SHAIRI: “YALIYOPITA YAMEPITA” NA MATHIAS MNYAMPALA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: “YALIYOPITA YAMEPITA” NA MATHIAS MNYAMPALA (/showthread.php?tid=2000) |
SHAIRI: “YALIYOPITA YAMEPITA” NA MATHIAS MNYAMPALA - MwlMaeda - 01-04-2022 TUJIKUMBUSHE KALE YETU
Mathias Eugen Mnyampala, mmoja wa washairi maarufu na wa daraja la juu katika ulimwengu wa Kiswahili alitunga shairi liitwalo “YALOPITA YAMEPITA”. Shairi hili alilitunga baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 akiwa na nia ya kuwaasa washairi wa wakati wake kukomesha magombano na mivutano yao ya kishairi na badala yake watunge tungo aali zenye kuadilisha jamii (ikumbukwe kuwa miaka ya kabla ya uhuru malumbano ya washairi yalishitadi sana hadi kufikia hatua ya kuwagawa washairi katika makundi). Katika shairi hilo tunamuona Mathias Mnyampala akiwataja washairi bulibuli kama ilivyo desturi ya washairi kuzinduana na kuhamasishana kwa kutajana majina (kumbe jadi hii ya kutajana majina ndani ya tungo hatuianzi siye wa zama hizi). Katika shairi hilo Mnyampala alisema:
Hapana cha upinzani, cha ugomvi na matata
Watunzi na ubishani, vile watunzi kuteta Sasa wanayo imani, umoja wamefumbata Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Ya uhuru yatungeni, ya ugomvi yamepita
Tanganyika ni amani, nchi haina salata Washairi unganeni, na utunzi kutakata Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Bwana Gonga muhisani, mtunzi mwenye kunata
Khamisi bini Amani, mwenye tungo za kutata Ugomvi jama acheni, tungeni ya kumemeta Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Msanifu Makarani, mwenye tungo za kuvuta
Bwana Miraji rubani, mtunzi usiyesita Pia na Makwayasoni, mtunzi mwenye mafuta Ya ugomvi tuacheni, na tutunge ya uhuru Bwana Juma Ujijini, na Adamu nawaita
Mheshimiwa wa dini, Sheikh Amri Kaluta Wambieni suluhuni, madaraka tumepata Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Nawe Bwana Damiani, shauri hili kamata
Na kule Magharibini, ni Idrissa kakita Waaseni ya uhuni, waungwana kutafuta Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Mandevu wa Buguruni, na Shaha wanaye Chata
Kazimoto na Imani, Kiwato na Chamatata Tanganyika tukuzeni, kiwango tumekigota Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Mwaruka na Selemani, waacheni kuwasuta
Na Palla wa Uteteni, Bini Mchuchuli Sheta Na adui pendaneni, hata kama ni msuta Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Shinyanga ni Khalfani, fundi kucheza karata
Na Unguja kisiwani, washairi bora sita Kwa umoja shikaneni, pamoja kujipakata Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Tama Bwana Shaabani, na Saidi msojuta
Mahamudu Hamduni, na Snow mwenye kuseta Nawe Bwana Saadani, na kurumbiza fuata Ya ugomvi yamepita, na tutunge ya uhuru Shime washairi wa leo tushike busara na hekima iliyomo ndani ya shairi hilo la Sheikh Mathias Mnyampala kwani shairi lake limehifadhi mafunzo yenye adili yasiyochujuka kwa zama zote
Hassan R. Hassan
Chuo Kikuu cha Dodoma
**Wakatabahu**
|