SHAIRI: HALI HALISI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: HALI HALISI (/showthread.php?tid=2106) |
SHAIRI: HALI HALISI - MwlMaeda - 01-11-2022 HALI HALISI
Hali ya watunga hoja, ujinga kutokosowa
Hali ya jinsi moja, kuandamania ndowa
Hali hii ni kioja, kwa dini wanaojuwa
Hii ndo hali halisi, ya uwongo sijazuwa
Hali ya walo na pesa, kuzidi kuongezewa
Hali ya waso na hisa, kuishi kama wakiwa
Hali yanitesa hasa, ni nani wakuondowa
Hii ndo hali halisi, ya uwongo sijazuwa
Hali ya wale makada, ya tatizi kuyazuwa
Hali kwa wanuka shida, kushindwa kusaidiwa
Hali yaleta kaida, wabaya kusujudiwa
Hii ndo hali halisi, ya uwongo sijazuwa
Hali ya wapenda hoji, na tufani kuzolewa
Hali ya unyanyasaji, ja samaki kuvuliwa
Hali hino sitaraji, kwa nchi nilozaliwa
Hii ndo hali halisi, ya uwongo sijazuwa
Hali ya elimu bora, vyuoni walopatiwa
Hali hakuna ajira, na walishahaidiwa
Hali mbaya itagwira, chalinze walitongowa
Hii ndo hali halisi, ya uwongo sijazuwa
Hali ya wenye ubavu, vya wanyonge kukwapuwa
Hali kwa wenye uvivu, kufikiri fikiriwa
Hali ya pembe za ndovu, weziwe tuzo kupewa
Hii ndo hali halisi, ya uwongo sijazuwa
Hali ya kila utungo, mzuri tamati huwa
Hali ni kwenye ukingo, mashuwa yangu yapwewa
Hali likamili lengo, kalamu chini natuwa
Iwapo siyo halisi, nasubiri kosolewa
|