SHAIRI : MOLA WAPE WANIPAO (2) - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : MOLA WAPE WANIPAO (2) (/showthread.php?tid=2023) |
SHAIRI : MOLA WAPE WANIPAO (2) - MwlMaeda - 01-05-2022 Utunzi kwako Wahabu, ewe langu kimbilio
Ni mengi yanonisibu, toka kale hadi leo
Ndo nakuomba Muhibu, yatende nitarajio
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao
Kikumbuka zangu zama, sitendi ila kilio
Mwenyewe nilisimama, mawio hadi machweo
Hakika nilijituma, kuvuta mafanikio
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao
Kwa miaka thelathini, ndani menipa mkao
Miguu inga mwilini, ikakosa mtembeo
Yalo nje siyaoni, ila kwa masimulio
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao
Kwa busara na hekima, kwangu waleta gawio ‘Kirudi vua salama, naletewa kitoweo
Mwenyezi wajaze mema, wamiminie mafao
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao
Tamaa za wangu mke, kazijengea uzio
Ni radhiye asumbuke, juu yangu kila leo
Ili nisidhalilike, tukavaa moja nguo
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao
Ya- Rabbi ijapofika, kwako yake marejeo
Nitwae mimi haraka, yeye umpe kikao
Nahofu kudhalilika, kiondoka yangu ngao
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao
Illahi usiwanyime, wape kwangu iwe ngao
Wote wake kwa waume, hata na kizazi chao
Nipate ishi Makame, zidisha riziki zao
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao.
Siyo kwa yangu mapenzi, hapa kubwaga kituo
Mwili umeshika ganzi, ambatana na legeo
Ni ipi tiba watunzi, nimechoshwa na zinguo
Illahi usiwanyime, wape wote wanipao
MBARUKU ALLY
MOTO WENU
08/04/2016
Nikiwa Dodoma
|