MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
DHANA NA HISTORIA YA SARUFI MAPOKEO

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
DHANA NA HISTORIA YA SARUFI MAPOKEO
#1
Dhana na historia ya sarufi mapokeo
Dhana ya Sarufi
Sarufi ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala lugha katika matumizi yake ambayo hujumuisha matamshi, maumbo, miundo na maana (Saluhaya, 2010:72).Massamba na wenzake (1999) Sarufi ni kanuni, sheria au taratibu zinazotawala kila moja kati ya viwango vinne vya lugha ambavyo ni umbo-sauti (fonolojia), umbo-neno (mofolojia), miundo maneno (sintaksia) na umbo maana (semantiki).Matinde (2012:211) Sarufi ni taaluma ya lugha inayochunguza na kuchanganua vipashio na kanuni mbalimbali zinazotawala muundo wa lugha.Massamba (2004) anasema, sarufi ni taaluma ya lugha inayohusu uchunguzi na uchanganuzi wa kanuni za vipengele mbalimbali vya lugha.Kwa ujumla sarufi inaweza kuelezwa kama kanuni, sheria na taratibu zinazomuongoza mzungumzaji au mwandishi kuzungumza au kuandika tungo sahihi zinzoeleweka kwa msikilizaji wa lugha ileile. Kama ni mzawa wa lugha, mtumiaji huwa tayari anazo kanuni hizo (hata katika uzungumzaji), yaani kanuni anakuwa nazo akilini baada ya kusomaau kuishi na watu wa lugha hiyo. 
 
Dhana na historia ya sarufi mapokeo. Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999) wanaeleza kuwa, sarufi mapokeo ni sarufi elekezi ikisisitiza usahihi wa lugha kwa kuonesha sheria ambazo hazina budi kufuatwa, mathalani kufanya muundo fulani wa sentensi usomeke kwa usahihi au sheria ambazo hazina budi kufuatwa ili kufanya matamshi fulani yakubalike kuwa ndio sahihi.Matinde (2012:211) anaeleza kuwa, mkabala huu wa sarufi mapokeo ni mkabala wa awali ulioshughulikia sarufi ya lugha. Waasisi wake walikuwa wanafalsafa wa Ugiriki. Habwe na Karanja (2004:129) anataja wanafalsafa hao kuwa ni Plato, Aristotle, Dionysus Thrax, na Priscian. Katika kipindi hiki sarufi ilishughulikiwa sambamba na falsafa, dini, fasihi, balagha na mantiki. Plato alikuwa wa kwanza kugawa sentensi katika sehemu kuu mbili mtenda (subject) na kitendwa (object). Hatimaye Aristotle akaendeleza kazi ya mwalimu wake kwa kugawa sentensi katika sehemu kuu tano ambazo pia ndizo aina za maneno; nomino, kitenzi, kivumishi, kiunganishi na kielezi.Miaka ya 100 K.K, mwanasarufi Myunani Dionysus Thrax aliandika kitabu cha sarufi ambacho ni cha awali kabisa kilichoitwa “Techne Grammatike (The Art of Grammar)”. Mwanasarufi huyu aliainisha sehemu saba za sentensi ambazo ni nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kiunganishi, kielezi na kiingizi.
 
Dhana ya Neno Habwe na Karanja (2007:71) wanafafanua kuwa, neno ni kipashio cha kiisimu kinachoundwa na mofimu moja au zaidi.Saluhaya (2010:135) anadai kuwa, neno ni mkusanyiko wa sauti zinazotamkwa au kuandikwa kwa pamoja na kuleta maana.Massamba na wenzake (1999:43) katika samikisa wakitilia maanani maelezo ya Lyons (1968:194-208), neno linaweza kufafanuliwa katika misingi ya kiumbo-sauti (yaani, kwa kuchunguza sauti zinazounda umbo zima), kiothografia (yaani kwa kuchunguza herufi zinazotumika katika kuliandika umbo hilo), na kisarufi(yaani kwa kuchunguza kile kinachowakilishwa na umbo husika katika lugha).Hivyo basi, tunaweza kufasili neno kama silabi au mkusanyiko wa silabi (sauti) unaoandikwa au kutamkwa ili kuleta maana. Maana hiyo yaweza kuwa kamili, yaani inayotoa taarifa kamili au isiwe kamili, yaani ambayo haitoi taarifa kamili kwa msomaji au msikilizaji.
 
