MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
Sifa za kifani za utendi andishi wa Kiswahili katika Utenzi wa Ras 'lGhuli

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
Sifa za kifani za utendi andishi wa Kiswahili katika Utenzi wa Ras 'lGhuli
#1
Sifa pambanuzi za kifani za utendi andishi wa Kiswahili zinavyojitokeza katika Utenzi wa Ras ‘lGhuli


Ikisiri
Utendi wa Ras I’Ghuli kama tunavyoelezwa na Leo Van Kessel (1973,dibaji) kuwa unatokana na kisa kimoja cha Kiarabu kiitwacho Futuhu ‘lYamani maana yake ni kushindwa au kutiishwa kwa Yemeni. Kisa hicho cha Kiarabu husimulia jinsi nchi ya Yemeni ilivyoshindwa na kutekwa na majeshi ya Waislamu. Mwanzoni kisa hiki kiliandikwa katika lugha ya kigeni (Kiarabu). Hivyo si Waswahili wengi walioweza kukielewa ndipo Mwalimu Mgeni bin Faqihi aliamua kukibadili kisa hicho kutoka katika usimulizi wa kawaida kuwa utenzi na  kukiandika kwa lugha ya Kiswahili lakini kwa kutumia hati za Kiarabu ili kiweze kusomwa na watu wengi zaidi. Kwa kuwa kisa hicho kwa asili kilikuwa kinawahusu Waarabu na Uislamu na kiliandikwa kwa lugha ya Kiarabu swali la kujiuliza je kutafsiriwa kwa kisa hicho kwa lugha ya Kiswahili lakini kikiandikwa kwa kutumia hati za Kiarabu na baadaye kuandikwa kwa haati za Kirumi, je tunaweza kuujumuisha utendi huo kuwa ni utendi wa Kiafrika au Kiswahili? Hivyo makala haya yanakusudia kuuhakiki utendi huo kama una sifa za kuitwa utendi wa Kiswahili au la. Hivyo basi kukamilisha lengo hilo kazi hii imegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ni utangulizi katika sehemu hii tutatoa fasili ya utendi, muhtasari wa kitabu na usuli wa mwandishi na sehemu ya pili, kwa kuwa kulishawahi kutolewa mawazo kuwa hakuna utendi wa Kiafrika tutaongozwa na vigezo kama vilivyopendekezwa na Mulokozi (1999) kuuhakiki utendi huo kama unakidhi vigezo vya kuitwa utendi wa Kiafrika kabla hatujazama kuutazama utendi huu kama una sifa za kuitwa utendi wa Kiswahili. Sehemu ya tatu tutajikita kuangalia kama Utendi wa Rasi ‘lGhuli unakidhi vigezo vya kuitwa utendi wa Kiswahili tukimakinikia vigezo vya kifani na kimuundo. Na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
1.0   Utangulizi
Dhanna ya utendi ni dhanna iliyowashughulisha wataalamu mbalimbali. Mathalani, Chaligha (20013:82) anatueleza kwamba, mtaalamu Bowra (1930) anatumia fomula kuelezea maana ya utendi kuwa ni U=M+V (Utendi =Muziki + Vita) akiwa na maana utendi ni tukio la kimuziki unaozungumzia vita na miungu kwa njia ya ushairi ulioandikwa. Kwa upande wake Mulokozi (2009), anasema, utendi ni utungo mrefu wa kishairi wenye kusimulia hadithi ya ushujaa na mashujaa, na utenzi ni utungo wowote mrefu wa kishairi, aghalabu wenye kutoa mawaidha ya kidini au ya kidunia au kusimulia habari fulani. Aidha, Belcher (1999: xiv) anasema kuwa, tendi ni masimulizi ya papo kwa papo yanayohusu masuala ya kihistoria ambayo hutolewa hadharani mbele ya hadhira na yeli maalumu. Anaendelea kufafanua kuwa, tendi nyingi huambatana na muziki. Aidha Wamitila (2003:333) anasema kuwa, utendi ni shairi refu la kisimulizi linalozungumzia kwa mapana na mtindo wa hali ya juu matendo ya mashujaa au shujaa mmoja.
