleza kuwa, uzungumzinafsiya
unahusu monolojia, yaani mhusika anajizungumzia peke yake. Kutokana na
kujizungumzia huko, wasimuliwaji hupata fursa ya kufahamu kile kinachoendelea
katika akili ya mhusika, kwa hivyo wasimuliwaji huweza kubaini sifa au tabia za
mhusika huyo pamoja na maudhui yanayoibuliwa.
Katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo mbinu hii imetumiwa na msimulizimwandishi
katika kuwajenga baadhi ya wahusika wake. Miongoni mwa wahusika
wanaojengwa kwa mbinu hii ni Mugala. Huyu alikuwa mama yake Kasala ambaye
alihamishiwa kisiwani kutokana na kuhisiwa kuwa alikuwa mchawi. Msimulizimwandishi
anatumia mbinu hii katika kumsawiri Mugala katika ukurasa wa 19
anasema:
Tumaini alipofika mbali sana, Mugala alianza kucheka hali akizungumza polepole.
Sasa ilikuwa zamu yake kumcheka mwenziwe.
“Samaki amejileta mwenyewe ndani ya chungu. Kenge akikosa chakula huachama;
nzi wakiona mdomo wake mwekundu hufikiri ni nyama na kuingia kwa wingi.
Akiona wamekuwa wengi hufunga mdomo na kuwatafuna. Nimekwishakata shauri
kuumaliza ukoo wao. Na nitaumaliza. Lakini, huyu mtoto ni mzuri vile kwamba
nimemwonea huruma. Oh! Ninakumbuka katika kazi yetu huruma ni kosa kubwa sana. Siku ile niliyoapa msituni, kwa kuuma kidole gumba, kwamba sitamhurumia
mtu yeyote bado naikumbuka. Kwa hiyo nitamchukua mtoto huyu. Lakini hakuna
haraka. Nitamwacha kwa muda afanye mapenzi yake na Leonila.”
Katika dondoo hilo tunamwona Mugala akijizungumzia peke yake baada ya Tumaini
kuondoka. Huu ni uzungumzinafsiya wa moja kwa moja kutokana na mawazo ya
Mugala kuweza kubainika wazi bila kuingiliwa na mtunzi. Kutokana na
kujizungumzia huku, tunabaini kuwa Mugala ni muuaji tena asiye na huruma
kunatokana na kiapo alichokula msituni. Zaidi ya kumsawiri Mugala, mbinu hiyo
inaibua dhamira ya uchawi na ushirikina.
Tumaini ni mhusika mwingine ambaye amesawiriwa kwa kutumia mbinu hii ya
uzungumzinafsiya. Katika ukurasa wa 19 tunasimuliwa kuwa, akiwa njiani kutoka
katika mji wa Kasala kuonana na Mugala, Tumaini alisikia kama sauti ya ndege
akiimba. Hata hivyo, sauti hiyo haikuwa ya ndege bali ilikuwa sauti ya moyo wa
Tumaini. Katika ukurasa huo tunasimuliwa:
Akiwa njiani kurudi nyumbani, Tumaini alisikia sauti kama ya ndege akiimba kwa
huzuni: “Tumaini usidhani kwamba umefanya jambo zuri. Huyo mzee amekwisha
kuwa kama mtoto mdogo. Wewe umemchezea kama picha. Tumaini, hii ndiyo
heshima yako kwa watu kama hawa! Tumaini huna huruma; utakuja kuwa kama yeye
siku moja!”
Hiyo haikuwa sauti ya ndege. Sauti ya moyo wake ndiyo ilikuwa ikisumbua.
Tunapochunguza dondoo hilo tunabaini kuwa, Tumaini alikuwa akijizungumzia
nafsini mwake. Huu ni uzungumzinafsiya usio wa moja kwa moja kwa sababu sauti
inayosikika ni ya msimulizi nafsi ya pili. Uzungumzinafsiya huu unatuwezesha
kubaini sifa ya utovu wa nidhamu aliokuwa nao Tumaini na umuhimu wa kuheshimu
wazee. Ni kutokana na kugundua kuwa alimkosea Mugala, alianza kujuta yeye
mwenyewe.
