SIMULIZI: KISA CHA MAUTI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Hadithi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=48) +---- Thread: SIMULIZI: KISA CHA MAUTI (/showthread.php?tid=979) |
SIMULIZI: KISA CHA MAUTI - MwlMaeda - 08-21-2021 TUNZI: Juma S. Katanga (Jushaka) “LAZIMA afe! Lazima afe!” Komandoo Mlasi Kasanura Bamba alirudia tena kujiapiza. Damu ilikuwa imetapakaa sakafuni chumba kizima. Maiti kumi zisizo na vichwa zilikuwa mbele ya macho yake na nyingine zilikuwa zimetapakaa hovyo nje. Grand Kapakacha alikuwa bado kajificha nyuma ya mlango bunduki mkononi ,jambia kiunoni. Ni operesheni kabambe kweli kweli. Je, mambo haya yakoje? Ungana na mwandishi katika riwaya hii ya kusisimua.
BAADA ya kuona yule dereva hazinduki na bado damu zikiendelea kumtiririka masikioni, Grand K. hofu ilimwingia akadhani tayari ameishaua! “Balaa gani tena hili jamani la asubuhi asubuhi “, alilalama Grand K. kichini chini huku akimkodolea macho yule dereva pale chini. Akatimka mbio haraka na kuwaita wale walinzi wake wa nyumba waje kumsaidia. “Hajafa huyu, bado mzima! Amezirai tu!” alisema yule mlinzi Mzee ambaye muda mfupi uliopita alipata kisanga cha kupigwa na kutemewa makohozi na Grand K. kwa kosa la kulala usingizi juu ya magunia. “Sasa nyie endeleeni tu kumpa huduma ya kwanza, mimi nawahi mjini kwenye shughuli zangu nimeishachelewa sana!” aliagiza Grand K huku akiingia ndani ya gari na dereva mwingine.
Grand K na huyo dereva mwingine sasa walichoma mafuta kuelekea mjini huku dereva huyo akiwa amegubikwa na hofu moyoni kwa kuamini kwamba ipo siku na yeye yanaweza kummkuta kama hayo yaliyomkuta mwenzake aliyezimia leo.
“Leo utanipitisha kwanza kwa Bwana Ziro, kisha kwa yule Mhindi wangu, halafu utanipeleka pale Kisutu Chef’s Pride nikapate Yoga, sawa?… Baada ya hapo nitakwambia tena twende wapi”, Grand K. alimweleza dereva katika namna ya kuamuru. Tangu hapo ikawa sasa ni amri tu, “kata kushoto…..kata kulia!…..simama!….rudi nyuma kwanza!…..ingia kushoto…….mbele kidogo….!!” Na yule dereva akabakia kutii amri na kuitikia tu “Sawa Mzee!…..sawa bosi!….”
Baada ya mwendo mfupi hivi walifika nyumbani kwa Bwana Ziro, rafiki mkubwa wa Grand K. wanayeshirikiana katika biashara na miradi yake mbalimbali. Grand K. na Bwana Ziro ni marafiki vipenzi kwelikweli tena wa kufa na kuzikana. Siri zake zote Grand K. ni za Bwana Ziro na za Bwana Ziro zote ni za Grand K. Hakuna litakalomgusa mmoja halafu mwingine lisimguse. Walikuwa ni kama chuma na sumaku au pacha wawili.
Bwana Ziro yeye anaishi Mwenge jijini lakini maskani yake makubwa ni kwenye kituo cha Tax cha Mnazi Mmoja pale barabara ya Lumumba jijini ambapo mara nyingi hupenda kushinda pale akipiga soga , kucheza bao au drafti na wazee wa pale.
Baada ya kufika nyumbani kwa Bwana Ziro, Grand K. aliteremka na kuingia ndani. “Ooohooh….. Paka Mweusiumefika!”, alitania Bwana Ziro huku akitabasamu kwa furaha baada ya kumwona Grand K. “….Ohooh….Paka Mwanga haujambo?” alirudishia Grand K. kwa utani huku nae akicheka pia. Wenyewe Grand K. na Bwana Ziro wamezoea kuitana kwa majina hayo ya kimafumbo kila wanapowasiliana ili kuwatambua maadui zao au watu wasiowataka katika mambo yao. Basi wao na kundi lao zima la uharamia husalimiana kwa ishara hizo hizo kila wanapo wasiliana katika simu. Hapo kwa Bwana Ziro walizungumza kimya kimya kwa muda halafu mara Grand K. akaaga. “Nakutakia bravo rafiki yangu, Paka Mweusi hakosi nyama!”, alimalizia Bwana Ziro kumwambia Grand K. ambaye alikuwa akichapulisha mwendo kuelekea nje alikomwacha dereva na gari.
*************
BAADA ya kutoka kwa Bwana Ziro, sasa walielekea kwa yule Mhindi Bw. Somji Patel ambaye anaishi Upanga Mtaa wa Mathurada. Gari lilikata kona na kupinda upande wa kushoto wa barabara ya Morogoro likaingia barabara ya Umoja wa Mataifa. Halafu likapinda tena kona karibu na msikiti wa Tambaza likaingia kulia kwenye barabara moja ndogo ya lami. Liliongoza mbele kidogo likapinda kona kushoto na kusimama katika jumba moja kubwa la kifahari lililozungushiwa ukuta na mitambo maalum ya kuzuia wezi.