Ama kwa hakika tukiwaangalia wataalamu wote hawa kimsingi hawatofautiani sana isipokuwa wengine wamejikita zaidi kutoa fasili zinazoegemea katika utendi simulizi na wengine wamejikita katika utendi andishi na wapo wengine ambao fasili zao zimejumuisha aina zote za utendi yaani utendi simulizi na utendi andishi. Mathalani Bowra anauona utendi kama kazi iliyoandikwa akijikita zaidi katika utendi andishi wakati Belcher, Molokozi na Wamitila wote wanakubaliana kuwa utendi ni shairi/nyimbo ndefu za kisimulizi wakijikita katika kigezo cha utendi simulizi.
Kutokana na maelezo ya wataalamu hao kuhusu tendi, tunaweza kujumuisha mawazo hayo kwa pamoja kwa kusema, utendi ni masimulizi marefu yenye umbo la kishairi yanayoelezea visa kuhusu mashujaa na matendo yao ya kishujaa, historia na ustawi wa jamii. Tendi inaweza kuwa katika umbo la usimulizi ama uandishi mara nyingi utendi ukiwa katika usimulizi uwasilishaji wake huambatana na muziki.
1.1    Muhtasari wa Utendi wa Rasi ‘lGhuli
Utendi wa Rasi ‘lGhuli unatokana na kisa cha Kiarabu kiitwacho Futuhu ‘lYamani ikiwa na maana kushindwa au kutiishwa kwa Yemeni. Kisa hicho cha Kiarabu husimulia jinsi nchi ya Yemeni ilivyoshindwa na kutekwa na majeshi ya Waislamu yakiiongozwa na Mtume Muhamadi[1] mwenyewe, Seyyidna Ali bin Abi Talibu[2](kuanzia sasa Seyyidna Ali) na Seyyidna Umar bin Khatab kunako karne 6. Tafsiri ya utendi huu umepewa jina la Rasi ‘lGhuli linalotokana na jina la kebehi la mtawala wa makafiri wa Yemeni ambaye jina lake halisi aliitwa Mukhariki bin Shahabu. Jina hili la kebehi Ras ‘lGhuli lina maana ya Kichwa cha Nyoka.
Kwa ujumla utendi huu una beti zipatazo 4584. Kuanzia ubeti wa 1-43 ni nyongeza ya mshairi ambapo anaanza kwa kumsifu Mungu na anaeleza sababu ya kutafsiri kisa hicho kutoka lugha ya Kiarabu hadi Kiswahili. Kisa chenyewe kinanzia aubeti 44- 4,565 na kuanzia ubeti 4,566 hadi 4,584 ni nyongeza ya mshairi ambapo anamalizia kwa kuomba dua.
Visa vya utendi huu vimepangwa katika sehemu viii (nane). Utendi unaanza Muhamadi akielezwa jinsi mtawala wa Yemeni Mukhairiqi bin Shahabu (Rasi ‘lGhuli) anavyo wadhulumu watu wake. Muhamadi anatokewa na malaika Jiburili na kumtaka kumtuma mtu kwenda kupeleleza nchi ya Rasi ‘lGhuli.
Malaika Jiburili anamweleza Muhamadi habari za kukamatwa kwa Zuberi, Sayyidna Umari anatumwa kuipeleleza nchi ya Rasi ‘lGhuli. Mtume anaamua kupeleka jeshi kupambana na Rasi ‘lGhuli. Rasi ‘lGhuli anaazimia kuishambulia Madina, mapigano makubwa yanaanza majeshi ya pande zote mbili yanapigana siku kucha Muhamadi anamuomba Mungu dua, Mungu anaitikia sala yake anawatuma malaika kusaidia jeshi la Waislamu kupambana na makafiri na anatuma na tufani ya mvua makafiri wanashindwa na kukimbia wengine wanasilimu. Majeshi ya Waislamu yanateka miji kadhaa. Rasi l’Ghuli anaomba msaada kwa majeshi mengine. Majeshi ya Waislamu yanazidiwa nguvu mpaka anapowasili Sayyidna Umar majeshi ya makafiri yanashindwa na kukimbia.
