SHAIRI: MOYO USIRUDI NYUMA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: MOYO USIRUDI NYUMA (/showthread.php?tid=2033) |
SHAIRI: MOYO USIRUDI NYUMA - MwlMaeda - 01-06-2022 1- Moyo ninasisitiza, yalonenwa huko nyuma.
Kifani ninateleza, yapendeze nayosema.
Ushindwapo kujikaza, sinao mimi uzima.
Moyo wangu nisikiza, hakuna lilo daima.
2- Songa mbele tena wima, hata usiku wa giza.
Kwima papo ukikwama, shingo usije geuza.
Uyumbapo ninazama, usimamapo nasoza.
Moyo wangu nisikiza, hakuna lilo daima.
3- Walonena wa hekima, yashike mwiko kupu’za.
Mapambano yasokoma, maisha wametweleza.
Hashindi mshika tama, machozi anojijaza.
Moyo wangu nisikiza, hakuna lilo daima.
4- Duniani tangu zama, hayeshi ya kuumiza.
Mtumaini daima, Mola Mlezi Muweza.
Tama nafunga nudhuma, Sisitizo namaliza.
Moyo wangu nisikiza, hakuna lilo daima.
Alhaaj Osan Omari Ngulangwa.
(Lilengani)
(Lulu za Nyaminywili)
Nyaminywili, Rufiji.
29 Rabiul Thani 1439.
17 Januari 2018.
|