SHAIRI : MANENO YA KISWAHILI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : MANENO YA KISWAHILI (/showthread.php?tid=1975) |
SHAIRI : MANENO YA KISWAHILI - MwlMaeda - 01-03-2022 Kwanza kaa ufikiri, maneno haya yapime Usimle kwa kikiri, kaa kwanza mtazame Litaja kunguza kweli, kaa lenye moto shume Ayapingaye maneno, si mswahili wa ndani Kata mchongoma ule, ela situmie shoka Kayaaza maji tele, na kata imekatika Katibu wa kata ile, duniani katutoka Ayapingaye maneno, si mswahili wa ndani Kweli mepatiwa pasi, ya kusafiri nchini Nguo ukapiga pasi, ili wende safarini Mitihani ulopasi, hairidhishi lakini Ayapingaye maneno, si mswahili wa ndani Bi haji kufuma kamba, mwenyewe keshazoea Wala hana jingi vumba, kamba samaki muruwa Jamaa yule kwa kamba, uongo amebobea Ayapingaye maneno, si mswahili wa ndani Paa pia ukitua, juwa huwi kama njiwa Ninaomba kumjua, paa aloliezua Ukila utasinzia, paa mtamu sawia Ayapingaye maneno, si mswahili wa ndani Kwenye nyumba za kupanga, kuna vituko pomoni Refa apiga kipenga, panga lipo kiunoni Mipango uliyopanga, yote ya kihayawani Ayapingaye maneno, si mswahili wa ndani Ua lakini ujue, hilo silo jambo jema Ua wa bibi somoe, umeanguka mchana Ua lipi niangue, nimpe aloegama Ayapingaye maneno, si mswahili wa ndani Maneno haya tapenda, kwenye lugha kiyajua Taa, pamba, nalo ganda na neno litwalo jua Kwa kweli yalivyoundwa, ni utamu kitumia Ayapinganye maneno, si mswahili wa ndani @haki zote zimehifadhiwa #mzee m. y |