Vita vinaanza upya Rasi ‘lGhuli anawapa silaha askari wake. Muhamadi naye anaandaa vikosi viwili vya jeshi moja linaongozwa na Sayyidna Ali na lingine linaongozwa na Sayyidna Umari. Majeshi ya Rasi ‘lGhuli yanashambuliwa. Majeshi ya Rasi ‘lGhuli yanalivamia jeshi la Waislamu katakati ya mapambano Rasi ‘lGhuli anakimbia na kukimbilia mjini anaingia gerezani bila kutarajia anamkuta Sayyidna Ali.  Wanapigana hatimaye Sayyidna Ali anafanikiwa kumuua kwa kumkata kichwa na kuamuru kichwa chake kitundikwe katika lango la mji ili kila anayepita akione. Makafiri wanakimbizwa mpaka milango ya mji wanapoona kichwa cha Rasi ‘lGhuli wanafadhaika wengine wanasilimu wasiosilimu wanauwawa Mtume Muhamadi anaweka utawala mpya na kurudi na watu wake Madina baada ya ushindi. Kwa ufupi kisa cha utenzi huu kiliandikwa katika muktadha wa kuanzishwa na kuenezwa kwa dini ya Kiislamu huko Saudia Arabia na Yemen.
Tunataarifiwa kuwa, utendi huo hughanwa au kusomwa wakati wa sherehe kama vile matanga, harusi, n.k. na mghani maarufu wa utendi huo tunaambiwa kuwa alikuwa ni Mwalimu Sefu bin Hamidi wa Bagamoyo Leo Van Kessel (keshatajwa, dibaji).
1.2 Usuli  kuhusu mwandishi wa Utenzi wa Ras ‘lGhuli
Kwa mujibu wa Mhariri wa utenzi huu, Bwana Leo Van Kessel anatueleza kuwa, Mgeni bin Faqihi alikuwa ni Mtumbatu kutoka Unguja aliyehamia Bagamoyo.[3] Inasemekana kuwa alizaliwa mwanzoni mwa karne ya 19. Huko Bagamoyo alikuwa akifundisha dini ya Kiislamu katika vyuo vya Kiislamu. Alitumia muda wa miaka mitano kukamilisha utendi huu kwani inasemekana alianza kuandika utendi huu mwanzoni mwa miaka ya 1850 na kuukamilisha mwaka 1855. Ni miongoni mwa  washairi na watunzi wazuri wa kazi za fasihi kutoka Zanzibar waliopata kuwepo. ama kuhusu tarehe ya kufariki kwake bado mpaka sasa haijuikani.
Aidha kwa kuwa, kazi hiyo inaitwa Utenzi wa Ras ‘lGhuli na kwa kuwa unatokana na kisa cha kiarabu na unazungumzia habari za Waarabu na dini ya Kiislamu. Je huu ni utendi? Kumbuka si kila utenzi unaweza kuwa utendi. Hivyo ili kutegua kitendawili hiki itatulazimu kwanza kuondoa utata huo kwa kuangalia sifa za utendi wa Kiafrika ili kuuona utenzi huu kama unakidhi sifa hizo na tunaweza kuuweka katika kundi la tendi, ndipo sasa tuingie katika msingi wa hoja yetu, ya kuthibitisha kama utenzi huu una sifa za utendi wa Kiswahili ama la.
2.0 Sifa za utendi wa Kiafrika
Ama kuhusu sifa za utendi, wataalamu mbalimbali wameainisha vigezo au sifa za utendi wa kiafrika. Miongoni mwa wataalamu hao ni, Finnegan (1970) Okpewho (1979), Johnson (1986),  Mbele (1986), Belcher (1999), Mulokozi (1999), kwa kuwataja wachache. Aidha Utendi wa Rasi ‘lGhuli ni utendi unaonekana kuzingatia vigezo vya utendi kama vilivyopendekezwa na Mulokozi (1999:11) baada ya kufanya  majumuisho ya mawazo ya watafiti mbalimbali na kupata vigezo vipya vya utendi wa kiafrika ambavyo ni: (a) Utendi kuwa na sifa ya usimulizi yaani huwa na umbo la kihadithi, (b) Ni nudhumu yaani hutolewa kishairi na huwasilishwa kwa kughanwa hususani pamoja na ala ya muziki, © Huhusu matukio au masuala muhimu ya kihistoria na/au kijamii, (d) Huelezea habari za ushujaa na mashujaa, (e) Matini yake kwa kawaida hutungwa papo kwa papo na (f) Utendi hutawaliwa na muktadha wa utunzi na uwasilishaji wake kwa jamii.
