09-06-2021, 04:21 PM
Usanifishaji Wa Kiswahili
Usanifishaji wa lugha ni mchakato unaowezesha kupatikana kwa lugha moja yenye namna moja ya uzungumzaji na uandishi. Usanifishaji hutokea katika mazingira yenye vilugha (lahaja) vingi. Ulinganifu wa vilugha hivyo ili kupata lugha moja itakayotumiwa kirahisi katika mawasiliano. Historia ya mchakato wa usanifishaji wa Kiswahili iligubikwa na malumbano juu ya lahaja ipi iwe ya msingi kati ya Kiamu, Kimvita na Kiunguja ambapo ilikubalika kwa sauti moja kuteua Kiunguja kuwa ndio msingi wa ‘Kiswahili Sanifu’ katika kikao kilichofanyika mjini Mombasa mnamo mwaka 1928 na kufuatiwa na uundwaji wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mwezi Januari mwaka 1930. Kamati ilitumia muda mwingi kwenye kipindi cha miaka ya 1930 hadi 1947 katika kuweka ithibati katika mtindo wa tahajia, na sifa bainifu za kisarufi za Kiswahili Sanifu (angalia Whiteley 1969, Massamba 1996). KKAM ilifanya kazi yake kama chombo chenye sauti moja kwa Afrika ya Mashariki yote na ilitunga kamusi mbalimbali, ilipitisha vitabu vya shule, sheria na uandishi wa habari chini ya kamati ya KKAM (Gibbe 1983, Mbaabu 1991, 2007, Maganga 2008).
Umuhimu wa usanifishaji wa Kiswahili
- hutambulisha utamaduni wa mtanzania nje ya nchi yake
- husaidia kusawazisha matamshi ili lugha iwe na namna moja ya uzungumzaji na uandishi mf; kilolo-kioo, niumba-nyumba
- kuifanya lugha itumike kwa namna moja kwa watumiaji wake wote
- hukuza msamiati wa lugha kwa kuchukua maneno toka lahaja mbalimbali
- hurahisisha mawasiliano miongoni mwa watumiaji wa lugha inayohusika
- huondoa tofauti za kikabila zinazoleta migogoro ndani ya jamii
- hukuza sanaa ya jamii pana ya kitanzania.
Hatua za usanifishaji wa Kiswahili
- Uteuzi wa lahaja ya usanifishaji miongoni mwa lahaja zilizokuwepo mf. Katika Kiswahili lahaja ya Kiunguja ndio iliyoteuliwa.
- Kurahisisha matamshi ili yawe ya aina moja nchi nzima
- Kuundwa kwa chombo cha usanifishaji mf. Kamati ya lugha ya Afrika Mashariki (Interterritorial Language –swahili Committee,1930)
- Kutayarisha kamusi na vitabu vya sarufi ya lugha inayohusika
- Kuitangaza lahaja iliyosanifishwa ili itambulike kwa watu wengine
- Kuandaa wataalam wenyeji wa usanifishaji watakaoshughulika na usanifishaji baada ya wageni kuondoka
Wataalamu wa kizungu ndio walioshughulika na usanifishaji wa Kiswahili. Baada ya uhuru TUKI (TATAKI), BAKITA na vyombo vingine vya ukuzaji wa lugha ndivyo vinavyoshughulika na usanifishaji wa lugha.
Usanifishaji wa lugha ya Kiswahili ulifanywa na Waingereza wakati wakitawala makoloni ya Tanganyika, Kenya na Uganda. Walilenga kupata lugha ya kufundishia katika makoloni yote ya Afrika Mashariki kwa hiyo mwaka 1925 Gavana wa Tanganyika Sir Donald Cameroon aliitisha mkutano Dar es Salaam, mkutano huo ulihusisha wakuu wa elimu wa nchi za Afrika Mashariki ili kujadili jinsi ya kupata lugha moja ya kufundishia kutokana na kuwepo kwa lahaja nyingi. Katika mkutano huo wajumbe waliteua lugha ya Kiswahili itumike kufundishia katika hatua za awali.
Mwaka 1928 mkutano mwingine uliitishwa mjini Mombasa ambapo lahaja ya kiunguja iliteuliwa kuwa lahaja ya usanifishaji.
Matukio wakati wa usanifishaji wa Kiswahili
- Kuitishwa kwa mkutano na Gavana wa Tanganyika (1925) ulioshirikisha nchi zote za Afrika Mashariki mjini Dar es Salaam ili kujadili na kuchagua lugha moja ambayo ingetumika shuleni katika nchi zote nne.