Tumaini anaendelea kusawiriwa na mbinu hii katika ukurasa wa 32 ambapo
anaonekana akitafakari kitendo cha wanakijiji kumnyanyasa Mugala na hatimaye
kuhamishiwa katika kisiwa cha wachawi. Tukio hili linamfanya Tumaini atafakari
mwenendo mzima wa maisha yake na hatima yake pale kijijini. Katika ukurasa huo
tunasimuliwa:
Alipofika kitandani mawazo mengi yalimwingia kichwani. Alianza kufikiri.
“Nafikiri Mugala alikuwa mtu mwema, hasa kwangu. Alinisaidia kupata chakula
nilipokuwa nina njaa. Lakini kwa muda wa siku moja tu amechukiwa na kila mtu
kwa ajili ya matendo yake mabaya. Mtu ambaye ameshindwa kuishi na raia
amechoka maisha. Huu ni ukweli mtupu. Mugala alipigwa na watoto wadogo, alitemewa mate, lakini hata jamaa zake walimtazama tu. Kumbe raia wakikususa
unakuwa kama mnyama! Mimi je? Huenda labda watu wamekwishaanza
kunikasirikia kwa kuharibu binti zao! Kuna mambo mawili ninayoweza kufanya; au
nirekebishe mwenendo wangu na niendelee kuishi humuhumu kijijini; au nitoroke
niende nchi za mbali kabla mtumbwi haujatoboka…”
Katika dondoo hilo tunaona Tumaini akijizungumzia peke yake. Kujizungumzia huko
kunatokana na matendo aliyofanyiwa Mugala, matendo ambayo yanamfanya Tumaini
ajitathimini mwenendo wake na hatima yake pale kijijini. Kutokana na dondoo hilo
Tumaini anasawiriwa kama mtu aliyekuwa na uwezo wa kugundua hatari inayomnyemelea
na ambaye alikuwa akiujua ukweli lakini alikuwa akiupuuzia. Pia, kutokana
na kujizungumzia huko tunajuzwa umuhimu wa kuishi vizuri na watu. Zaidi ya
dondoo hilo, katika ukurasa wa 120 msimulizi-mwandishi anaendelea kumsawiri
Tumaini kwa kutumia mbinu hii. Katika ukurasa huo tunasimuliwa kuwa:
Alipokuwa akiosha vyombo, Tumaini alikuwa ameshindwa kupata usingizi. Alikuwa
sasa akizungukazunguka humo chumbani. Mawazo haya yalikuwa yakimzunguka
kichwani
“Siwezi kutukanwa na mwanasiasa anayetegemea kura yangu! Haiwezekani! Mimi
sikumkataza kunenepa! Na hata hivyo ninakula jasho langu. Tabu niliyoipata zamani
imenifunza kutafuta pesa. Nilikata shauri kufanya kazi; nikawa nashinda shambani
asubuhi na jioni. Na sasa nimepata mali. Halafu huyu mwanasiasa ananiita
mnyonyaji! Mali niliyosumbukia mwenyewe wakati watu wengine walikuwa
wakishinda kwenye kangara! Haiwezekani! Potelea mbali vijiji vyao vya ujamaa
ambavyo vimerudisha nyuma maendeleo ya watu wengi. Haiwezekani!”
Katika dondoo hii msimulizi-mwandishi anamchora Tumaini akijizungumzia. Katika
kujizungumzia huko, Tumaini anatuwezesha kutambua msimamo wake kuhusu sera
ya vijiji vya ujamaa ambavyo vilikuwa ni matokeo ya Azimio la Arusha. Hivyo,
mbinu hii inamjenga au kumsawiri Tumaini kama mtu aliyekuwa akipinga sera ya
vijiji vya ujamaa kwa sababu aliamini kuwa vijiji hivyo vilikuwa vikirudisha nyuma
maendeleo. Zaidi ya kumsawiri Tumaini, mbinu hii inaibua dhamira ya suala la
upokezi wa Azimio la Arusha miongoni mwa Watanzania. Katika dondoo hilo
inaonekana kuwa Azimio la Arusha lilikumbana na upinzani wa wanajamii kama
anavyofafanua Senkoro (2011:88), “kwa wakulima, kwa vile hawa ni tabaka lililo
gumu sana katika kubadili wenendo wake na kaida zake za maisha; ilikuwa vigumu
kwao kulipokea Azimio kwa urahisi.”
