Masimulizi ya Alfu Lela U Lela - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Hadithi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=48) +---- Thread: Masimulizi ya Alfu Lela U Lela (/showthread.php?tid=937) |
Masimulizi ya Alfu Lela U Lela - MwlMaeda - 08-20-2021 Masimulizi ya Alfu Lela U Lela
UTANGULIZI
Hakika asasi za hadithi za ALFU LELA U LELA ni Asia hasa Arabuni, Bara Hindi, na Ajemi. Asasi hii inasemekana imetoka katika kitabu kimoja cha Ki-Persia cha hadithi za majini kiitwacho Hazar Afsanah (Visa Elfu Moja) kilichotafsiriwa Kiarabu katika mwaka 850. Wanazuoni wa sasa waliotafiti zaidi juu ya hadithi hizi wanasema kuwa chanzo hasa cha ALFU LELA U LELA ni Bara Hindi na Persia. Walakini, wasimulizi wa nchi mbalimbali wa hadithi hizi, kila walipozisimulia, waliongezea hadithi na visa vingi vya kikwao mpaka zikaongezeka idadi na kuwa vitabu chungu nzima!
Hadithi hizi zipendwazo sana na walimwengu na zilizotafsiriwa kwa lugha nyingi, zimeletwa Ulaya, kwa mara ya kwanza, na Mfaransa Antoine Galland (1646-1715) aliyekuwa na taaluma ya mambo ya Kiarabu na aliyesafiri sana Mashariki ya Kati nyakati hizo; halafu zikatafsiriwa kwa Kijerumani mwaka 1865 na Gustav Weil, mtaalam wa Mashariki ya Kati.
Ijapokuwa hadithi hizi zilitafsiriwa kwa Kiingereza, kwa mara ya kwanza (1706-8) na mtu asiyejulikana, tafsiri kamili kwa lugha ya Kiingereza ya vitabu ilifanywa na John Payne (1882-4). Walakini, tafsiri iliyopendwa zaidi ni ile ya Sir Richard Burton ya vitabu 10 ya mwaka 1885-6.
Kwa Kiswahili, hadithi hizi, ambazo zilitoweka baada ya Uhuru, zilitafsiriwa na Edwin W. Brenn katika mwaka 1928 chini ya uongozi, ufupishaji, na uhariri wa Mmisionari F. Johnson. Wao walizifupisha na wakazibadili (kwa mfano safari ya saba na ya mwisho ya Sindbad) kwa sababu zisizojulikana.
Mimi, katika vitabu hivi vipya nimetoa tafsiri mpya kutoka katika vitabu vya lugha mbalimbali bila kuzihariri wala kuzifupisha isipokuwa sehemu fulani fulani tu ambazo nimeona huenda zikaeleweka vibaya.
Kwa kuwa hadithi hizi ni za asili ya Kiarabu, kwenye fahrisi nimejaribu, kadiri nilivyoweza, kutumia maneno fulani fulani ya asili ya Kiarabu kama yaandikwavyo au yatamkwavyo kwa lugha hiyo na kama yalivyotumiwa katika tafsiri nyingi. Walakini, maneno hayo nimeyaeleza kwa Kiswahili kama yajulikanavyo na yalivyoandikwa katika kamusi ya Kiswahili Sanifu.
Sina budi kusisitiza humu kuwa kabla Wareno, wazungu wa kwanza kukanyaga mwambao wa Afrika Mashariki mnamo mwaka 1498 chini ya uongozi wa nahodha Vasco da Gama wakivinjari Afrika kutafuta njia ya kuelekea Bara Hindi, Waswahili, toka enzi na enzi, waliingiliana na wafanyabiashara na mabaharia kutoka Ajemi (Persia), Arabuni na Bara Hindi. Kuna ushahidi kamili wa kihistoria unaothibitisha pia kuwa hata Wachina na Wa-Indonesia wa kale walifika mwambao wa Afrika Mashariki kuitwako Uswahilini. Hivyo basi, ngano, visa, na hadithi nyingi za Kiswahili zilizosimuliwa na Waswahili toka enzi za kale, kuna nyingi zilizoathiriwa na nchi hizo na kuna za asili ya nchi hizo ambazo, baada ya miaka nenda, mwisho zikawa za Kiswahili. Kwa hiyo, kuzikana au kuzifutilia mbali ni kinyume cha kanuni za fasihi. Haiwezekani, kwa mfano, kwa sababu fulani fulani, ngano, hadithi au visa vya Kizulu, Kirusi au Kijapani, vikabadilishwa na kudai kuwa ni vya Kiingereza, Kiarabu au Kichina! Fasihi ikiwa ni nzuri, hutasfiriwa kwa lugha nyingi za dunia kwa manufaa ya walimwengu. Lakini fasihi hiyo hubaki ya asasi yake. Hivyo basi, nimeona ni kkheri picha za tafsiri hii mpya ya ALFU LELA U LELA ziwe za kiasili kama zilivyochapishwa katika matoleo ya kwanza ya lugha mbalimbali kwani Shahrazad au Sindbad hawakuwa wa asili ya Kiafrika!
Kwa kumalizia, naishukuru famila yangu na binti yangu kwa uvumilivu wao wa kuukabili upweke walioukabili nilipokuwa nikitumia wakati wangu mwingi kuzitafsiri hadithi hizi ofisini, wakati ambao wangefurahi kuwa nami! Namshukuru pia Salehe Awadh Mazrui wa E-PLUS Duesseldorf, Ujerumani, kwa utaalam na msaada wake wa ki-kompyuta ulionifaa sana, kwani kila kompyuta yangu ilipokwama, yeye, bila kusita, alitoka Dusseldorft kuja upesi Cologne kulitatua tatizuo! Namshukuru pia Lutz Diegner kwa msaada wake wa kunifafanulia kwa Kiswahili maana ya maneno magumu ya Kijerumani. Shukran za dhati nazitoa kwa sahibu yangu, mshairi mashuhuri Abdilatiff Abdalla ambaye sasa ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Leipzig, Ujerumani kwa kuupitia mswada huu, kwa ushauri wake, na kwa kuiandika Dibaji ya vitabu hivi. Kwa kumalizia, tafsiri hii isingewezekana kama si nafasi na msaada wa hali na mali niliopewa na Taasisi ya Lugha za Kiafrika, Chuo Kikuu cha Cologne, Ujerumani.
