MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
RIWAYA PENDWA KATIKA FASIHI YA KISWAHILI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
RIWAYA PENDWA KATIKA FASIHI YA KISWAHILI
#1
Riwaya Pendwa Katika Fasihi ya Kiswahili

J.S. Madumulla
Katika miaka ya themanini makini ya mhakiki wa fasihi yameelekezwa au kwa usahihi zaidi, yameanza kuelekezwa kwenye aina ya riwaya ambayo hapo nyuma haikupata kushughulikiwa kwa upana kwa sababu ilikuwa haijajitokeza kwa nguvu. Ijapokuwa dalili za aina hii ya riwaya zimekuwako katika fasihi ya Kiswahili tangu miaka ya hamsini, lakini katika miaka ya themanini riwaya hii imejitokeza zaidi. Hata hivyo, kwa kuwa riwaya hii ni ‘ngeni’ katika Fasihi ya Kiswahili, imekuwa na matatizo kadhaa ya msingi ambayo pindi yakitaaliwa vizuri yanaweza kusaidia kuiainisha na kuibainisha vizuri zaidi. Matatizo hayo ni ya kihistoria, kiistilahi, kifafanuzi, kimawanda, n.k.
Kiistilahi
Mpaka sasa hapajawa na istilahi muafaka ya Kiswahili ya kuliwakilisha neno la Kiingereza la ‘popular literature’ au ‘popular novel.’ Pamekuwa na majina kadhaa kwa ajili ya riwaya hii, kama vile riwaya ya mitaani, riwaya maarufu, riwaya ya taharuki, riwaya ya vijana, n.k. Ijapokuwajina la ‘riwaya pendwa’ ndilo linaelekea kujitokeza zaidi, na ndilo litakalotumiwa katika sura hii, na hata kupendekezwa lipokelewe kuwa istilahi ya aina hii ya riwaya, lakini hapanajina mpaka sasa ambalo limekuwa na mashiko zaidi. Kwa kuiita riwaya hii ‘riwaya ya mitaani’ kutokana na kukosa maduka maalum ya kuiuzia, ni sawa na kuidunisha kama kitu kisichofaa, kitu cha mitaani tu. Hivyojina hilo lisingeisadifu aina hii ya riwaya.
Ingewezekana kabisa kuiita riwaya hii ‘riwaya ya taharuki’ kwani, kama tutakavyoona mbele, sifa moja kuu na ya msingi ya riwaya hii ni hiyo ya taharuki. Lakini tungesita kupendekeza iitwe hivyo kwa sababu si aina hii tu ya riwaya inayotumia kipengele cha taharuki kama mbinu muhimu ya kifasihi na kiujumi. Hivyo jina hilo pia lisingefaa sana. Kisha kuna jina la ‘riwaya ya vijana.’ Ni kweli ikitazamwa kwa haraka inaonekana kuwa riwaya hii ni uwanja wa vijana, hususan katika mashule, miji na vyuo. Lakini uchunguzi wa makini ungeonyesha kuwa, iwe kwa waandishi au kwa wasomaji, riwaya hii imeziteka pia hisia za wasio vijana, licha ya udogo wa idadi yao kwa sasa hivi. Kwa hiyo linabaki jina la ‘riwaya-pendwa.’ Hili linatokana na ukweli kwamba aina hii ya riwaya inapendwa na idadi kubwa ya watu, bila kujali umri wao wala matabaka yao. Huko Ulaya, tayari mwishoni mwa karne ya 18 aina hii ya uandishi ilikwishaingia katika hatua mpya kwa kupata wasomaji wengi waliotoka katika matabaka mbalimbali (H. Foerster na W. Foerster, 1986). Aina hii ya riwaya katika Tanzania inazidi kuziteka hisia za wasomaji wengine, bila kujali umri wala tabaka, na hivyo kulifanya jina la riwaya-pendwa kuwa muafaka kama istilahi yake.
