SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI (/showthread.php?tid=799) |
SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI - MwlMaeda - 08-08-2021 YAMENIGANDA MAPENZI Mapenzi anayejua, kwa hili simshangazi, Haya yakisha kutua, kukung’uta hauwezi, Vile hukung’ang’ania, kama chawa kwenye vazi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Miaka imekimbia, tutengane na lazizi, Fikirani hunijia, kumkataza siwezi, Picha inanirudia, matukio ya miezi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Heri angekuwa Tanga, Shinyanga kwenda siwezi, Uchumi unanizinga, huko mbali sikatizi, Sasa nimebaki bunga, sioni lenye tatuzi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Niliapo ni msiba, hayakatiki machozi, Uso wangu nauzima, nizuie michirizi, Haki nimekuwa zoba, mwenyewe ninajihizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Jambo linaniumiza, mtu huyo ni mzazi, Ameoa naeleza, na watoto kwa majazi, Ijapo najikataza, kufanya makumbukizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Akituma zake picha, mimi chali sijiwezi, Nawaza kila kukicha, nimezidi siku hizi, Roho yanambia ‘acha’, ila moyo mchokozi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Tatizo wake upole, kufoka huyu hawezi, Nakumbuka siku zile, mweledi wa mapepezi, Basi ilikuwa vile, bila yeye sijilazi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Bwana huyu mtalamu, mithili kaenda kozi, Yale mambo ni matamu, hadharani sielezi, Ni kama mbuzi kwa ndimu, alikuwa mganguzi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Yana ajabu mapenzi, yakianza hayasizi, Marefu kama utenzi, wenye beti jozi jozi, Na ukiwa mwanafunzi, hutaweza piga mbizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Nilidhani Mjaluo, kwa urefu mchokozi, Weusi wenye vutio, afaa kwa matumizi, Nikakiweka kituo, kwake sikupitilizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Kijana wa kimanyema, kiliko chake kizazi, Ni mkoani Kigoma, Tabora yake makazi, Kwa sasa amesha hama, yupo Shinyanga kikazi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Kweli mahaba huua, kwa hili sibishilizi, Nimekonda hadi pua, sijisifu siku hizi, Heri zirudi hatua, hadi kwenye mwaka juzi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo DSM 0753738704 RE: SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI - MwlMaeda - 08-08-2021 Mkonikoni kasema, yana mauja mapenzi, Yakisha kukuandama, mwili unapata ganzi, Maungo yanazizima, kama umepigwa konzi, Pole sana fielida, mapenzi ndivyo yalivyo. MTU hupata madhila, ukishikwa kimahaba, Mawazo hukutawala huwa ni kama msiba, Usiku huwezi lala, wala huli ukashiba, Pole sana fielida, nduvyo yalivyo mapenzi. Mapenzi yanaadhibu, mapenzi yanaumiza, Kama hayajakusibu, kwa wajuao uliza, Walowahi pata tabu, ndani ya hilo gereza, Pole sana fielida, njoo nikupoze moyo. Mapenzi ya nusunusu, hatima yake kiwewe, Leo. Unapigwa busu, kesho hayuko na wewe, Ni kuwekwa mahabusu, matesoni ufungiwe, Yanakata kama kisu, utalia kwa mayowe, Mkonikoni kasema mapenzi yanaumiza Kivuli cha Mvumo Mfaume R.R RE: SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI - MwlMaeda - 08-08-2021 Filieda humpati,sasa yupo kiganjani Anipikia chapati,nafaidi Biriani Hii ni yangu bahati,umtoe fikirani Kivuli sijihashuwe,chombo nimeshamiliki Nilifanza mikakati,nikamvuta nyumbani Sasa ni wangu wakati,wa kupata burudani Kama ukikosa bati,kasake nyasi porini Kivuli Kivuli sijihashuwe,chombo nimeshamiliki Tutashikana mashati,hila nikizibaini Hili toto hulipati,hapa sifanyi utani Vita yangu ni ya nyati,muhali kupita nyani Kivuli sijihashuwe,chombo nimeshamiliki Abdul Ndembo Mburahati sekondari |