Cologne, Ujerumani
Juni,2 003
SULTAN SHAHRIYAR NA SULTAN SHAHZA-MAN
HAPO KALE paliondokea Sultani mmoja wa Kisassanid aliyekuwa na enzi kubwa sana iliyoenea toka Bara Hindi mpaka Uchina. Jeshi lake kubwa lenye nguvu, liliweza kuishinda na kuiteka kila nchi ya jirani mpaka sifa za utawala wa Sultani huyo zikaenea kila pembe ya dunia. Alipofariki, akaacha wana wawili waliokuwa mashujaa na hodari wa kupanda farasi, hasa mkubwa aliyeitwa Shahriyar aliyerithi kiti cha enzi cha baba yake. Yeye alifuata nyayo za baba yake mpaka raia zake wote wakampenda. Mdogo wake aliyeitwa Shahzaman akawa Sultani wa nchi ya Samarkand.
Basi ndugu wawili hawa wakendelea kutawala nchi zao kwa furaha na kwa haki kwa muda wa miaka ishirini mpaka siku moja Sultani Shahriyar akaingiwa na hamu ya kutaka kumwona mdogo wake. Basi akamwamuru Waziri wake Mkuu aende Samarkand akamwalike Shahzaman.
Baada ya safari ndefu ya siku nyingi katika jangwa, mbuga na nyika, Waziri Mkuu akawasili katika mji mkuu wa Samarkand. Bila kuchelewa akafikishwa mbele ya Sultan Shahzaman aliyefu- rahi sana kupokea salamu na ujumbe kutoka kwa kaka yake; na yeye, bila kuchelewa, akatoa amri safari ya kumzuru kaka yake itayarishwe. Matayarisho yalipokamilika, Shahzaman akatanguliza msafara wake wa ngamia na farasi ulioshehenzwa vyakula na za- wadi za kila namna ukiongozwa na watumishi na wajakazi wake wa kumhudumia wakati wa safari yake ndefu. Kabla hajaondoka, walakini, akamchagua Waziri wake Mkuu amshikie madaraka yake mpaka atakapojaaliwa kurudi.
Usiku Sultani Shahzaman akakumbuka amesahau zawaidi muhimu aliyodhamiria kumpelekea kaka yake. Basi bila kuonekana na mtu, akatoka hemani mwake, akarejea kwenye kasri lake. Alipo- ingia ndani, la haula! akamkuta mkewe amekumbatiwa kimapenzi na mtumwa wake mmoja! Kuona vile, akapigwa na butaa; haku- weza kuamini yale aliyoyashuhudia pale penye sofa! Akafikiri,
“Kama kitendo kama hiki kinaweza kutokea wakati sijafika mbali, iblisi huyu atafanya nini nitakapokuwa mbali?” Hapo akafuta up- anga wake, akawaua wote wawili pale pale.
Aliporejea kwenye kambi, akaamuru msafara uendelee. Akaendelea na safari yake kwa huzuni na majonzi mengi mapaka akafika mji mkuu wa kaka yake.
Sultan Shahriyar aliposikia mdogo wake anawasili, akatoka kwa furaha na kwa shangwe astahiliyo Sultani kwenda kumlaki mdogo wake. Alipomwona, akamkubatia, akamkaribisha jijini mwake lililojiandaa kumpokea mikono miwili.
Lakini wakati Sultan Shahriyar alipokuwa akimfurahisha na kumtumbuiza mdogo wake, mawazo ya Sultan Shahzaman yakawa yako kwa yule mkewe na vile vitendo vyake vya ufisadi alivyokuwa akivifanya pale sofani.
Ijapokuwa alikuwa na huzuni na majonzi mengi hivyo, hakuna yeyote aliyejua wala aliyemweleza mkasa ule. Lakini Sultan Shahriyar alitambua kuwa kuna lililokuwa likimkera mdogo wake lakini hakutaka kuuliza. Alifikiri labda ni mambo ya utawala wa nchi au kuondoka kwake ndiko labda kulikokuwa kukimtia wasiwasi. Basi baada ya siku chache Sultan Shahriyar akaona ni kkheri amwa- like mdogo wake waende wakawinde ili apate kumliwaza; lakini Shahzaman akajibu kuwa anaumwa na hawezi kwenda kokote. Hapo Sultan Shahriyar aende peke yake.
Wakati Shahzaman alipokuwa ameketi peke yake karibu na dirisha la chumba chake lililoelekea bustanini huku akiwaza juu ya yale masaibu yaliyompata, mara mlango mmoja ukafunguka na wajakazi ishirini wakiongozana na watumwa ishirini wakatokea. Katikati yao alikuwemo malkia, mke wa kaka yake, ambaye uzuri wake ulikuwa hauna kifani. Wote arobaini wakelekea moja kwa moja mpaka penye chemchemi ya maji iliyokuwa ikitiririka. Hapo wakvua nguo, wakakaa majanini. Mara malkia akaita, “Masud, njoo utekeleze kazi yako!”
