SHAIRI : HALI HALISI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : HALI HALISI (/showthread.php?tid=2005) |
SHAIRI : HALI HALISI - MwlMaeda - 01-04-2022 SHAIRI : HALI HALISI
Dawa ingekuwa sumu,ningekunywa kwa dakika.
nitangulie kuzimu,nikapate pumzika.
ila Mungu ni Rahimu,kwake tamaa naweka.
Musione tabasamu,moyoni nimeyaweka.
Umekunjuka wajihi,nikaapo ninacheka.
ila naapa wallahi,maini yanikatika.
basi musinikebehi,musione ni dhihaka.
Mungaona nafurahi,moyoni nimeyaweka.
Mezama kina kirefu,cha huzuni na wahaka.
ningalikuwa dhaifu,yote yangebainika.
ila ni Mola Raufu,mjawe nasitirika.
Ningawa mchangamfu,moyoni nimeyaweka.
Japo hujichangamsha,kuficha yalofichika.
moyo huutononesha,yasije kudhihirika.
kila la kunikondesha,nabeba bila kuchoka.
Nilipo nina bashasha,moyoni nimeyaweka.
Nimeeleza vilivyo,ukingoni nimefika.
mujue ndivyo ilivyo,mewapa ilo hakika.
na hivyo muniwazavyo,sivyo imeeleweka.
Vyovyote munionavyo,moyoni nimeyaweka.
SARAI MAULID +254726765519
MOMBASA KENYA.
|