Tatizo hili la istilahi kwa aina hii ya riwaya haliko katika fasihi ya Kiswahili tu, bali hata kwa mataifa mengine. Kwa Wajerumani kuna maneno kama vile “Trivialroman,’ ‘Unterhaltungsroman,’ ‘Kitschroman,’ ‘Abenteuerroman,’ ‘Schundroman,’ n.k. (Woerterbush der literaturwissenshaft, 1986) ambayo yanaelezea vijikondo vya riwaya hii vinavyoingiliana mno kiasi kwamba ni vigumu ama kuona mipaka yao ama kuona ni istilahi ipi ingekuwa bora kuliko zingine, ijapokuwa ‘Kitschroman’ na ‘Schundroman’ tungeziweka katika ngazi ya chini kabisa.
Historia yake
Huko Ulaya aina hii ya riwaya inasemekana kuwa na mizizi yake katika riwaya ya kilimbwende ya kikabaila (romance of chivalry) na riwaya ya unyang’anyi, na vilevile riwaya ya baadaye, yaani karne ya 18, ya kisaikolojia (k.v. Pamela iliyoandikwa na S. Richardson, 1740). Kama ilivyogusiwa hapo nyuma, mwishoni mwa karne ya 18 aina hii ya riwaya ilijitanua zaidi kwa kuwapata wasomaji wengi zaidi na hata wasanii wake kuongezeka.
Katika Tanzania aina hii ya riwaya ililetwa kwa mara ya kwanza katika Fasihi ya Kiswahili na Mohammed Said Abdulla alipoiandika riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale(1957/8). Msanh huyu, yaani Abdulla, inaelekea aliathiriwa na Doyle katika uandishi wa riwaya, na hususan katika mjengo wake. Baadaye katika miaka ya sitini Katalambulla alijitokeza kuendelea na riwaya ya aina hii. Katika miaka ya themanini uandishi wa aina hii ya riwaya uliongezeka maradufu. Madumulla (1988) alidai kuwa ongezeko la riwaya hii katika miaka ya themanini limelazimishwa na kukua kwa mahusiano ya kiuchumi na kijamii ya kibepari ambayo yameilazimishajamii kuyakabili maisha kwa mbinu zinazosadifiana nayo. Mabala (1989) alisema kuwa kuzuka kwa wingi kwa riwaya hii kulionyesha kuzuka kwa namna ya fasihi iliyoendana na mafcakwa ya wakati huo. Tutakipitia tena kipengele hiki huko mbele.
Katika Tanzania na hasa katika miaka ya themanini, riwaya hii ilikuja na sifa moja ya aina yake: haikupitia tena milango ya kawaida ya riwaya iliyozikuta, hasa milango ya kiuchapishaji na kisoko. Milango hiyo ilikuwa imefungwa dhidi yake kwa muda mrefu mno, hivyo waandishi wake wakaanzisha taasisi zao za uchapishaji, baadhi yao zikiwa na uhai wa muda mfupi tu, na walianzisha masoko ya mtaani, waandishi wenyewe wakiwa ni ‘duka la vitabu lijongealo’ na pia wahazini na wahasibu wake wakuu. Sababu ni kwamba vyombo vya udhibiti wa fasihi vilichelea kwamba aina hii ya fasihi iliichupa mipaka ya ujumi wajadi wa mazingira yake, na badala yake iliukaribisha pasi na simile ujumi wa kigeni. Suala la mapenzi, mathalani, katika jadi za Kitanzania, kwa kiasi fulani, na kwa muda mrefu lilikuwa ni suala la faragha. Mambo yanayohusu sehernu za siri, matusi madogo na makubwa, miiko, n.k. ni baadhi ya masuala nyeti ambayo ujumi wa Kitanzania una mkabala wake maalum nayo. Katika riwaya-pendwa mambo hayo yalijitokeza kama ndivyo vikolezo na vivutio vyake.
Kifafanuzi
Arnold (1980) akiifafanua fasihipendwa (popular literature) aliandika:
Quote:
is in the final analysis applied to what people need and often want, and not to what they read because nothing else is available, or what they read because forces opposed to their true prosperity claim they want it.