Mara pandikizi la mtumwa likatokea ambalo, mara tu lilipofika, likamkumbatia malkia na kufanya naye mapenzi pale bustanini! Wale watumwa wengine nao, hali kadhalika, wakawa wanazini na wale wajakazi. Wakaendelea na mapenzi yao mpaka kulipoanza kuchwa na wakati wa Sultani kurejea kutoka mawin- doni ulipokaribia.
Shahzaman alipoona vile, akafikiri, “Wallahi, mkasa ulioni- pata mimi si mkubwa kama huu ninaoushuhudia hapa!”
Hapo ile huzuni aliyokuwa nayo ikamtoka, akaanza kula na kunywa kwani toka alipowasili kwa kaka yake chakula kilikuwa hakimshuki rohoni.
Sultan Shahriyar aliporejea, akashangaa kumwona mdogo wake amebadilika na sasa yumo katika hali nyingine kabisa.
“Imekuwaje, ndugu yangu,” Sultan Shahriyar akahoji kwa mshangao, “kuwa nilipoondoka ulikuwa dhaifu uliyepauka uso na sasa unaonekana mwenye siha nzuri hivi?”
“Mintaarafu siha yangu sasa na unyonge niliokuwa nao awali,” akajibu Shahzaman, “nitakusimulia sababu lakini sithubutu hata kidogo kukufunulia sababu zilizoleta mabadiliko hayo; lakini jua kuwa, baada ya kupokea mwaliko wako, nilianza safari ya kuja huku. Kwa kuwa nilisahau lile jiwe la tunu nililokupa zawadi, ili- nibidi nirejee nyumbani nikalichukue.”
Nilipoingia ndani, nikamkuta mke wangu amekumbatiwa na mmoja wa watumwa wangu wamelala kwenye sofa wakifanya mapenzi! Unaweza kukisia jinsi nilivyohisi! Ghadhabu zilizoni- panda zilinifanya niwaue paho hapo wote wawli; halafu nikarejea kwenye msafara, nikaendelea na safari ya kuja huku wakati moyo wangu umejaa huzuni na majonzi.”
Aliposikia maneno hayo, Sultan Shahriyar akamsihi mdogo wake amweleze na ile sehemu iliyobaki. Shahzaman, baada ya kusita na kulazimishwa, akawa hana budi kumweleza kaka yake yote aliyoyashuhudia pale bustanini.
Akipigwa na mshangao na kupandwa na ghadhabu, Sultan
Shahriyar akasema: “Siamini hayo unayoyasema mpaka niyashuhu- dia mwenyewe kwa macho yangu!”
“Kama ni hivyo,” akapendekeza Sultan Shahzaman, “basi tangaza unakwenda tena kuwinda halafu rudi upesi uje hapa ujifiche nami, nawe utayashuhudia yale niliyoyashuhudia.”
Basi siku ya pili Sultan Shahriyar akatangaza madhumuni yake ya kwenda tena kuwinda. Hapo kundi lake la kuwinda likatoka mjini huku limebeba matumizi ya Sultani wakati akiwa mawindoni.
Baada ya kubaki kidogo kambini kule mawindoni, Sultan Shahriyar akatoa amri kwa watumishi wake kuwa wasimruhusu yeyote kuingia hemani mwake; halafu akajibadili kwa kuvaa mavazi mengine, akatoka bila kuonekana na mtu yeyote, akarejea hadi kwake alikomkuta mdogo wake akimsubiri.
Basi wote wawili wakajibanza karibu na lile dirisha lililoele- kea bustanini. Mara malkia na wajakazi walewale wakatokea tena wakifuatwa nyuma na watumwa walewale. Walipofika bustanini, wakayatenda yaleyale waliyoyatenda siku ile ya kwanza!
Kuona vile, Sultan Shahriyar akapigwa na bumbuazi na mshangao mkubwa sana. Akamgeukia mdogo wake, akamwambia, “Ndugu yangu mpenzi, tuuache ufalme na tutokomee ulimwen- guni tukatafute kama tutawapata waliokumbana na mikasa kama yetu.”
Baada ya Shahzaman kukubali, wakatoka kwa siri, wakasafiri kwa masiku mpaka siku moja wakafika pwani penye ufukwe mmoja mzuri mweupe wa bahari ukingoni pake pameota majani mazuri yaliyoptiwa na chemchemi ya maji safi baridi. Hapo wakashuka juu ya farasi zao, wakatawadha, wakasali sala ya adhuhuri.
Wakati walipokuwa wamepumzika kwenye kivuli cha mti mmoja mkubwa uliokuwa ukingoni wakila chakula chao cha mchana, mara bahari ikachafuka, ikaanza kutoa mapovu na maw- imbi yakaanza kupanda juu. Ghafla pale baharini pakazuka jabali refu ajabu!
Lo! kuona vile wale ndugu wawili wakapigwa na mshangao; haraka wakapanda juu ya ule mti! Walipokuwa juu, wakatazama baharini, wakaona kumbe lilikuwa si jabali bali ni jini lililobeba kasha kubwa kichwani!
Lile jini likatoka mle baharini, likaelekea pale mtini wal- ipokuwa wale ndugu wawili. Baada ya kukaa chini, likafungua lile kasha, likatoa sanduku alilolifungua. Mle sandukuni makatoka msichana mmoja mzuri kama nini!
“Mwanamwali mzuri, mtoto wa watu niliyemnyakua kwao usiku wa arusi yake,” likasema lile jini, “nataka kupumzika hapa kidogo.”
Baada ya kutamka maneno hayo, lile jini likaweka kichwa chake juu ya paja la yule msichana, na mara likachotwa na usingizi likalala fofofo pale kivulini!
Katika kutazama kwake huko na huko, yule msichana akanyanyua macho juu kule mtini; mara akawaona wale ndugu wawili. Kuwaona tu, akawaashiria washuke wasiogope; lakini wale Masultani wakamsihi ayasalimishe maisha yao.