Ama kwa hakika, ingawa vigezo hivi vinavyotajwa na Mulokozi (keshatajwa) kujikita zaidi katika utendi simulizi, na tukiuchunguza Utendi wa Ras ‘iGhuli tutaona kuwa unakidhi vigezo hivyo. Hebu tuanze kuangalia vigezo hivyo jinsi vinavyojitokeza katika utendi huo. Tukianza na:
Kigezo cha masimulizi yaani utendi kuwa katika umbo la kihadithi. Utendi wa Ras ‘lGhuli ni miongoni mwa tendi ambazo zinakidhi kigezo hiki cha usimulizi. Leo van Kessel (keshatajwa, viii) anatubainishia hili anapotuambia kuwa, mshairi ni msimulizi bingwa. Anatuhadithia wingi wa mambo ya kusisimua yaliyojiri wakati wa vita. Ukiisoma utendi huu utagundua kuwa ni masimulizi yaliyo katika umbo la kihadithi  yanaeleza habari za kuinukia kwa dini ya Kiislamu na mapambano ya vita yaliyoongozwa na Seyyidna Ali bin Abi Talib, Seyyidna Umar bin Khatab na Mtume Muhamadi kunako karne ya sita na ushindi walioupata katika vita hivyo kuwashinda makafiri na Mtume Muhamadi kusimika utawala mpya na kurejea Madina ambako walipokelewa kwa furaha. Rejea ubeti wa 4560-4563. Ama kwa hakika tukichunguza beti hizi utaona kuwa utendi huu umekaa kisimulizi msimulizi anatusimulia hadithi ya kuinukia kwa dini ya Kiislamu na vita vya mapambano kati ya majeshi ya Waislam na makafiri na ushindi wa majeshi ya Muhamadi na namna walivyorejea Madina na kupokelewa.
Sifa nyingine ambayo inajitokeza katika utendi huu ni kuwa na sifa ya nudhumu. Wamitila (keshatajwa, 171) anaeleza nudhumu ni tungo za kifasihi zenye matumizi ya lugha yanayozifanya tungo hizo kubaguliwa au kubainika kama zisizo za kinathari. Anaendelea kufafanua kuwa tungo hizo hutumia mapigo kwa utaratibu maalumu aghalabu neno hili hutumiwa kwa maana ya tungo za kishairi. Kwa maelezo haya yanatupa maana kuwa utendi unatakiwa kuandikwa au kutolewa kishairi na kuwasilishwa kwa kughanwa. Utendi huo una sifa ya kishairi na vipengele vifuatavyo ndivyo vinavyoufanya utendi huu kuwa na sifa ya kishairi:
(a)    Utendi umeundwa na beti, Wamitila (keshatajwa, 243) anasema ubeti ni kifungu cha mshororo mmoja mmoja au mishororo kadha katika shairi na ambacho kinajitosheleza. Utendi wa Rasi ‘iGhuli umeundwa na beti 4584 na kila ubeti umeundwa na vipende vinne vya mistari ambavyo vinajitosheleza na hivyo kubeba sifa ya ushairi.
(b)   Kila ubeti umeundwa na vina na mizani 8 kwa kila kipande cha mstari. Abedi (1953: 15) anasema tenzi nyingi zaidi huwa zenye mistari minne na mizani nane kama inavyojitokeza katika Utendi wa Rasi ‘iGhuli.(rejea beti za utenzi huo). Tukitazama beti hizo tunaona kuwa, kila kipande kimeundwa na mizani nane (8) na kuhusu vina kila ubeti umebeba vina vyake huku kukiwa na kina bahari cha ri kinachojitokeza katika beti zote. Sifa zote hizo zinaufanya utendi huo kuwa na sifa ya kishairi. Ikumbukwe kuwa tendi nyingi za Kiswahili huundwa na beti ambazo kila ubeti huundwa na mistari minne ingawa pia zipo tendi zenye kutumia mistari zaidi ya mine katika beti, mfano mzuri ni Utenzi wa Vita vya Kagera msimulizi amechanganya mistari zaidi ya minne. Tendi nyingine za Kiswahili zinazotumia mistari mine kwa kila beti ni kama vile Utendi wa Fumo Liyongo, Al-inkishafi, Mwanakupona kwa kutaja chache.
