SHAIRI : RAIS ANAYEFAA KWA MUNGU ATATOKEA - MwlMaeda - 01-04-2022
- Kampeni zimeanza, uchaguzi wasogea
Ilani wanatangaza, kuwanadi wagombea
Swali la kujiuliza, nani anayetufaa?
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea.
- Wengi wamejitokeza, ikulu kugombania
Mazuri wayatangaza, tupate kuwachagua
Kama ukiwachunguza, ni vigumu kuamua
Raisanayefaa, kwaMunguatatokea
- Chama gani kinaweza, kuivusha Tanzania?
Kero zetu kumaliza, watu waache kulia?
Rushwa kuitokomeza, ufisadi kufukia
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Sifa za anayeweza, kuwa Rais sawia
Ni amchaye Muweza, Muumbaji wa dunia
Mwenye kujinyenyekeza, watu kuwatumikia
Rais anayefaa, kwa Munguatatokea
- Asiyekwenda kuuza, mali za Watanzania
Wala kujipendekeza, kwa wanaotuibiaMwenye sifa ya kuweza, maovu kuyakemeaRais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Asiyejitanguliza, kwake kujipakulia
Awezae kufukuza, wanaotuharibia
Mwenye kuitekeleza, katiba ya Tanzania
Raisanayefaa, kwa Mungu atatokea
- Yule asiyewabeza, fukara kuwabagua
Aweza kuwatangaza, mali wanotuibia
Vijana nao ajuza, aweze kuwatetea
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Awezae kuzitunza, mali zote zaraia
Wageni wanowekeza, wazingatie sheria
Aweze kuwahimiza, kodi zetu kulipia
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Kilimo kiwe cha kwanza, njuga akikivalia
Viwanda wamedumaza, yeye ajekufufua
Ajira kuzitokeza, uchumi kuufufua
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Utalii kuukuza, kipato kuongezea
Ufanisi kuukaza, huduma za jumuia
Ukali kuongeza, uzembe ujepotea
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Kila ninakoangaza, simjui anofaa
Mola peke anaweza, kutupatia Kifaa
Maombi tukiongeza, Yeye atatusikia
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Yeye atakayeweza, usukani kuchukua
Pasi kutudidimiza, ni vigumu kumjua
Mungu kumtanguliza, ndio njia nawambia
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Wengi wamejitokeza, wakidai wanania
Ya machungu kumaliza, ikulu wakiingia
Kumbe myoyoni wawaza, faida kujipatia
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Wagombea nakataza, mziepuke ghasia
Yaache yenye kukwaza, kote mtakotembea
Sera zenu kueleza, pasi kuleta udhia
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Ninarudia kukaza, jibu la Watanzania
Maombi jambo la kwanza, Mola asikie dua
Mmoja kumchomoza, hata kama wajemia
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Shairi nalikatiza, hapa sitaendelea
Maneno niloeleza, nibudi kuzingatia
Mungu uliye Muweza, ibariki Tanzania
Rais anayefaa, kwa Mungu atatokea
- Rodgers Namwenje0764 222244
|