“Kama hamtashuka,” akasema yule msichana, “nitaliamsha hili jini na bila shaka yoyote litawaadhibu vikali.”
Waliposhuka, msichana akawaambia, “Mkitaka usalama wenu, ni lazima mfanye mapenzi nami sasa hivi tena papa hapa!”
Sultan Shahriyar na Sultan Shahzaman wakakataa katakata lakini yule msichana akasisitiza kwa hasira, “Kama hamtafanya nitakavyo, nitaliamsha jini sasa hivi!”
Baada ya kuwalazimisha kufanya alivyotaka, wale ndugu wawili wakabaki naye kwa muda alioutaka yule msichana, halafu akatoa kijaluba kibindoni mwake, akakifungua, akatoa pete tisini na nane zilizotungwa kwa uzi wa hariri, akasema huku akitabasamu kwa maringo, “Mnaona, wote wenye pete hizi wamelala nami wakati hili jini li haadhir, limelala kama mfu, na nyinyi ni lazima mnipe pete zenu sasa hivi!” Wakampa.
“Jini hili,” akaendelea yule msichana, “limeniteka nyara usiku wa arusi yangu; likanifungia sandukuni kisha likalitia sanduku ndani ya kasha kubwa hili mnaloliona ambalo hulifunga kwa kufuli saba, halafu hulizamisha katika lindi la bahari kuu ili eti nilindike! Ani- takapo, kama leo, hunitoa. Laiti lingejua hila za wanawake!”
Sultan Shahriyar na Sultan Shahzaman kusikia maneno yale, wakastaajabu sana, wakaambiana, “Kama kitendo kama hiki linaweza kutendewa jini lenye nguvu kama hili sembuse siye! hakika mikasa iliyotupata sisi haiwezi kulinganishwa na nusu ya vitendo vya msichana huyu!”
Basi bila kukawia wakarejea makwao. Mara tu alipoingia ka- tika kasri lake, Sultan Shahriyar akaamuru malkia na wale watumwa wake wote wakatwe vichwa.
Basi toka siku hiyo Sultan Shahriyar akawa hana imani tena na wanawake; ikawa kila siku ni kumwoa mwanamwari mzuri na kumwua asubuhi ya pili. Akaendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka mitatu mapaka msiba mkubwa ukaenea kote mjini na ukamkumba takriban kila aliyekuwa na binti mzuri mle jijini; wengi wakalihama jiji kwa kuwakhofia mabinti zao.
Kazi hii ya kuhuzunisha ya kumtafutia Sultan mwanamwari alifanyiwa na Waziri Mkuu mpaka ikafikia siku ambayo Waziri Mkuu alishindwa kumpatia Sultani mwanamwari wa kumwoa; akarejea kwake akiwa na wasiwasi na woga wa ghadhabu za Sultani.
Waziri Mkuu alikuwa na mabinti wawili; mkubwa aliitwa Shahrazad na mdogo aliitwa Dunyazad. Shahrazad alikuwa si mzuri wa sura tu bali pia alikuwa mwenye akili, busara, na ujuzi wa kila elimu ya falme za kale. Alizidurusu na kuzihitimu vizuri mpaka akawa aalim wa mambo mengi. Siku ile akamwona baba yake ni mnyonge mwenye wasiwasi mwingi; akamwuliza lililokuwa likim- kera. Waziri Mkuu akamweleza yale yaliyokuwa moyoni mwake.
Ndipo Shahrazad akasema, “Baba, niache mimi niolewe na Sultani; yatakuwa mawili: kufa au kuokoa maisha ya wasichana wenzangu waangamiao vibaya kila siku.”
Ijapokuwa Waziri Mkuu alifanya juu chini kumshawishi binti yake aache kusudio lake, hakufuzu, kwani Shahrazad aling’ang’ania tu akubaliwe kuolewa na Sultani.
“Kumbuka yaliyompata punda katika kisa hiki kifuatacho,” akaonya Waziri Mkuu; ndipo akamsimuliwa Shahrazad
KISA CHA PUNDA, FAHALI NA MKULIMA
HAPO kale, akaanza Waziri Mkuu, paliondokea mkulima mmoja tajiri aliyekuwa na kundi la wanyma wa kila namna na aliyejaaliwa kujua lugha zao. Hakuna aliyejua siri hiyo kwani ali- yemfundisha alimwonya asiitoe ama sivyo atakufa!
Basi katika banda moja mkulima huyo aliwaweka wanyama wawili: punda ampandaye aendapo safarini, na fahali amlimiaye shamba lake. Ikawa kila jioni, baada ya kazi, fahali humwendea punda aliyewekwa mahali pazuri penye nafaka nyingi na maji safi ya kutosha, ili aongee naye.
Kwa kuwa yule mkulima hakuwa na safari nyingi, ikawa kazi ya yule punda ni kula na kupumzika tu mle bandani wakati mwenzake fahali anababuka kwa kazi ngumu ya kukokota jembe zito kule shambani!
Siku moja yule mkulima alimsikia fahali wake akimwambia punda, “Bahati ilioje hiyo uliyo nayo mwenzangu! Mimi humenyeka kutwa shambani ilhali wewe mwenzangu wapumzika kutwa humu bandani ukilishwa na ukinyweshwa vizuri bila hata kupandwa na bwana wetu!”
Punda akamwambia fahali, “Tumia akili, rafiki yangu; bila kutumia akili mambo hayaendi. Kwa hiyo, nakushauri ufanye hivi: kesho utakapotiwa hatamu kwa madhumuni ya kupelekwa shamba, jibwage chini ujifanye mgonjwa! Usinyanyuke hata kama watakutandika mijeledi mia! Ukinyanyuka, jibwage tena chini; na watakapokurudisha hapa na kukuletea nyasi, susa kabisa kuzila! Fanya hivyo kwa muda wa siku mbili tatu upate kupumzika!”