(hatimaye inahusu kile ambacho watu wanakihitaji na aghalabu wanakitaka, na siyo kile wakisomacho kwa sababu ya kutokuwepo kitu kingine, au kile wakisomacho kwa sababu nguvu ambazo zinapingana na kile ambacho wanakitaka zinadai kuwa wanaldtaka…)
Arnold alikuwa akiizungumzia hali ya fasihi-andishi yenye kulenga umma katika Tanzania ya miaka ya 1970. Hali hiyo aliiona katika vijitabu vya Mazungumzo ya Mchana na vingine vihusianavyo na Mpango wa Elimu ya Ujamaa na Kujitegemea vilivyoandikwa na Msuya katika miaka ya sabini. Ni katika kuangalia uwezekano wa kuenea kwa urahisi kwa vijitabu hivyo miongoni mwa umma, na hasa wale waliojishirikisha kusoma kwa njia ya Elimu ya Watu Wazima na kuuhusisha mpango mzima na itikadi na nadharia za Kijamaa (bila kujali suala la kupokeleka), ndipo tunaweza kuuona uzito wa ufafanuzi na hoja ya Arnold. Vinginevyo kuna maswali ya kujiuliza kuhusu usadifu wa ufafanuzi huo: Je, fasihi ya Msuya ilikuwa na ukubalifu kiasi kikubwa hata kuitwa ‘popular’ (pendwa)? Fasihi ya Msuya inawapa vijana nafasi gani? Aidha inazima kiu ya kifasihi kwa vijana waliomaliza shule za msingi na sekondari kwa kiasi gani? n.k. Zaidi ya hayo fasihi-pendwa iliyopendekezwa na Arnold inazidi kupoteza uzito wake tukitilia maanani kuwa mipango ya Elimu ya Watu Wazima ilizidi kufifia katika miaka ya themanini. Tena fasihi ya Msuya ni vigumu kusemekana kuwa ilisomwa kwa ‘kupendwa,’ ila ni rahisikusemekana kuwa ilisomwa kwa sababu ndiyo iliyokuwepo kama vitabu vya kiada na ziada katika mpango wa Elimu ya Watu Wazima. Kwa jinsi hiyo, fasihi hiyo ina matatizo ya kuitwa ‘fasihi-pendwa’ ya wakati huo au hata baadaye.
Hata hivyo, kama tulivyogusia, ‘upendwa’ aliouzungumzia Arnold wakati huo ulikuwa ni wa kisiasa na kiitikadi ambao unahusiana na ufafanuzi wa Brecht wa ‘kitu-pendwa’ ambacho hakina budi kiwe:
Quote:
Intelligible to the broad masses, adopting and enriching their forms of expression; assuming their standpoint, confirming and correcting it, representing the most progressive section of the people so that it can assume leadership.
(ni chombo kinachoeleweka kwa umma; kikizipokea na kuzitajirisha namna zao za kujieleza; kikiuchukua, kuuthibitisha na kuusahihisha msimamo wao; kikiiwakilisha sehemu ya kimaendeleo (zaidi) ya watu, ili hatimaye iweze kuuchukua uongozi).
Arnold alifikiria hivi kutokana najinsi fasihi hiyo ilivyoanzishwa na kusambazwa, ijapokuwa ilikuwa bado kuzitimiza sifa za ufafanuzi huu. Muda wake wa kuitwa ‘fasihi-pendwa’ ulikuwa bado sana.
Mabala (1989) baada ya kuitalii aina hii ya riwaya pamoja na tahakiki zake chache ambazo zilikuwa zimejitokeza hadi hapo, aliona kwamba aina hii ya riwaya ilibainishwa na wahakiki kwa namna isiyokubalika vizuri kama ifuatavyo:
Quote:
Popular literature is that which has been produced by the non-literate who do not belong to the academic establishment and therefore are unsophisticated. By the same token, serious novels are written by members of academic establishment who are colleagues of the critics thus making it easy for their seriousness to be recognized. Thus ‘popular’ carries a pejorative meaning which explains the resentment of the writers branded as popular…
(Fasihi-pendwa ni ile ambayo imeandikwa na wasio wasomi ambao hawamo katika taasisi za kitaalam na kwa hiyo si weledi. Hali kadhalika, riwaya-dhati zimeandikwa na watu wasomi ambao ni wenzao na wahakiki. Uhusiano huu unafanya udhati wa kazi zao ujulikane. Hivyo neno ‘pendwa’ lina maana hasi ambayo inachukiwa na waandishi wa aina hiyo ya fasihi…)
Kwa mtazamo huo, Mabala anadhani kuwa kuiona aina hii ya fasihi kwa namna hiyo kuna kasoro, kwani vigezo vyake haviko katika maudhui na fani za fasihi hiyo bali katika ‘utu’ wa waandishi.