- Kuchagua lahaja ya Kiunguja kuwa lahaja ya usanifishaji ili itumike katika shughuli rasmi katika Afrika Mashariki, mkutano ulifanyika (1928) mjini Mombasa na wajumbe kutoka nchi zote nne akiwemo Prof Carl Meinholf mwanaisimu mashuhuri alihudhuria.
- Kuundwa kwa kamati ya ukuzaji na usanifishaji wa lugha ya Kiswahili (1930) iliyoitwa The Inter-Territorial Language (Swahili) Committee.
- Kuundwa kwa shirika la uchapaji wa miswada lililoitwa The East African Literature Bureau (EALB, 1948)
- Kuiweka kamati ya lugha chini ya Chuo cha Afrika Mashariki cha uchunguzi wa jamii (East African Institute of Social Research) cha Makerere (1952).
- Kuanzishwa kwa vyombo vya habari kama redio na magazeti. Magazeti kama vile: Mambo Leo, Habari za Mwezi, Tazama, Barazani, Kiongozi, Afrika Kwetu, n.k. Redio ilianza rasmi matangazo mwaka 1950 kwa lugha ya Kiswahili ikijulikana kama Sauti ya Dar es Salaam na baadaye Sauti ya Tanganyika.
- Kuundwa kwa chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanganyika (UKUTA, 1959) ili kushughulika na sanaa ya ushairi na ngonjera.
Kipimo cha Lahaja ya usanifishaji/Sababu za kuteuliwa kwa Lahaja ya Kiunguja
- Lahaja ya usanifishaji ilipaswa kuwa na ulinganifu katika eneo kubwa kimsamiati na hati za maandishi.
- Iwe inaandikika
- Iwe na mawanda mapana kimatumizi
- Iwe ni kipimo cha kutambulisha matumizi sanifu na yasiyosanifu
- Iwe na historia ndefu kimatumizi
- Iweze kubadilika kulingana na mazingira na wakati
- Ipokee msamiati toka lahaja/lugha nyingine
Kuundwa kwa kamati maalumu ya lugha
Mkutano wa Mombasa ulipendekeza kiundwe chombo maalumu ambacho kingesimamia na kuratibu utumizi wa Kiswahili na kutilia mkazo usanifishaji wake. Mnamo tarehe 1 Januari 1930 kamati ya kukuza na kusanifisha Kiswahili iliundwa na kuongozwa na Fredrick Johnson kama Katibu wake wa kwanza. Kamati hiyo ilijulikana kama The Inter-Territorial Language (Swahili) Committee, ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya nchi zote za Afrika Mashariki, yaani Tanganyika, Zanzibar, Kenya na Uganda.
Majukumu ya kamati ya Lugha
- Kueneza mtindo mmoja wa lugha ya Kiswahili katika nchi zote za Afrika Mashariki
- Kuleta ulinganifu wa kisarufi kwa kuchapisha vitabu vya sarufi vitakavyokubalika
- Kuwatia moyo kwa makusudi waandishi ambao ni wenyeji wan chi hizi ili waweze kuandika vitabu vya lugha ya Kiswahili
- Kuleta ulinganifu wa matumizi ya maneno yaliyopo na maneno mapya yatakayoundwa kwa kusimamia uchapishaji wa kamusi za shule na nyinginezo
- Kutoa ushauri juu ya utunzi wa vitabu kwa watu wote wenye hamu au nia ya kuwa waandishi wa vitabu vinavyokusudiwa
- Kuhariri vitabu vya Kiswahili vinavyotarajiwa kutumika shuleni pamoja na vitabu vya hadithi za kuburudisha
- Kutafsiri katika Kiswahili vitabu vya lugha ya Kiingereza vilivyochaguliwa kutumika shuleni kama vitabu vya kiada au vya ziada au kutunga moja kwa moja vitabu hivyo
- Kujibu maswali mbalimbali yanayohusu lugha ya Kiswahili na fasihi yake
- Kila mwaka kutoa vitabu vya Kiswahili vya kiada na ziada
- Kutoa kamusi na kuandaa vitabu vya shule vya Kiswahili sanifu
Mafanikio ya kamati
Katika jitihada za utekelezaji wa majukumu yake, kamati ilipata mafanikio mbalimbali kama vile:
- Iliweza kuchapisha kamusi ya Kiswahili sanifu iliyojulikana kama Standard Swahili – English Dictionary pamoja na Standard English – Swahili Dictionary
- Iliweza kutoa jarida lenye makala mbalimbali kuhusu lugha ya Kiswahili lililoitwa Bulletin of Inter – Territorial Language (Swahili) Committee.