Mfanyakazi alipompeleka shamba asubuhi ya pili, yule fahali akajifanya mgonjwa wa kufa! Na aliporudishwa bandani na kuletewa nyasi, akafuata ushauri wa mwenzake punda. Ndipo mkulima akamwambia mfanyakazi wake, “Leo mwache fahali apumzike, mchukue punda akafanye kazi yake!”
Jioni, baada ya kufanyishwa kazi kweli kweli, yule punda akarudishwa bandani yu hoi taabani! Alipoingia ndani, yule fahali akamshukuru punda kwa ule ushauri wake mwema uliomfaa sana; lakini punda hakujibu kitu ila alijuta kimoyomoyo kwa kumshauri haraka mwenzake bila kufikiri matokeo yake yatakuwaje!
Siku ya pili mfanyakazi akaja tena, akamchukua punda, akaenda akamfanyisha tena kazi kutwa mpaka jioni. Aliporudishwa hoi, yule fahali akamshukuru tena mwenzake.
“Laiti nisingemshauri!” Punda akajuta kimoyomoyo; hapo akamgeukia mwenzake akamwambia, “Sahib yangu, nilipokuwa nikirudi, nilimsikia bwana wetu akimwambia mfanyakazi: ‘kama fahali hakupona, kesho mpeleke machinjoni akachinjwe!’ Kwa kuwa u rafiki yangu mpenzi, nimeona ni kkheri nikuarifu mapema upate kujua mambo yalivyo!“”
Fahali kusikia vile, akamshukuru tena mwenzake, akamwam- bia, “Kesho nitajitolea mwenyewe kwenda kazini!”
Asubuhi ya pili mkulima na mkewe wakenda kule bandani kumwangalia fahali huku wakiongozana na mfanyakazi. Wal- ipofika, wakamwona fahali anatimka mbio mle bandani huku akitoa mashuzi kuthibitisha kuwa yu mzimwa wa kigongo! Hapo mkulima akaanguka kicheko akacheka sana!
“Una cheka nini, mume wangu?” Akataka kujua mkewe. Mume akamjibu, “Linalonichekesha halifai kuambiwa mtu; si wewe wala si mwingine.”
Mke akashikilia lazima aambiwe; mume akakataa katakata mpaka kule nyumbani kwao kukawa hakuna tena furaha isipokuwa bughudha, manung’uniko na kununa kwa mke aliyedai sharti aam- biwe lililomchekesha mumewe siku ile.
Alipoona hali ya nyumbani mwake imekuwa mbaya, siku moja mume akamwambia mkewe, “Nitilie maji nikaoge nivae nguo tohara nisali ndipo nitakapokuambia kile kilichonichekesha siku ile; lakini ujue kuwa mimi si mumeo tena maana nikikuambia, nitakufa!”
Mke asijali; mradi atimiziwe lile alilolitaka. Basi akafanya kama vile alivyoambiwa na mumewe.
Alipokwisha sali, mume akamwambia mkewe, “Kwanza nakwenda kuwaaga wazee wangu, ndugu zangu, na jamaa zangu. Nitakaporudi, nitakuambia kilichonichekesha siku ile.”
Wakati alipokuwa akielekea kwa wazazi wake, njiani mkulima akamkuta jogoo wake amewakusanya makoo hamsini akiwabe- beza huku wote wakiwa katika hali ya furaha na ya maridhawa. Lakini mbwa wake aliyekuwa karibu na aliyekuwa amejikunyata kwa huzuni na majonzi, akamwambia jogoo, “Mbona mwenzetu huna huzuni?”
“Kwa nini niwe na huzuni?” Jogoo akataka kujua. “Unacheka na kufurahi na makoo wako ilhali unajua kuwa bwana wetu atakufa leo; huna hata huruma?” Akasema mbwa kwa huzuni.
“Nini kitakachomwua bwana wetu? Mbona namwona yu mzima wa kigongo tena anaonekana ana afya nzuri?” Akauliza tena jogoo.
“Sababu,” akajibu mbwa, “ni mkewe ashikiliaye kuambiwa neno ambalo bwana wetu akimwambia, atakufa!”
Jogoo kusikia vile akasema, “Basi bwana wetu ndiye mjinga wa mwisho! Hebu nitazame mimi; nina makoo hamsini wanitiio wote kwani nawafurahisha na nawaridhisha vilivyo bila tatizo lolote ilhali bwana wetu ana mke mmoja tu amsumbuaye na kumwumiza kichwa kutwa kucha! Kama mkewe hasikii maneno yake, basi aende dukani akanunue hainzarani amtandike mikwaju mpaka mke ashike adabu na akome kuulizauliza mambo yasiyomhusu!”
Yule bwana kusikia maneno ya jogoo, akaenda zake moja kwa moja mpaka dukani, akanunua bakora nyembamba ya mtobwe, akarudi nayo nyumbani kwake. Alipoingia ndani, akamwita mkewe chumbani. Alipokuwa ndani, akaubana mlango vizuri, akamtandika mkewe bakora za kutosha mpaka mke akakoma kuzaliwa! Mke akataka kujua sababu ya kupigwa vile; ndipo mumewe akamjibu, “Lililonichekesha siku ile na ulilialo sikuzote ndilo hili; na kama unataka zaidi sema!”
“Toba ya Rabbi!” akalia mke kwa maumivu makali huku akipiga mayowe, “Nimekoma, mume wangu, wala sitaki tena kulijua lile lililokuchekesha siku ile!”