Aidha sifa nyingine kama ilivotajwa na Mulokozi ni utendi kuelezea matukio au masuala muhimu ya kihistoria au kijamii. Utendi wa Rasi ‘iGhuli una sifa hii kwani unahusu masuala ya kihistoria hususani historia ya kuanzishwa kwa Uislamu huko Saudi Arabia na Yemen katika karne ya saba.
Kigezo kingine kinachojitokeza katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli ni utendi kuelezea habari za ushujaa na mashujaa.[4] Mashujaa wanaozungumziwa katika utendi huu ni Mtume Muhammad na masahaba wake kama vile Seyyidna Ali bin Abdala Talib na Seyyidna Umar bin Khatab. Mathalani msimulizi anatueleza jinsi shujaa Ali alivyofanikiwa kumuua Rasi ‘iGhuli anatueleza kuwa Rasi ‘iGhuli baada ya kuona mapigano yamepamba moto anaamua kukimbilia mjini na kuingia na kumkuta Ali wanapigana hatimaye Ali anaibuka shujaa kwa kumkata kichwa Rasi ‘iGhuli na kichwa chake kutundikwa juu ya lango la mji. Rejea kuanzia ubeti wa 4528-4532.
Aidha utendi huu unakidhi hata vigezo vya utendi vilivyotolewa na Ruth Finnegan (1970:108-109) hususani kigezo cha urefu na uunganifu ambavyo havijitokezi katika vigezo vilivyoainishwa na Mulokozi. Mathalani kwa upande wa Urefu shairi hili linakidhi kigezo hiki. Leo van Kessel (keshatajwa, viii) anatueleza kuwaUtendi wa Rasi ‘lGhuli ndio utenzi mrefu kuliko zote zilizopata kuchapishwa katika lugha yoyote ile ya Kiafrika. Utendi huo una beti 4584.
3.0 Sifa pambanuzi za kifani za utendi andishi wa Kiswahili zinavyojitokeza katikaUtenzi wa    Rasi ‘lGhuli    
                    
Tunapozungumzia utendi wa Kiswahili tunatakiwa kuhusisha na dhana nzima ya fasihi ya Kiswahili. Tunaarifiwa kuwa mwanzo mwa miaka ya 1970 hadi 1990 dhana ya fasihi ya Kiswahili ilizua mjadala mkubwa miongoni mwa wanataaluma wa fasihi. Wapo waliokuwa wanaona kuwa kuna fasihi ya Kiswahili na upo upande mwingine uliona kuwa hakuna fasihi ya Kiswahili. kwa kuwa si lengo la makala haya kujikita katika mjadala huo. Itoshe kusema kuwa, wataalamu hao walikubaliana kwamba, fasihi ya Kiswahili ni ile inayotumia lugha ya Kiswahili na hata iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, Sengo (1987), Mazigwa (1991). Aidha Synambo na Mazrui (1990) wanasema kuwa fasihi ya Kiswahili ni ile iliyoandikwa kwa Kiswahili tu na iwapo inazungumzia utamaduni wa Kiswahili au utamaduni mwingine. Hivyo basi, kwa mawazo hayo tunaweza kusema kuwa utendi wa Kiswahili ni utendi ulioandikwa au kusimuliwa kwa lugha ya Kiswahili na unaozingatia fani na maudhui (utamaduni) ya Waswahili wenyewe au jamii nyingine maadamu umeandikwa kwa lugha ya Kiswahili.
Ama kwa hakika, utendi andishi wa Kiswahili una sifa zake pambanuzi za kifani ambazo huweza kutumika kuzitofautisha na tendi nyingine zisizo za Kiswahili. Wamitila (keshatajwa, 41) anaeleza fani kuwa ni dhana inayotumiwa kuelezea muundo au mpangilio wa kazi fulani ya kifasihi au hata sehemu zake. Anaendelea kufafanua kuwa fani huelezea mbinu na mtindo wa kuyawasilisha yaliyomo au maudhui. Njogu na Chimerah (2008:312) wanasema, fani ni usanifu wa kazi ya fasihi. Wanaendelea kufafanua kwamba, fani ni vipengele mbalimbali vya sanaa na jinsi kazi hiyo inavyojengwa ili kupata maana yake. Hivyo basi katika utendi tunapoangalia fani tunaangalia tunaangalia vipengele mbalimbali vya sanaa ya utendi wa Kiswahili ama mbinu au mtindo anaoutumia msimulizi kuwasilisha mawazo yake kwa hadhira.