- Ilipitia miswada mbalimbali ya vitabu vya Kiswahili ili kutoa vibali vya uchapishaji wake
- Ilifanya uchunguzi wa lahaja mbalimbali za Kiswahili
- Kurahisisha mawasiliano miongoni mwa jamii za Afrika mashariki kwa kutumia lugha moja ya Kiswahili
Matatizo yaliyojitokeza wakati wa usanifishaji wa Kiswahili
Kazi ya usanifishaji wa Kiswahili wakati wa Waingereza haikupita kirahisi tu, ilikumbana na matatizo mbalimbali kama vile:
- Kutokubaliwa kwa lahaja ya usanifishaji: Kuchaguliwa kwa Kiunguja na kuachwa kwa Kimombasa kuliletata mgogoro mkubwa uliofanya Kiswahili sanifu kikataliwe na kuonekana kuwa ni njama za kudhoofisha na kudhalilisha Kimombasa kilichokuwa na historia ndefu kuliko Kiunguja.
- Kutoshirikishwa wenyeji: kutokana na mchakato mzima wa usanifishaji kufanywa na wageni wenyeji walijiona wamedharauliwa mno na hivyo wakapinga muelekeo wa kugeuza lugha ya Kiswahili toka tabia na asili yake wakapendekeza sarufi iimarishwe kwa kuangalia vilugha au lahaja nyingine.
- Tatizo la fedha za kuendeshea kamati: serikali ya kikoloni ilitoa fedha kidogo sana kwa ajili ya usanifishaji wa Kiswahili hali iliyofanya kamati ya lugha ishindwe kufanya kazi zake ipasavyo na matokeo yake yakawa ni kulegalega kwa maendeleo ya lugha hasa maeneo ambayo hayakushawishi kwa shughuli za uzalishaji mali.
- Tatizo la vitabu: kamati ya usanifishaji ilimudu kutoa vitabu vichache ambavyo havikutosheleza mahitaji ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili, hali hii ilifanya kazi ya usanifishaji iwe ngumu mno.
- Kutothaminiwa kwa machapisho ya usanifishaji: wazawa wengi hawakuthamini machapicho yaliyotolewa na kamati ya lugha kwa sababu yalikuwa na kasoro nyingi zilizotokana na matumizi ya sarufi ya Kiingereza kusanifishia Kiswahili. Hali hii ikafanya baadhi ya maneno kuandikwa tofauti na yanavyotamkwa hasa na wabantu. Mf:
Kibantu Matamshi Kiswahili sanifu
Inge nnge nge
Umbwa mmbu mbu
Inzi nnzi nzi
Umbu mmbu mbu
- Matumizi duni ya Kiswahili: Kiswahili hakikupewa hadhi na nafasi ya kutosha kama ilivyo kwa lugha ya Kiingereza, mathalan Kiswahili kilionekana kama lugha ya makabwela tu kutokana na kutumiwa na manamba, madarasa ya chini shuleni, pamoja jumbe,akida na liwali walioonekana kama vibaraka wa wazungu.
Kuteuliwa kwa kiunguja kulivyodumaza lahaja nyingine
- Lahaja teule hupata hadhi ya juu, hivyo matumizi ya lahaja nyingine yanaonekana kama ni ya watu wa hali ya chini.
- Lahaja sanifu huandikwa katika vitabu vya sarufi sanifu na kamusi, hivyo kutumika katika mifumo rasmi kama elimu.
- Lahaja rasmi huteka mawasiliano yote ndani ya jamii husika na kufanya lahaja nyingine kupoteza idadi kubwa ya wazungumzaji.
- Lahaja sanifu huweza kupitishwa kuwa lugha ya taifa kama ilivyo kwa Kiswahili na matokeo yake lahaja nyingine hukosa utambulisho mpana kitaifa na hata nje ya taifa.
- Lahaja sanifu huchukua maneno ya lahaja nyingine na kufanya lahaja nyingine zikose sifa ya usiri katika mawasiliano na kufanya wenye lahaja zao wasiache.
Mwl Maeda