Mbinu ya Mazungumzo baina ya Wahusika
Mbinu hii imetumika kwa kiasi kikubwa katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo,
ambapo msimulizi-mwandishi amewapambanisha wahusika ili wazungumze wao kwa wao. Msokile (keshatajwa:44) anaeleza, “kadiri wanavyoendelea, wazo la mhusika
pamoja na tabia yake hujulikana taratibu katika kazi hiyo.” Katika riwaya hiyo,
wahusika mbalimbali wamejengwa au wamesawiriwa kwa kutumia mbinu hii.
Miongoni mwa wahusika hao ni Mama Resi na Tumaini. Katika riwaya hiyo,
msimulizi-mwandishi amewapambanisha wahusika hawa katika sehemu mbalimbali
za simulizi yake. Kwa mfano, katika ukurasa wa 71 Tumaini anaoneka akizungumza
na Mama Resi kama ifuatavyo:
“Imekwendaje hata ukaoa msichana ambaye hakusoma?”
“Ni mapenzi tu, Mama Resi.”
“Mapenzi gani hayo! Mimi ninafahamu kwa nini umemwoa. Umemwoa ili uweze
kumwonea. Unataka mwanamke ambaye unaweza kumwamrisha kama mtoto mdogo,
karibu kama mtumwa.”
“Wewe na Dennis mko sawa?”
“Mimi na bwana wangu tunaamini katika jambo hili usawa. Hata mimi ninaweza
kutoa maoni yangu mbele ya bwana wangu…”
“Mama Resi, jambo la usawa linakuharibu mawazo yako bure. Jambo la maana katika
jamii yoyote ni heshima. Bwana na mke, hata kama wanajidai kwamba wao ni sawa,
wasipopeana heshima jamii yao haitakuwa thabiti kamwe.”
Katika dondoo hilo tunaona Tumaini akipambanishwa na Mama Resi katika
mazungumzo. Ni katika mazungumzo hayo ndipo tunapogundua mitazamo ya
wahusika hawa kuhusu usawa kati ya mwanamume na mwanamke. Kupitia mazungumzo
hayo msimulizi-mwandishi anawasawiri wahusika hawa kuwa ni watu
waliokuwa wakitofautiana kimtazamo na kifikra. Wakati Tumaini anasawiriwa kama
mtu aliyekuwa akiamini katika heshima; Mama Resi anasawiriwa kama mtu
aliyekuwa akiamini katika haki na usawa wa kijinsia. Usawa huo anaouamini Mama
Resi, kwa Tumaini ulikuwa ni usawa uliojikita katika mtazamo wa Kizungu wakati
kwa mtazamo wa Kiafrika usawa ni wa kuheshimiana (ukurasa wa 72). Kutokana na
mazungumzo hayo, pia inaibuliwa dhamira ya Uafrika dhidi ya Umagharibi. Katika
dhamira hii tunaelezwa kuwa kwa mtazamo wa Kiafrika heshima ni jambo la msingi
wakati kwa mtazamo wa Kimagharibi usawa wa kijinsia ndio jambo la msingi bila
kujali iwapo usawa huo unazingatia utu.
Pia, mbinu hii imetumika kuwapambanisha Tumaini na Dennis katika mazungumzo
yao. Kupitia mazungumzo yao (ukurasa wa 63-64) tunabaini mtazamo wa kila
mhusika kuhusu maisha. Katika ukurasa wa 63 Tumaini anasawiriwa kama mtu
aliyeamini kuwa, ulimwengu hauwezi kuwa na taabu kama mtu ana pesa, nyumba, na
gari. Wakati Tumaini akisawiriwa hivyo, Dennis anasawiriwa kama mtu aliyeamini
kuwa furaha ya mwanadamu haiwezi kuletwa na vitu kama nyumba hasa ukizingatia
kuwa “nyumba za binadamu zinaonesha upungufu wa uhuru alionao” (ukurasa wa
64). Kutoka na mbinu hii ya mazungumzo tunaweza kubaini ujumbe ambaomsimulizi-mwandishi anataka tuupate. Mathalani, katika ukurasa wa 64 tunaelezwa
kupitia Dennis kuwa furaha katika maisha hailetwi na wingi wa vitu ambavyo mtu
anavimiliki.
Aidha, Leonila na Anastasia wamepambanishwa ili kubainisha uhusiano wao. Katika
riwaya hiyo inaonekana Leonila na Anastasia walikuwa marafiki kabla ya
kuhitilafiana kutokana na wote kumuhitaji Tumaini. Kuhitilafiana huko kunasawiriwa
kwa kutumia mazungumzo yao katika ukurasa wa 25-26:
“Vipi dada; mbona hivi!”