Aidha Mabala anaendelea kusema kuwa waandishi wa aina hii ya fasihi, hasahasa ni vijana ambao bado wangali wakijifunza sanaa hii huku wakiwa wameathiriwa na jamii ambamo wanaishi, na ambao wamejaribu kulitafutia jibu tatizo kubwa la uhaba wa vitabu vya kusoma kwa wakazi wa mijini. Wameonyesha mwamko unaogusa wa kushughulika na masuala muhimu ya kijamii na wanayatetea maandishi yao hata dhidi ya uhakiki wa kirasimu wa miaka ya themanini. Aidha Mabala anaona ni vigumu kuitenganisha riwaya-pendwa kutoka kwenye riwaya-dhati. Ndiyo maana anahitimisha kuwa riwaya-pendwa ni aina mpya ya fasihi ya mjini ambayo inasomwa kwa upana na vilevile inavibainisha vipengele vya kimaendeleo vya utamaduni wa umma.
Kwa kuwa ni vigumu kuitenganisha riwaya-pendwa na riwaya-dhati, Mabala hakujaribu kueleza tofauti zao kimaudhui au kifani. Hii inawezekana kuwa mhakiki huyu alielemea zaidi katika kuitetea nafasi ya mwandishi wa riwaya-pendwa ili ainuliwe kufikia kiwango cha mwandishi wa riwaya-dhati katika hadhi ya usanii. Suala hili ni la msingi kisanii:na limeanza kusemewa tayari (Madumulla, 1988). Pamoja na ugumu wa… kutenganisha riwaya-pendwa na riwaya-dhati, ingefaa hata hivyo tuone ni vipi ufafanuzi na sifa zake vinaweza kuangaliwa, na vipi makundi haya mawili tunaweza kuyatenganisha.
Katika lugha ya Kijerumani kuna aina ya fasihi/riwaya inayoitwa Unterhaltungsliteratur (inayoweza kufasiriwa kisisisi kama fasihi ya kuburudisha). Hii inakaribiana sana na fasihi-pendwa. Foerster na Foerster (1986) wanaifafanua kama:
Quote:
zusammenfassende Bezeichnung fuer massenwirksame, vor allem erzaehlende Literatur mit ausgepraegter Unterhaltungsfunktion und entsprechenden eigentuemlichen Strukturen und Themen….
(Ni ufafanuzi unaokusanya pamoja fasihi, hususan za kinathari, anibazo zinapendwa kwa mapana sana, zikiwa na dhima hayana ya kuburudisha, na ambazo muundo na dhamira zake ni vya pekee…)
Wanatahadharisha kuwa katika ufafanuzi huu, lazima kutofautisha kati ya kuburudisha kwajumla kunakoweza kujitokeza katika fasihi yoyote ya kisanaa na ile dhima maalum ya kuburudisha ambayo imo katika kazi na tanzu za fasihi ya kuburudisha yenyewe (au fasihi-pendwa) ambamo hali ile ya kufurahisha imepewa nafasi ya mbele katika mahusiano ya ujumi na muundo wa hadithi. Mambo muhimu yanayojitokeza katika fasihi ya namna hiyo ni pamoja na:
Quote:
– kiasi kikubwa cha taharuki na utendaji
– mtiririko unaofuatika wa wahusikana matukio
– Mhusika mkuu ni mhusika-mkwezwa
– dhamira zakezinapendwa na wengi
– mandhari yameundwa kwa namna ya pekee
– mtindo ni rahisi uliotumia lugha ya kila siku
– kuenzi jinsi ya kike kama chombo cha anasa, na uhalifu.
Zaidi ya hayo, katika aina hii ya fasihi kuna uwezekano wa kubeba dhima nyingine za kimawasiliano, kimaadili, kisiasa, licha ya dhima kuu ya kuburudisha. Aidha fasihi hii, kama ilivyo fasihi-dhati, ina viwango mbalimbali vya usanii, na wasomaji wake wanatoka katika matabaka mbalimbali.
