SHAIRI : UTAMU WA NDOA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : UTAMU WA NDOA (/showthread.php?tid=1983) |
SHAIRI : UTAMU WA NDOA - MwlMaeda - 01-04-2022 UTAMU WA NDOA
Kuna vilivyo vitamu, Ndoa ni zaidi yao
Tena ile ilodumu, Utamu kila uchao
Ndoa rahaye adhimu, Heshima ikiwa ngao
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Tunafaidi ndoani, Yangu hamu kuwajuza
Utamu uso kifani, Kwa dhati nawaeleza
Ndoa jambo la thamani, Kubwa sauti napaza
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Tunavila vya halali, Haramu twaikimbia
Vya karibu sio mbali, Bila ya kufakamia
Ikiwa nzuri kauli, Ndoa haitokimbia
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Ndoa ni jambo la enzi, Walioana wahenga
Tena jambo la mapenzi, Ni wajibu kuichunga
Ndoa hitaki ushenzi, Wala magomvi kujenga
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Utamu wanaujua, Wanandoa majumbani
Magonjwa wakiugua, Kudekea mapajani
Jamani tuombe dua, Ndoa ziwe na amani
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Wanandoa marafiki, Mahaba kiunganishi
Jitengeni wanafiki, Wacheni uchonganishi
Ndoa tamu hivunjiki, Toeni wenu uzushi
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Yapikwa mahanjumati, Ndoani papakuliwa
Halua na kalimati, Vitamu sana vyaliwa
Samaki wali chapati, Utamu wa kuchachawa
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Amwambie mume mke, Mume nakupenda sana
Mume kidogo acheke, Ndomana tumeoana
Basi uje unishike, Pingamizi kwako sina
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Njoo tuoge bafuni, Mume wangu “mai dia”
Kisha tulale chumbani, Usiku umewadia
Leo sijui kwanini, Hamu imenizidia
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Ndoa yazaa watoto, Faraja ya wanandoa
Pia huzidi kipato, Ridhiki MUNGU hutoa
Utamu ndoa si ndoto, Nawambia wasooa
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
Hatima nimeifika, Tamu ya ndoa kunena
Kwaherini naondoka, Ishala tutaonana
Ndoa sifa kuipaka, La kuongezea sina
Tamu kuliko asali, Ndoa jaala ya MOLA
(Kitogo wa Kitogo, Mwananchi wa Kawaida, Julai 31, 2018, Morogoro)
|