 “Mimi sikuelewi,” Anastasia alijibu.
 “Mbona umenipindulia serikali yangu!”
 “Nani amekwambia!”
 “Nimesikia kwamba kitanda cha bwana wangu siku hizi kimekuwa chako!”
 “Sikufahamu kama alikuwa amekwisha toa mahari! Tangu lini dada yangu, huyu
akawa bwana wako?”
“Hufahamu kwamba ninamtunzia mtoto wake!”
 “Samahani dada yangu, yeye mwenyewe aliniambia kwamba amekwisha kupiga
chaki.”
 “Umesema nini? Sema tena nisikie!”
Katika dondoo hilo Leonila na Anastasia wanachorwa wakiwa wanazungumza.
Wahusika hawa wanasawiriwa kama watu waliokuwa marafiki lakini baadaye walihitilafiana
kwa sababu ya kugombea mwanamume, Tumaini. Kupitia dondoo hilo,
uhusiano kati ya wahusika hawa unaonekana kubadilika kutoka ule wa kirafiki na
kuwa wa kiuadui. Hivyo, zaidi ya kusawiriwa kwa uhusiano baina ya Leonila na
Anastasia, pia unasawiriwa mgogoro wa kimapenzi uliopo baina ya wahusika hao.
Mbinu ya Uwasilishaji Dhahiri
 Mbinu hii inahusisha kutaja moja kwa moja na kwa uwazi sifa za mhusika fulani
katika matini husika. Hii ina maana kwamba sifa na matendo ya mhusika yanaelezwa
waziwazi na msimulizi. Mbinu hii ya kuwaumba wahusika husaidia kumfanya
msomaji asipate taabu katika kutambua wasifu wa ndani na wasifu wa nje wa
mhusika. Pia, mbinu hii humsaidia msomaji kutambua kiini cha kisa, wazo au
dhamira (Msokile, 1992:43).
Katika riwaya hii, mbinu ya uwasilishaji dhahiri imetumiwa na msimulizi-mwandishi
katika kuwajenga wahusika wake. Miongoni mwa wahusika waliojengwa kwa
kutumia mbinu hii ni Dennis. Katika riwaya hii tunaelezwa kwa uwazi kuwa, “Dennis
alikuwa kifungua mimba” (uk. 5), na “aliishi kwenye nyumba kubwa” (ukurasa wa
60). Maelezo haya kuhusu Dennis yanaonesha wazi kuwa mtu huyo alikuwa ni nani na aliishi maisha ya namna gani. Kwa mfano, tunaelezwa wazi kuwa Dennis aliishi
kwenye nyumba kubwa ya serikali; hali hii inamjenga Dennis kama mtu aliyekuwa na
unafuu wa maisha kuliko watu wengine.
Mhusika mwingine aliyejengwa kwa kutumia mbinu hii ni Mulele. Mhusika huyu
anaelezwa kama mtu ambaye “alikuwa akijishughulisha na kilimo” na ambaye
“alikuwa akiupinga ujamaa” (ukurasa wa 33). Zaidi anajengwa kama “mtu mkarimu”
(ukurasa wa 38) na ukarimu wake unaelezwa wazi kuwa alikuwa akitengeneza pombe
na kuwakaribisha jirani zake kunywa bila malipo. Kutokana na maelezo hayo,
tunaweza kumuelezea Mulele kama kiwakilishi cha watu ambao hawakuwa tayari
kuupokea ujamaa kwa sababu tayari wao walikuwa wakiishi kijamaa katika vijiji vyao
kwani walikuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali. Kutokana na kusawiriwa
huko, tunabaini dhamira ya ukarimu, na zaidi tunajuzwa kuwa ujamaa ni jadi ya
Waafrika.
Mhusika mwingine aliyesawiriwa kwa kutumia mbinu hii ni John, rafikiye Tumaini.
Katika ukurasa wa 47, msimulizi-mwandishi anamsawiri John kwa uwazi kuwa,
“aliacha shule alipofukuzwa baada ya kuwagomesha wenzake kula chakula,” na
“aliishi kama mhuni.” Kutokana kusawiriwa huko, kadiri simulizi inavyoendelea
tunaelezwa John akifanya matendo ambayo hayakubaliki kama vile, kufanya tendo la
ndoa na wake wa rafiki zake, ulevi, na kadhalika. Matendo haya hayana budi
kufanywa na mhusika huyu kutokana na namna alivyosawiriwa tangu mwanzo.