Ama kwa hakika Utenzi wa Rasi ‘lGhuli unakidhi sifa za kuitwa utendi wa Kiswahili kutokana na kubeba sifa pambanuzi za kifani za utendi wa Kiswahili. Utendi wa Kiswahili una sifa pambanuzi zifuatazo za kifani ambazo kwa hakika zinajitokeza katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli:
Kwanza ni matumizi ya fomula. Wamitila (2003:49) anasema fomula ni istilahi inayotumiwa kuelezea kiunzi cha msuko au sifa fulani ambazo hutumiwa katika uundaji wa kazi za kifasihi. Anaendelea kufafanua kuwa usimulizi na utambaji wa hadithi katika fasihi simulizi hutangulizwa na kianzio cha fomula. Katika tendi za Kiswahili kuna mwanzo wa kifomula ambapo msimulizi huanza na kuomba dua na kumsifu Mungu na Mtume. Fomula hii inajitokeza katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli ambapo msimulizi anaanza kwa kuomba dua na kumsifu Mungu kama anavyoanza katika ubeti wa 1-8:
1.      Awali bisumi ‘llahi                         
 Jina la mola ‘llahi                                  
               Pweke asiye shabihi                             
               Ndiye wahidi qahari.           (unaweza angalia pia katika ubeti 2-8)
Tukiziangalia beti hizo zinatuonesha kuwa msimulizi anaanza kwa kuomba dua na kumsifu Mungu (Allah). Hii ni fomula inayojitokeza katika tendi za Kiswahili. kwa mfano katika utendi mwingine wa Kiswahili wa Utendi wa Fumo Liyongo tunaona sifa hii ya fomula ya kuanza na dua na kumsifu Mungu au Mtume ikijitokeza katika ubeti wa 1. Pia tukiangalia Utendi wa Al-Inkishafi tunaona fomula hii pia ikijitokeza, rejea ubeti wa kwanza wa utenzi huo.
Aidha utendi wa Kiswahili unakuwa katika mpangilio wa beti. Utendi wa Rasi ‘lGhuli nao ni utendi unaoundwa na beti, una beti 4,584 na kila ubeti umeundwa na vipande vinne vya mstari ambapo kila kipande kina mizani nane (8). Aidha beti hizo huwa na vina vinavyofanana katika vipande vya mwanzo na kina cha kipande cha mwisho ni kinabahari ambacho huishia na -ri kuanzia ubeti wa kwanza hadi wa mwisho. Hili tunaweza kuliona tukitaza beti zote kuanzia ule ubeti wa kwanza hadi wa mwisho. Beti hizo tatu tukiziangalia zinatuonesha kuwa kila ubeti una vipande vinne vya mstari na kila kipande kina mizani 8. Kina bahari kikiwa ni –ri. Abedi (keshatajwa, 16) anasema kila utenzi wa mizani nane huimbika vizuri.
Vilevile matumizi ya majigambo ni sifa nyingine inayoitambulisha utendi wa Kiswahili. tendi za Kiswahili huwa na matumizi ya majigambo. Wamitila (keshatajwa, 107) anaeleza majigambo kuwa ni aina ya maghani (au sifo) yanayohusu kujisifu au sifa. Anaendelea kufafanua kuwa majigambo hutongoa utungo wa kujisifu kuhusiana na kitendo fulani, ushujaa, urijali au matendo muhimu. Katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli tunaona kabla mashujaa hawajaanza kupambana huanza kujigamba kwanza na kuanza kuelezea sifa na uwezo wao mbele za adui zao. Mfano mzuri ni Sayyidna Ali anajigamba mbele ya adui wake Zuheri na Zuheri kwa upande wake anajigamba mbele ya adui yake huyo. Hebu tuangalie ukurasa wa 43 kuanzia ubeti wa 845-847.
