SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI (/showthread.php?tid=2494) |
SHAIRI: YAMENIGANDA MAPENZI - MwlMaeda - 04-02-2022 YAMENIGANDA MAPENZI Mapenzi anayejua, kwa hili simshangazi, Haya yakishakutua, kukung’uta hauwezi, Vile hukung’ang’ania, kama chawa kwenye vazi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Miaka imekimbia, tutengane na lazizi, Fikirani hunijia, kumkataza siwezi, Picha inanirudia, m atukio ya miezi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Heri angekuwa Tanga, Shinyanga kwenda siwezi, Uchumi unanizinga, huko mbali sikatizi, Sasa nimebaki bunga, sioni lenye tatuzi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Niliapo ni msiba, hayakatiki machozi, Uso wangu nauziba, nizuie michirizi, Haki nimekuwa zoba, mwenyewe ninajihizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Jambo linaniumiza, mtu huyo ni mzazi, Ameoa naeleza, na watoto kwa mashazi, Ijapo najikataza, kufanya makumbukizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Nikiona zake picha, mimi chali sijiwezi, Nawaza kila kukicha, nimezidi siku hizi, Roho yanambia ‘acha’, ila moyo mchokozi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Tatizo wake upole, kufoka huyu hawezi, Nakumbuka siku zile, mweledi wa mapepezi, Basi ilikuwa vile, bila yeye sijilazi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Bwana huyu mtalamu, mithili kaenda kozi, Yake mabo ni matamu, hadharani sielezi, Ni kama mbuzi kwa ndimu, alikuwa mganguzi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Yana ajabu mapenzi, yakianza hayasizi, Marefu kama utenzi, wenye beti jozi jozi, Na ukiwa mwanafunzi, hutaweza piga mbizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Nilidhani Mjaluo, kwa urefu mchokozi, Weusi wenye vutio, afaa kwa matumizi, Nikakiweka kituo, kwake sikupitilizi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Kijana wa Kimanyema, kiliko chake kizazi, Ni mkoani kigoma, Tabora yake makazi, Kwa sasa ameshahama, yupo Shinyanga kikazi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Kweli mahaba huua, kwa hili sibishilizi, Nimekonda hadi pua, sijisifu siku hizi, Heri zirudi hatua, hadi kwenye mwakajuzi, Sipendi sasa naumwa, yameniganda mapenzi. Mtunzi Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 |