Zilizoonyeshwa hapo juu ni sifa za fasihi-pendwa kwa jumla. Riwaya-pendwa ya Kiswahili ina sifa hizo pamoja na nyingine chache ambazo ni:
Quote:
– uigaji wa mawazo na, mara nyingine hata matendo kutoka kwenye fasihipendwa za nchi zilizoendelea
– upangaji wa haraka wa mtiririko wa matukio kiasi kwamba sehemu zingine zinakosa upatanifu na mantiki
Katika sifa hizo zote zilizotajwa na zisizotajwa za riwaya-pendwa sifa za taharuki na utendaji ndizo zinachukua nafasi muhimu zaidi. Waandishi wamejitahidi kutumia mbinu ya misukumo-pofu kadhaa ili kuvichelewesha vilele katika masimulizi yao. Katika ucheleweshaji huu ndimo ambamo ufundi wa mwandishi unajibainisha katika kuvisuka visa visivyomchosha msomaji, ufundi wa kuwaokoa wahusika wanaokandamizwa na sheria kwa knonewa na kuwaonyesha walikojificha wahalifu. Mifano iko kadhaa. Vitabu karibu vyote vya Mohammed Said Abdulla vinaonyesha jinsi Inspekta Seif anavyotuongozea kwenye misukumo-pofu. Anatupeleka kwa wahusika wasio na hatia ambao, kwa mantiki yake yeye inspekta, wanaonekana kuwa wahalifu. Lakini misukumo-pofu hii inakuja kuwekwa sawa na Bwana Musa ambaye anaonyesha dosari za Inspekta Seif. Katika kufanya hivyo anaturejesha kwenye msukumo mkuu. Pale tunapofika tu kwenye msukumo mkuu tunapambana na kilele ambacho kinatuongozea kwenye suluhisho, au ‘peripetie’. Vitabu vya Katalambulla na Musiba vinaelemea kwenye mkabala huu. Au kwa kifupi, masimulizi yote ya kipelelezi yametumia mbinu ya misukumo-pofu katika ujenzi wa taharuki ndani ya mtiririko wa matukio yao.
Ijapokuwa dhima muhimu ya riwaya-pendwa ni kuburudisha, lakini kazi hizo haziko katika kiwango kimoja tu cha usanii. Kutofautiana huku kwa viwango vya usanii ndiko kunazifanya kazi hizi ziweze kupangika katika aina kadhaa.
Aina za riwaya-pendwa
Mapema tumeona kuwa Mabala anaelekea kudai kuwa waandishi wa riwaya-pendwa wameelezwa na wahakiki wa fasihi kuwa si wasomi, na maandishi yao hayana weledi. Hali kadhalika, waandishi wa riwaya-dhati ni wasomi na wametetewa na wahakiki kwa sababu ni wasomi wenzao. Vingincvyo, aonavyo Mabala, hakuna tofauti kati ya riwaya pendwa na dhati.
Lakini ukweli ni kwamba wengi wa waandishi wa riwaya-pendwa ni wale waliosoma kufikia Sekondari; na katika waandishi wa riwaya-dhati baadhi yao wana elimu ya Chuo Kikuu. Wengi wa waandishi wa riwaya-pendwa hawana kazi maalum isipokuwa uandishi. Na huenda wamefanikiwa kuanzisha miradi fulani baada ya kupata mtaji kutoka kwenye maandishi yao. Suala hili ni la msingi. Hili ndilo linaloonyesha kwanmi riwaya-pendwa imefurika. Kwa sababu inawaruzuku na kuwakimu waandishi wake. Tena imekuwa muhimu zaidi katika miaka ya themanini ambayo matatizo ya kiuchumi yamezidi. Hili linaeleza vile vile sababu ya kuwepo kwa sifa za nyongeza zilizogusiwa awali katika riwaya-pendwa ya Kiswahili. Kwa upande mwingine, wengi wa waandishi wa riwaya-dhati ni watu wenye kazi zao tayari. Hivyo uandishi ni kazi ya ziada kwao. Hapa haina maana kwamba waandishi wa riwaya-dhati hawapendi fedha. Tunaangalia suala la jinsi maudhui na fani vinavyomudiwa. Inawezekana kwamba katika uandishi wa kazi zao wanajipatia muda wa kutosha wa kuyapanga mawazo yao, na elimu yao pia inawasaidia katika ufuaji na uchanganyaji wa sanaa, maudhui, lugha, uhalisia, falsafa, n.k. Waandishi wengi wa riwaya-pendwa wameanzisha taasisi za uchapishaji na namna yao ya masoko wakilazimishwa na hali halisi ya maisha. Hali hiyo ya maisha ndiyo inayoyalazimisha na kuyadhibiti hata maudhui ya kazi zao. Hata hivyo, mtazamo huu hauhalalishi au kuweka sheria kuwa kila kazi inayoandikwa na ‘msomi’ ni ya dhati, na nzuri, na zile zinazoandikwa na wengine ni ‘fasihi-pendwa’ na chapwa. Mtazamo huo hauna mantiki, ni mtazamo wa kimhemuko. Badala yake, pawepo na bidii za kuitalii na kuifahamu zaidi riwaya-pendwa. Kazi hii ni kichocheo cha utafiti huo.