    845. Jina langu takwambia                    847.   Ndimi samba maarufu
            Ndi mimi Shekhe Alia                               Ndimi mvunda sufufu
Ibunu amu Nabia                                      Wajapo kuwa elfu
            Muhamadi ‘lBashiri.                                  Siwajali sifikiri.
Kwa upande wake Zuheri naye anamjibu Sayyidna Ali akijigamba kuanzia ubeti wa 865-868 (Rejea beti hizo).
Pia unaweza angalia ubeti 867 na 869. Beti hizo zinatuonesha namna mashujaa hao walivyokuwa wakijagamba kila mmoja akijisifu mbele ya mwenzake na mara baada ya kumaliza majigambo hayo huanza kupambana kwa kupigana rejea ubeti 887-892 (uk. 45). Sifa hii ya majigambo tunaona pia ikijitokeza katika Utenzi wa Nyakiiru Kibi.  Majigambo hayo yanaoneshwa na    Kanyamaishwa na Nyakiiru Kibi. (rejea ubeti 383-389)
Sifa nyingine ya utendi wa Kiswahili inayojitokeza katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli ni sifa ya matumizi ya Kiswahili cha Lamu kwani ndiyo husemekana kuwa ni Kiswahili cha kishairi. Taylor akinukuliwa na Mbaabu (2007:15) kuhusu lahaja ya Lamu (Kiamu) kuhusishwa na ushairi anasema kuwa, ni ukweli unaotajwa na Waswahili wenyewe kwamba Kiamu kinasifika kwa utajiri wa lugha ya kishairi. Hivyo basi katika utendi huo sifa hii inajitokeza kwani kuna matumizi makubwa sana ya Kiswahili au msamiati kutoka lahaja ya Kiamu.maneno kama ndia likiwa na maana ya njia ubeti wa 447, nti likiwana maana ya nchi katika ubeti wa 524, matolikiwa na maana ya macho katika ubeti wa 437 na 462, mtana likiwa na maana ya mchana katika ubeti wa 565 kwa kutaja maneno machache.
Matumzi ya Kiswahili cha kale ni sifa pambanuzi nyingine ya utendi wa Kiswahili. Wamitila (2010:73) anasema utanzu wa ushairi unatumia msamitai wa kale ukilinganishwa na utanzu wa riwaya au wa tamthiliya. Sifa pia  inajitokeza  katika Utendi wa Rasi ‘lGhuli. Utendi umetumia msamiati wa kale baadhi ya msamiati wa kale unaojitokeza katika utendi huo ni, akima likiwa na maana ya akisimama katika ubeti wa 785 na 818,akita likiwa na maana ya akaita katika ubeti wa 789 na 884.
 Si hivyo tu, utendi wa Kiswahili una sifa ya kuchanganya wahusika wanadamu na wasio wanadamu. Msokile (1993:32 )  anaeleza kuwa wahusika ni watu , wanyama au vitu katika kazi ya kisanaa ya kifasihi. Kwa mfanoUtendi wa Rasi ‘lGhuli unachanganya wahusika binadamu ambao wanaongozwa na Mtume Muhamadi na masahaba na wafuasi wa Kiislamu, pia kwa upande mwingine kuna binadamu makafiri wanaongozwa na Rasi ‘lGhuli lakini pia msimulizi amechanganya na wahusika wengine wasio binadamu kama vile malaika, Mungu n.k. Mathalani katika ukurasa wa 13-19  ubeti wa  350-362  anasema;
354. Kiwasili Jiburili                             359.  Kanituma nikujie
                        Akamwambia Rasuli                              Na maneno nikwambie
         Akusalamu Jalali                                     Tuma mtu amwendee
         Salamu nyingi kathiri.                            Sultani wa kufari.