* * *
BAADA YA Waziri Mkuu kusimulia kisa hiki, Shahrazad akasema, “Hakuna chochote kitakachonibadili nia katika jitihada yangu niliyoikusudia kuitekeleza.”
Basi Waziri Mkuu ikawa hana budi kumpamba bintiye kwa lebasi za hariri na vito vya tunu kabla hajampeleka kwa Sultani. Lakini kabla hajaondoka, Shahrazad akamwambia Dunyazad, “Mdogo wangu, nitakapopelekwa kwa Sultani, nitakuagiza uje. Usiku, kabla hakujapambazuka, uniamshe, useme, ‘Dada yangu, tafadhali nakusihi unisimulie moja ya hadithi zako tamu za kusi- simua ili nipate kuipitisha sehemu iliyobaki ya usiku huu tutaka- okuwa pamoja kwa mara ya mwisho.’ Halafu nitakusimulia visa ambavyo, Inshaallah, natumaini vitakuwa ni chanzo cha mwisho wa msiba uukabilio umati wa mji huu.”
Basi Waziri akamchukua Shahrazad mpaka kwa Sultani. Sultan Shahriyar alipoufunua ushungi wa Shahrazad, akastaajabu sana kuona uzuri wake usio kifani.
Basi usiku wa manane, baada ya starehe na maburudiko, Shahrazad akamwambia Sultani kwa unyenyekevu, “Ewe Seyyid yangu, nina mdogo wangu nimpendaye kuliko mboni za macho yangu; nataka kumuaga kabla hakuja kucha. Nakusihi niidhinie aje niagane naye kwa mara ya mwisho.”
Mara ileile Sultani akatoa amri Dunyazad akaletwe. Alipofika, akamkumbatia dada yake na kabla hakujapambazuka, akasema, “Dada yangu mpenzi, tafadhali nakusihi unisimulie moja ya hadithi zako nzuri ili tuipitishe sehemu ya usiku huu tutakaokuwa pamoja kwa mara ya mwisho.”
Hapo Shahrazad akamgeukia Sultan Shahriyar, akasema, “Itakuwa ni furaha kwangu iwapo Sultani ataniridhia.”
Sultani, ambaye hakuwa na usingizi wakati ule, akakubali na kumsikiliza Shahrazad akasimulia
KISA CHA MBILIKIMO MWENYE KINUNDU
KATIKA jiji la Basrah, akaanza Shahrazad, paliishi mshona nguo mmoja aliyefanikiwa sana katika kazi yake na aliyependa sana mambo ya starehe, anasa na mzaha. Ilikuwa ni desturi yake jioni
Sultan Shahriyar, Shahrazad na Dunyazad
kwenda na mkewe nje matembezini kujistarehesha. Jioni moja, wakati walipokuwa wakirejea kutoka katika starehe zao, njiani wakakutana na mbilikimo mmoja mwenye kinundu aliyekuwa akiwatumbuiza watu. Kwa kuwa alikuwa na nishai ya divai, yule mbilikimo akawa anapiga dumbak na kuimba kwa furaha. Mshonan- guo na mkewe walifurahishwa sana na vitendo vya yule mbilikimo; wakamwalika kwao ili usiku ule awe mgeni wao.
Walipowasili nyumbani, mshona nguo akaenda haraka sokoni, akanunua samaki mkubwa wa kuchoma, mikate ya kiajemi, zaituni, ndimu, na vitamutamu vya kumalizia maakuli.
Aliporudi navyo, wote watatu wakaketi, wakawa wanakula kile chakula. Kwa kuwa mke wa mshona nguo alikuwa ni mcheshi na mpenda mzaha, akamtilia yule mbilikimo kipande kikubwa cha samaki mdomoni, akamlazimisha akimeze. Kwa bahati mbaya, kile kipande cha samaki kilikuwa na mwiba mkali uliojificha. Yule mbi- likimo alipokimeza, ule mwiba ukamsakama kooni asipate pumzi, akaanguka chini. Walipomkagua, wakastaajabu kuona amekufa!
La Haula! Mshonanguo kuona vile, akanyanyua mikono juu, akaomboleza: “Hakuna mwenye nguvu na mwenye uwezo isipokuwa Mwenyezi Mungu aliyemwacha mtu huyu kufa kwetu ghafla namna hii!”
“Kilio chako hakitatusaidia kitu chochote,” akasema mkewe, “iliyobaki ni kutafuta njia ya kujisalimisha na maiti huyu!”
“Tutafanya nini?” Akauliza mshona nguo huku akitetemeka
Mshonanguo akagutuka kumwona mbilikimo amekufa! kwa khofu.
“Nyanyuka upesi!” Akatamka mkewe, “tutamfunika shuka na kumbeba nje usiku huu huu wakati mimi nikiongoza njia nikilia, ‘mwanangu ni mgonjwa, maskini mwanangu ni mgonjwa! Nani atatuelekeza kwa mganga?’”
Mshona nguo akalikubali shauri la mkewe; wakamfunika shuka yule mbilikimo, mshona nguo akambeba wakati mkewe akiongoza njia akiomboleza: “Maskini mwanangu ana ndui! Nani atamtibu ugonjwa huu alionao?”
Watu waliowaona na waliosikia maombolezo ya yule mwa- namke, wakawakwepa huku wakinong’onezana: “Msiwasogelee, wana ugonjwa mbaya wa kuambukiza!”
Basi mshona nguo na mkewe wakaendelea kumbeba yule mbilikimo huku wakiuliza nyumba ya mganga mpaka wakaifikia nyumba ya mganga mmoja Myahudi, wakaubisha mlango. Ulipo- funguliwa na mjakazi, mke wa mshona nguo akamweleza yule mjakazi, “Mpelekee bwana wako fedha hizi umwambie tafad- hali tunamsihi ashuke upesi chini aje amwangalie mwenzetu aliye mgonjwa sana.”