Kwa ujumla, riwaya-pendwa ya Kiswahili inaweza kuangukia katika aina tatu. Ya kwanza ni aina ya Abdulla. Aina hii sifa yake kubwa ni ya upepelezi na uchanganuzi wa kadhia kwa kutumia mantiki au fomula maalum. Kunaweza kuwa na uhalifu au dhuluma katika mtiririko wa matukio. Polisi wanajitahidi kulitatua tatizo lakini wakati mwingine wanashindwa. Hivyo katika visa vingine msaada wa mpelelezi binafsi unatakiwa. Aina ya pili ni ya Musiba. Sifa kuu ni ya upelelezi na kupambana na majambazi na majasusi kwa kutumia nguvu. Hapa kunahitajika mhusika mkuu anayeweza kufikiri haraka haraka, kutumia silaha na viungo vya mwili kwa ustadi katika vipindi vya dhiki na raha. Mhusika mkuu ni bingwa wa kufikiri na kutenda na mara nyingine anafanya makosa madogo madogo yanayomwingiza katika majaribu ambayo hatimaye atayashinda. Hapa upelelezi na mapenzi vinakwenda pamoja. Inaelekea kama wapelelezi wakubwa ni wajuzi au ‘wachezeaji’ wakubwa wa mapenzi pia. Kipengele hiki kinachangia sana katika kuidhalilisha aina hii ijapokuwa inaweza kuwa imebeba dhamira nzito zinazoigusa sana jamii ya wakati huu. Aina hizi mbili zina uigaji wa hali ya juu wa riwaya-pendwa za nchi zilizoendelea, k.v. kivazi, vifaa, vijitabia fulani, namna ya lugha, n.k. Hii inathibitisha tu jinsi waandishi wetu walivyo wachunguzi wepesi kuhusu mambo yanayofanyika katika sehemu nyingine za dunia. Na jinsi gani wanayachambua na kuyapokea na kuyatumia mambo hayo kwa manufaa ya mazingiria yao ni jambo ambalo tayari limo katika majadiliano baina ya wanafasihi.
Aina nyingine ya riwaya-pendwa ni ile ya Mbunda Msokile. Riwaya hii imesukwa kwa namna ambayo imeelemea kwenye riwaya-dhati, hususan kwa maadili yake na, kwa kiasi fulani, uwiano kati ya wahusika na uhalisia. Hata hivyo kazi za aina hii zinaingizwa kwenye riwaya-pendwa kutokana na kuitilia mkazo mno dhima ya kuburudisha na kuzishughulisha zaidi hisia za huruma au chuki za msomaji badala ya mchangamano wenye kuwiana wa hisia, tafakari na mantiki. Katika aina hii kwa kawaida upelelezi haumo. Pindi uhalifu unapotokea polisi na njia nyingine za kisheria zinatumika.
Mawanda ya riwaya-pendwa
Mawanda makuu ya riwaya-pendwa ni uhalifu (wizi, uuaji, ujambazi, dhuluma, unyang’anyi, uporaji, n.k.), mapenzi, ujasusi na upelelezi. Kwa riwaya-pendwa za zamani kipengele cha jasira (adventure) kilikuwa ni muhimu pia. Migogoro mikubwa na midogo, misukumo-pofu na mikuu imejengwa kwa kujiduru katika mawanda haya. Masimulizi mengi ya Muhammed Said Abdulla yanahusu uhalifu (dhuluma na mauaji) na upelelezi. Yale ya Musiba yanahusu ujasusi, upelelezi na mapenzi. Ya Simbamwene ni uhalifu wa aina nyingi kidogo, mapenzi na upelelezi, n.k. Ijapokuwa tunajaribu kuyatenganisha hivi, lakini katika kusoma riwaya mbalimbali za aina hii inajibainisha kuwa kuna mwingiliano mkubwa baina ya aina hizi.