Dhana ya Sentensi Matinde (2012:157) anafafanua sentensi kuwa ni neno au fungu la maneno lenye uarifishaji mkamilifu. Sentensi huwa na muundo uliokamilika na hujitegemea kimaana.Kwa ujumla sentensi ni kipashio kikuu katika tungo chenye uwezo wa kutoa taarifa iliyo kamili au isiyo kamili na huwa na muundo wa kiima na kiarifu.Ufafanuzi wa aina za maneno kwa mujibu wa wanasarufi wa kimapokeoWataalamu wengi wa sarufi ya Kiswahili sanifu wanaelekea kukubaliana kwamba katika lugha hii kuna aina za maneno zisizopungua saba. Aina hizi za maneno zimewahi kujadiliwa kwa kina katika vitabu kadhaa vya sarufi vinavyojishughulisha na sarufi miundo na sarufi maumbo. Baadhi ya wataalamu wa sarufi mapokeo waliojadili aina hizo ni Kapinga (1983), Nkwera, Tumi, Mohamed, Massamba na wenzake (1999) na Kihore na wenzake (1999). Aina hizo ni pamoja na:
 
Nomino
Nomino ni jina linalotaja kitu, kiumbe, hali, dhana au tendo lolote liwalo. Tukiyachunguza kwa makini maelezo haya tunaona kwamba yanaashiria kuwa katika uamilifu wake nomino hufanya kazi ya kukipambanua au kukibainisha kitajwa kwa madhumuni ya kukitofautisha na vitajwa vingine. Kwahiyo nomino si mtajwa tu bali pia ni mtajwa bainishi.Katika sarufi za kimapokeo, nomino zilijulikana kama majina lakini katika sarufi za kisiku hizi neno jina au majina limeonekana kuwa la kawaida mno na kwamba haliwezi kuwa na mashiko yenye kukidhi mahitajio ya kiistilahi. Kwahiyo neno nomino limependekezwa litumike badala yake (Massamba na wenzake, 1999:39 katika Samikisa. Wanasarufi mapokeo wameweka migawanyo ya nomino kama ifuatavyo:a) Nomino jumuishi – hizi ni nomino zinazohusu majina ambayo hayakibainishi wazi kitu kinachotajwa. Kwa mfano mbuzi, gari, chuo, mtu, kalamu na nyumba.b) Nomino mahususi – ni yale majina ambayo yanataja vitu, dhana, na viumbe fulani maalumu na kwa kutoa ubainishi ambao ni wa wazi zaidi. Baadhi ya nomino mahususi ni kama vile Masalu, Ijumaa, Februari, Mwanza, Mariam, Herman, Viktoria, Tanzania na Rufiji.c) Nomino kikundi – hizi ni nimino ambazo huhusu majina yanayotaja vikundi kadhaa vya viumbe. Katika nomino hizi, jina moja huwa linataja jumuiya yenye sifa za namna moja. Kwa mfano baraza, jeshi, familia, shule, bunge, genge, mahakama, kombania na kwaya.d) Nomino dhahania – ni nomino zinazohusu majina ya vitu, dhana, na viumbe ambavyo kiukweli tunaweza kuviona katika akili tu lakini hatuwezi kuvibainisha kwa macho. Kwa mfano Uchawi, uzee, malaika, mizimu, Mungu ,usingizi na uchovu.e) Nomino mguso – ni nomino zinazohusu majina ya vitu ambavyo tunaweza kuviona kwa macho na kuvitambua katika uyakinifu wake, na utambumbuzi huu huweza kutokana na kuvigusa, kuvishika au kuvionja kama vile asali, chumvi, kiti, tofali, na tonge.f) Nomino za hesabu – hili ni kundi la nomino ambalo hutumia kigezo cha uwezekano wa kuhesabika katika uainishaji wake. Hapa tunatofautisha kati ya nomino zinazowakilisha vitu vinavyohesabika na vile visivyohesabika. Nomino za vitu vinavyohesabika ni kama vile watoto, vitu, visu, mifuko na viatu. Nomino zisizohesabika hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haviwezi kugawika, kwa mfano makamasi, mafuta, maji, matope, sukari, mchanga, uji, na nywele.


Vitenzi
Ni aina ya neno linalotoa taarifa juu ya tendo linalofanyika au linalotendwa na kiumbe au kitu. Wanasarufi mapokeo wamevigawa vitenzi katika aina kuu tatu ambazo ni:a) Kitenzi kikuu – ni kitenzi ambacho kinaweza kujitokeza peke yake katika sentensi. Mfano anakula, anampiga, tunacheza, wamechoka na anaimba.b) Kitenzi kisaidizi – ni kitenzi ambacho kinaandamana na kitenzi kikuu katika sentensi. Kwa mfano alikuwaanalima, tunapenda kusoma, na amechoka kucheza. Hivyo, maneno yaliyo katika hati mlazo ni vitenzi visaidizi.c) Kitenzi kishirikishi – ni kile cha umbo ni na si ambacho kinachukuliwa kuwa kinashirikisha vipashio vingine katika sentensi. Kwa mfano Kahigi ni mwalimu bora, huyu msichana si mwerevu.