Tukiziangalia beti hizo tunaona kuwa kuna wahusika malaika wanajitokeza katika utendi huo. Ukirejea beti ya 354 na 359 tunamwona malaika Jibilii akimpa amri Mtume Muhamadi kwenda kwa Rasi ‘lGhuli. Aidha kuhusu wahusika Malaika rejea pia ukurasa wa 189 ubeti wa  3761 – 3770 ambapo tunawaona Malaika wakijitokeza kusaidia majeshi ya Muhamadi katika vita.  Aidha kuna mhusika Ibirisi anajitokeza katika utendi huu, tunamwona ibirisi akijibadilisha maumbo ya watu mbalimbali ili kuwahadaa Waislamu, kwa mfano kuna wakati anajibadilisha na kuingia katika sanamu ni kuwahadaa watu kuwa yeye ni Mungu kama msimulizi anavyotuambia katika ubeti wa 473-476. Tuangalie beti chache:
              473. Ibilisi maluuni                                      475. Sikuzaa sikuzawa
        Achondoka iyo hini                                      Naua na kufufua
        Akangia sanamuni                                        Naumba nikiumbua
        Sultani kumghuri.                                         Ndimi wahidi Qahari.
Vilevile, kuna wakati ibirisi anajigeuza  Kharid mmoja wa masahaba wa Mtume Muhamadi na kwenda kuwaambia kuwapa taarifa za uongo kuwa Muhamadi ameuwawa. Rejea ubeti wa 2397- 2399. Kwa ujumla wahusika kama Lata, Uza na Manata, miungu ya uongo wa kike, Ibirisi na shetani ambao si binadamu wanajitokeza katika kazi hii.
Kwa upande mwingine sifa ya matumizi ya sintaksia au sarufi ya kisimulizi kama sifa ya utendi simulizi pia inajitokeza katika Utenzi wa Rasi ‘lGhuli. Wamitila (keshatajwa, 84) anaeleza muundo wa sintaksia unaweza kuwa msingi muhimu wa kuakisi jinsi mawazo ya mhusika au wahusika wa kifasihi walivyo. Sintaksia katika usimulizi ina maana upatanisho wa kisarufi unaoibua usimulizi fulani katika ngano mara nyingi hujitokeza viambishi vya -ki-. Hebu tuangalie ubeti wa 99 (ukurasa 5) na ubeti wa 353 ukurasa wa 18: anaposema;
99.Wakikamata wanangu                          353. Akishuka mualimu
Wakiwafunga kwa pingu                                   Ametukua alamu
Wakiwakusa matungu                                       Akibalighi salamu
Na mwenyewe hubusuri.                                   Akitikia Bashiri.
Hitimisho
Katika makala haya tumefanya uhakiki kwa kuchambua Utenzi wa Rasi ‘lGhuli kama unastahili kuitwa utendi wa Kiafrika na vilevile kama unafaa kuwekwa katika kundi la tendi za Kiswahili. ili kujibu maswali hayo tulijikita zaidi kuangalia vigezo vya utendi wa Kiafrika lakini pia tukaangalia utendi huo kama unakidhi vigezo vya kuitwa utendi wa Kiswahili kwa kumakinikia zaidi katika sifa pambanuzi za kifani na kimuundo za utendi wa Kiswahili. Ama kwa hakika baada ya kupitia vigezo hivyo na utendi husika tunakubaliana kuwa Utenzi wa Rasi ‘lGhuli kama tulivyoona hapo juu ni utendi unaokidhi sifa za kuitwa utendi wa Kiafrika kutokana na kukidhi vigezo vya utendi wa Kiafrika kama vilivyotajwa na Mulokozi (keshatajwa, 11) lakini pia unakidhi vigezo vya kuwa utendi wa Kiswahili na hii si kwasababu tu umeandikwa kwa lugha ya Kiafrika au Kiswahili ni kwa sababu umekidhi vigezo vyote vya utendi wa Kiafrika na Kiswahili.
[1] Majina mengine ya Mtume Muhamadi kati utenzi huu ni kama vile, ‘lBashiri, Mursali, Rasua, Rasuli
[2] Majina yake mengine yanayojitokeza katika utenzi, Shekhe Ali, Aba ‘lHasani, Haidari (samba), Imamu, Jabali Abu Qubesi
[3] Ni wilaya inayopatikana Tanzania Bara katika Mkoa wa Pwani.
[4] Shujaa ni mtu mwenye moyo thabiti anayeweza mambo hata kama ni ya hatari TUKI (1981:258). Aidha Mlokozi (1999:11) anataja sifa za shujaa kuwa ni nguvu za kimwili na nguvu za kiume, kuwa na nguvu za uganga na sihiri, kuwa na mshikamano na kundi au jumuiaya fulani.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 2 Guest(s)