Fani: Namna ya jumla ya uandishi wa riwaya-pendwa:
Msomaji makini wa riwaya-pendwa atagundua kuwa waandishi wake wameweza kuchapisha sanjari ya vitabu kadhaa kwa kipindi kifupi tu, na bado wanakuwa na uwezo wa kuendelea kutoa sanjari nyingine. Hii inatokana na namna fulani ya kanuni ambayo inafuatwa katika uandishi wao. Kanuni hii tutaiita ‘topo’. Kuna topo la kimaudhui ambalo linayachunga mawanda ya dhamira wanazoziandikia waandishi. Mathalani, Abdulla akichungwa na topo la kimaudhui, ameendelea kuandika sanjari za vitabu kuhusu uhalifu na upelelezi. Kisha kuna topo la kifani ambalo linazichunga mbinu za kuyaandikia maudhui. Msuko wa malukio, matumizi ya misukumo-pofu, ujenzi wa peripetie, suluhu, ni vipengele ambavyo, kimsingi, havibadiliki sana. Hii inathibitishwa na matumizi ya wahusika wakuu walewale katika sanjari nzima ya vitabu. Vilevile mwandishi anajitahidi kujenga uhusiano kati ya kitabu chake kipya na kile cha nyuma kwa kumrejesha msomaji kwenye matukio fulani katika vitabu vilivyopita (Abdulla, Simbamwene, Musiba, n.k.). Waandishi wamefanya hivyo ili kuonyesha mwendelezo wa matukio kwamba wanafanya hivyo si kwa bahati nasibu tu, bali kwa makusudi mazima.
Katika kuandika riwaya kisanjari kwa mbinu za wahusika wakuu walewale na urejeshi wa matukio fulani, waandishi wameifanya kila riwaya katika sanjari ionekane kama tuko (episode) moja linalojitegemea katika mfululizo wa matuko. Hii imemwezesha mwandishi mmoja kutoa matuko (episodes) mengi katika kipindi kifupi. Hata hivyo aghalabu matuko hayo yamekuwa ni mafupi mno, tena yaliyosanwa kwa kuharakishwa kiasi kwamba upatanifu wa matukio umekuwa na uchapwa fulani, hususan katika ujenzi wa msuko wa matukio na wahusika.
Athari za riwaya-pendwa kwa jamii
Riwaya-pendwa, kwa vyovyote vile, ina nafasi yake katika jamii. Ikiwa ina nafasi yake ina wajibu pia, ijapokuwa kupokeleka kwa wajibu huo ni suala la kujadiliana. Mabala anaandika.
Quote:
..Just as people’s culture is a mixture of progressive elements and ruling class mystifications, ignorance and obscurantism, the popular novels reflect the mixture as a whole both in the characters and settings and in the philosophy of the authors writing them. Almost without exception, the novels expound lumpen bourgeois and proletarian values which have’ so influenced urban dwellers throughout Tanzania.
(Jinsi utamaduni ulivyo mchanganyiko wa mawazo ya kimaendeleo na ya tabakatawala ambayo yanakanganya na kupotosha, ndivyo riwaya-pendwa zinavyoaldsi mchanganyiko (huo) mzima katika wahusika na mandhari na katika falsafa za waandishi wake. Karibu riwaya- (pendwa) zote zinaelezea amali za kibepari na kijamaa ambazo zimewaathiri wakazi wa mijini wa Tanzania nzima).