Vivumishi
Ni kipashio ambacho hutoa maelezo zaisi juu ya nomino au kiwakilishi chake. Maelezo kama hayo kwa kawaida huwa namna au jinsi nomino ilivyo, yaani inavyoonekana, inavyofikiriwa, tabia, au idadi yake. Mfano wa vivumishi ni kama vile chafu, dogo, refu, vivu, zuri, embamba, na fupi. Vivumishi vimeweza kugawanywa katika aina kuu zifuatazo:a) Vivumishi vya sifa – ni vivumishi vinavyotaja tabia au namna vitu vilivyo au vinavyoonekana. Kwa mfano ema, nyenyekevu, pole na katili.b) Vivumishi vya idadi – ni vivumishi vinavyoonesha jumla au hesabu ya vitu. Aina hii ya vivumishi tunaweza kuigawa katika makundi mawili ambayo ni kundi linaloonesha idadi kwa jumla na kundi linaloonesha idadi kwa hesabu. Kwa mfano ingi, chache, haba na kidogo vilievile tano, tisini, elfu , milioni na tatu.c) Vivumishi viulizi – ni vivumishi vinavyouliza maswali kuhusiana na nomino inayoandamana navyo. Mfano watu wangapi, miti mingapi, mayai mangapi, watoto wangapi, na viti vingapi.d) Vivumishi vya pekee – ni maumbo enye na enyewe ambayo katika Kiswahili ndiyo tu huchanganya aina na viambishi vya upatanisho wa kisarufi vinavyojitokeza navyo kimatumizi. Mfano m-tu m-refu, m-ti mrefu, miti mirefu.


Viwakilishi
Ni aina mojawapo ya maneno katika sarufi ya lugha ambayo uamilifu wake ni kuwakilisha nomino katika miktadha mbalimbali. Kwa mfano viwakilishi nafsi, viwakilishi viashirii, viwakilishi viulizi, viwakilishi vimikilishi, viwakilishi vya idadi na viwakilishi jumla.


Viunganishi
Ni neno linalotumika kuviweka pamoja vipashio mbalimbali ili kuvifanya viwe kipashio kikuu kimoja. Kwa mfano na, au, wala, na lakini katika sentensi zifuatazo:Baba na Mama wanalima.Unapenda chai au uji.Hana huruma wala upendo.Wanasarufi mapokeo wamevigawa viunganishi katika makundi makuu mawili kwa kuzingatia msingi wa kimaana kama vile viunganishi vya hadhi sawa na viunganishi vihusishi.


Vielezi
Ni neno linalotumika kuelezea zaidi juu ya kitenzi. Mfano sana, mno, kabisa, polepole, harakaharaka, zaidi, sawasawa na barabara. Wanasarufi mapokeo wameviainisha vielezi katika aina kuu mbili yaani vielezi halisi na vielezi viingizi. Mfano wa vilelezi halisi ni kama vile mno, sana, bure, hasa, kabisa, ovyo, haraka na sasa. Kwa upande wa vielezi viingizi ni kama vile pu, mwa, na bwe .


Viingizi
Ni aina ya maneno inayodokeza hisia za msemaji kama vile ya hali yake ya kufurahi, kushangaa, kushtuka, na uchungu. Haya ni maneno kama vile Lo! Alaa! Lahaula! na Aa! Maneno kama haya kwa kawaida huwa yanatumika kabla ya sentensi na aghalabu huwa hayana mfungamano wa kisarufi na sentensi inayofuata. Aina hii ya neno pia huitwa vihisishi. Jina vihisishi limekitwa zaidi katika misingi ya kimaana yaani linahusu zaidi hisia mbalimbali zinazobebwa na maneno hayo. Viingizi navyo vimegawanywa katika makundi mawili nayo ni viingizi halisi na viingizi vya taswira.


Ufafanuzi wa aina za sentensi kwa mujibu wa wanasarufi mapokeo
Kwa upande wa sentensi, wanasarufi mapokeo wanaainisha aina tatu za sentensi kwa kuzingatia uamilifu wake. Aina hizo ni kama zifuatazo:i) Sentensi taarifa – hizi ni sentensi zenye kutoa taarifa fulani.Kwa mfano: Kiranja amechelewa kufika shuleni.Kahigi kaandika kitabu cha sarufi ya Kiswahili.ii) Sentensi ulizi – aina hii ya sentensi huwa ina pengo katika sehemu yake ya taarifa. Sentensi hizi hutaka kupata taarifa fulani.Kwa mfano: Adam ameweza kucheza mpira?Kalamu yako ni ipi?iii) Sentensi Agizi – aina hii ya sentensi humuingiza msikilizaji kutenda kitendo fulani. Aghalabu sentensi ya aina hii haina sehemu ya kiima.Kwa mfano: Toka nyuma uende mbele.Mwite kiranja wako.Kwa ujumla, wanasarufi mapokeo kwa kiasi fulani wanatofautiana katika uainishaji wa aina za maneno kwani kuna wengine wametaja aina kumi za maneno badala ya saba. Kwa mfano Habwe na Karanja (2004:130-139) wao wanaainisha aina kumi za maneno ambazo ni nomino, vitenzi, viwakilishi, vivumishi, vielezi, vihusishi, viunganishi, vionyeshi, vihisishi na vibainishi. Hivyo ni vigumu kutambua idadi halisi ya aina za maneno kwa mujibu wa sarufi mapokeo.
MAREJELEO
Habwe, J. & Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi: Phoenix Publishers.Habwe, J. & Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili.Nairobi: Phoenix Publishers.Kapinga, M.C. (1983). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Saalam: TUKI.Massamba, D.P.B na Wenzake (1999). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA); Sekondari na Vyuo. Dar es Saalam: TUKI.Matinde, R.S. (2012). Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia; Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) LTD.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)