Mbinu hii, zaidi ya kumsawiri John, inaibua dhamira mbalimbali kama vile uhuni,
umuhimu wa elimu, na kadhalika.
Hitimisho
Tunapochunguza kuhusu mbinu zilizotumika kuwajenga wahusika, zaidi ya kusawiri
sifa za wahusika na kudokeza dhamira, zimefanikisha kufafanua falsafa
iliyofumbatwa katika jina la riwaya: Dunia Uwanja wa Fujo. Falsafa hii inayaona
maisha kuwa ni fujo tupu (Senkoro, 2011). Fujo hizi zinaonekana kila mahali, vijijini
mpaka mijini. Aidha, fujo hizi zinaokana katika maeneo mbalimbali kama vile; katika
siasa, lugha, ndoa, na kadhalika. Kwa mfano, katika mbinu ya matendo tumeeleza
matendo kadhaa kama ya Tumaini kumtorosha Anastasia; Mama Resi kukataa
kushuka kwenye basi na kadhalika. Matendo haya yanasawiri fujo zinazoendelea
ulimwenguni. Kitendo cha Tumaini kumtorosha Anastasia ni fujo kwa jamii kwa
sababu misingi ya ndoa inakiukwa. Aidha, kitendo cha Mama Resi kutoshuka kwenye
basi ni fujo. Kimsingi matendo hayo yanadokeza falsafa iliyofumbatwa katika jina la
kitabu. Kwa hivyo, mbinu zilizobaishwa katika makala haya zina mchango mkubwa
katika kuelewa mawazo ya riwaya au falsafa inayohusika.
Marejeleo
Bal, M. (1997). Narratology: Introduction to the Theory of Narrative (2nd edition). Toronto:
University of Toronto Press.
Diegner, L. (2002). “Allegories in Euphrase Kezilahabi’s Early Novels,” katika Swahili
Forum IX, uk. 43-74.
Kezilahabi, E. (2007). Dunia Uwanja wa Fujo. Nairobi: Vide-Muwa Publishers Limited.
Madumulla, J. S. (2009). Riwaya ya Kiswahili. Dar es Salaam: Mture Educational Publishers.
Mlacha, S. A. K. (1991). “Point of View as Stylistic Device in Kiswahili Novels,” katika
Kiswahili: Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Juz. 58, kur. 54-61. Dar es
Salaam: TUKI.
Mohamed, S. A. (1995). Kunga za Nathari ya Kiswahili: Tamthilia, Riwaya na Hadithi Fupi.
Nairobi: East African Educational Publishers.
Mohochi, E. S. (2000). “Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini” katika Nordic Journal
of African Studies 9 (2), uk. 49-59.
Msokile, M. (1999). Misingi ya Hadithi Fupi. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
 Mulokozi, M. M. (1983). “Dunia Uwanja wa Fujo (Mapitio ya Kitabu),” katika Kiswahili:
Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Juz. 50/1, kur. 1-12. Dar es Salaam:
TUKI.
Njogu, K. & Chimerah, R. (2008). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu (Chapa ya
Pili). Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Senkoro, F. E. M. K. (1982). Fasihi. Dar es Salaam: Press and Publicity Centre.
Senkoro, F. E. M. K. (2011). Fasihi. Dar es Salaam: KAUTTU.
Shen, F. (2006), “Narrative Strategies in Robert Cormier’s Young Adult Novels.” PhD
Dissertation, Ohio State University.
Wafula, R. (2002). “Language and Politics in East African Swahili Prose: Intertextuality in
Kezilahabi’s Dunia Uwanja wa Fujo ‘The World a Playground of Chaos,’” katika
Obeng, S. G. & Hartford, B. (wah.), Surviving Through Obliqueness: Language of
Politics in Emerging Democracies, uk. 19-29. New York: Nova Science Publishers
Inc.
Wamitila, K. W. (1997). “Contemptus Mundi and Carpe Diem Motifs in Kezilahabi’s Works”
katika Kiswahili: Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Juz. 60, kur. 15-24.
Dar es Salaam: TUKI.
Wamitila, K. W. (2008). Kanzi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi: VideMuwa
Publishers Ltd.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)