FASIHI SIMULIZI: MUHADHARA WA NANE: SEMI NA VITENDAWILI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Semi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=49) +---- Thread: FASIHI SIMULIZI: MUHADHARA WA NANE: SEMI NA VITENDAWILI (/showthread.php?tid=722) |
FASIHI SIMULIZI: MUHADHARA WA NANE: SEMI NA VITENDAWILI - MwlMaeda - 08-01-2021 MUHADHARA WA NANE: SEMI NA VITENDAWILI
Semi ni tungo au kauli fupifupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Semi zinajumuisha tanzu kama vile methali, vitendawili, mafumbo, misimu, lakabu na kauli tauria (Mulokozi 1996). Semi hugawanywa katika vipera kama vile:
– Misemo
– Vitendawili
– Methali
– Mafumbo
– Mizungu
– Lakabu, n.k
Kitendawili ni usemi wenye kuchochea fikra na udadisi wa jambo. Huwa ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbue.
Muundo wa kitendawili
Vitendawili vingi huwa na muundo mmoja tu. Muundo wa kimapokeo huwa na sehemu nne ambazo ni:
(a) Kiingizi/kitangulizi – fanani huanza kwa kusema…. kitendawili ….. na hadhira hujibu …… tegaaaa.
(b) Fumbo lwenyewe – mf. Kuku wangu katagia mibani?
© Swali la msaada – mf. Tudokeze basi (iwapo jibu linafahamika huwa hakuna haja ya swali la msaada)
(d) Jibu la fumbo – iwapo wote watashindwa kutoa jibu mtegaji hupewa mji na kisha kutoa jibu.
Mtindo wa kitendawili
Vitendawili huwa na mtindo wa majibizano. Mtambaji hutoa kitangulizi cha kitendawili na fumbo lenyewe mf. Kitendawili……kuku wangu katagia mibani.
Mtambiwa hujibu tega na kutoa jibu la kitendawili chenyewe – nanasi.
Dhima ya vitendawili
(i) Vitendawili hutegwa kwa lengo la kukomaza fikra na falsafa.
(ii) Hutegwa ili kuburudisha na kuliwaza
(iii) Hutumiwa kama chombo cha kufanya bongo ziwe na ustadi,busara na mahiri wa urazini katika kupambana na maisha.
(iv) Huwaandaa vijana kuelewa mazingira yao yalivyo.
(v) Hutumika kufunza adabu za vizazi vilivyopita.
(vi) Hufanya vijana wawe wepesi wa kufikiri,kuamua na kutoa majawabu maridhawa.
(vii) Huchochea itikadi za jamii kwa vijana
(viii) Hutajirisha na kupamba mazungumzo
(ix) Hutumiwa kwenye kuanzisha,kutofautisha,kukatisha au kukamilisha hadithi.
USANIFU WA VITENDAWILI
Vitendawili hujipambanua kwa lugha ya kawaida vikijihusisha zaidi na silica,itikadi,utamaduni,uchumi,siasa na uhusiano wa matabaka ya kijamii.
Vitendawili vya Kiswahili vina utanashati mkubwa wa lugha. Vina matumizi makubwa ya tamathali za usemi,lugha ya kishairi na mafumbo.
Mbinu zitumiwazo katika vitendawili
(i) Mliolio
Vitendawili huwa na mbinu ya tanakali za sauti katika uwasilishaji wake.
Mfano:
– Parakacha ti – ugonjwa wa matende
– Pa funika,pa funua – unyayo wakati wa kutembea
(ii) Ushairi
Ni mbinu ya kutumia mapigo ya kimuziki kwa utaratibu maalumu wakati wa kuwasilisha kitendawili.
Mfano:
– Mchana uu,usiku uu- macho
– Futi kafutika futi, futi kafutika futi – kumbi,fuu,nazi,maji. (kumbi limefunika kifuu,kifuu kimefunika nazi na nazi imefunika maji)
– Huku ng’o na kule ng’o – giza
(iii) Tashihisi
Ni mbinu ya kuvipa uhai na uwezo wa kutenda kama binadamu vitu visivyo na uwezo huo.
Mfano:
– Popo mbili zavuka mto – macho
– Popote niendapo ananifuata – kivuli
– Kila nipitapo nasikia wifiwifi – mbaazi
(iv) Dhihaka
Hii ni mbinu ya kumhujumu na kumdunisha mtu kwa kutumia vitendawili.
Mfano:
– Kitu kidogo kimemtoa mfalme kitini – haja
– Kamba ndogo imefunga dume zima – usingizi.
|