Hivi ndivyo riwaya-pendwa inavyoonekana kwa mhakiki mmojawapo. Je, wasomaji wengi wanaiona hivyo? Hata hivyo, linalosisitizwa ni lile lililogusiwa tayari hapo nyuma, kwamba dhima ya msingi ya riwaya-pendwa imekuwa ni ile ya kuburudisha. Kuna baadhi ya dhima ambazo zinaweza kujitokeza bila makusudio wala matazamio ya mwandishi. Huenda hoja ambayo inachukuana kwa namna fulani na dondoo la hapo juu ni ile ya Madumulla (1988) kwamba:
Quote:
– riwaya-pendwa imejitokeza katika miaka ya themanini kutokana na kustawi kwa mahusiano ya kibepari. Ni fasihi ambayo haifumbati tu uozo wa kibepari, bali pia ni zao halisi la uozo huo.
– riwaya-pendwa imejitokeza kwa wingi si kwa lengo la awali la kuziba pengo la upungufu wa maandishi ya kifasihi, bali kwa lengo la awali la kujikwamua kiuchumi.
– riwaya-pendwa inadhihirisha kiasi gani fasihi-pendwa ya kigeni ilivyoathiri mawazo ya kisanii ya waandishi wetu.
– riwaya-pendwa ni matokeo ya mwigo ambayo yameathiri uasili wa waandishi wetu katika ubunaji kimaudhui na kifani.
Baadhi ya wahakiki wamedhani kuwa fasihi-pendwa ni mwendelezo wa maandishi na filamu za magharibi za uhalifu, mapenzi, ugaidi, ujasusi na upepelezi. Wasomaji wengi wameifanya riwaya-pendwa kama kibadala au kijalizo cha filamu. Katika Hofu, kwa mfano, Musiba tayari amempeleka mhusika wake mkuu, Willy Gamba, Japani ambako amesomea mbinu za kupigana za kininja. Katika mapambano dhidi ya majasusi, Willy Gamba anakutana na maninja wenziwe ambao walikuwa pamoja kwenye mafunzo huko Japani. Wanapopigana, wanafuata sheria za kininja. Katika Hofu mada kuu inahusu ukombozi kusini mwa Afrika, na riwaya za Musiba zingesaidia sana kuwaamsha watu na kuwajuvya kuhusu suala hilo. Lakini lililowekwa mbele ni uhodari wa wahusika wakuu katika kutenda: Katika kuwindana, kupikuana kwa maarifa, kupigana kwa silaha na mikono mitupu na kufanya mapenzi. Mada ya ukombozi inafuatia nyuma ikinyemelea kwa mbali. Watu wanaosoma mikasa wanafikiria zaidi vipi Willy Gamba atawamudu maadui zake kuliko vipi na lini ukombozi utakamilishwa. Kwa sababu ukombozi ‘hauonekani’, kwani umefichwa na utendaji, kwa hiyo mada hiyo nzito inakuwa ni ‘kiziba macho’ tu cha vyombo vya udhibiti na wala hakina athari au uzito wowote, ila kidogo mno ndani ya kichwa cha msomaji. Aidha kiujumi na utendaji unaojitokeza humo unaziteka nafsi za wasomaji wengi; na wanalitazamia kwa hamu andiko lijalo la mwandishi kama Musiba.
Hitimisho
Katika mahusiano ya miaka ya themanini ya kijamii, ingekuwa vigumu kwa Tanzania kutokuwa na fasihi-pendwa, kwa sababu ya kuwepo kwa mazingira maridhawa kwa ajili ya fasihi ya namna hiyo. Je, iendelee hivyohivyo? Mpaka lini? Maswali ni magumu. Hata hivyo, kiwango ilichonacho riwaya-pendwa ya Kiswahili kinalilia kuboreshwa. Ingawa ni mwigo wa akina Doyle, Christie, Flemming, Robbins, Chase, n.k. lakini ukomavu wa waigwa haujafikiwa, hususan katika msuko wa matukio, ujenzi wa wahusika na mandhari, n.k.
Licha ya dhima kuu ya kuburudisha, riwaya-pendwa inaakisi, bila kukusudia, hali halisi ya Tanzania ya wakati wa riwaya hiyo hususan katika mahusiano ya kijamii na kiuchumi. Riwaya-pendwa ingeweza kujipatia dhima kubwa zaidi kwa kuyaweka makusudi yake makuu si, katika kuburudisha bali katika kuchochea fikra za kimaendeleo, za usawa wajinsi, za ustawi wajamii, n.k. kwa wasomaji wake. Dhima ya kuburudisha iende sambamba na masuala hayo.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)