Mjakazi alipokwenda kumwita bwana wake, mke wa mshona nguo akamwambia mumewe: “Tumwache maiti hapa tutowekee upesi!”
Akisaidiana na mke wake, mshona nguo akamsimamisha wima yule mbilikimo, akamwegemeza kwenye ngazi, halafu waka- toka mle haraka, wakatoweka.
Kule juu mganga Myahudi kuona zile fedha, akashuka haraka. Wakati alipokuwa akishuka ngazi gizani, akampiga kumbo yule mbilikimo aliyeegemezwa pale ukutani, akamwangusha chini. Mganga kumtazama, akashtuka kumwona amekata roho. Akafikiri yeye ndiye aliyemwua kwa kumpiga kumbo. Lo masalale! Yule Myahudi akaomboleza kwa kutaja majina ya mitume Musa, Harun, Ezra na Joshua bin Nun!
Baada ya kufikiri kidogo, akambeba yule mbilikimo mpaka juu kwa mkewe, akamweleza yaliyotokea.
“Usisimame hapo kama nguzo!” Akafoka mkewe. “Kama maiti huyu atakutwa hapa asubuhi, ujue tutaangamia! Tumbebe haraka mpaka darini tukamtupe chini kwenye nyumba ya jirani yetu Mwislamu.”
Jirani yao alikuwa Mwislamu mtumishi katika jiko la Mfalme ambako alikuwa na tabia ya kuchelewa kurudi usiku. Nyumba yake iliyokuwa mbali na kwa Mfalme, siku zote waliingia paka waliofuata mapanya waliofuata jibini na nafaka zilizojaa mle; na usiku mbwa walikuwa na tabia ya kuingia jikoni mwake kula makombo.
Basi yule Myahudi na mkewe wakambeba yule mbilikimo, wakapanda naye juu ya dari yao, wakamshusha ndani ya nyumba ya jirani yao Mwislamu, wakamsimamisha kwenye ukuta wa jikoni,
halafu wakatoweka mara moja bila kuonekana na mtu.
Baada ya muda, yule Mwislamu, mtumishi wa Mfalme, usiku akarejea kwake, akaufungua mlango, akawasha mshumaa. Kuona umbile la mtu lililoegemea ukutani jikoni mwake, akagutuka, akatamka kwa hamaki: “Kumbe anayekula jibini na nyama humu jikoni mwangu si paka, si mapanya, wala si majibwa bali ni wewe! Kumbe nimeua bure takriban paka na mbwa wote wa mtaa huu bila kumshuku mtu! Basi leo utanitambua!”
Hapo akanyakua rungu lililokuwa karibu, akampiga nalo yule mbilikimo kifuani, akaanguka chini. Kuona hainuki, yule mtumishi akaingiwa na wasiwasi. Alipomwinamia, akapiga kelele: “Hakuna mwenye nguvu na mwenye uwezo isipokuwa Allah! Mungu ailaani jibini, nyama, na usiku huu uliokuleta hapa kwangu na mkono wangu ukawa ndio sababu ya kifo chako!”
Na alipoona aliyemwua ana kinundu, yule Mwislamu aka- ongeza: “Lahaula! Kuwa na kinundu haikutosha ukaongeza na wizi juu! O Allah, nirehemu kwa kitendo changu kiovu!”
Usiku ulikuwa ukianza kutoweka polepole na mapambazuko yalikuwa yakikaribia wakati yule mtumishi alipombeba yule mbi- likimo akatoka naye nyumbani mwake. Akaelekea naye moja kwa moja mpaka sokoni. Wakati huo barabara zote zilikuwa tupu hazina watu. Alipofika sokoni, akaendelea na mzigo wake mpaka kwenye duka moja. Hapo akamwegemeza yule mbilikimo kweye ukuta wa lile duka, akatoweka zake!
Baada ya muda, Mkristo mmoja, ambaye alikuwa ni mhasibu wa Mfalme, akapita pale akielekea kwenye hamamu ya jiji. Kwa kuwa alikunywa divai nyingi usiku ule, akawa anayumbayumba huku na huko akijisemea: “Mwisho wa dunia umewadia!”
Alipokaribia pale pa yule mbilikimo, akasimama, akaanza kukojoa bila kumwona yule mbilikimo aliyeegemezwa pale. Ilitukia kuwa mapema jioni iliyotangulia yule Mkristo aliwahi kunyang’anywa kilemba chake na ikambidi anunue kingine.
Basi alipokuwa akikojowa, mara akamwona yule mbilikimo,akafikiri ni mwizi anayemvizia anayetaka kumnyang’anya tena kilemba chake kipya! Mkristo akamrukia yule mbilikimo, akamkaba roho, akamwangusha chini huku akimtwanga magumi na kupiga makelele ya kumwita mlinzi wa pale sokoni.
Mlinzi alipofika, akamwona Mkristo amemkalia yule mbi- likimo kifuani huku akimpiga.
“Nyanyuka na wacha kumpiga Mwislamu” Akafoka yule mlinzi; na alipomwona yule mbilikimo amekufa, mlinzi akapiga mayowe ya mshangao akiita: “Jamani njooni! Jambo baya sana limetokea! Mkristo amemwua Muumini!”
Majuto mjukuu! Kuona yale aliyoyafanya, yule Mkristo akaanza kumwomba Yesu na Maria na kujuta kwa ulevi aliounywa usiku ule.
Yule mlinzi akamkamata yule Mkristo, akamtia pingu, akampeleka moja kwa moja mpaka nyumbani kwa hakimu mkuu wa jiji.