Dereva alipiga hodi mara tatu mara wakaona lango kubwa la kuingilia magari linafunguliwa na mtu mmoja mweusi wa makamo hivi ambaye bila shaka alionekana kuwa mmoja wa walinzi wa Bwana Somji.
“Vipi huyu bwana tumemkuta?” aliuliza Grand K. huku akiteremka kutoka garini. Kabla hata yule mlinzi hajajibu mara wakasikia sauti ya Somji mwenyewe ikijibu kwa furaha kutokea mlango wa ndani “Ohoo Bwana K. iko nakuja! Karibu muzuri dugu yangu.” Na mara Somji mwenyewe alitokea akiwa tumbo wazi. “Welcome my friend… Kuja kwa ndani”, Somji alimkaribisha Grand K. huku wote wawili wakiongozana kuelekea Sitting-Room.
Ni nadra sana kumuona Somji akitoka mwenyewe kuja kumpokea mgeni nje isipokuwa kwa wageni wake maalum kama Grand K. Mara nyingi Bwana Somji hungojea wageni waingie wenyewe ndani baada ya kutoa idhini kwa walinzi wawaruhusu kupita kama ni wageni wa maana. Ama kwa wageni wengine wa hali za chini basi hawaruhusiwi japo kukanyaga kizingiti cha mlango. Majibu yao yote hupatiwa hapo hapo mlangoni kupitia kwa wale walinzi. Lakini sio Grand K. Yeye akifika hapo Bwana Somji humchangamkia na kumnyenyekea utadhani yeye Somji ni mtumwa wa Grand K.
Baada ya kuingia ndani ya jumba hilo kubwa la kifahari lenye vyumba lukuki ndani, Somji na Grand K. walikwenda moja kwa moja hadi Sitting Room ambapo mke wa Somji alikuja kumlaki mgeni huyo maalum na kuwaletea vinywaji. Mara Somji akamtaka mkewe awapishe pale sebuleni yeye na Grand K. kwamba wana mazungumzo ya faragha. Mke wa Somji akawapisha pasi na tabu wakabaki wawili hao peke yao hapo ukumbini.
Bwana Somji ni mshirika mkubwa wa biashara na kikundi cha kina Grand K. ambacho yeye Grand K. na wenzie akina Bwana Ziro walikipa jina la “G-12 Operation”. Kikundi ambacho shughuli zake halisi hazijulikani.Hakuna anayezijua isipokuwa wenyewe akina Bwana Ziro. Basi Grand K. na Somji walizungumza kwa sauti ya chinichini ya kunong’ona pale sebuleni juu ya mambo yao fulani ya siri. Halafu wakaonekana kama vile wanabishana juu ya kitu fulani hivi kila mmoja akipinga maelezo ya mwenzake. “Pana bana, mimi iko mpa veve natosha bana”, alionekana kulalamika yule Mhindi. “Somji unaniangusha bwana rafiki yangu”, alijibu Grand K. huku akionekana kumbembeleza Somji kitu fulani. Miongoni mwa mambo waliyokuwa wakiyajadili hapo sebuleni kumbe ni pamoja na mauzo ya jumba moja la kifahari ambalo Grand K. amemuuzia Somji. Jumba hilo lililoko kule Kinondoni Shamba jijini ni mali ya urithi iliyokuwa ya marehemu kaka yake Grand K. aitwae Kasanura Bamba. Bwana Kasanura Bamba aliuawa miezi mitatu iliyopita kwa kupigwa risasi ya kichwani na mtu mmoja asiyejulikana. Lakini baadae wengi walimshuku huyo huyo Grand K. kwamba ndio aliyehusika na mauaji ya kaka yake huyo kama si yeye mwenyewe aliyemuua. Grand K. na kaka yake huyo Bw. Kasanura Bamba ni baba mmoja mama mmoja. Yeye Grand K. au Grand Kapakacha, jina lake halisi ni Kapakacha bin Bamba na huyo kaka yake ni Kasanura bin Bamba. Wote walizaliwa huko huko kwao Nkasi mkoani Rukwa. Hivyo baada ya kumuua kaka yake, Grand K. aliichukua nyumba hiyo ya urithi wa watoto wa Mzee Kasanura Bamba na kuiuza kwa Bw. Somji Patel. Sasa leo ndio alikuwa amefuata malipo ya nyumba hiyo hapo kwa Bwana Somji.
Baada ya kushindwa kuafikiana bei na Somji, Grand K. aliamua kumpigia simu rafikiye kipenzi Bwana Ziro ili kumtaka ushauri. “Hallow!”, Grand K. aliinua mkono wa simu na kuita pale sebuleni kwa Somji. “Hallow! PAKA Mweusi?”, aliita Grand K. katika simu. “Hallow PAKA Mwanga?”, ilijibu sauti ya upande wa pili ambayo bila shaka ilikuwa ni ya Bwana Ziro. Mara sauti hiyo ya upande wa pili ikaita tena, “PAKA shume?”. Sauti ya Grand K. nayo ikajibu, “Hakosi nyama!… Nani mchawi ?”. “Mbwa Koko!“, ilijibu sauti ya Bwana Ziro huku akicheka kwa sauti kubwa kwelikweli mle ndani ya simu. Somji alibaki kaduwaa tu akijionea malimwengu akabaki kamkodolea macho Grand K. pale kwenye simu.
|