Asubuhi aliposimuliwa yaliyotokea, hakimu akatoa amri yule Mkristo anyogwe. Hapo mnadi akapiga mbiu ya mgambo, akatangaza mabarabarani kosa la yule Mkristo na mahali ataka- ponyongewa kesho.
Wakati wa kunyongwa ulipowadia, halaiki ya watu ikajiku- sanya katikati ya jiji kwenye uwanja mkubwa kuja kushuhudia kunyongwa kwa Mkristo. Baada ya muda, mnyongaji akatokea huku hakimu mwenyewe akiwa haadhir. Mnyongaji akamtia yule Mkristo kitanzi shingoni, akawa anasubiri amri kutoka kwa hakimu.
Mara yule Mwislamu, mtumishi wa Mfalme, akajitokeza mbele ya ule umati wa watu huku akipiga makelele: “Tafadhali usimnyonge! Muuaji si yeye bali ni mimi! Mimi ndiye mwenye hatia niliyemuua yule mbilikimo!”
Hakimu kusikia maneno yale, akamhoji: “Kwa nini umemuua?”
“Mauaji yake yametokea,” akajibu Mwislamu, “wakati niliporejea nyumbani kwangu jana usiku. Nilimkuta jikoni mwangu, nikampiga rungu, akaanguka chini, akakata roho. Kwa kuwa nili- ogopa, nikambeba mpaka sokoni. Hivyo, ni mimi ndiye niliyemuua Mwislamu mwenzangu. Basi mimi ndiye nistahiliye kunyongwa si huyu Mkristo. Sitaki roho ya Mkristo itolewe kwa kosa nililolifanya mimi.”
Aliposikia hayo, hakimu akamwachia yule Mkristo, akamwa- muru mnyogaji amtie kitanzi yule Mwislamu aliyekiri kosa lake.
Mnyongaji akamwongoza yule Mwislamu, akaelekea naye mpaka kwenye kitanzi. Alipokitundika shingoni mwake, mara yule mganga Myahudi akajitokeza hadharani akipiga kelele: “Ngoja, usimnyonge! Huyo Mwislamu hana kosa bali mimi ndiye niliye- muua huyo mbilikimo mwenye kinundu!”
Yule Myahudi naye akaeleza jinsi alivyomuua mbilikimo halafu akaongeza. “Je, dhambi yangu ya kuua mtu haitoshi? Ni lazima mwingine auawe kwa kosa nililolifanya mimi?”
Kusikia vile, hakimu akatoa amri yule Myahudi anyongwe badala ya yule Mwislamu. Lakini kitanzi kilipotiwa shingoni mwa Myahudi, mara mshona nguo naye akajitokeza mbele, akakapiga kelele: “Jamani, msimnyonge Myahudi! Hakuna yeyote aliyemuua mbilikimo isipokuwa mimi!”
Na yeye naye akaueleza ule umati uliohudhuria pale jinsi alivyomuua yule mbilikimo mwenye kinundu.
Hakimu kusikia vile akastaajabishwa sana na kisa cha yule mbilikimo mwenye kinundu, akatamka: “Kisa hiki kinastahili kuandikwa.” Hapo akatoa amri yule Myahudi aachiliwe na badala yake anyongwe yule mshona nguo.
“Inavyoonekana,” akalalamika mnyongaji, “leo jua litakuchwa bila yeyote kunyongwa!”
Ilitukia kuwa yule mbilikimo mwenye kinundu alikuwa mcheshi na mfurahishaji kipenzi wa Mfalme. Alipoona mcheshi wake hajafika kwenye kasri lake usiku kucha na asubuhi ya pili, Mfalme akatoa amri akatafutwe. Waliotumwa wakarudi, wakamwarifu Mflame kifo cha mbilikimo wake na jinsi kila mmoja wa wale watu alivyokiri kosa la kumuua.
“Nenda haraka kwa hakimu ukawalete mbele yangu wote hao waliokiri hilo kosa.” Akaamuru Mfalme.
Mjumbe akatoka haraka, akaelekea kule ambako mnyongaji alikuwa tayari kukikaza kitanzi shingoni mwa mshona nguo.
“Ngoja! Ngoja! Usimnyonge!” Akapiga kelele yule mjumbe wa Mfalme huku akijipenyeza katika ile halaiki ya watu iliyo- hudhuria pale. Kabla mnyongaji hajakivuta kitazi, yule mjumbe akamwarifu hakimu amri ya Mfalme. Hakimu naye, bila kuchelewa, akawapeleka wote kwa Mfalme: mshona nguo, Mriskto, Myahudi, Mwislamu mtumishi wa Mfalme, na ile maiti ya yule mbilikimo mwenye kinundu.
Wote walipofikishwa mbele ya Mfalme, wakajiangusha ki- fudifudi chini, wakaibusu sakafu, halafu kila mmoja wao akaanza kueleza yaliyompata.
Mfalme akastaajabu sana, akaamuru kile kisa kiandikwe kwa wino wa dhahabu. Halafu akawauliza wote waliokuwa haadhir: “Je, mmepata kusikia kisa cha ajabu kama hiki cha huyu mbilikimo mwenye kinundu?”
Yule Mkristo aliyehusika na kile kisa cha mbilikimo mwenye kindundu akawa wa kwanza kujitokeza mbele, akamsimulia Mfalme na waliokuwa hadhirina kisa kifuatacho:-
KISA CHA MKRISTO
“Seyyid yangu,” akaanza yule Mkristo, “mimi si mwenyeji wa hapa bali ni mwenyeji wa Misri na muumini wa madhehebu ya kikoptiki. Nimekuja hapa kuleta bidhaa mbalimbali kutoka kwetu kwa madhumuni ya kufanya biashara. Baba yangu alikuwa dalali mkubwa aliyejulikana sana. Alipofariki, nikaendelea na kazi yake.
|